Zitto Kabwe: Sitagombea Urais TFF
Ijumaa
ya Aprili 21, mwaka huu, gazeti la michezo na burudani nchini,
Mwanaspoti, liliandika habari kwenye ukurasa wake wa kwanza yenye
kichwa: "Zitto ajitosa Urais TFF, Rage amkubali."
Upande
wangu, licha ya kwamba habari hiyo ilichapishwa bila kupata maoni
yangu, lakini haikuwa ngeni. Hii ni kwa sababu kabla ya habari hiyo
nilikuwa nimeshapokea maombi kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo
viongozi wakubwa wakinitaka nigombee Urais TFF.
Baada
ya habari hiyo kuchapishwa na kupata umaarufu mkubwa, nilipokea maombi
mengi zaidi pamoja na shinikizo lenye kunitaka muda ukifika wa uchukuaji
fomu, nijitokeze nichukue fomu ya kuwania Urais TFF.
Msukumo
ni mkubwa na maswali ni mengi kipindi hiki ambacho dirisha la uchukuaji
fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi TFF limefunguliwa.
Kila
ombi na shinikizo ambalo nimepokea, nimelibeba kwa unyenyekevu mkubwa.
Bila shaka wanaoniomba na kunishinikiza wanavutwa na mambo mawili; mosi,
soka letu kutoleta nuru kwa Watanzania. Pili, imani kubwa kwamba
kupitia uongozi wangu nuru ya soka letu itadhihirika.
Hata
hivyo, yapo mambo mawili nimeyatafakari; Mosi, mahitaji ya soka letu na
nguvu ya maarifa inayohitajika kulikwamua. Pili, nafasi yangu kama
mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo.
Kuhakikisha
kazi ya kulikwamua soka letu inafanikiwa na nuru inadhihirika kwa
wapenda soka wote nchini, inahitaji uwekezaji mkubwa wa muda, vilevile
uwekezaji mkubwa wa maarifa ya kiuongozi.
Soka
la Tanzania lipo hapa kwa sababu ya uwekezaji usioridhisha wa maarifa
ya uongozi, hiyo inatokana pia na viongozi wanaopata nafasi ya
kulitumikia shirikisho letu la mpira wa miguu nchini, kutowekeza muda
wao barabara kwenye soka.
Nikiwa
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, ninadaiwa mambo mawili, uwekezaji wa muda na
uwekezaji wa maarifa ya kiuongozi ili kukiandaa vema chama chetu
kushiriki uchaguzi kati ya miezi 28 mpaka 40 inayokuja.
Mwaka 2019, Chama kitashiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mwaka 2020, Chama chetu kitashiriki Uchaguzi Mkuu.
Hivyo
basi, kwa kuongezea na uwakilishi wangu wa Jimbo la Kigoma Mjini ambako
Chama chetu kinaongoza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, naona
kuwa lipo eneo ambalo nitashindwa kulitimizia wajibu wake nikivaa kofia
ya tatu ya Urais wa TFF.
Nimetafakari
na kuchukua uamuzi kwamba Uongozi wa ACT-Wazalendo na Ubunge ni nafasi
ambazo ninazo tayari, wakati Urais TFF ni nafasi mpya.
Kwa
hali hiyo na kwa mapenzi makubwa ya soka la Tanzania, nimeamua
nisichukue fomu ya kugombea Urais wa TFF, kwani naweza kuomba kazi
ambayo nitashindwa kuitumikia kwa muda wa kutosha kutokana na majukumu
yangu kwenye Chama na ubunge.
Uamuzi
huu umezingatia mapenzi makubwa kwa soka letu. Nikijitokeza kuwania
Urais wa TFF leo halafu nikakosa muda mzuri wa kutimiza matarajio ya
wapenda soka nchini, utakuwa usaliti mkubwa kwa maendeleo ya soka la
Tanzania.
Nawashukuru
wote walioniomba na kunishinikiza nichukue fomu. Nawaambia kuwa kwa
sasa tujielekeze kupata viongozi bora miongoni mwa watakaojitokeza.
Wakati mwingine mazingira yakiruhusu, nitaweza kutii maombi hayo.
Asante sana.
Zitto Zuberi Kabwe Ruyagwa
Post a Comment