ad

ad

YANGA YAWEKA REKODI KOMBE LA MAPINDUZI

YANGA imeshindwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kisiwani Zanzibar, lakini hiyo haikuzuia timu hiyo kuacha rekodi ya kipekee katika michuano hiyo.


Ikicheza kwenye Uwanja wa Amaan, Yanga ilipata kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKU ambao walikuwa hawapewi nafasi ya kusonga mbele katika mechi hiyo ya robo fainali ya michuano hiyo.

Lakini pamoja na kipigo hicho, Yanga imeanza rekodi ya kuwa timu ambayo imekuwa na mashabiki wengi katika kila mechi ambapo katika mechi ya jana almanusura fujo zitokee ambapo umati wa watu ulikuwa mkubwa kiasi cha kusababisha baadhi ya mashabiki kukaa katika sehemu ambazo hawakutakiwa kukaa.

Askari polisi walilazimika kuingilia kati mara kadhaa kuwapa maelekezo mashabiki uwanjani hapo ambapo wengi walikuwa wa Yanga, lakini amani ilitawala mwanzo mpaka mwisho wa mchezo huo.

Akizungumzia kupoteza kwa mechi hiyo, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema kuwa walipoteza nafasi nyingi na ndiyo maana walipoteza mchezo huo.“Tunarejea Dar kujipanga kwa ajili ya ligi kuu, tutayafanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwa kuwa bado naamini tuna timu nzuri, washambuliaji wetu (Amissi) Tambwe na (Kpah (Sherman) walikosa nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza, nafikiri wangefanikiwa kuzitumia, tungefuzu,” alisema Cannavaro.

Bao pekee la JKU liliwekwa wavuni na Amour Mohamed Omary katika dakika ya 72 baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya na kushindwa kuondoa mpira katika eneo la hatari.
Na Sweetbert Lukonge, Zanzibar

No comments

Powered by Blogger.