ad

ad

LOWASSA AOGOPA KUZUNGUMZA KATIKA BONANZA

 Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa akiwa katika maandamano ya kupinga mauaji ya Maalbino yaliyofanyika kwenye Viwanja vya TCC Chang'ombe, Temeke

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ameogopa kuzungumza katika bonaza lenye ujumbe wa “Tunalaani na Kupinga Mauaji ya albino”.
Hofu ya lowassa kuzungumza katika bonaza hilo, inaelezwa kuwa ni matokeo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumuonya kuacha kutumia makundi mbalimbali ya kijamii kwa kile kinachoitwa “kusaka urais”.
Bonaza hilo limeandaliwa na Temeke Family Joggig Club na kufanyika leo katika viwanya vya TCC Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Lowassa – Waziri Mkuu aliyejiuzuru kwa kashfa ya ufisadi wa Richmond na Mbunge wa jimbo la Monduli, Arusha ndiye alikuwa mgeni rasmi katika bonaza hilo.
Akizungumza baada ya kutakiwa kufanya hivyo na waandaaji wa bonaza hilo Lowassa amesema: “Haya mauaji ya Albino yanatufanya tuonekane ni majambazi. Yanatuharibia sana sifa. Albino 76 waliouwawa si wachache. Ni maisha ya binadamu.”
Lowassa amesema: “Naiomba serikali kuunda kamati ili tuchukue hatua kama nchi. Nawashukuru kwa kunialika. Ili nisipate ugomvi na CCM kwamba, nautumia ukumbi huu kwa mambo yangu ya siasa namwachia Abbas Mtevu (Mbunge wa jimbo la Temeke) yeye atazungumza,” amesema Lowassa.
Ernest Kimaya – Mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania, amesema Mauaji ya watu wenye ualbino yaliongezeka kwa kasi nchini kuanzia mwaka 2006.
“Hadi sasa hivi wameuawa watu wenye ualbino 75, waliojeruhiwa kwa kukatwa viungo ni 35. Tunasikitika kukueleza kuwa makaburi 15 yamefukuliwa ili kuchukua viungo vya ndugu zetu marehemu,” amesema Kimaya.
Kimaya amesema changamoto zilizopo ni kwamba watu wenye ualbino wana matatizo ya kupata kansa ya ngozi na uoni hafifu.
Aidha Kimaya amesema: “Hili la mauaji ya Albino yanafanya Chama cha Albino kuwa na mzigo mkubwa wa kuelimisha jamii na kutatua matatizo yanayowapata huku kukiwa na uhaba wa rasilimali fedha”.
“Suluhisho la kumaliza tatizo hili ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii, ione Albino ni sehemu ya jamii yao, kuwashirikisha katika masuala ya ujenzi wa taifa letu na vyombo vya usalama kujipanga sawasawa na kukabiliana na wale wanaoleta madhara haya,” amefafanua Kimaya.
Salim Ahmed Salim – Msemaji msaidizi wa klabu hiyo amesema dhumuni la bonaza hilo ni kulaani na kupinga mauaji na ukataji wa viungo vya albino. Lengo lingine ni kuwaambia umma kwamba Albino ni binadamu kama binadamu wengine. Wanastahili upendo furaha na kuishi bila ya kupata huzuni na hofu katika mioyo yao.
“Tunakusudua kufika katika mikoa iliyokithiri kwa mauaji ya albino kama vile Mwanza , Shinyanga na Tabora ili kutoa elimu na kuhamasishja wananchi kushiriki kuwalinda watu wenye ualbino pili ni kutaka serikalia na vyombo vya usalama wa raia kuwa na mkakati madhubuti wa kuwalinda albino,” amesisitiza Salim.
Lowassa ameungana na wanachama wa klabu hiyo kutembea umbali wa kilometa 5 kwa Mwendo wa dakika 25 katika maeneo ya barabara ya Taifa, barabara ya Mandela, barabara ya Temeke, barabara ya Chang’ombe na kuishia katika viwanja vya TCC Chang’ombe.
CHANZO: MWANAHALISI ONLINE

No comments

Powered by Blogger.