Kitanzi, Kisu au Bastola - 8

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Alishinda akimuangalia Salima alivyokuwa akioga na kuvaa nguo zake na hata pale alipokuwa akitembea ndani ya korido za jengo hilo. Nafsi yake ilianza kujaa tamaa ya kufanya mapenzi na msichana huyo.
SONGA NAYO...
Salima kwa upande wake aliamka asubuhi na mapema akiwa na nia ya kumuuliza Madam Flaviana kama mpenzi wake, Dedan alikuwa amepatikana. Akatembea akikatiza korido kadhaa akikielekea chumba ambacho alielekezwa tangu jana yake kuwa ni cha Madam.
Kama vile Madam Flaviana na Salima walikuwa na fikra sawa, kabla hata Salima hajabisha hodi kwenye mlango wa chumba hicho, Madam Flaviana naye alikuwa akitoka mlangoni. Wote wakakutana kwenye korido.
“Waoh! Salima, umeamkaje leo? Nifuate tukapate kifungua kinywa,” alisema Madam Flaviana kwa mshtuko kwani hakutegemea kama Salima angekuwa hapo mlangoni kwa wakati huo.
“Madam, polisi wamepata taarifa zozote kuhusu Dedan?” Salima alimuuliza Madam Flaviana bila kupepesa macho yake.
“Hapana mpaka sasa bado hatujasikia lolote, lakini polisi walikuwa wakihitaji picha zake ili wamtafute kiurahisi, si unazo?”
“Ndiyo ninazo ngoja nikuletee,” alisema Salima na kukimbilia chumbani kwake mara moja ambapo alirudi na picha kibao za Dedan na kumkabidhi Madam Flaviana achague ipi moja wapo iliyokuwa ikionekana vizuri ili aipeleke haraka polisi wakamtafutie mpenzi wake.
Mara baada ya Madam Flaviana kuzipata picha hizo alifurahi kimoyomoyo akijua kuwa kama Dedan ndiye yule mtu aliyekamatwa na kikosi kazi kilichoongozwa na Side jana yake, basi huo ndiyo ulikuwa mwisho wake. Akamsikitikia Salima kwa kutokujua dhumuni lake kisha akainua simu na kumpigia Side akimtaka aonane naye mara moja ili amuoneshe picha hizo kama zilikuwa zikifanana na huyo mtu waliye naye huku Salima akizugwa kuwa Madam alikuwa akiongea na ofisa fulani wa polisi.
Baada ya kunywa chai, Madam Flaviana alimpeleka Salima kwenye jukwaa kubwa na kumfundisha jinsi ya kutembea kama mamiss ‘catwalk.’ Akamfundisha pia na maneno machache ya kumkarimu mtu kwa lugha ya Kiarabu bila Salima mwenyewe kujua kusudi la somo hilo kuwa ni kumuandaa kwa ujio wa Prince Khalfan, mgeni kutoka Falme za Kiarabu.
Kwa kuwa Salima alionekana na mawazo mengi kuhusu Dedan, Madam Flaviana aliona ni vyema amshawishi Salima kunywa pombe ili angalau apoteze mawazo. Madam Flaviana akajifanya kama vile alikuwa akimfundisha Salima majina mbalimbali ya vinywaji vikali na ladha yake, ambapo ilibidi Salima aonje na kutambua ladha ya kila pombe aliyopewa, somo ambalo Salima alivutiwa nalo na kujikuta siyo tu akionja, bali akinywa pombe hizo kwa kiwango kikubwa hadi akapoteza fahamu.
Haraka wasichana waliokuwa wakihudumia mahali hapo wakambeba Salima na kumpeleka chumbani kwake kisha wakarudi na kuendelea na shughuli zao. Madam Flaviana akautumia muda huo kukutana na Side ili amuoneshe picha za Dedan alizozipata kutoka kwa Salima.
***
“Vipi mume wangu mbona haupo sawa leo?” aliongea Sonia akimtazama mumewe Side ambaye tangu alipopokea simu ya Madam Flaviana aliyemtaarifu kuwa picha za Dedan zilikuwa zimepatikana alikuwa na wasiwasi mkubwa huku mikono yake ikitetemeka.
Side alikuwa akiomba kimoyomoyo huyo kijana waliyemteka na kumhifadhi kwenye godauni la kiwanda cha vyuma ‘BIASI,’ asiwe Dedan kweli, kwani kwa vyovyote kama ni yeye basi kifo chake kilikuwa kikimkaribia. Akajikaza na kuvaa shati lake ambapo alikosea kufunga baadhi ya vifungo kwa uoga na wasiwasi.
“Niambie ni nani sasa waliyekutuma ukamuue?” Sonia alizidi kumtwanga maswali Side, utadhani alikuwa akimfahamu vyema Side kiasi cha kutambua hata baadhi ya siri zake za kazi.
“Nitakwambia nikirudi,” Side aliondoka na kufunga mlango kwa nguvu huku Sonia akibaki njia panda asijue ni kipi kilichokuwa kikimsumbua mumewe japo kuwa alipatwa na hisia kuwa lazima damu itamwagika mahali fulani.
***
Sonia alikumbuka vyema siku ambayo alimuona Side akitetemeka kwa hofu ya kuua kama alivyomuona siku hiyo. Alikumbuka ambavyo alitamani kuifutilia mbali tarehe na mwezi ule ili isahaulike kabisa kutoka kwenye kalenda.
Siku hiyo yeye Sonia, alikuwa ndiye mtu aliyetakiwa kuuawa na Mr. John Chakos.
Itaendelea wiki ijayo.
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Sonia alikumbuka vyema siku ambayo alimuona Side akitetemeka kwa hofu ya kuua kama alivyomuona siku hiyo. Alikumbuka ambavyo alitamani kuifutilia mbali tarehe na mwezi ule ili isahaulike kabisa kutoka kwenye kalenda. Siku hiyo yeye Sonia, alikuwa ndiye mtu aliyetakiwa kuuawa na Mr. John Chakos.
ENDELEA...
Side aliyeiseti vyema bunduki yake katikati ya paji la uso wa Sonia, hakuweza kufanya chochote zaidi ya kumtazama kwa huruma.
Sonia alikumbuka kuwa katika saa hizo zilizokosa nuru, ndipo alipomuona Side akiwa katika hali kama hiyo aliyomuona nayo muda mfupi uliopita.
Ni wazi Side alikuwa akitetemeka kwa hofu ya kutekeleza kile alichotumwa na bosi wake. Hatimaye Side aliishusha silaha yake na kumtorosha Sonia kwa siri akimficha hapo katika Kijiji cha Ulongoni, nje kidogo ya mji na kuanza maisha mapya.
Kwa msaada wa Side, Sonia alikuwa hai mpaka siku hiyo, hivyo Sonia hakusita kulipa fadhila kwa kukubali kuishi na mwanaume huyo kwa kuwa ni siku nyingi alikuwa akimuonesha wazi kuwa alikuwa akimpenda, lakini hakuweza kumwambia kutokana na hali ya maisha ilivyo ndani ya jumba la ‘Serenity.’
Kanuni zilijieleza wazi; Sonia alipaswa kuwa malaya wa kimataifa na Side alikuwa kibaraka wa kuhakikisha hayo yalifanyika bila kuuliza swali au kuingilia upande usiomhusu, kwa hiyo chochote alichojisikia moyoni mwake kuhusu Sonia kilipotea na upepo mpaka siku hiyo.
Kwa vile Side alikuwa akiaminiwa sana na Chakos, hakukuwa na mtu yeyote aliyefuatilia kama alikuwa ameshafanya mauaji kama alivyokuwa ameagizwa au lah, kwani kwa kufoji maiti ya msichana mwingine, Side aliweza kumshawishi Mr. Chakos kuwa alitekeleza kila kitu kama alivyotumwa na bosi wake.
Tangu siku hiyo, Sonia alikuwa ni mtu wa kukaa nyumbani tu huku muda wote akiufunika uso wake kwa baibui na nikabu ili watu wasijue kuwa yupo hai kwa kuwa kama angetambulika, hatari isingekuwa kwake pekee, bali hata kwa mumewe na watoto wake pia.
Kwa uoga, Sonia alikaa chini na kusali akiomba kwa Mola wake kila kitu kiende salama kwa mumewe na huyo mtu aliyekuwa katika hali ya kuitetea roho yake.
***
Diana na Zubeda walikuwa katika vyumba vyao chini ya Madam Bernadeta ambaye alikuwa ni kiongozi wa hosteli yao. Katika kila upande wa jengo kulikuwa na hosteli moja na kiongozi wake ambaye kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha kila msichana alifanya kama alivyokuwa akiagizwa kutoka ngazi ya juu ambayo ni Madam Flaviana, naye akiongozwa na Mr. John Chakos.
Chakos naye alikuwa chini ya Mr. George japokuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuiona sura yake, hakuna, hata Chakos mwenyewe hakuwa akimfahamu mbali na kupewa maelekezo ya sauti na maandishi.
Siku hiyo, Madam Bernadeta alikuwa na ujumbe kwa msichana Diana ambaye alikuwa akihitajika mara moja na utawala. Pasipo kujua jambo aliloitiwa, Diana alisimama na kumfuata Madam Bernadeta mara moja na kufungua mlango wa chumba kilichokuwa ghorofa ya juu kabisa.
Mara milio ya risasi ikifuatiwa na sauti kali iliyoashiria maumivu makali ilisikika kwa mbali kutoka ndani ya chumba hicho. Kufumba na kufumbua kukawa na damu kila mahali, zikichirizika kutoka katika mwili wa Diana.
“Safisha chumba na hakikisha hakuna mtu atakayejua kuhusu jambo hili, sawa!” Iliongea sauti ya kiume kutoka kwenye spika zilizokuwa ukutani ikimwambia Madam Bernadeta aliyekuwa amejibana nyuma ya chumba alichoingia Diana.
“Ha…hakuna mtu atakayefahamu bosi,” alijibu Madam Bernadeta kwa uoga.
“Vizuri, kesho asubuhi atakuja msichana mpya, jina lake ni Salima. Mpokee na mfahamishe kila kitu anachotakiwa kukifanya, nitakuwa nikifuatilia kila kitu!”
“Sawa Mr. Chakos,” alijibu Madam Bernadeta huku sauti kali ya Mr. John Chakos ikipotea taratibu kwa njia ya mwangwi na kukiacha chumba alichoingia Diana kikiwa na ukimya wa hali ya juu.
“Ooh, my God!” alihuzunika kimoyomoyo Madam Bernadeta mara baada ya kuuona mwili wa Diana ukiwa sakafuni hali ukiwa na matundu mengi ya risasi. Aliyafumba macho ya Diana ambayo bado yalikuwa yakitazama kisha akaiburuza maiti yake mpaka kwenye sinki kubwa lililojaa uji wa shaba iliyoyeyushwa na kuitumbukiza humo mpaka ikayayushwa na uji huo wa moto.
“Ulichokitaka umekipata, si ulitaka kurudi nyumbani?” aliongea peke yake Madam Bernadeta huku akichora ishara ya msalaba hewani kama padri aombeavyo maiti.
***
“Angalia!” aliongea Madam Flaviana huku akimpatia bahasha ndogo Side aliyeipokea kwa mashaka na kuifungua.
“Ndiye, siye?” aliuliza Madam Flaviana akimtazama Side aliyekuwa akizikodolea picha alizozitoa ndani ya bahasha ile.
Itaendelea siku ya kesho.
Post a Comment