ad

ad

NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 15




ILIPOISHIA:
“Nitafanya hivyo, namuomba Mungu muda uliobaki tuvuke salama.”
“Basi nikutakie usiku mwema.”
“Na wewe pia, nashukuru kwa msaada wako.”
SASA ENDELEA...

Nilirudi ndani na kumkuta mume wangu akikoroma katika usingizi mzito, nilimuomba Mungu alale vilevile hadi asubuhi. Lakini kwangu sikupata tena usingizi hadi kunapambazuka. Alfajiri nilishukuru wazazi wa mume wangu walikuja baada ya kuchelewa kupata taarifa ya ajali ya Victor.
Nilipowaona nilijikuta nikibubujikwa machozi kuwaona wazazi wa mume wangu.
“Vipi kuna usalama?”
“Upo, lakini mdogo sana wazazi wangu,” niliwajibu kwa sauti ya kilio.
“Yupo wapi mumeo?”
“Amelala, lakini simuelewi tangu apatwe na ajali.”
“Kamuamshe.”
Nilikwenda ndani kumuamsha mume aliyekuwa bado amelala, baada ya kumuamsha aliamka.
“Vipi mke wangu? Niache nilale bado nina usingizi.”
“Wazazi wamekuja.”
“Wanasemaje?” aliniuliza bila kunitazama.
“Mume wangu hujui yaliyokutokea?”
“Ooh! Nilisahau, acha niamke nikawaone.”
Alinyanyuka kitandani na kuvaa nguo kisha tulitoka pamoja sebuleni walipokuwa wamekaa wazazi.
“Shikamooni,” aliwasalimia huku akikaa kwenye kochi karibu na walipokuwa amekaa.
“Marahaba baba, pole sana.”
“Asante.”
“Unavyoiona ile ajali ni ya kawaida au mauzauza?” baba mkwe alimuuliza mume wangu.
“Wazazi wangu nina imani maisha yangu hayana muda mrefu hapa duniani,” mume wangu alisema kwa sauti ya chini huku akitazama chini.
“Kwa nini?” mama mkwe aliuliza.
“Mambo ninayokutana nayo hata kuyazungumza siwezi.”
“Mambo gani mume wangu?”  nilimuuliza baada ya kushtushwa na kauli ya mume wangu na kujiuliza kwa nini aseme maneno kama yale kwa wazazi wake wakati mimi mkewe sijui lolote zaidi ya ajali mbaya na matukio yaliyomkuta.
“Mke wangu mengine nikikuelezea unaweza kufa kwa presha, lakini siri nzito ninayo mwenyewe.”
“Siri gani tena mume wangu?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.
“Nashindwa nianzie wapi kuielezea, usiku kwangu ulikuwa mgumu sana tena sana maishani mwangu na sikuamini kama nitaliona jua la leo.”
“Kivipi?” nilimuuliza mume wangu ambaye alionesha ana siri nzito moyoni mwake lakini hakutaka kuisema.
“Unajua sisi wanadamu ni viumbe wabaya sana, sisi tuna utajiri gani? Gari mbili, kiwanja hata nyumba hatujamaliza wananitoa roho?” mume wangu kufikia hapo aliinama na kutulia huku akilia kilio cha kwikwi.
“Sasa mama sikiliza,” baba mkwe alisema na kunifanya nimwangalie yeye.
“Hapa hakuna muda wa kupoteza, twende moja kwa moja kwa mganga tuangalie tulikosea wapi.”
Kwa vile lilikuwa limebakia gari moja, nilimpigia simu Jimmy aje atuchukue, atupeleke kwa mganga. Lakini ilikuwa bahati nzuri alikuwa na yeye yupo jirani kuja kujua hali ya mume wangu kabla ya kwenda kazini. Alipofika alituchukua na kutupeleka kwa mganga Mtoni Mtongani.
Baada ya kufika tulipokelewa na mganga na kuingizwa kwenye chumba cha huduma. Sote tulikaa kwenye mkeka, baada ya mganga kumaliza shughuli zake, aliingia chumbani na kukaa mbele yetu. Kama kawaida alichukua kitabu chake na kukisoma kwa muda kisha alinyanyua macho na kutikisa kichwa akisema:
“Mmh! Jana kijana alikuwa anakufa kifo kibaya, yaani hata asingeomba maji. Ile iliyotokea si ajali ya kawaida, wale waliokuja kukukodi ni majini wa kutumwa. Si walikuwa mwanamke na mwanaume waliovaa kiheshima kama Wapemba?”
“Ndiyo,” mume wangu alijibu.
“Basi wale hawakuwa watu kama ulivyofikiria, walikuwa majini ambayo ndiyo waliolizima lile gari ili ugongwe na kufa ili kionekane ni kifo cha kawaida. Dawa niliyokupatia ndiyo iliyokusaidia bila hivyo ungebakia jina na watu kuona wewe ni mzembe kuingiza gari barabarani bila kuangalia.”
“Ina maana waliokufa si watu wa kweli?” mume wangu aliuliza, muda huo alikuwa kwenye hali ya kawaida kabisa.
“Wale hawakuwa watu, kile ni kiini macho kuona watu wamekufa ili hata wewe ukifa, ijulikane umekufa na abiria wako wawili.”
“Mbona inasemekana zile maiti zilichukuliwa na kupelekewa hospitali?”
“Niamini mimi kuwa pale hakukuwa na watu, kama mnabisha, nendeni mkaangalie zile maiti kama zitakuwepo. Pia kaliangalieni gari kama utakuta kuna damu.”
“Ni nani aliyefanya hivyo?”
“Kwa kweli kila nikimtafuta naona kiza, inaonekana amejizatiti baada ya kutegua mtego wa awali. Lakini bado nitapambana naye mpaka pumzi za mwisho.”
“Na huu mkono?”
“Pigo ulilopigwa limepitia hapo, lakini hakuna tatizo nitalitatua,” kauli ya mganga ilinipa moyo na kunifanya nipunguze mawazo kidogo.

“Kuna kitu gani kinachomtisha kiasi cha kusema ana imani maisha yake yamebaki kuwa mafupi sana?” Baba mkwe aliuliza.
“Ni wasiwasi wake tu kutokana na vitu vinavyomtokea ndotoni.”
“Vitu gani?”
“Usiku alipolala ile safari ilijirudia upya, alichokiota ndicho ambacho kingetokea.”
“Kipi hicho?” Niliuliza.

“Ameota baada ya gari kuzimika na kugongwa hakutoka na kugongwa kichwa chake kikapasuka na mkono huu ulinyofoka na kuangukia upande wa pili. Maumivu ya kunyofoka mkono na kupasuka kichwa aliyasikia kiasi cha kushtuka usingizini na kuendelea na maumivu yale.
“Acha alie kama mtoto mdogo, jana usiku kateseka sana na angeweza kufa kwa maumivu yale, baada ya kunyamaza vile ndiyo ilikuwa mwisho wa safari yake. Lakini kinga niliyompa bado ilimsaidia sana badala ya kufa alipoteza fahamu. Maumivu yale yangemuandama kila usiku na mwisho asingevumilia angeamua kujiua kwa kunywa sumu au kujinyonga kutokana na maumivu makali sana ambayo yangekimbilia moyoni mwake.
Na ugonjwa ule siku zote hospitali huwa hauonekani zaidi ya kwa wataalam kama sisi.”

Nilikubaliana na mganga kwani mume wangu kila alipokwenda hospitali na kupimwa ugonjwa haukuonekana.
“Kwa hiyo utatusaidia vipi?” Mama mkwe aliuliza.
“Dawa nitakayompatia leo itamaliza kila kitu wala msihofu.”
Baada ya kusema vile alianza kumshughulikia mume wangu kwa sisi kutolewa chumbani. Baada ya nusu saa alitoka akiwa amechanjwa sehemu iliyomletea maumivu na kupakwa dawa. Baada ya matibabu tulipewa tena dawa za kuoga na kufusha kisha tulirudi nyumbani.

Tulipofika mume wangu alionekana amechoka sana, baada ya chai aliingia chumbani kulala. Alipovua nguo na kulala ndipo nilipomuona vizuri alivyochanjwa kuanzia juu ya bega hadi chini ya mkono, mbavuni mpaka kiunoni na kupakwa dawa nyeusi iliyochanganywa na mafuta mazito.
Wakwe zangu siku ile hawakuondoka walilala palepale kusikilizia hali ya mume wangu ambayo iliendelea vizuri. Usiku alilala vizuri kitu kilichotufanya tuamini mganga ameweza kutatua tatizo, hata yale matatizo ya maumivu ya mkono hayakuwepo, alilala vizuri.

Siku ya pili tuliamka salama, pamoja na mkono kuisha maumivu tatizo lingine lilikuwa kukosa nguvu kitu kilichofanya atumie mkono wa kushoto katika kazi zake zote. Niliamini baada ya muda kutokana na matibabu na kauli ya mganga atarudi katika hali yake ya kawaida.
Baada ya kufungua kinywa na kuhakikisha hali ya mume wangu imetulia nilikwenda Polisi Chang’ombe kuangalia gari alilopata nalo ajali mume wangu ili nilinganishe na mastaajabu ya watu.

Kwa vile baadhi ya maaskari walikuwa wakinifahamu waliponiona walinitania.
“Shemeji umekuja kuona maajabu ya Musa?” Swali lile lilizidi kuniweka njia panda na kujawa na mawazo mengi juu ya ajali ilivyokuwa.
“Ndiyo shem, la kusikia si sawa na la kuona.”
Walinipeleka kwenye magari yaliyokuwa yamewekwa sehemu moja, mengi yalionekana kupata ajali za kugongwa lakini mengine yalikuwa mazima, sikujua na yale yapo pale kwa ajili gani.
Nilipofika nilijikuta nikilitafuta gari letu na kushindwa kuelewa lipo upande gani hadi askari niliyeongozana naye aliponiambia:
“Hili hapa shemu.”
“Hili?” nilishtuka.
“Ndiyo.”
“Hapana...hapana, siyo hili,” nilijikuta nakataa baada ya kuliona gari lililokuwa kama chapati.
“Ndilo hili shemu si unazijua namba zake, angalia.”
Nilichungunza gari, lilikuwa limekunjika vibaya, baada ya kulichunguza, niligundua ndilo lenyewe. Nilijikuta nikitokwa na machozi nisiamini kama kweli mume wangu alitoka salama kwenye ajali ile.
“Sasa shemu unalia nini?” aliniuliza askari aliyenipeleka kuliona gari.
“Siamini...siamini...kama mume wangu alitoka salama kwenye ajali hii!” nilisema huku nimeshikilia kifua na machozi yakiendelea kunitoka.
“Mumeo lazima atakuwa ameaga kwao, ajali hii hakuna anayeweza kukubali kama dereva alitoka salama labda useme gari liligogwa bila dereva ndani.”
“Mmh! Mungu mkubwa sifa ni haki yake, asante Mungu.”
Nilimshukuru Mungu kwa kupiga ishara ya msalaba kwa kuyaokoa maisha ya mume wangu kwenye ajali ile.
Nilizidi kuamini kila kitu kwa Mungu kinawezekana kama alivyoweza kumuokoa Musa kwa Firauni. Pia kumponya Yona katika tumbo la samaki na mitume wengine wote aliowaponya pale uwezo wa kibinadamu ulipofika kikomo. Kutokana na kuamini kila tuliloahidiwa na Mungu kuwa hakuna zito mbele yake. Niliamini hata mume wangu naye alimnusuru kwa njia hiyohiyo japo sikujua kipi kikubwa alichokifanya kwa Mungu kupewa kinga kama ile.
Nilirudi nyumbani bado nikiwa na picha ya gari letu lilivyokuwa na kupona kwa mume wangu. Nilijiuliza nini hatima yetu kama watu kila kukicha wanatafuta mbinu za kutupoteza. Niliamini ule ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa kumtumikia yeye mimi na mume wangu, japo bado nilikuwa na wasiwasi wa kuchanganya nguvu za giza na Mungu aliye hai aliyetukataza kumshirikisha kwa miungu mingine kwa vile yeye ni mwenye wivu.
Lakini niliamini bado tuna nafasi ya kutubu na kukubaliwa, kwa vile Mungu wetu ni mpole msikivu na mwenye huruma. Nilipanga baada ya kumaliza tiba ya mume wangu tuanze kazi ya kumtumikia Mungu kwani niliamini kupona kwa mume wangu haikuwa nguvu ya mganga bali uwezo wa Mungu kutuonesha kuwa hakuna mwenye uwezo zaidi yake. Pia ni ili tuamini kuwa yupo na mwenye kutenda kile kisichotarajiwa na mwanadamu.
***
Mwezi ulikatika bila mabadiliko makubwa ya hali ya mkono wa mume wangu. Kila tuliporudi kwa mganga alitubadilishia dawa huku tukizidi kupoteza fedha bila mafanikio. Kilichonishtua sana kilikuwa kuuona mkono wa mume wangu ukipungua na kuanza kusinyaa. Kwa kweli kitu kile kilinishtua sana na kutaka ufumbuzi kwani hali ilishakuwa mbaya.
Hata biashara zangu nazo zilianza kuyumba kwani sikuwa na uwezo tena wa kuongeza vitu dukani kutokana na fedha nyingi kuipeleka katika matibabu ya mume wangu. Mume wangu naye kutokana na mawazo ya ugonjwa, alianza kupungua siku hadi siku kila nilipomwangalia roho iliniuma sana na kufikia hatua ya kuwachukia wanadamu.
Sikuamini kitu chetu wenyewe kifikie hatua ya kututesa vile, moyoni nilifikia hatua ya kujilaumu kununua gari. Niliona heri ningeongeza maduka kuliko gari lililotuletea dhahama nzito kama ile. Kuchanganyikiwa kubaya, kila mganga niliyeelekezwa nilikwenda.
Nilielekezwa sehemu moja huko Muheza, Tanga, kwa vile muda huo fedha ilikuwa imeniishia, ilibidi niuze kiwanja na nyumba iliyokuwa imefikia dirishani kwa bei ya kutupa ili tu niokoe uhai wa mume wangu. Nilikwenda Muheza vijiji vya ndanindani, nilipofika nilikutana na mapya kuwa mkono wa mume wangu kuna vitu vimewekwa vinavyomnyonya kila siku.
Sikuamini vitu vilivyotolewa kwenye mkono wa mume wangu, kulitolewa sindano ndogo za kushonea zaidi ya kumi, viwembe sita na pini ndogo tano.
“Basi hivi mwanangu ndivyo vilivyokuwa vikimtesa mumeo,” mganga alinionesha na kunifanya nipigwe na butwaa.
Nilichanganyikiwa na kujiuliza vitu vile viliingiaje mwilini kwa mume wangu.

Itaendelea LEO

No comments

Powered by Blogger.