Hujuma nzito ndani ya kambi ya Dk. Magufuli
Hatimaye mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameibuka hadharani na kuzungumzia
tatizo la kuwapo kwa baadhi ya wafuasi wa chama chake kumhujumu kwa
kuunga mkono harakati za upinzani.
Akizungumza kwenye viwanja vya Zimbiilo, Wilaya ya Muleba Kusini
jana, Magufuli alisema anatambua kuwapo kwa baadhi ya wanaCCM
wanaojionyesha kumuunga mkono nyakati za mchana lakini inapofika usiku
hubadilika na kuwaunga mkono wapinzani.
“Naomba na nyinyi msiniangushe maana wengine mchana mnakuwa CCM,
usiku mnahamia vyama vingine, mimi nina moyo kama nyie jamani
msiponichagua nitakwazika sana Wanamuleba,” alisema Magufuli.
Hivi sasa, Magufuli amekuwa akichuana vikali na Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
anaeywakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF). Wote
wawili wamekuwa wakivutia maelfu ya wananchi karibu katika kila
mikutano yao ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25.
Kadhalika, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo,
alizungumzia pia tatizo hilo la kuwapo kwa wanachama wa CCM ambao
wamekuwa wakisaidia wka kificho kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya
Ukawa, Lowassa.
Bulembo alifichua hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kumnadi Dk. Magufuli katika Jimbo la Bukoba Vijijini.
Akieleza zaidi, Bulembo alisema ana ushahidi kwamba ziara ya
Lowassa mkoani humo iliratibiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho na
hivyo akawataka kuamua moja, ama kuitumikia CCM kwa dhati au kuondoka
CCM mara moja na kumfuata Lowassa. “Msidhani hatuwafahamu. Mikakati yote
na namna mnavyofadhili Ukawa na Lowassa tunafahamu, tena tunawafahamu
kwa majina na nawaambia ole wenu... msipoondoka wenyewe, tutawafukuza
baada ya Dk. Magufuli kushinda,” alisema Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM.
“Anayempenda Lowassa na Ukawa avue magwanda ya CCM na awafuate
huko. Hatutaki watu ambao mchana ni CCM usiku ni Lowassa… hili ni gari
kubwa. Wengine wanashuka, wengine wanapanda,” alisema Bulembo.
Alisema yeyote mwenye kinyongo na CCM hafai kubaki ndani ya chama
hicho kwa sababu (chama hicho) kina wanachama wengi na hakiangalii uwezo
wa mtu kifedha.
“Tunawajua mnaomng’ang’ania Lowassa. Lakini nawahakikishia kuwa
mtalia baada ya uchaguzi wa mwaka huu... mnajifanya CCM lakini
mnafadhili upinzani, mwisho wenu unakuja,” alisema Bulembo.
KUKOMESHA MAFISADI
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alirudia kauli yake kuwa kamwe
hatalea mafisadi wanaorudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa manufaa yao
binafsi.
Alisema watu wenye tama ya fedha ndiyo wameifikisha nchi pabaya kwani fedha nyingi zimeishia mikononi mwao.
Alisema atahakikisha Tanzania haiendelei kuwa shamba la bibi kwa
sababu yeye hakuomba urais kwa majaribio bali kupambana na wezi wote wa
mali za umma.
IKULU NJIA NYEUPE
Kuhusiana na safari ya Ikulu baada ya Oktoba 25, Magufuli alisema
njia ni nyeupe kwake kwa sababu hakuna mgombea yeyote mwenye sifa
zinazofanana naye.
Dk. Magufuli alisema kwa namna wananchi wanavyompokea kwenye
mikutano yake, ni dalili ya wazi kwamba hakuna kizingiti cha yeye
kushindwa kuingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu.Alisema Ikulu ni ya CCM
na wapinzani wamebaki kuwa wasindikizaji wa chama hicho na kwamba, hata
wao (wapinzani) wanajua fika kwamba hawataweza kuingia Ikulu.
“Ikulu ni ya Magufuli. Wengine ni kama wale wasindikizaji wa
harusi. Wanamuleba msirubuniwe,” alisema Dk. Magufuli huku wananchi hao
wakishangilia kwa kiitikio cha “Rais! Rais! Rais!”
RANCHI 52
Akiwa katika viwanja vya Polisi Kamachumu, Wilaya ya Muleba
Kaskazini, Dk. Magufuli alielezea kukerwa na namna ranchi 52
zilivyobinafsishwa vibaya na kuwasababishia wananchi wengi wabaki bila
ardhi, huku akimshushia waziri mmoja wa serikali ya Rais Kikwete. Hata
hivyo, hakutaja jina la waziri huyo. “Katika vitu vilivyoniumiza nikiwa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi ni namna ranchi hizi zilivyogawiwa ovyo ovyo,
simtaji waziri huyo maana wote mnamjua. Lakini cha ajabu hao hao ndiyo
wanakuja kwenu kuomba kura,” alisema.
Aidha, alisema akiingia madarakani atahakikisha anawezesha
kuongezeka bei ya kahawa na kuiongezea thamani ili wakulima wa zao hilo
wainuke kiuchumi.
KAGASHEKI: Ufisadi halmashauri ushughulikiwe
Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Balozi Hamis
Kagasheki, alimuomba Dk. Magufuli kushughulikia ufisadi uliopo katika
halmashauri nyingi nchini.
Kaghasheki alitoa ombi hilo katika mkutano huo wa kampeni jana.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment