NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 9

ILIPOISHIA:
“Ooh! Ujauzito wa nani?” mzee Sifael alishtuka.
“Wa kwako.”
“Mimi?”
SASA ENDELEA...
“Kwani nani aliyenibaka?”
“Hata kama nilikubaka lakini ujauzito si wangu,” mzee Sifael alijifanya kuruka futi mia.
“Sikiliza baba toka nifike hapa sijawahi kukutana kimwili na mwanaume na wewe ndiye uliyeniingilia mara ya mwisho, kwa hiyo naomba uniambie utanisaidiaje kabla sijamwambia mama?”
“Ha...ha...pana usifanye hivyo.”
“Sasa niambie utanisaidiaje?”
“Mmh! Mbona mtihani mzito.”
“Sasa mimi nifanye nini?”
“Ni kweli ujauzito ni wangu?”
“Wewe unafikiri wa nani?”
“Huna rafiki wa kiume?”
“Sina.”
“Siyo kitu, kesho tutafanya zoezi la kutoa hiyo mimba.”
“Hapana suala la kutoa ujauzito wangu sahau.”
“Una maana gani kusema hivyo?”
“Katika kitu ambacho sitakifanya maishani mwangu ni kutoa mimba.”
“Sasa tutafanyaje? Njia nzuri ni kuitoa tu bila hivyo tutaharibu kila kitu.”
“Tafuta njia yoyote ya kutatua tatizo hili, lakini mimba sitoi hata kwa mtutu.”
“Lakini kwa nini Ester, huoni kama inaweza kuleta tafrani nzito ndani.”
“Najua lakini katu sitatoa mimba,” nilisimamia msimamo wangu.
“Kwa nini Ester hutaki kutoa mimba?”
“Siwezi kupona mara mbili, mara ya kwanza nilichungulia kaburi, nikirudia nitakufa.”
“Nitakupeleka kwa wataalamu.”
“Hata kwa Mungu sikubali.”
“Kwa hiyo tutafanyaje?”
“Tafuta njia yoyote lakini si kutoa.”
“Fanya hivi...hili suala njoo kesho kazini tuzungumze vizuri hapa si pazuri.”
Kabla ya kuingia ndani mzee Sifael alinirudisha nyuma na kuniambia.
“Sikiliza Ester ukiulizwa na mama yako mwambie umepata mchumba Muislam, sawa?”
“Sawa.”
Baada ya kukubaliana tuliingia ndani, walipotuona walisema kwa pamoja.
“Mmh! Mtu na mtoto wake mna siri gani?”
“Siyo lazima kuijua ndiyo maana tumezungumza wawili,” mzee Sifael aliwajibu.
Sikujibu kitu, nilifika na kukaa pembeni ya mama.
Muda wote niliokaa na mama sikuulizwa swali lolote mpaka muda ulipofika wa maombi ili kila mmoja aende chumbani kwake. Kama kawaida baba aliongoza maombi kuonesha kweli roho mtakatifu kamuingia kumbe alikuwa shetani mkubwa. Nilimuona muongo mkubwa aliyenifanya niichukue dini kwa kuamini mashetani kama wale ndiyo wachafuzi wa dini za watu huku wakionekana wapo mbele kumtukuza Bwana kwa midomo yao kumbe wachafu mioyoni.
Tokea nilipobakwa na jinsi tabia ya mzee Sifael aliyokuwa akijionesha mbele za watu, moyo uliniuma na kufikia hata kuiona ibada yote aliyokuwa akiongoza ni ya kinafiki tofauti na mwanzo nilikuwa nikimwamini.
Baada ya maombi ambayo kwa upande wangu niliyaona ya kinafiki tulikwenda kulala, usiku ulikuwa mrefu kwangu niliwaza hiyo kesho angeniambia kitu gani tofauti na utoaji wa ujauzito. Pamoja na kuwa na mawazo mengi usingizi ulinipitia na kushtuliwa alfajiri kwa ajili ya maombi ya asubuhi ya kumshukuru Mungu kutulaza salama pia kumuomba atuvushe siku salama.
Baada ya maombi kabla ya kuondoka baba alimueleza mama:
“Baadaye Ester aje kazini.”
“Saa ngapi?”
“Kuanzia saa tano.”
“Nina imani amekusikia.”
Baada ya kusema vile aliondoka na kuniacha na mama nikifanya usafi na kazi zote muhimu kabla ya kwenda kuonana na baba.
Saa tatu na nusu mama aliniomba nijiandae kwenda kwa baba, baada ya matayarisho yote nilikwenda kazini kwa baba.
Nilipofika hakutaka tuzungumzie pale, alinipeleka kwenye hoteli moja iliyokuwa tulivu na kuagiza vinywaji kabla ya mazungumzo. Siku hiyo alikuwa mpole kupindukia, nami nilikuwa kimya muda wote nimsikie anataka kuniambia nini.
Kabla ya kusema nilishangaa kumuona mzee mzima akitokwa machozi na midomo ikimcheza kuonesha alikuwa na wakati mgumu mbele yangu kitu ambacho sikutaka kukipa nafasi kwa kuamini kosa langu lolote ni kifo changu.
Niliendelea kujiapiza sitakubali hata kwa mtutu wa bunduki kutoa mimba kwa vile yaliyonikuta sitayasahau mpaka naingia kaburini. Baada ya kujifuta machozi aliniita jina langu kwa sauti ya chini.
“E..e..ster.”
“Abee baba.”
“Kwanza samahani.”
“Bila samahani baba.”
“Najua nililolifanya kwa kweli halikukufurahisha.”
“Ni kweli, lakini lilishapita.”
“Bado mwanangu, lililopita lilikuwa dogo lakini hili ni kubwa sana.”
“Sasa tutafanyaje na imeshatokea?”
“Kwa nini hutaki tuitoe hiyo mimba?”
“Baba nimekueleza hata kwa mtutu wa bunduki siitoi.”
“Kwa nini Ester?”
“Nilikueleza niliujaribu mchezo huu mpaka leo nazungumza na wewe ni Mungu tu, nilikuwa nimekwishapelekwa mochwari.”
“Kwa sababu gani?”
Sikutaka kumficha, nilimweleza maisha yangu ya uhusiano na mpenzi wangu wa kwanza mpaka aliponipa ujauzito na kisha kunishauri kama yeye kuutoa ujauzito na matokeo yake. Baada ya kunisikiliza alitulia kwa muda na kushusha pumzi nzito. Alitulia akiangalia juu akigongesha vidole kwenye meno kisha aliniita tena.
“Ester.”
“Abee.”
“Inaonekana mlikwenda kwenye hospitali za uchochoroni.”
“Nimekwambia hivi, hata kama zingekuwa hospitali za barabarani, sikubali yaliyonikuta nayajua, ungekuwa ni wewe ndiye yamekukuta usingethubutu kunishauri nitoe mimba.”
“Sasa ukiulizwa mimba ya nani utasemaje?”
“Ya kwako.”
“Ha!” Alishtuka mpaka akasababisha vinywaji kumwagika.
“Unashtuka nini, unataka niseme ya nani wakati baba wa mtoto ni wewe?”
“Ester, chondechonde, utaharibu sifa yangu kuanzia ndani mpaka kanisani, si unajua kabisa mimi ni kiongozi wa kanisa?”
“Huo uongozi wa kiroho au ushetani?”
“Wa kiroho Ester, nilichokifanya hata mitume waliotangulia wapo waliofanya makosa kama mimi lakini walisamehewa.”
“Hata mimi nilikusamehe, lakini bado roho mchafu yupo ndani yako kwa kutaka kukiua kiumbe kisicho na hatia. Umefanya dhambi ya kuzini, tena kwa kunibaka, dhambi hiyo hujatubu unataka kuua, wewe ni mtu wa aina gani?” nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.
“Unafikiri ukisema hii mimba ni yangu nitaweka wapi sura yangu?”
“Kwani uliponibaka ulitegemea nini?”
“Nikwambie mara ngapi shetani alinipitia?”
“Acha kunichekesha ina maana huyo shetani kazi yake kukupitia wewe tu kila siku?”
“Sijawahi kufanya kitendo kama hiki ndiyo maana nina wasiwasi kuna mkono wa mtu, siwezi kumbaka binti yangu niliyemlea mwenyewe,” mzee Sifael alizungumza akiamini kabisa sijui historia ya uchafu wake wa nyuma.
“Baba unajua unazungumza na mtu mzima, sasa kama nisingemuua mwanangu kutokana na akili za kitoto sasa hivi ningekuwa mama fulani hivyo usizungumze kama unazungumza na mtoto mdogo.”
“Kwa nini?”
“Hii tabia yako ya asili ya kubaka wasichana wanaokaa ndani mwako na kujificha kwenye kivuli cha ucha Mungu kama mzee wa kanisa naijua vizuri.”
“Ester ni maneno gani hayo, mimi nimekuona mtoto kivipi?”
“Unajua najua kila uchafu wako uliosababisha mama akimbie nyumbani, kwa hili ulilonifanyia si geni ni kawaida yako.”
“Estaaa! Nani kakwambia uongo huo?”
“Si kujua nani kaniambia, jua naelewa kila kitu juu ya uchafu chako.”
Kauli yangu ilimfanya aone aibu na kuwa na kazi nzito mbele yangu, niliamini utapeli aliokuwa akiutumia kwa wasichana waliotangulia kwangu ulikuwa umejulikana.
“Ester naomba msaada wako nipo tayari kukupa kiasi chochote cha fedha ili kuficha aibu hii.”
“Naweza kukusaidia kwa njia yoyote tofauti na ya kutoa ujauzito huu.”
“Basi niambie wewe unafikiria nifanye nini ili tuweze kuificha siri hii?”
“Labda niondoke nyumbani.”
“Wakikuuliza unakwenda wapi utajibu nini?”
“Sitawaaga nitaondoka bila kuaga.”
“Utakwenda wapi?”
“Popote ambako ni mbali na hapa ili niweze kujifungua salama na kuanza maisha yangu mapya.”
“Nikikupa milioni moja itatosha?”
“Mmh! Nina imani itatosha,” nilikubali kwa kuamini fedha zile zilikuwa ni nyingi sana.
“Basi kesho nitakupatia ili ukajiandae na safari yako.”
“Sawa.”
“Lakini kesho usiage kama unakuja kwangu.”
“Kwa hilo shaka ondoa.”
Tulikubaliana na siku ya pili nikapewa fedha ili nijiandae kuondoka, niliamini ile ndiyo ingekuwa njia mwafaka ya kuokoa ndoa ya mama Mather ambaye alikuwa bado ana vidonda ambavyo niliamini havitapona kutokana na uchafu wa mumewe ambao umejificha katika kivuli cha kumuabudu Mungu.
Nilijiuliza kama wote wanaojiita wachunga kondoo wa Bwana kama wana tabia za mzee Sifael, hao kondoo zizini watabakia wangapi? Wasiwasi wangu ulikuwa kama kweli mzee Sifael ambaye ana heshima kubwa mbele ya waumini wa kanisa ambao humsalimia kwa kumshika mkono kwa unyenyekevu wakiamini mkono wake una chembe za baraka kutokana na ucha Mungu wake, kama alistahili heshima ile.
Basi, mpaka Kristo atakaporudi zizi litakuwa tupu kwa kondoo wote kugeuzwa mishikaki na wachungaji uchwara wanaomcha Bwana kwa midomo yao lakini mioyo yao imeoza na inanuka huku harufu yake ikiwa haivumiliki.
Nilifikiria jinsi mama Mather alivyompokea Bwana moyoni lakini mumewe ni shetani, machozi yalinitoka bila kizuizi.
Kwa kweli siku ile niliporudi nyumbani sikupenda kuwa karibu na watu zaidi ya kujifungia ndani kujiuliza nimekubali kuondoka nitakwenda wapi? Na huko niendako nani atakuwa mwenyeji wangu.
Siku za nyuma niliwajua wasichana wengi waliokimbilia mjini kutafuta kazi labda wangeweza kunisaidia.
Niliamini kama ningekuwa sina ujauzito ningeweza kwenda mjini kwa tiketi ya kutafuta kazi, Lakini kwenda na ujauzito nilijiuliza nitaishi vipi na hata nikishikwa na uchungu nani atakayenisaidia.
Lakini moyoni niliapa kwamba nikipata fedha nitaondoka tu, nilijua nikiendelea kuwepo pale huenda hali yangu ya ujauzito ingeonekana na kuwafanya wawe na maswali ambayo ningeshindwa kuyajibu.
Nikiwa nimejilaza ndani, niliwaza niende mkoa gani ambao kidogo una unafuu wa maisha, wazo la haraka lilikuwa kwenda Dar es Salaam ambao nilielezwa na watu pamoja na changamoto kubwa lakini una unafuu kubwa ya maisha kama utajishughulisha.
Nami niliamini kutokana na fedha nitakayokuwa nayo basi niwe mjasiriamali kama marehemu mama alivyokuwa akifanya katika kuyaendesha maisha yake.
Niliamini kwa muda ambao ujauzito wangu unakuwa, nami nitakuwa tayari nimeishapata mwanga wa kufanya shughuli yoyote. Swali likabaki nitaondokaje na nguo zangu lazima nitaulizwa na nyumba haikuwa na mlango mwingine ambao ningeweza kuutumia kutoka ndani bila kuonekana.
Sikujua nitafanyaje lakini nilipanga kuondoka siku ya pili yake pale nitakapokwenda kuchukua fedha. Sikutaka kurudi tena nyumbani kuogopa kupata wakati mgumu wa kutoroka.
Lakini sikutaka kuumiza kichwa, nilipanga akirudi baba nimweleze na yeye atajua atanisaidia vipi.
Kwa vile nilikaa ndani kwa muda mrefu, nilitoka na kukaa na mama ambaye muda mwingi alikuwa peke yake akisoma Biblia.
Niliposogea karibu yake alinitazama, nilijikuta nikikwepesha macho yangu, hakuendelea kunitazama badala yake aliendelea kusoma Biblia yake. Hakusoma sana aliiweka pembeni na kunigeukia.
“Ester,” aliniita.
“Abee mama.”
“Una tatizo gani mwanangu?” aliniuliza huku akinitazama usoni.
“Mimi?” Swali lile lilinishtua kwa vile sikulitegemea.
“Ester, kwani swali hili nimemuuliza nani?”
“Mimi.”
“Hebu nieleze una tatizo gani?”
“Sina tatizo,” nilikataa kwa kuamini hajui lolote juu ya ujauzito wangu, labda kitu kingine.
“Ester mwanangu una tatizo, mimi ndiye mama yako japo sijakuzaa lakini sasa hivi ni zaidi ya mama yako naomba unieleze usinifiche kitu, una tatizo gani linalokusumbua?”
“Mama mbona mimi nipo sawa,” nilijitetea.
“Hapana, mi mtu mzima nina uzoefu wa kumjua vizuri mtu, si wewe Ester ambaye mwanzo alikuwa Salha ninayemjua, kuna mabadiliko makubwa sana hasa toka siku ile iliyoweweseka usiku.”
“Mama nipo sawa ni wasiwasi wako tu.”
“Si kweli, unaonesha kila siku ukiilazimisha furaha usoni mwako lakini kuna kitu kizito moyoni mwako. Hata ndugu zako wameishaniuliza una tatizo gani, lakini sikutaka kukuuliza haraka, nilijitahidi kuona labda utabadilika lakini tangu jana kuna kitu kingine kimetokea hata ule uchangamfu wako umepotea.
“Umekuwa mwenye mawazo kila unapokuwa peke yako, unakuwa unahama kabisa kimawazo na kubakia mwili tu lakini wewe haupo sawa kabisa. Nakuomba mwanangu nieleze tatizo lako ni nini? Basi mweleze hata baba yako kama unaona huwezi kuniambia mimi.”
TUKUTANEKESHO
Post a Comment