Pluijm: Nimenasa siri zote za Platinum
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.
Nicodemus Jonas na Hans Mloli
YANGA kesho Jumapili inacheza na FC Platinum ya Zimbabwe mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, amesema amenasa mbinu zote za wapinzani wao na ni lazima wawafunge.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, kikosi chake jana Ijumaa asubuhi kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume na baada ya mazoezi hayo, akatamka: “Nashukuru kikosi changu kipo vizuri, nawajua wapinzani wangu, najua uzuri na ubaya wao, hivyo najipanga kushinda mechi hii.”
Pluijm anayesifika kwa kujua soka la Afrika na namna ya kukabiliana nalo, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, amebahatika kupata video ya mechi moja ya FC Platinum na Sofapaka na ameshajua ubora na udhaifu wao.
FC Platinum imepata nafasi ya kucheza na Yanga baada ya kuitoa Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-2, kwani ilishinda mabao 2-1 katika michezo yote.“Nimetazama vizuri mechi yao moja na Sofapaka, wapinzani wetu wana kasi sana uwanjani na wanatumia nguvu, hivyo nimewaandaa wachezaji wangu kukabiliana nao na kwa mazoezi tuliyofanya, hakika tutafanya vizuri kama tukicheza kama timu,” alisema Pluijm.
Hata hivyo, Pluijm alisema hataidharau FC Platinum hata kidogo katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa kwani ni wazuri sana kwenye kucheza kitimu (team work). “Wana wachezaji wengi wanaocheza kama timu na huwezi kusema utamzuia mmoja, wote wanajua wanachofanya, kazi ya wachezaji wangu ni kucheza kwa kufuata maelekezo tu,” alisema Pluijm.
Yanga inacheza mechi hii baada ya kuitoa BDF XI ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2, kwani awali ilishinda mabao 2-0 jijini Dar es Salaam lakini ikafungwa ugenini mabao 2-1.
Wakati huohuo, kikosi cha FC Platinum iliyoanzishwa mwaka 1995, kilitarajiwa kuwasili jana usiku kutoka Zimbabwe. Usiku huo pia waamuzi wa mchezo huo wanaoongozwa na Djamal Aden Abdi wa Djibouti ambaye ndiye mwamuzi wa kati, walitarajiwa kuwasili.
CHANZO: CHAMPIONI
Post a Comment