Hali mbaya, Ngoma aomba ulinzi Cecafa,TFF
Dar es Salaam
KUTOKANA na kuchezewa kwa kupaniwa akiwa uwanjani, mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kumuwekea ulinzi.
KUTOKANA na kuchezewa kwa kupaniwa akiwa uwanjani, mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma, ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kumuwekea ulinzi.
Hiyo ni siku chache baada ya mshambuliaji huyo kupewa kadi nyekundu kwenye mechi ya Kombe la Kagame dhidi ya Gor Mahia ambapo alitolewa nje baada ya kurudisha rafu aliyochezewa kwa kumsukuma mlinzi wa timu hiyo pinzani.
Mshambuliaji huyo, amerejea uwanjani kwenye mechi dhidi ya KMKM akimalizia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa huku akitengeneza nafasi mbili za mabao.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ngoma alisema kuwa, ni vyema TFF kama wenyeji wa michuano hiyo na waandaaji Cecafa kuzungumza na waamuzi ili wachezeshe kwa haki kutokana na wachezaji wa timu pinzani kumchezea rafu za makusudi wakiamini atarudishia kama ilivyotokea katika mechi dhidi ya Gor Mahia.
Ngoma alisema, tayari ameshajua aina ya soka la Tanzania na Afrika kwa jumla ambalo wanatumia nguvu nyingi ili kumtoa mchezoni kwa kumchezea rafu za makusudi.
Aliongeza kuwa, anawahakikishia Wanayanga wote kutorudia makosa aliyoyafanya kwenye mechi dhidi ya Gor Mahia, badala yake atapunguza hasira na atacheza soka pekee.
“Ile kadi nyekundu niliyopewa dhidi ya Gor Mahia, imenifanya nipate uzoefu wa soka la hapa nchini na Afrika kwa jumla, kiukweli kabisa nikuhakikishie tu lile kosa halitajirudia tena.
“Ile mechi mimi ndiye niliyesababisha timu ikose ushindi dhidi ya Gor Mahia, lakini nikwambie kitu, TFF na Cecafa wanatakiwa kuongea na waamuzi wao kuwa watumie kanuni 17 za ndani ya uwanja ili kutulinda sisi washambuliaji tunaochezewa kwa kupaniwa,” alisema Ngoma.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, alithibitisha kukaa na mchezaji huyo mara baada ya kupewa kadi nyekundu wakimtaka kutotumia hasira akiwa ndani ya uwanja.
“Ujue Ngoma hakuwa analijua soka la Tanzania na Afrika Mashariki, lakini mara baada ya Gor Mahia tulikaa naye mimi na Pluijm (Hans) na kuzungumza naye tukimtaka kupunguza hasira. Wachezaji wa huku wanakuondoa mchezoni kwa makusudi ili upate kadi nyekundu,” alisema Mkwasa.
CREDIT:CHAMPIONI

Post a Comment