ad

ad

Yanga yaipa masharti 5 TFF



Wachezaji wa Yanga.
Nicodemus Jonas,
Dar es SalaamKAMA ulidhani walikuwa wanatania, ndiyo ufahamu kuwa jamaa walikuwa ‘serious’! Siku chache baada ya uongozi wa Yanga kuhoji kuhusu kanuni iliyompitisha straika wa Simba, Ibrahim Ajibu kucheza kwenye mchezo wa Prisons wakati akiwa ana kadi tatu za njano, uongozi huo umekwenda mbali na kuilima Shirikisho la Soka nchini (TFF) barua ya masharti matano kuhusu maamuzi hayo.

Sokomoko hilo limekuja baada ya TFF kuipa mamlaka Simba kumtumia Ajibu katika mechi na Prisons iliyopigwa wiki iliyopita huku pia ikimruhusu kucheza katika mchezo na Yanga hapo kesho wakati alitakiwa kutumikia adhabu kutokana na kuwa na kadi tatu za njano, lakini TFF kupitia kwa katibu na watendaji mbalimbali wamekuwa wakisisitiza kuwa kanuni zao zimefanyiwa marekebisho tangu Februari, mwaka huu.
Hata hivyo, Yanga pamoja na klabu za Azam, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Kagera Sugar na Coastal Union zimepinga kuwepo kwa mabadiliko hayo kwani hakuna taarifa rasmi iliyotumwa kwa klabu husika, zaidi ya Simba tu.

Akizungumza Katibu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, amefunguka kuwa katiba barua hiyo kwenda TFF, wameambatanisha masharti matano na mojawapo likiitaka TFF, Simba kukatwa pointi sita na kupigwa adhabu kali kama fundisho.
“Hakuna taarifa zozote kuhusu kanuni kubadilishwa, iweje zianze kutumika ilhali hazijawafikia walengwa? Soka letu limekuwa likiendeshwa kienyeji zaidi lakini katika hili lazima tusimame kidete kutetea haki yetu.

“Bado tunajiuliza hayo mabadiliko yalifanywa lini na kwa sababu ipi ya msingi? Tumeamua kuwaandikia barua TFF na ninaipeleka leo (jana) na tunawapa maazimio yenye masharti matano kuhusu msimamo wetu. Mojawapo ni watendaji wa Bodi ya Ligi kujiengua kwa kushindwa utendaji, pili, Klabu ya Simba ipokwe pointi sita, maana kabla ya Ajibu walikuwa wamemtumia Banda (Abdi) kwenye mchezo na Coastal kimakosa, maana hakuna aliyejua kama kulikuwa kuna marekebisho ya kikanuni,” alisema Dk Tiboroha na kufunguka msimamo wao kwa Ajibu kucheza mchezo wa kesho.

“Sisi hatuna shida na mchezaji, wao wakitaka wamtumie maana watakuwa wanaturundikia pointi. Acheze tu, tutajua mbele kwa mbele.”Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba ambaye aliwahi kufanya kazi TFF, alikwenda mbali na kufafanua sheria kuhusu mabadiliko.
“Popote pale hakuna ligi inayoweza kufanya marekebisho ya kanuni katikati ya ligi. Kila kitu hufanywa kabla ya ligi kuanza na hiyo ndiyo huwa ni ‘platform’ ya ligi inayofuata. Sasa katika hili la Simba na TFF sijawahi kusikia popote. Hata sisi hatuna taarifa rasmi.”
Simba pekee ndiyo ina taarifa za kuwepo kwa marekebisho ya kanuni huku baadhi ya viongozi wakikaririwa wakisema ni kutokana na makamu wa rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kuwa mmoja wa watendaji wa TFF, jambo ambalo limepingwa vikali.
Kanuni inayofahamika mpaka sasa kwa klabu 13 achilia mbali Simba ni ile ya No 37 inayomtaka mchezaji kukosa mchezo mmoja baada ya kuonywa kwa kadi ya njano kwenye michezo mitatu mfululizo.

No comments

Powered by Blogger.