PETER CECH ATUA ARSENAL RASMI
Arsenal
imekamilisha usajili wa golikipa wa Chelsea Peter Cech na anatarajiwa
kukipiga na klabu yake ya zamani akiwa ametinga uzi wa Emirates kwenye
mchezo wa ngao ya jamii utakaopigwa Agosti 2 mwaka huu kwenye uwanja wa
Wimbley
Cech amesajiliwa kwa dau la pauni
milioni 11 baada ya majadiliano marefu kati ya Arsenal na Chelsea juu
ya kumsajili Cech yalioanza tangu msimu ulipomalizika na hatimaye
wakafikia makubaliano na kipa huyo mwenye umri wa miaka 33 akasaini
mkataba wa kuitumikia klabu ya Arsenal ukiwa ni usajili wa kwanza
kufanywa na kocha wa Arsenal, Arsene Wenger.
Jose Mourinho alikuwa hataki
kumuuza Cech kwenda kwa wapinzani wake wa jiji moja la London (Arsenal)
japokuwa taarifa hizo hazikuwa na uhakika wowote.
Awali Paris Saint-Germain
iliipelekea ofa Chelsea kwa ajili ya kumsajili mkongwe huyo wa kimataifa
kutoka Jamhuri ya Czech, lakini Cech alisema yeye anapenda zaidi
kuendelea kukipiga kwenye vilabu vya jijini London ambapo ndipo ilipo
familia yake.
Kutua kwa Cech kwenye kikosi cha
Arsenal kunafungua mlango wa kutokea kwa moja ya golikipa wa kikosi
hicho kati ya Wojciech Szczesny au David Ospina ambaye amekuwa
akifukuziwa na klabu ya Fenerbahce na yeye amekuwa akitaka kukikacha
kikosi hicho cha washika bunduki akikataa kuanzia benchi.
Kuondoka kwa Cech kwenye kikosi
cha Chelsea, hiyo inamaanisha pia kocha wa magolikipa Christopher
Lollichon ataambatana nae kuelekea Arsenal.
Nahodha wa Chelsea John Terry
amewaambia mashabiki wa Arsenal kuwa, Cech pekee ataisaidia timu yao
kuvuna pointi 12 hadi 15 ndani ya msimu mmoja.
Cech amekipiga Stamford Bridge
kwa muda wa miaka 11, Terry ameuambia mtandao mmoja wa michezo (Talk
SPORT) kuwa, sasa Arsenal wanaweza wakawania ubingwa na siyo nafasi ya
pili kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa muda mrefu.

Post a Comment