NICKI MINAJ MALKIA WA HIP HOP
Na Hans Mloli
UNAPOTAJA majina ya wasanii wakali wa Hip Hop kimataifa jina la Nicki Minaj lazima litakuwemo kwenye 5 bora, ubora wa kazi zake pamoja na vituko vyake vimemfanya awe bora kila kukicha.
Weka mbali vituko na mavazi yake ya kimitego, Nick Minaji ambaye jina lake halisi ni Onika Maraj ameonyesha uwezo mkubwa akiwa chini ya usimamizi wa Lebo ya Young Money Entertainment na ndiye malkia wa Hip Hop nchini Marekani kwa miaka kadhaa sasa.
Alipotokea Nicki Minaj
Licha ya kuipeperusha vema Marekani lakini Minaj ni mzaliwa wa Trinidad & Tobago, aliyeanza kuliona jua mwaka 1982. Akiwa na miaka mitano wazazi wake walitengana, akachukuliwa na bibi yake ambapo alihamia New York, Marekani.
Akiwa na umri wa miaka 19 alijiingiza kwenye maigizo, alifeli na kuangukia kwenye kazi ya uhudumu wa mgahawa, huko nako alishindwa baada ya kufukuzwa kazi katika migahawa 15 kwa sababu mbalimbali.
Alianza kuingia kwenye muziki rasmi kuanzia mwaka 2004 lakini ilikuwa ni mpaka miaka minne baadaye ndipo alipoanza kupata mafanikio.Mwaka 2009, alifanikiwa kukutana na bosi wake wa sasa, Lil Wayne na kusaini dili kujiunga na Young Money, hapo ndipo safari yake ya mafanikio ilipokolea.
Kufunika katika Tuzo za BET
Baada ya kuonekana katika kazi kadhaa za lebo yake, alipata mwaliko kutoka katika Tuzo za Black Entertainment Television (BET) mwaka 2009 kwa kufanya mitindo huru ‘freestyle’ katika kipengele cha Cypher ambacho kilizidi kumtangaza duniani kote.
Rekodi kwa rekodi BET
Nicki ambaye ana uhusiano wa kimapenzi na rapa Meek Mill ameendelea kubeba tuzo kila mwaka ikiwemo ile ya mwaka huu aliotwaa wiki iliyopita katika kipengele cha Msanii Bora wa Hip Hop Mwanamke.
Tuzo hiyo ni ya sita, ilimfanya kufikisha tuzo sita ambazo ni nyingi za kipengele hicho akimpiku Missy Elliott ambaye ametwaa mara tano.Hivyo, Nicki anashika nafasi ya pili kwa kuwa msanii wa kike aliyetwaa mara nyingi tuzo hiyo nyuma ya Trina mwenye tuzo tisa.
Nicki amewafunika hata wanaume mastaa wakiwemo Lil Wayne, Jay Z, Kanye West, Alicia Keys na 50 Cent kwa kuwa amefikisha tuzo 10 za BET kwa jumla, nyuma ya Beyonce mwenye 19 na Chris Brown mwenye 14.
Atamba katika Jarida la Forbes
Umaarufu umemfanya aingize fedha nyingi kiasi cha kushindana na mastaa wa kiume, Jarida la Forbes limemtaja mara kadhaa kuingia kwenye orodha ya wasanii 10 bora wa Hip Hop walioingiza fedha nyingi ndani ya mwaka.
Bifu za kumshusha
Lil Kim aliwahi kutengeneza ‘bifu’ za hapa na pale alipoona Minaj anazidi kuteka dunia ya Hip Hop lakini ubora wa Minaj ukamfanya Kim apotee kimyakimya.
Bifu za aina hiyo pia zilitokea kwa wasanii wengi hasa wa kike akiwemo Iggy Azalea lakini naye aligonga mwamba. Hivyo mpaka sasa inaaminika kuwa Nick Minaj ndiye Malkia wa Hip Hop.
KAULI YA MINAJI WIKI HII
Najua Meek anatamani mtoto lakini sipo tayari kubeba ujauzito kwa sasa.

Post a Comment