Msuva, Cannavaro wazima disco la ubingwa Yanga
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Simon Msuva.
Nicodemus Jonas,Dar es Salaam
YANGA imeahirisha zile sherehe za kufurahia ubingwa wa 25 ilioupata timu yao katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa wachezaji waliochangia kupatikana kwake hawapo nchini.
Sherehe hizo zilipangwa kufanyika leo makao makuu ya Yanga kwenye Uwanja wa Kaunda, lakini kukosekana kwa wachezaji waliopo Taifa Stars wakiwemo Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Simon Msuva, Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul na Salum Telela kumestopisha ‘pati’ hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, ameliambia Championi Jumamosi, isingekuwa vizuri kwao kufanya sherehe hiyo leo huku wachezaji hao wakikosekana kwani wamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo.
Muro alisema kutokana na hali hiyo, sherehe hizo sasa zitafanyika siku ya Sikukuu ya Iddi Pili, baadaye mwezi huu.
“Tumeahirisha sherehe zetu kwa kuwa wachezaji wengi hawapo, pia viongozi wengi wapo katika mambo ya uchaguzi na hata waumini wa Dini ya Kiislam, wapo katika mfungo, hivyo tumesogeza mbele hadi Iddi Pili,” alisema Muro.
Wakati huohuo, Muro alisema katika kujiandaa na Kombe la Kagame, Yanga itacheza mechi za kirafiki dhidi ya KMKM Jumatano ijayo na Kombaini ya Jeshi la Polisi wikiendi ijayo.

Post a Comment