ad

ad

DIDIER KAVUMBAGU WA AZAM FC, NARUDI YANGA

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Didier Kavumbagu, raia wa Burundi, ametamka wazi kuwa mkataba wake na klabu hiyo umebakiza miezi miwili na kufunguka kuwa yupo tayari kurejea Yanga ili akaifunge Simba ambayo imekuwa ikiwasumbua Wanajangwani hao kwa muda mrefu.
 

Wakati Kavumbagu akitamka hayo, siri ya mshambuliaji wa Yanga, Kpah Sherman raia wa Liberia kutofunga mabao imefichuliwa na mchezaji ambaye walicheza naye pamoja nchini Norway.

Kuhusu Kavumbagu ambaye amefunga mabao tisa katika Ligi Kuu Bara msimu huu, aliitoa kauli hiyo baada ya timu yake hiyo ya zamani kufungwa bao 1-0 na Simba, jambo ambalo anaamini inawezekana kukwepeka hasa kama yeye akiwepo katika kikosi hicho.
Kwa mujibu wa kanuni za soka, Mrundi huyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine yoyote.
 
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kavumbagu alisema kuwa anaamini uwepo wake katika kikosi cha Yanga kinachonolewa na Hans van Der Pluijm utachangia kwa kiasi kikubwa kuwafunga Simba.

“Mimi sina tatizo na Yanga wala kocha wao, niliondoka kwa amani, sikugombana na yeyote iwe shabiki au mchezaji, lakini kwa sasa akili yangu ipo Azam na ninaipa nafasi pia timu yangu kufanya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.

“Kiukweli kabisa mimi nipo tayari kurudi kuichezea Yanga katika msimu ujao wa ligi kwa ajili ya kuiongezea nguvu safu yao ya ushambuliaji, nitafanya hivyo endapo tu tutakubaliana maslahi na mahitaji yangu mengine.

“Kabla ya kufanya hivyo, jambo la kwanza ninatoa nafasi kwa Azam kuzungumza na mimi juu ya mkataba mpya lakini mbali na hapo nipo tayari kwenda kwingine kokote endapo tu tutakubaliana mahitaji yangu ikiwemo kuboreshewa dau la usajili na mshahara wangu wa mwezi,” alisema Kavumbagu.
Yanga imekuwa na wakati mgumu kila inapokutana na Simba katika miaka ya hivi karibuni, huku safu yake ya ushambuliaji ikionekana kuwa na ukakasi katika kucheka na nyavu msimu huu.

Washambuliaji wa timu hiyo hawajafunga mabao ya kutosha. Amissi Tambwe amefunga mabao mawili kwenye ligi tangu atue klabuni hapo, Danny Mrwanda yeye amefunga moja, Jerry Tegete mabao mawili, Mrisho Ngassa (2), Kpah Sherman na Juma Javu hawana mabao, anayeongoza ni kiungo mshambuliaji Simon Msuva ambaye amefunga mabao saba.

Kuhusu Sherman ni kuwa, kiungo wa Mtibwa Sugar, Henry Joseph ambaye aliwahi kucheza soka na Sherman raia wa Liberia, amefunguka juu ya tatizo la ufungaji la mchezaji huyo ambalo ndilo linalomkumba kwa sasa.

Henry ambaye alicheza na Sherman nchini Norway katika kikosi cha Kongsvinger, amesema kuwa tatizo hilo halijaanza leo wala jana bali ni muda mrefu amekuwa hana ujanja katika kufunga licha ya kuwa ni mzuri katika kuichezesha timu.

“Muda mwingine tuwe wakweli tu, Sherman tangu anakuja kufanya majaribio Kongsvinger B alikuwa anaweza kufanya vitu vingi vizuri lakini kwenye kufunga ndiyo alikuwa na tatizo, kwa hiyo si kwamba ana gundu au labda kuwe na imani za tofauti juu ya jezi anayovaa, ila kwake naona ndiyo imekuwa hivyo.

“Jambo la msingi kocha wa Yanga ajue jinsi ya kumtumia lakini suala la kufunga jamaa ana matatizo sana hapo, hata kule muda mwingine alikuwa anakuja timu ya wakubwa kufanya mazoezi, alitumika kama mtu wa kuwapa wenzake pasi za mwisho,” alisema Henry.
Waandishi: Wilbert Molandi na Saphyna Mlawa & Hans Mloli

CHANZO: GAZETI LA CHAMPIONI IJUMAA

No comments

Powered by Blogger.