ad

ad

MPENZI WA KUPITIWA NA SHETANI KILA SIKU WA KAZI GANI?

Kila mmoja anafahamu umuhimu wa mapenzi katika maisha ya binadamu. Ndiyo maana kila siku watu wamekuwa wakihakikisha wanawapata wapenzi ambao watawaongezea furaha katika maisha yao.
Ambao wameyakosa mapenzi ya dhati wameathirika sana kisaikolojia na kushindwa kutimiza majukumu yao ya kila siku ipasavyo huku wengine wakifikia hatua ya kukatisha maisha yao kwa kujiua. Hiyo yote inaonesha ni jinsi gani mapenzi yana nafasi katika maisha yetu.
 

Kwa kuzingatia hilo nimeona nitumie safu hii kuwaelimisha na kuwakumbushia juu ya mambo mbalimbali ambayo kama ukiyazingatia yanaweza kuyafanya maisha yako ya kimapenzi yakawa bora. Kilio ambacho nimekuwa nikikipata kutoka kwa wasomaji wangu wengi ni kutokuwa na imani kama wale waliotokea kuwapenda nao wanawapenda kwa dhati pia.

Lakini mara nyingi jibu ambalo nimekuwa nikilitoa ni kwamba, unapoingia katika uhusiano na mtu ambaye umempenda kwa dhati ni vyema ukajijengea imani kwamba na yeye pia anakupenda licha ya kwamba hujaufungua moyo wake na kulithibitisha hilo.

Mpende, muamini na weka akilini mwako kwamba, kamwe  hawezi kukusaliti licha ya kwamba kinyume chake pia ni sawa. Nasema kinyume chake pia waweza kuwa sawa kwa sababu unaweza kumuamini mtu lakini kumbe ni mtu wa kupitiwa na shetani kila siku.

Hiyo itakusaidia kuendelea kuishi maisha ya furaha na amani. Lakini kama utatumia muda wako mwingi kuhoji kama kweli mpenzi wako anakupenda ama laa,utakuwa ukijiumiza tu na mwisho wa siku huwezi kupata jibu lililo sahihi.
 
Tutambue tu kwamba, katika maisha kuna kitu kuridhika. Unapokuwa na mtu ambaye anakupa kila aina ya furaha maishani mwako bila kuonesha tabia zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, mpende na muamini.

Hata kama kuna uwezekano wa yeye kuwa anaficha makucha yake  na kuyachomoa pale anapokuwa mbali na wewe, kwa sababu huna uhakika na hujawahi kumuona, muamini na acha maisha yaendelee.
  Nasema hivyo kwa sababu, tukianza kuchunguzana hakuna ambaye ni msafi kwa asilimia mia moja. Kila mtu anajiamini mwenyewe lakini huwezi kuiamini nafsi ya mwenzako kwa asilimia zote.
Ndiyo maana nikasema, unapoingia katika uhusiano na mtu ambaye umetokea kumpenda sana, ongea na moyo wako!
 
Mapenzi ya siku hizi usipoangalia yanaweza kukufanya ukawa mwendawazimu. Hii ndiyo inayosababisha baadhi ya watu kufikia hatua ya kusema kwamba, hawahitaji kuwa na wapenzi katika maisha yao.
Elewa kwamba, una haki ya kupenda na kupendwa, ukishampata yule  unayedhani atayafanya maisha yako kuwa ya furaha, mpende kwa dhati na muamini kwamba hawezi kukusaliti lakini usiache kuchunguza nyendo zake, ukibaini kuwa ni mtu wa kupitiwa na shetani kila siku, huyo hana nafasi kwenye maisha yako.
Powered by Blogger.