ad

ad

UTAMJUAJE MCHUMBA WAKO KAMA ANA MAPENZI YA DHATI?

WAPENZI wasomaji wa safu hii bila shaka mko poa na mnaendelea na shughuli za kila siku. Kama kawaida ni Jumamosi nyingine tunakutana katika safu hii kuweza kupeana mambo mbalimbali yahusuyo maisha ya uhusiano.

Bila kupoteza muda, mada iliyopo hapo juu inajieleza. Ni wengi sana wameumia kwa kumpenda mtu asiyekuwa na penzi la dhati. Raha ya mapenzi, wapendanao mpendane, mheshimiane na kweli muoneshe kutoka moyoni kwamba mna mapenzi ya dhati.
Tofauti na hapo, mmoja wenu anapokosa penzi la dhati, upande wa pili hugeuka kuwa maumivu. Anampenda mtu pasipo kujua kwamba mwenzake ni ‘msanii’, penzi lake ni la wiziwizi tu.Mbaya zaidi, anaishi na mwenzake kwa muda mrefu akiamini kwamba yupo kwenye mikono salama mwisho wa siku anaambulia maumivu, anakuja kuachwa solemba kwani mwenzake hakuwa na penzi la dhati, hakuwahi kuheshimu hisia za mwenzake hata siku moja.
Mtu mwenye penzi la wizi huwa haumizwi hata kidogo na maumivu ya mtu mwenye penzi la dhati. Hatajali hata kidogo hisia zako, atakachokuwa anakiangalia kwa upande wake ni kukutumia kadiri ambavyo yeye anaona inafaa.
Anaweza kukutumia kwa maana ya kuhitaji tendo la ngono kama si kukutumia kwa kuhitaji fedha zako na pengine hahitaji kitu chochote lakini basi tu anaamua kuwa na wewe ‘kukuibia’ hisia zako.
Ili uweze kujua mpenzi wako ana mapenzi ya dhati au la ni vyema tukajifunza viashiria vifuatavyo ambavyo ukiona mwenzi wako anavifanya basi ujue ana mapenzi ya dhati na akiwa havifanyi basi ujue hana mapenzi ya dhati na wewe uweze kuchukua hatua stahiki.
1.MKWELI
Hakuna kitu kizuri kwenye uhusiano kama kuelezana ukweli. Mnapoelezana ukweli hamuwezi kutetereka. Ukiona mpenzi wako anakudanganyadanganya kila wakati ujue huyo hawezi kuwa na mapenzi ya dhati.
Mwenye penzi la dhati siku zote anamueleza mpenzi wake ukweli juu ya penzi lake, anamueleza ukweli kwamba anampenda mwenzake na hata siku moja hawezi kuongopa juu ya jambo lolote linalohusu penzi lao.

2. KUKUSHIRIKISHA
Mpenzi yeyote ambaye ana mapenzi ya dhati huwa anamshirikisha mwenzake kwa kila jambo. Anamueleza mwenzake hata kama jambo ambalo wakati mwingine si la muhimu sana lakini anaona ni vyema kumshirikisha mwenzake ili aweze tu kulijua.
Anamshirikisha mwenzake katika mipango ya maendeleo, anamshirikisha katika kujadili mustakabali wa penzi lao. Wanajadili kwa pamoja kwamba wafanye nini ili kuweza kufikia hatua nzuri ya penzi lao. Ili kufika huko, wanatakiwa wafanye nini ili penzi lao lizidi kustawi na kufikia hatua nzuri ya kuoana na baadaye familia.
Ukiona mtu anajiamulia mambo yake, anakuwa msiri na mambo ya kifamilia, hamjadili mipango ya penzi lenu basi ujue wazi hapo kuna walakini.
3. KUJALI
Ili uweze kumjua kwamba mwenza wako ana penzi la dhati pia unapaswa kuwa na mwenza ambaye anakujali. Lazima aoneshe kukujali kwa shida na raha. Akujali katika uzima na ugonjwa.Siyo akufurahie wakati wa uzima halafu pale unapomwambia unaumwa, anaingia mitini na kujifanya kama hakujui. Lazima akujali kwa uzima na ugonjwa, akiingia mitini wakati ugonjwa basi lazima uwe na shaka naye.
Tena kama umeshamueleza au ameshapata taarifa lakini ukaona bado haoneshi kujali hata kwa kukuuliza kwamba unaendeleaje basi hakika huyo hawezi kuwa na penzi la dhati.Mtu ambaye anataka kukuona ukiwa mzima tu, mara nyingi anakuwa na mipango yake moyoni. Wewe anakufanya kama chombo cha starehe tu.
Itaendelea wiki ijayo!

No comments

Powered by Blogger.