ad

ad

NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 14



ILIPOISHIA
Sikuridhika, nilipiga tena simu ambayo iliita bila ya kupokelewa na niliporudia ilikatwa na kuzimwa kabisa.
Moja kwa moja nilijua mume wangu amefariki, hapo nilihisi kizunguzungu, sikutembea umbali mrefu nilianguka chini na kupoteza fahamu mpaka nilipozinduka na kujikuta nikiwa hospitali.
Sasa endelea...

Daktari baada ya kunisikiliza aliniuliza:
“Kwa hiyo, bila kufanya uchunguzi zaidi ulijua mume wako amefariki?”
“Ndiyo, kutokana na maelezo niliyopewa kuwa katika ile ajali hakuna kitu  kilichotoka ndani na watu wawili walikufa palepale mmoja lazima atakuwa mume wangu.”
“Lakini haukuwa na uhakika?”
“Ndiyo.”
“Hayo ndiyo makosa mnayoyafanya watu wengi, kuwaza kitu msichokuwa na uhakika nacho.”
“Kwa hiyo mume wangu hajafa?” Nilimuuliza daktari baada ya kuona kama nilidanganywa.
“Hajafa.”
“Lakini alipata ajali?”
“Ndiyo.”
“Kuna watu walikufa?”
“Kwa maelezo niliyopata watu wawili walikufa palepale ila mumeo kwa uwezo wa Mungu alipona.”
“Kama amepona yupo wapi?”
“Alikuja kukuona lakini tumemuomba akatulie nyumbani kutokana na maumivu ya mkono.”
“Amevunjika?”
“Hapana ni maumivu ya ndani kutokana na maelezo yake.”
“Na gari?”
“Kwa kweli sijui lolote kuhusiana na gari zaidi ya kumuon alipokuja kukuona na kuelezwa alipata ajali mbaya.”
“Nitawezaje kumuona?”
“Kwa vile hali yako si mbaya sana ulikuwa na mshtuko tu, nitakuruhusu ukamuone mzee nyumbani.”
Baada ya daktari kuhakikisha afya yangu ipo sawa, niliruhusiwa kurudi nyumbani. Akili yangu muda wote ilimuwaza mume wangu na si kitu kingine, Salome na wasichana wangu wa dukani waliitwa na kuelezwa nimeruhusiwa, walikodi teksi hadi nyumbani. Nilipofika baada ya kuteremka niliwahi ndani kumuona mume wangu.
Nilimkuta amejilaza kwenye kochi, mkono wake mmoja akiwa ameuning’iniza kwenye bandeji aliyoifunga begani.
Aliponiona alinyanyuka na kunifuata kunipokea, nilimkumbatia mume wangu huku nikitokwa machozi ya furaha.
“Pole mume wangu.”
“Asante, pole na wewe.”
“Kupona kwako ndiyo uzima wangu, vipi mkono?”
“Ni maumivu tu ya kuanguka lakini nimeelezwa sikuvunjika.”
“Pole sana mpenzi wangu, nasikia kuna watu walifariki?”
“Hata mimi nimesikia, wakati wa ajali sikuwa na fahamu.”
“Kwani waliokufa walikuwa wapi?”
“Walikuwa abiria walionikodi.”
“Mmh! Vipi gari?” Niliuliza kwa shauku ya kujua.
“Tutazungumza, tulia kwanza mke wangu.”
Nilishangaa kushindwa kunijibu kuhusu gari, kutokana na maelezo niliyoyapata awali gari lile lisingerudi tena barabarani.
Sikutaka kuliendeleza hilo, kwangu muhimu alikuwa ni mume wangu na wala siyo gari. Nilimuacha mume wangu apumzike na kuzungumza na shoga yangu ambaye tulikuwa tuna mwezi mmoja hatujaonana kutokana na shughuli za kutafuta maisha.
“Mmh! Shoga nakuona umekuja kama siku ile shaghalabaghala kwani taarifa zilikufikiaje?”
“Wee acha mbona leo ningekufa kabla yako.”
“Kwa nini?”
“Taarifa zilizonifikia kuwa wewe na mumeo mmefariki kwenye ajali mbaya, nilipandwa na presha na kushikwa na kizunguzungu. Yaani nashukuru kuwepo na shemeji yako naona ningetangulia miye.”
 Baada ya kunipa huduma ya kwanza aliniuliza tatizo lilikuwa ni nini, nilimweleza taarifa za vifo vyenu.
“Na yeye alipiga simu yako iliyopokelewa na msichana wako wa dukani, aliyesema kuwa hawaelewi chochote juu ya kifo cha mumeo ila wewe upo hospitali baada ya kuanguka na kupoteza fahamu, ndipo nilipokuja wangu wangu. Wakati nakuja nilikuta gari moja limebondeka vibaya huku watu wakilishangaa na kusikia wakisema wamekufa watu wawili.”
“Basi gari hilo alikuwa anaendesha shemeji yako.”
“Weweee!” Solome hakuamini kusikia vile eti mume wangu amepona kwenye ajali ambayo mimi sikuiona. Nilibakia na maswali mengi kuhusiana na ajali iliyomshangaza kila mtu kusikia eti mume wangu ametoka salama.
“Ina maana ilikuwa ajali mbaya sana?”
“Sana...kwa yeyote atakayeiona ile gari ilivyokunjwa ukimwambia kuna mtu ametoka salama hawezi kukubali.”
“Mmh! Mbona unanitisha kwa kusema hivyo, kwani ikoje?”
“Si ya kuhadithiwa, kama shemeji haendi kanisani huu ni wakati wake wa kumshukuru sana Mungu kwani bado anampenda.”
Nilibaki na maswali mengi kichwani mwangu kuhusiana na ajali hiyo ambayo mume wangu alikuwa amepona kimuujiza. Marafiki zake walizidi kujazana kuja kumpa pole, kila mmoja akilishangaa gari na yeye kuwa hai.
“Kaka kama hukufa leo, hufi tena,” mmoja wa rafiki zake alimtania.
“Kifo ni ahadi nimeamini kwa ajali ya leo, mtu hawezi kufa bila siku yake kutimia,” mwingine alichangia na kuzidi kunichanganya mtoto wa kike.
 Kwa vile hali yangu na mume wangu zilikuwa za kuridhisha na muda ulikuwa umekwenda sana, niliwaruhusu shoga yangu Salome na wasichana wangu wa dukani wakapumzike kwani siku nzima waliipotezea kwangu.
Baada ya kuondoka shoga na wasichana wangu wa dukani, nikabakia na kazi ya kupokea  majirani na marafiki kuja kutupa pole kutokana na ajali mbaya iliyompata mume wangu.
Siku ile tulipata muda wa kupumzika saa 4:00 usiku baada ya watu kukubali kutuacha tupumzike. Pamoja na mwili kuwa na uchovu, bado sikutaka kulala mpaka nijue nini kilichomsibu mume wangu kukutwa na masahibu kama yake, hasa mshangao wa dunia kupona kwake kulikokuwa kama ngamia aliyepenya kwenye tundu la sindano.
Tukiwa kitandani kabla ya kulala, nilimuuliza mume wangu:
“Mume wangu hebu nieleze ilikuwaje? Maana kupona kwako kila mtu anayekuja anakuona kama ngamia aliyepenya kwenye tundu la sindano!”
“Mpaka sasa sielewi na siamini kama nipo hai,” mume wangu alisema kwa sauti ya chini yenye kusikika ikifuatia michirizi ya machozi.
“Ilikuwaje mume wangu?” nimuuliza nikimkazia macho.
“Katika siku niliyokuwa na kismati cha biashara ni leo, tangu asubuhi gari langu limekuwa likikimbiliwa na wateja kila liliposimama kituoni hata kama nitakataa abiria walikataa kupanda teksi nyingine. Nilikuwa nimerudi kutoka Pugu kupeka abiria.
Hata kabla sijapumzika, walikuja abiria wawili, mtu na mkewe na kuniomba niwapeleke Kigamboni. Nilitaka kuwakatalia lakini bahati nzuri teksi iliyokuwa kijiweni ilipata abiria hivyo sikuwa na budi kukubali kuwapeleka.
“Baada ya kupanda  na kukubaliana bei, niliondoa teksi kijiweni kuelekea Kigamboni kupitia Barabara ya Sokota nipitie Mbozi hadi Keko inayoungana na Barabara ya Mandela. Nilipofika kwenye makutano ya Barabara ya Sokota na Mandela, kabla ya kuvuka niliangalia kulia na kushoto na kuona barabara nyeupe ila lori la mafuta lilikuwa mbali sana karibia na Vetenari.
“Nilikanyaga mafuta kuwahi kuvuka, hamadi! Sikuamini gari lile kuliona limefika karibu yetu. Nilikanyaga mafuta ili niwahi kuvuka japo sikuwa na uhakika kama nitafanikiwa, kwa ajabu ya Mungu gari lilizimika. Kilifuatia kishindo kizito cha gari letu kugongwa na kushtukia nimerushwa juu na kutua chini nikiwa nimepoteza fahamu.
“Niliposhtuka nilijikuta hospitali, baada ya uchunguzi nilionekana sina jeraha lolote mwilini zaidi ya maumivu kidogo ya mkono wa kulia ambayo baada ya kuchomwa sindano ya maulivu yalitulia mpaka muda huu,” mume wangu alimaliza kusema huku machozi yakiendelea kumtoka na kuufanya moyo wangu uzidi kuniuma.
“Mmh! Pole sana mpenzi wangu. Mungu akulinde na balaa lingine.”
“Amina.”
“Na gari?”
“Mke wangu gari halifai, nilipotoka hospitali nilipitia polisi pale Chang’ombe. Wee acha tu, kwa ajali ile, siamini na sitaamini kama nilitoka salama, kile kilikuwa kifo,” mume wangu alisema kwa sauti ya majonzi.
“Jamani, sasa hii itakuwa amri ya Mungu au bado watu wako wanakufuata?” nilimuuliza mume wangu kutokana na wasiwasi wa matukio.
“Watakuwa haohao.”
“Mbona yule mzee alisema hawawezi tena?”
“Wanadamu tuache tu, tuna kila hila kuhakikisha tunatimiza ubaya wewe, kwa jinsi lile gari lililosogea kama mshale wakati navuka, nasema si bure ni mkono wa mtu. Tena mtu huyo anataka roho yangu.”
“Basi turudi kwa yule babu?”
“Kuna umuhimu huo.”
“Vipi gari linaweza kupona?”
“Haliwezi, limeharibika vibaya, injini haifai imepasuka vibaya, lile gari mke wangu sasa ni skrepa.”
Japo roho iliniuma kupoteza gari, lakini kupona kwa mume wangu lilikuwa jambo muhimu kwa kuamini gari linapatikana si roho ya kiumbe ikitoka imetoka.
“Haliwezi, limeharibika, injini haifai, imepasuka vibaya  mke wangu.”
Japo roho iliniuma kupoteza gari lakini kupona kwa mume wangu lilikuwa jambo muhimu kwa kuwa na imani kuwa gari linapatikana si roho ya kiumbe, ikitoka imetoka.
SASA ENDELEA...

BAADA ya mazungumzo marefu nilimruhusu mume wangu aende kulala mara aliposema  anajisikia maumivu ya mbali sehemu ya bega lililoshtuka.
Nami kwa vile nilikuwa nimechoka  kiasi cha kumruhusu mtoto wangu kwenda kulala na msichana wa kazi, sikuchelewa kupitiwa na usingizi mzito.
Katikati ya usiku nilisikia sauti kwa mbali kama mtu ananiita. Niliposhtuka nilimsikia mume wangu akilalamika kwa sauti ya maumivu makali.
“Mungu wangu nakufa miye...ooh mke wangu nakufa.”

 Niliwasha taa na kumkuta akitokwa na machozi kama mtoto mdogo huku mkono mmoja kashikilia bega linalomuuma.
“Vipi mume wangu?” nilimuuliza macho yakiwa yamenitoka pima.
“Nakufa mke wangu...nakufa...nakufa,” mume wangu alilalamika alikuwa na maumivu makali.
“Mungu wangu! Nini tena mume wangu?”

“Mamaa...nakufa kaniitie kaka...nakufa mke wangu...mama...mama...uko wapi nakufa kifo kibaya mwanao.”
“Mume wangu unaumwa nini?”nilimuuliza huku nikitetemeka.
“M...mm...kono...mkono...na...na...kufa...kichwa kinapasuka nakufa mke wangu huku najiona,” mume wangu alilalamika kama mtoto huku makamasi yakimtiririka kama maji.

Mume wangu alijitupa chini kutoka juu ya kitanda mzima mzima kama mtu aliyerushwa na kuanza kugaagaa akipiga kelele za maumivu makali ya mkono na kichwa, kila muda ulivyokwenda ndivyo sauti yake nayo ilivyopungua, mwishowe kabisa alinyamaza na kutulia tuli.
Wakati huo nilikuwa nahangaika na kushindwa sehemu ya kumshika, nilijiuliza nifanye nini mtoto kike kila dakika duniani nilikuwa mgeni kwani kucheka kwangu kulikuwa kidogo lakini kulia kila kukicha.
Baada ya kutulia nilimfuata na  kumshika, cha ajabu nilipomgeuza alilegea kitu kilichonishtua na kuanza kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani.

Wazo lililonijia haraka ni kumpigia simu rafiki yake Jimmy. Nilimpigia Jimmy huku nikiangua kilio.
“Nini tena shem?” Jimmy alishtuka.
“Njoo.”
“Kuna nini tena shem?”
“Victor.”

“Victor! Kafanya nini tena?”
“Jimmy njoo haraka.”
“Nakuja.”
Kwa vile alikuwa hakai mbali alifika haraka sana, akaanza kushangaa kutokana na hali aliyomkutana nayo mume wangu, baada ya kumuona aliniuliza huku  macho yake yakiwa yamemtoka pima.
“Shem vipi tena! Mbona hivi?”

Nilimueleza hali iliyomtokea na kushangaa sana, tulimchukua haraka na kumuwahisha Hospitali ya Amana.
Muda wote mume wangu alikuwa kama mtu aliyelala usingizi mzito lakini pumzi zake zilikuwa zikisikika kwa mbali sana.
Tulipofika tulipokelewa na mgonjwa kubebwa  kwa kitanda cha magurudumu hadi wodini. Kabla ya kuhudumiwa tuliulizwa matizo yake, ajabu kabla sijajibu Victor alishtuka alipokuwa amelala na kufumbua macho kisha akajinyoosha na kujishangaa kuwa pale.
“Vipi mke wangu?” aliniuliza.

“Si unaumwa wewe?” nilimjibu huku nami nikimshangaa.
“Mimi?” Mume wangu alizidi kushangaa huku akikunja uso baada ya kutaka kauegemea mkono unaomuuma.
“Jamani haya makubwa, si ulikuwa ukiumwa mkono na kichwa kiasi cha kulia kama mtoto mdogo mpaka akapoteza fahamu.”
“Sina kumbukumbu hizo, mbona nilikuwa nimelala baada ya kuhisi kama mkono unataka kuniuma, zaidi ya hapo sikumbuki kitu.”
“Kweli mume wangu?” nilizidi kumshangaa mume wangu.

“Kweli kabisa.”
“Kwani kuna tatizo gani?” daktari aliuliza.
Nilimueleza yote ambapo mume wangu alishangaa sana, alichukuliwa vipimo vingine japokuwa vya awali vilionesha hana tatizo lolote.
Jibu lilikuwa lilelile hana tatizo lolote, baada ya kudungwa sindano ya maumivu tuliruhusiwa kurudi nyumbani usiku uleule.
Njia nzima nilikuwa naona kama maajabu, mume wangu kusema hajui lolote lililotokea. Tulipofika nyumba wakati nikimsindikiza shemeji Jimmy alinieleza kitu:

“Shemeji, kwa ajali ya leo kuna kitu kizito naomba kesho asubuhi muwahi kwa yule mganga, nikimuangalia Victor namuona hayupo sawa kabisa, kuna jambo linaendelea ambalo hatulijui, tukifanya mzaha tutajuta baadaye.”
“Nitafanya hivyo, namuomba Mungu muda uliobaki tuvuke salama.”
“Basi nikutakie usiku mwema.”
“Na wewe pia, nashukuru kwa msaada wako.”
ITAENDELEA KESHO


No comments

Powered by Blogger.