ad

ad

Kitanzi, Kisu au Bastola - 5


ILIPOISHIA
HAKUWAHI kuwa na rafiki wala ndugu aliyepajua alipokuwa akiishi tangu ahamie kwenye mtaa huo mpya.
“Huyu atakuwa ni nani?” aliwaza Salima.
Endelea…
Kengele ya hatari ikalia kichwani mwake, akausogelea mlango na kufungua kidogo akichomoza kichwa chake kwanza ili kutotoa mwanya wa mtu huyo kuchungulia ndani ya chumba chake ambacho pasipo ubishi kilikosa hadhi ya kuitwa chumba, ingawa Salima  mwenyewe alifanya hivyo ili kumficha Dedan asionekane.
“Habari yako,” alisema mwanaume mrefu kidogo mwenye kila sifa ya kuitwa bosi au mkuu wa kitengo fulani kwa jinsi alivyovalia kiofisi na haiba yake.
“Sa…salama tu…nikusaidie nini?” alisema Salima kwa kigugumizi.
“Naitwa Saidi Hamis Kibona, eee.. Wewe ni Salima?”
“Haa...hapana haa..no, ni mimi, unashida gani?” kwa woga Salima alijikuta akikataa na kukubali kwa pamoja.
“Usiwe na hofu dada yangu, mimi ni wakala kutoka kwenye Kampuni ya kigeni iliyoingia nchini Tanzania. Mmm… Mara nyingi tumekuwa tukitembelea nchi kadhaa tukifanya sanaa ya urembo na wasichana mbalimbali hasa tunaowaona wana vigezo.”
“Kwa hiyo nikusaidie nini?”
“Kama nilivyokwambia awali, huwa tunafanya kazi na msichana tunayemwona ana vigezo, eee.. Salima nadhani bahati hii imekuangukia wewe.”
“Mbona sikuelewi! Hebu kwanza niambie jina langu umelijuaje?”
“Kwani una wasiwasi gani, nimeuliza nikatajiwa au kuna ubaya wowote dada yangu?”
“Hapana sikuwa na maana hiyo,” alijibu Salima akiwa bado na wasiwasi mkubwa.
“Usijali Salima, nadhani utanielewa vizuri, kwa sasa naomba nikupe fomu hii ambayo ina maelekezo yote kuhusu historia na jinsi kampuni yetu inavyofanya kazi zake.”
Side alifungua begi lake na kutoa bahasha ndogo akamkabidhi Salima.
“Maelekezo yote yapo humo. Tafadhali yasome taratibu na kama umevutiwa kufanya kazi na sisi, tuwasiliane,” alisema Side na kuondoka.
Salima alipokea bahasha ile kwa mshangao na kurudi chumbani kwake, lakini akaona siyo vizuri mgeni aondoke bila kumsindikiza. Akajitanda kanga mabegani na kutoka nje haraka akimuwahi Side.
“Ngoja nikusindikize mgeni,” alijibaraguza Salima kwa aibu baada ya nafsi yake kumsuta kwani awali hakuweza kumchangamkia wala kumkaribisha ndani kwa ukarimu, lakini hata kumsindikiza pia asiweze! Aliona siyo picha nzuri kwa mgeni huyo na pengine angeweza hata kuikosa kazi nzuri kutoka katika kampuni hiyo kwa kuwa tu hakuwa mkarimu kwa mtu huyo.
Side aligeuka na kumtazama Salima aliyemkimbilia. Wakatembea wakiongozana bila ya kuongea jambo lolote kimyakimya mpaka nje ya nyumba. Kwa mshangao Salima alimuona Side akiutoa ufunguo na kufungua mlango wa gari moja zuri na kuingia ndani yake.
“Salima, nafasi ni chache sana fanya maamuzi haraka sana hata leo jioni nijulishe kama umevutiwa na kazi yetu,” alisema Side huku akiwasha gari lake na kuondoka, moyoni akifurahi kwa mtego aliomtega Salima.
Watano kati ya wasichana aliokwisha wakabidhi kwa Mr. Chakos walikuwa wepesi sana kuwapata. Kwa maisha mabovu waliyokuwa wakiishi, hakupata tabu kunasa kwani wengi walipotajiwa tu kiwango cha fedha watakazolipwa waliruka kwa furaha bila kujali wangedhalilishwa kwa kiasi gani. Pesa ilikuwa na thamani hapa kuliko hata uhai wa mtu katika jiji hili na Side alilijua hilo fika.
Salima tu ndiye aliyekuwa tofauti na wasichana wenzake na kumfuata kwa njia ya kawaida kungesababisha kumpoteza msichana huyo. Kutokana uzuri wa sura na hata umbo lake.
***
Salima aliifungua haraka bahasha hiyo, akasoma na kuvutiwa na hadhi na mshahara mkubwa wa kazi hiyo. Akafurahi kuona hatimaye angeweza kupata fedha za kumtibia Dedan na kufanya mambo mengi ya kimaendeleo. Moyoni mwake alikubali kuajiriwa na kampuni hiyo akaitafuta simu ya Dedan na kuiwasha akidhamiria kumtaarifu Side ili asije akaipoteza nafasi ya kazi hiyo adimu.
Alipoiwasha simu mara meseji ziliingia kwa fujo, zote zikiwa zimetumwa na Caro moja ilisomeka kwa tarakimu ’91.’
“Huyu mwanamke mchawi hizi namba ana maanisha nini!” alistaajabu Salima na kuzipuuza.
***
Side akiwa na wasiwasi kama mtego wake utanasa au lah, alisimama kama punguwani akipiga hatua mbele na nyuma huku macho yake kila saa yakiiangalia saa yake ya mkononi.
Alitaka amalize kila kitu kabla hajampeleka Mr. John Chakos kuhakiki makazi ya Salima. Alitaka amshtukize bosi wake na pengine kwa kutaka kuonekana mfanyakazi bora kwa kukamilisha kazi zake mapema.
Kwa muda wote huo alikuwa akiisubiri simu kutoka kwa Salima kwani kwa mkwara aliomuonesha msichana huyo, isingekuwa rahisi kutobabaika na kuamini kwamba alikuwa hatanii kuhusu kazi hiyo.
Majira ya saa tano na nusu asubuhi, Dedan aliamka akihisi maumivu makali ya tumbo. Laiti kama angekuwa na ufahamu basi angetambua kwamba alisumbuliwa na njaa kali.
Kila siku alikuwa akilishwa na kufanyiwa kila kitu na Salima. Bado hakuwa na kumbukumbu kuhusu kitu chochote katika maisha yake na mbaya zaidi hata kutembea na kuongea ulikuwa mtihani.
Ingawaje alikuwa hakumbuki vitu vingi sana, lakini tabia ya asili ya kibinadamu ilimfanya kuwa na utambuzi juu ya  matendo yote ambayo huleta maumivu na yale yaletayo furaha, kwa hiyo alilia kwenye maumivu na kutabasamu au kucheka kwenye furaha.
Kwa mara ya kwanza Dedan akasimama na kutembea akikisogelea kiberiti kilichokuwa juu ya meza, akatoa njiti moja na kuisugua upande wenye baruti. Huenda jambo hilo alijifunza kwa kumuona Salima alipokuwa akiwasha moto kila alipokuwa akitaka kupika. Moto ukawaka huku ile njiti ya kiberiti ikiwa mkononi mwake.
Iliwaka huku moto ukishuka taratibu na kuongeza joto kwenye vidole vyake. Kwa maumivu ya kuungua akaitupa njiti ile chini kwa bahati nzuri ilizimika pasipo kuunguza kitu chochote.  
Kwa kiasi fulani mwanga wa kumbukumbu za kale ukapita akilini mwake. Siku hiyo akaanza kutambua kwamba kuna kitu kuhusu yeye hakijui. Akaangaza macho yake kila kona ya chumba kile kama mgeni huku akikosa majibu ya maswali kibao aliyokuwa nayo kichwani.
Akastaajabu yeye ni nani na alikuwa akifanya nini humo ndani! Kanga na nguo za kike zilizokuwa zimesheheni humo chumbani, kwa kiasi fulani zilimuogopesha. Hisia zake zikamtuma kwamba kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akiishi, mwanamke huyo ni nani? Alijiuliza.
Kitu ambacho pengine mwanadamu wa kawaida hukichukilia pasipo na uzito kwenye nyumba, ‘mlango,’ kwa Dedan mtazamo wake ulikuwa tofauti sana juu ya kifaa hicho muhimu kiasi kwamba alipouona tu aliutambua mara moja. Mbao nne zilizounganishwa pamoja, bawaba na kitasa chenye tundu la ufunguo ndiyo vilikuwa vitu muhimu sana kwa muundo wa milango mingi ya uswazi.
Kwa Dedan, mlango haukuwa njia ya kutoka nje na kuingia ndani tu. Hata katika ulimbukeni aliokuwa nao, bado aliuona mlango kama alama ya tumaini baada ya kiza cha utumwa na ufungwa. Ndani kulikuwa ni kizuizi chenye upweke wakati nje ilikuwa ni uhuru na furaha hatimaye.
Haya yote alijifunza alipokuwa mvulana mdogo sana. Shangazi yake Bi. Tabia alikuwa akimfungia mara kwa mara ndani, mchana na usiku bila kutoka nje huku adhabu kubwa aliyopewa na shangazi yake huyo ikiwa ni kuchomwa na moto mikononi.
Mambo hayo yote aliyavumilia kwa kuwa hakuwa na mzazi aliyekuwa hai kumtetea. Kwa hiyo aliishi katika mazingira hayo mpaka siku moja alipoweza kutoroka kwa kuufungua mlango kuelekea kwenye uhuru na furaha ya kuwa nje aliyokuwa akiitamani siku zote.
Nje ya mawazo hayo, Dedan aliutazama ule mlango kwa muda kisha akaukimbilia haraka, akauzungusha mkono wa kitasa na kujaribu kufungua, lakini haukufunguka. Akauvuta kwa nguvu; haukufunguka pia. Moyoni alijua halikuwa jambo rahisi kwani hata alipokuwa mtoto mdogo, pindi alipofungiwa mlango na shangazi yake alikuwa akitumia waya au msumari kuchokonoa tundu la mlango mpaka ufunguke.
Akaanza kuutafuta waya au msumari ndani ya chumba hicho, kwa bahati nzuri akaupata msumari mkubwa wa bati. Akausuguasugua ardhini na kuufanya bapa kisha akaupenyeza kwenye tundu la kitasa na kuanza kuchokonoa taratibu huku akiwa amefumba macho yake kana kwamba alikuwa akivuta hisia.
Kwenye mawazo yake aliiona sura mbaya ya shangazi yake ikimkaripia, hofu ikaanza kujijenga taratibu huku kila kitu ndani ya chumba hicho kikigeuka na kuwa kama vile cha shangazi yake huyo. Kwa mara nyingine mlango ukawa alama ya uhuru kwa Dedan, kwa muda huo alitaka sana kuwa huru tena.
 Akajitahidi kuchokonoa kitasa hicho na mara kikazunguka na kichuma cha loki kikajiachia na kurudi ndani kadiri alivyokuwa akiunyonga msumari huo.
Akaufungua mlango na kutoka nje kwa kupita koridoni hadi nje ya nyumba. Njiani akikutana na sura tofauti za watu wengi wakimtazama na kumshangaa kwa jinsi alivyovaa vibaya na jinsi uso wake ulivyomvimba kwa usingizi na njaa.
 Akakatiza mitaa kama chizi kwa bahati mbaya alikoswakoswa na magari mengi barabarani.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments

Powered by Blogger.