HALI TETE NDANI YA UKUMBI WA BUNGE JANA
Dodoma. Hali tete ndani ya ukumbi wa Bunge jana iliendelea
kutanda wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha kikao asubuhi
kutokana na kelele na baadaye chombo hicho kuwaadhibu wabunge saba wa
upinzani, wakiwamo watano waliozuiwa kuhudhuria hadi kumalizika kwa
Bunge la 10.
Hali hiyo ndani ya Bunge iliendelea kwa siku ya
pili mfululizo na mara zote kusababisha Spika kuahirisha vikao baada ya
shughuli za Bunge kushindwa kuendelea kutokana na kelele za wapinzani
wanaopinga kitendo cha uongozi kuwasilisha miswada mitatu kwa hati ya
dharura wakidai hakuna haja ya haraka hiyo.
Jana Spika Makinda, ambaye aliwahi kukumbana na
hali kama hiyo wakati wa mjadala wa sakata la Akaunti ya Escrow kwenye
Bunge la 18, aliibuka na dawa mpya na kuitumia Kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge kuwaadhibu wabunge hao saba.
John Mnyika, Moses Machali, Tundu Lissu, Felix
Mkosamali na Paulin Gekul, ambao wamekuwa wakipinga hoja mbalimbali za
Serikali ikiwa ni pamoja na miswada mitatu iliyotakiwa kuwasilishwa kwa
dharura kuanzia jana, wamefungiwa kushiriki vikao kuanzia leo hadi Bunge
litakapovunjwa Julai 9.
Wabunge wengine wawili, Mchungaji Peter Msigwa na
Rajab Mbarouk wamefungiwa kushiriki vikao viwili kuanzia leo baada ya
Kamati hiyo kuwatia hatiani wawakilishi hao wote saba kwa kudharau
mamlaka ya Spika.
Wengine watatu, Joseph Selasini, Khalifa Suleiman
Khalifa na Rajabu Abdalah wanatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo leo saa
4:00 baada ya wito wa kuwataka wahudhurie jana kuchelewa.
Kikao cha jioni cha Bunge hilo, ambacho kilipokea
taarifa ya kamati hiyo ya maadili na mapendekezo ya adhabu hizo,
kilichelewa kuanza kwa saa moja na dakika ishirini kusubiri kumalizika
kwa kazi ya kuwahoji watuhumiwa.
“Mashtaka yetu yaliendeshwa kwa haraka,
hatukupatiwa muda wa kutosha kujieleza wala kumtumia wakili,” alisema
Machali baada ya Bunge kuahirishwa.
“Pamoja na kuadhibiwa, hatutaogopa kusema kuwa
miswada hiyo ina matatizo ili Watanzania wafahamu na iwapo miswada hiyo
itapitishwa malalamiko ya vizazi vijavyo juu yatakayotokea kwenye sekta
ya gesi yatakuwa juu ya Serikali na CCM.”
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema
ni bora kufukuzwa kuliko kuendelea kushuhudia gesi ya Watanzania ikiuzwa
kwa nguvu bila ya huruma.
“Hii ni bora kuondolewa. Hukumu haikuwa ya haki na
tungeweza kukata kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni, lakini
mwenyekiti wake ni Spika hivyo basi tena, acheni wafanye wanachotaka
kukifanya,” alisema Lissu.
Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, alisema hata angefungiwa kushiriki vikao vyote, asingeathirika.
“Adhabu tuliyopewa leo inayonyesha kuwa hatuna Spika... Spika
yupo kiserikali zaidi hatendi mambo kwa haki. Akiamrishwa na Serikali
anafanya kama alivyoambiwa,” alisema Mchungaji Msigwa.
“Binafsi hainiathiri hata wangenizuia vikao vyote ningekuwa na furaha kwa sababu hatukuhojiwa,” alisema Msigwa.
Adhabu ya kutohudhuria vikao
Kwa kawaida vikao vya jioni vya Bunge huanza saa
10:00 jioni, lakini jana lilianza saa 11:20 jioni na wabunge walikuwa
wamejaa ukumbini tofauti na asubuhi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya maadili, Brigedia
Jenerali Hassan Ngwilizi alitoa hukumu hiyo baada ya kueleza kuwa
wabunge hao walikuwa wamevunja kanuni ya 74 (1) a,b ambayo inatoa zuio
kwa mbunge yeyote kusimama na kupiga kelele wakati Spika akiendesha
kikao.
Ngwilizi alisema kitendo cha wabunge hao kusimama
na kupiga kelele kiliathiri shughuli za Bunge, kitu ambacho ni kinyume
cha kanuni iwapo kitamlazimisha Spika kusitisha shughuli za chombo hicho
cha kutunga sheria.
Ngwilizi alisema kamati yake iliwahoji wabunge
saba walioitikia wito huo na baada ya majadiliano iliridhika kuwa
walifanya kosa hilo ambalo alisema halina tija.
Ngwili alipendekeza wabunge hao watano wazuiwe
kushiriki vikao vyote kuanzia leo na wengine wawili vikao viwili na
kupendekeza watatu waliosalia wafike mbele ya kamati leo kwa ajili ya
kuhojiwa, mapendekezo yaliyokubaliwa na Bunge na baadaye kujadiliwa kwa
kifupi kabla ya Spika kuahirisha kikao.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo,
Mchungaji Israel Natse alisema kuwa aliwaeleza wajumbe wenzake bayana
kuwa watuhumiwa walitakiwa kuruhusiwa kwenda mbele ya kamati wakiwa na
wanasheria wao au watu wengine wowote ambao wangewapendekeza, lakini
kikao kiligoma.
Alisema baada ya wenzake kugoma, aliweka bayana kuwa hawezi kushiriki kwenye uamuzi ambao unakiuka haki ya msingi ya mtuhumiwa.
Wakizungumza nje ya bunge mara baada ya kutoka
nje, Felix Mkosamali alisema kuwa hukumu hiyo ilitolewa kwa ubabe mkubwa
na hawakupewa nafasi ya kujitetea kwani ulitumika ubabe zaidi.
Rajabu Mbarouk ambaye alihukumiwa kutoshiriki siku mbili, alilia
na Spika akisema ndiyo chanzo cha vurugu hizo kwani alikuwa wa kwanza
kuvunja kanuni kwa kupeleka miswada kibabe.
Kwa upande wake Machali, alisema hukumu hiyo
ilikuwa ni ya kifisadi kwa kuwa mashtaka yao yaliendeshwa kwa haraka
bila ya kupatiwa muda wa kutosha kujieleza wala kumtumia wakili.
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alisema
bora ya kufukuzwa kuliko kuendelea kushuhudia gesi ya Watanzania ikiuzwa
kwa nguvu bila ya huruma.
“Hii ni bora kuondolewa, hukumu haikuwa ya haki na
tungeweza kukata kukata rufaa kwenye kamati ya Kanuni lakini Mwenyekiti
wake ni Spika hivyo basi tena, achene wafanye wanachotaka kukifanya,”
alisema Lissu.
Hukumu hiyo iliyotolewa jana haikujuisha jina la
mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde ambaye alitajwa asubuhi na
Spika kuwa mmoja wa watu waliotakiwa kufika mbele ya kamati.
Sakata la asubuhi
Mapema jana hali ilionekana kuwa ya kila upande
kuchukua tahadhari baada ya kikao cha juzi kulazimika kuahirishwa
kutokana na vurugu hizo. Baadaye wabunge walibaini kuwa miswada miswada
hiyo mitatu- Muswada wa Sheria ya Petroli, Muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na gesi na Muswada wa Sheria ya Uwazi na
Uwajibikaji katika Uchimbaji yote ya mwaka 2015- ilikuwa imeingizwa tena
kwenye shughuli za kazi. Kama ilivyokuwa juzi, jana mara baada ya
kipindi cha maswali na majibu kupita, wabunge walisimama wakitaka kuomba
mwongozo, lakini Spika alizuia kwani kulikuwa na kazi ya kupitisha
Muswada wa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa
mwaka 2015 ambao ulikuwa katika hatua ya kamati.
Hali ilibadilika ghafla baada ya kumalizika kwa
kazi ya kuupitisha muswada huo. Spika alimruhusu Waziri wa Nishati na
Madini, George Simbachawene kusoma Muswada wa Sheria ya Mafuta na
Petroli.
Waziri Simbachawene alipoanza kusoma, kelele za kuomba mwongozo zilianza.
Wakati huo, Lissu (CCM) na Khalifa Suleiman
Khalifa (Gando–Cuf) walikuwa wamesimama wakitaka mwongozo wa Spika
lakini hawakupewa nafasi ya kuzungumza.
Wakati Simbachawene akiendelea kusoma muswada huo
yalianza kusikika maneno kutoka kwa wabunge wa CCM wakisema “wamezoea
hao, usiwasikilize, achana nao”.
Kauli hizo ziliamsha hasira kwa wabunge wa upinzani ambao
walihamasishwa na kusimama wakitanguliwa na Felix Mkosamali na Ezekiel
Wenje ambao walianza kupiga kelele wakitaka wenzao wasimame.
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya wabunge
zaidi ya 40 kutoka upinzani kusimama wote na kuanza kupiga kelele na
kufanya maneno ya Waziri Simbachawene yasiweze kusikika kwa wabunge na
watu waliokuwa ndani ya ukumbi.
Hali hiyo ilimfanya Spika asimame na kumtaka
Waziri asiendelee kusoma Muswada na baadaye kutaja majina ya wabunge
kumi na moja ambao aliona walikuwa wanavunja sheria.
“Sasa wapiga kelele nawataja kwa majina, Tundu
Lisu (Singida Mashariki), Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Mnyika
(Ubungo), Paul Gekul (Viti Maalumu), na mbunge wa Rombo Joseph Selasini
wote kutoka Chadema.
Wengine ni Wabunge wa NCCR – Mageuzi Moses (Kasulu
Mjini) na Felix Mkosamali (Muhambwe) pamoja na wabunge wa Cuf Khalifa
Suleiman Khali (Gando), Rajab Ali Abdarah na Rajab Mbarouk (Ole),”
alisema Makinda.
Alisema wabunge hao wanatakiwa wafike mbele ya
Kamati ya Maadili na baadaye kutamka kuahirisha shughuli za Bunge huku
akiita kamati ya uongozi kukutana. Hiyo ilikuwa ni saa 5: 34 asubuhi.
Kilichotokea
Wakati Spika na makatibu wakitoka nje, wabunge wa
upinzani walipeana ishara za kutoka nje huku upinzani wakitaka waendelee
kuwa ndani ndipo zikaanza kelele kwa wabunge wa CCM kuanza kugonga meza
kwa kuimba “CCM, CCM,CCM”, huku wapinzani wakiimba “wezi M, wezi M,
wezi M”.
Wakiongozwa na Khalifa Suleiman Khalifa na Tundu
Lisu, wapinzani walikubaliana kwenda nje na kuanza kikao cha wazi ndani
ya ukumbi huku wabunge wa CCM na baadhi ya mawaziri wakiendelea
kusikiliza kila kilichokuwa kikifanyika.
Waziri wa Nchi, Sera Uratibu na Bunge, Jenister
Mhagama, aliwaita haraka wabunge wa CCM na kupaza sauti yake akisema:
“Msiwe wepesi wa kutoka, hii miswada ni lazima na lazima itapita hakuna
kuzubaa.”
Hata alipomaliza kuzungumza nao, wengi wa wabunge waliendelea kubaki ndani wakitaka kujua kinachofanywa na wenzao.
Katika kikao cha upinzani ambacho kilikuwa cha wazi,
walikubaliana kutorudi nyuma hata kama watafukuzwa wote ndani ya Bunge,
wakisema wanataka kurejesha heshima ya nchi.
“Hata kama itatokea sisi tulioitwa tukafukuzwa,
bado ninyi mtakaobaki ndani endeleeni kukomaa hadi mwisho. Msiogope
kufukuzwa na ikibidi hadi waweke mpira kwapani hawa,” alisema Lissu.
“Tukubaliane kuwa tutasimama pamoja na kukaa
pamoja, tutacheka pamoja na kulia pamoja. Naombeni msicheze mbali zaidi
ya kuwapa wenzetu nafasi ya kwenda kuswali,” alisema.
Lissu alisema kuwa uamuzi wa kuwafukuza
ulishafanywa tangu juzi na kwamba jana waliingia kwenye Bunge wakijua
nini kilikuwa kinaendelea na kuapa kuwa hawatashiriki dhambi kama
iliyofanywa mwaka 1997.
Nje ya ukumbi
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini John Mnyika
aliwaambia waandishi wa habari akisema: “Kinachofanywa na Serikali ni
kiini macho kwani hakuna makubaliano kwenye muswada huo.”
Mnyika alisema kuwa upinzani wanayo taarifa kuwa
kuna shinikizo kutoka mataifa ya nje wakitaka miswada hiyo isainiwe kuwa
sheria kabla Rais Jakaya Kikwete hajaondoka madarakani na akasema hali
ikizidi wataanika kila kitu hadharani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Richard
Ndasa alisema kuwa suala la muda wanalolilalamikia wapinzani halina
ukweli wowote. Ndasa alitolea mfano kuwa Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS) walishachambua na kutoa mapendekezo yao vizuri hivyo wapinzani
walikuwa na kazi ya kupinga kwa kuwa ziko dalili za mashinikizo kutoka
nje ya bunge.
Ulinzi wamarishwa
Tangu juzi ulinzi umekuwa ni mkali kwenye viwanja vya Bunge na polisi wa kawaida wameongezwa kwa kiasi kikubwa.
Taarifa zilizopatikana jana na kuthibitishwa na mmoja wa wabunge
wa CCM zinasema kuwa miswada huyo inawapa wakati mgumu kwani
wanalazimishwa kuipitisha.
Mmoja wa mawaziri ambaye alisema sio msemaji
aliliambia gazeti hili kuwa wameweka utaratibu maalumu wa kuhakikisha
wanashinda na tayari wameshawaita wabunge wao kote waliko ili waende
kuongeza nguvu.
CHANZO; MWANANCHI
CHANZO; MWANANCHI

Post a Comment