NGASSA APIGA BAO MBILI, AGOMA KUSHANGILIA JANA TAIFA
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa.
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, jana alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 5-1 ambao timu yake iliupata kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku akitoa sababu za kutoshangilia hata moja.
Licha ya kutoshangilia, Ngassa alikuwa akionyesha ishara ya kama analia, baada ya kufunga kila bao.
Yanga ilifanikiwa kupata ushindi huo ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa raundi ya kwanza. Mabao hayo yamemfanya Ngassa kufikisha mabao matatu kwenye michuano hiyo.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, mshambuliaji huyo ambaye hivi karibuni alikuwa hana uhusiano mzuri na uongozi wa Yanga, alisema hakushangilia kwa kuwa kuna msiba wa kocha Sylvestre Marsh.
“Aaah! Kweli ingekuwa ngumu kwangu kushangilia kwa kuwa kila mmoja anajua kuwa kuna msiba wa kocha Sylvestre Marsh, aliyefariki juzi, alikuwa kocha wangu, amenifundisha kwa kipindi kirefu sana, nisingeweza kushangilia,” alisema Ngassa.
Marsh ambaye alishawahi kumfundisha Ngassa alifariki juzi kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kansa ya koo kwa muda mrefu.
Post a Comment