KOPUNOVIC ATANGAZA VITA MPYA YA DAKIKA 810 SIMBA
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic.
WIKI moja baada ya kuifunga Yanga bao 1-0, Kocha wa Simba, Goran Kopunovic, ameonyesha sasa anachofanya ni kazi tu, ambapo amesema kuwa mambo ya Yanga yamepita na anachohitaji ni ushindi tu katika mechi tisa zilizosalia katika Ligi Kuu Bara, msimu huu.
Kocha huyo raia wa Serbia amesisitiza kuwa ushindi kwake ni muhimu na anachotaka katika mechi hizo ambazo ni sawa na dakika 810 ni ushindi na baada ya hapo anaamini ndiyo atakuwa na nguvu ya kufikiria ubingwa.
Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 31 na Azam waliopo nafasi ya pili wakiwa na 30.
Kopunovic ameliambia gazeti hili kuwa, ushindi wa Yanga kwao ni kama changamoto ya kuendeleza hicho alichokipanga cha ushindi mpaka mwisho, ndiyo maana hakuwa na haja ya kushangilia kwa muda mrefu.
“Siwezi kusema kwamba hatuutaki ubingwa, hilo ndiyo lengo letu lakini bado tuna mtihani mkubwa wa kushinda kwenye mechi nyingine tisa zaidi zilizopo mbele yetu, zote ni muhimu
na zinahitajika juhudi na kujituma kuweza kuyafikia haya tunayoyataka.
“Mechi ya Yanga ilikuwa ni moja ya mitihani migumu lakini tumeupita na sasa kuna mwingine, nashukuru wachezaji wamekuwa wakijitahidi na kujituma sana katika mechi zetu, naamini tukiendelea hivi tunaweza kuwa mbali sana ligi itakapoisha.
“Kutwaa ubingwa inawezekana lakini bado si rahisi kama mtu anavyoweza kudhani, bado tunahitaji juhudi na kujiamini zaidi, kilichobaki ni kuangalia zaidi kilichopo mbele yetu,” alisema Kopunovic.
Mechi hizo zilizosalia ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Mgambo JKT, Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Mgambo JKT tena, Mbeya City, Ndanda FC, Azam FC, halafu mwisho watamalizana na JKT Ruvu.
Wakati kocha huyo akitamka hivyo, kiungo wake mshambuliaji, Emmanuel Okwi, amedai kuwa timu yake ipo fiti na ana imani itashinda mechi ya Mtibwa ambayo itapigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.
“Yaliyopita yamepita, kwa sasa ninaelekeza nguvu zangu zote katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kuona ni jinsi gani tutafanikiwa kushinda na kuendelea kusonga mbele zaidi katika msimamo wa ligi kwani ligi bado ngumu,” alisema Okwi.
Post a Comment