Kampeni CCM, Ukawa balaa
KAMPENI za uchaguzi za mwaka huu kati ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni balaa kutokana na mafuriko ya watu, lakini zimesifiwa na wengi kwamba mpaka sasa zinakwenda kistaarabu ukilinganisha na miaka ya nyuma. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa mikutano yote mikubwa ya makundi ya wanasiasa hao inayokusanya watu wengi, imekuwa ikiisha salama na wakati wagombea urais, Dk. John Magufuli (pichani) wa CCM na Edward Lowassa wa Ukawa wamekuwa wakihubiri amani na utulivu katika nchi.
Mwanasheria Dk. Ngali Maita alipoulizwa maoni yake juu ya mwenendo wa kampeni aliliambia gazeti hili kwamba amefurahishwa kuona mikutano mikubwa inafanyika na hakuna fujo zinazotokea badala yake watu wanakuwa makini kusikiliza sera za vyama ili siku ikifika wafanye uamuzi sahihi. “Miaka ya nyuma kwenye kampeni, mikutano inayokusanya watu wengi ilikuwa haikosi vurumai, lakini mpaka sasa mwaka huu hayo sijayaona na badala yake wagombea wanamwaga sera na wanasisitiza amani,” alisema Dk. Maita. Mmoja wa wagombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli katika kampeni zake amekuwa akisisitiza amani, kwa mfano alipokuwa katika Jimbo la Kilindi hivi karibuni aliwataka wananchi kudumisha amani akasema: “Ndugu zangu hakuna kitu muhimu kama amani ya nchi yetu. Tuitunze amani. Tusibaguane kwa misingi yoyote ile.” Aliongeza kuwa ana dhamira ya kuwaunganisha Watanzania wote na ndiyo maana anaomba kura kwa wananchi wa vyama vyote na watu wa dini zote.

Mwanzoni kabisa mwa kampeni, Lowassa naye alisisitiza kuwa kampeni zao zitakuwa za amani, na imetokea hivyo kwani mikutano yao yote imekuwa ikiisha kwa amani licha ya kuhudhuriwa na watu wengi. Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mabango yenye picha ya Lowassa yamekuwa yakibanduliwa sehemu mbalimbali nchini licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa karipio na kueleza kuwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa sheria. Hali hiyo imejitokeza mkoani Iringa, ambako vijana wanaofanya kazi ya kuweka mabango hayo waliwekwa ndani na jeshi la polisi na jijini Dar es Salaam ambako bango lililokuwa limewekwa katika Soko la Kariakoo liliondolewa saa chache tu baada ya kubandikwa na hivyo kuzua mjadala kila kona lakini pia bango kubwa lililowekwa karibu na Kituo cha Mafuta cha Oil Com Mwenge limeng’olewa na mwandishi wetu alikuta wafuasi wa Lowassa wakilaani. Wakati wale waliokamatwa mkoani Iringa wakidaiwa kuwekwa ndani pasipokuwa na sababu yoyote hadi pale walipotolewa na maofisa wa Chadema, jijini Dar es Salaam bango hilo liliondolewa na uongozi wa Soko la Kariakoo kwa madai ya kubandikwa kimakosa. Hata hivyo, hivi karibuni wafanyakazi wa kampuni moja walifika sokoni hapo na kuanza kubandika bango hilo lililokuwa na picha ya Lowassa, likiwa na maandishi yanayosomeka; ‘Edward Lowassa…Ni wakati wa mabadiliko.’


Post a Comment