NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 7

ILIPOISHIA...
Wakati akimwita nilijiuliza nitawaeleza kitu gani ambacho watanielewa, kusema nimebakwa na baba mbele ya mama na dada Mather niliona aibu, pia niliamini kauli yangu ingekuwa sawa na upanga mkali ambao ungetenganisha nyumba ya mzee Sifael iliyodumu kwa zaidi ya miaka 30.
SASA ENDELEA...
Wakati huo nilisikia sauti za nyayo kuonesha kuna zaidi ya mtu mmoja waliokuwa wakija chumbani kwangu. Dada Mather aliwahi kuchukua upande wa kitenge na kunifunga. Ajabu katika watu waliokuja alikuwepo na baba mzee Sifael.
“Vipi Ester?” mzee Sifael alikuwa wa kwanza kuuliza.
Kauli ile ilinishtua na kujiuliza, anachouliza mzee Sifael ni kweli hakijui au ndiyo kujifanya mwema mbele ya watu? Nilijikuta nikiangua kilio nilivyofikiria ninavyoonewa bila kosa na mfanya kosa ndiye anajifanya mwema mbele ya watu.
“Ester umekuwaje mwanangu?” mama Mather aliniuliza akiwa amenikumbatia.
Nilishindwa kusema kwa kukumbuka kauli ya mzee Sifael kuwa kama nitasema ukweli nitaweza kuivunja ndoa yake iliyodumu zaidi ya miaka 30.
Nilijiuliza nitawaeleza kipi kinaniliza ambacho kilisababisha nivimbe macho, hivyo kuwa mekundu.
Ghafla mama Mather alianza kukemea kilichonisibu bila kupata jibu nalilia nini.
“Ewe baba wa mbingu na nchi kwa nini unampa mamlaka shetani kuichezea nyumba yangu? Naamini shetani hana mamlaka kwako naomba umtokomeze kwa jina la Yesu Kristo aliye hai. Ondoa pepo mchafu moyoni mwa Esther, muondolee mateso ya moyo.
“Ni wewe uliyetueleza tukikutegemea hakuna kitakachoshindikana, hakuna zaidi chini na jua ila wewe Mungu wa kweli.
Vunja nguvu za shetani ziteketeze kwa moto, zisionekane tena kwa jina la mwanao Yesu Kristo, shetani ameshindwa, toka... toka pepo mchafu... toka ndani ya moyo wa Ester toka ndani ya nyumba yetu...” mzee Sifael aliomba.
Ilikuwa ajabu katika maombi yale, baba mwenye nyumba ndiye aliyekuwa akitoa sauti ya juu kuliko wote mpaka jasho likamtoka. Nilijiuliza yale maneno aliyokuwa akiyatoa mzee Sifael alikuwa akimwambia Mungu gani na alitaka shetani gani atoke moyoni mwangu na ndani ya nyumba.
Niliamini basi shetani namba moja ni yeye aliyetakiwa kutoka ndani ya nyumba ya mama Mather aliyekuwa akimjua Mungu wa kweli na uzima. Baada ya maombi ambayo yalifanywa chumbani kwangu kwa wote kushirikiana kumfukuza pepo mchafu, huruma iliniingia nilipowaangalia mama na ndugu zangu Mather na Joyce ambao waliomba mpaka machozi yakawatoka.
Moyoni nilisema sitasema kilichonitokea mpaka naondoka mule ndani kwa kuamini kabisa mimi nilikuwa mpitaji tu, nilikuta upendo ndani ya nyumba hiyo hivyo lazima niuache!
Kauli yangu ya kweli ingekuwa sawa na moto kwenye kijiti kuutupa kwenye tenki la mafuta, niliamua kuzua uongo ambao nilijua itaonekana imani yangu ni finyu kwa kumpokea Yesu nusu na si kamili kwa kumtanguliza mbele kwa kila kitu.
Baada ya maombi ya zaidi ya nusu saa mama Mather aliniita kwa sauti ya chini huku akijifuta jasho kwa upande wa kanga...
“Ester.”
“Abee mama,” niliitika kwa sauti ya chini.
“Hebu nieleze nini tatizo?”
“Jana nimeota ndoto mbaya sana, mama yangu yupo kwenye mateso mazito kutokana na baba kunifukuza nyumbani. Inaonesha toka nilipofukuzwa, mama yangu kuzimu analia tu, amedhoofu kwa kitendo cha baba kumgeuka baada ya kufa.”
“Ooh! Kumbe ni hivyo, inabidi tufanye maombi kwa roho zote zilizo kuzimu.”
Tulifanya maombi ya kumuombea mama yangu kisha nilikwenda kuoga na kufanya maombi ya pamoja kabla ya wote kuondoka kwenda kazini na shuleni.
Mather kabla ya kuondoka alinifuata na kunieleza:
“Mdogo wangu najua umekuwa huna kazi za kukufanya uwaze maisha mengine kwani kila siku ukiwa ndani hakukupanui mawazo. Nakuhakikishia kukutafutia kazi ya kukuweka busy hata ukirudi nyumbani uwe umechoka.”
“Sawa dada nitashukuru.”
“Basi mdogo wangu, Bwana akutangulie kwa kila jambo, unapenda jioni nikuletee nini?”
“Chochote dada.”
“Nitakuletea baga.”
“Na nini?”
“Soda ya kopo.”
“Hapo umelenga.”
“Dada Ester tutaonana jioni,” Joyce naye aliniaga.
Mzee Sifael alionekana kuhitaji sana kuzungumza na mimi, nikajitahidi kumkwepa lakini hakuvumilia, aliniita na kunisogeza pembeni.
Sikuweza kuonesha mabadiliko yoyote kwa vile nilikwishaapia moyoni mwangu kuwa sitasema kwa mtu yeyote kitendo cha kinyama alichonifanyia mzee huyo.
Nilipofika pembeni nilijikuta nasahau maumivu yangu na kumuonea huruma mzee wa watu kwa jinsi alivyokuwa akikosa raha kama mgonjwa. Kabla ya kusema alichoniitia alinitazama, ghafla machozi yalimtoka, alitoa kitambaa mfukoni na kujifuta. Nilijiuliza anataka kuniambia nini, lakini sikujua.
“Ester mama...” aliniita.
“Abee baba,” nikaitika nikimwangalia machoni.
“Najua nimekukosea sana, najutia moyo wangu kwa kitendo cha kishetani nilichokutendea,” alisema. Sikumjibu kitu, nilimuangalia tu akiendelea kufuta machozi yaliyokosa kuzuizi na kuvuta kamasi nyepesi.
“Nashukuru kwa kuokoa ndoa yangu, nakuahidi sitarudia tena na Mungu shahidi yangu, kama nitafanya hivyo tena basi achukue uhai wangu. Ester nakuahidi kukupatia kitu chochote utakachokitaka ili kurudisha furaha yako.”
“Baba usinipe chochote, nimekusamehe kwani tumefundishwa kusamehe.”
“Asante mwanangu, utakunywa soda,” alitoa noti za elfu kumi ambazo sikujua ni kiasi gani, lakini sikuzipokea.
“Baba soda zipo ndani.”
“Basi chukua tu kwa matumizi mengine.”
“Baba si nimekusamehe, mbona unatafuta mengine?” nilijikuta nakuwa mkali kidogo.
Kauli yangu ilimfanya aniage na kuondoka, baada ya kuondoka nilirudi ndani kwani bado kichwa kilikuwa kikiniuma kwa mbali, nilimeza dawa na kujilaza kitandani. Kwa kweli siku ile kazi zote za ndani alifanya mama Martha peke yake.
Pamoja na mwili kuchoka sana na maumivu kutokana na kutolala na kuingiliwa kwa nguvu, sikulala muda mrefu, niliamka kumsaidia kazi mama japo alinitaka nipumzike. Niliamini kumuachia kazi zile ni kumhukumu kwa kosa lisilokuwa lake.
Nilimweleza nipo sawa hivyo naweza kufanya kazi zangu bila tatizo, pamoja na kunikubalia lakini kazi nyingine alizifanya yeye. Nikiwa nafanya usafi wa vyombo, nilijiuliza wanaume wana matatizo gani kwani huonesha huruma ya mamba anayokuonesha ukiwa nje ya mto lakini ukiingia ndani ya maji anakugeuza kitoweo.
Tukiwa jikoni tunapika, mimi nikiwa nakaanga mboga ya mchuzi huku mama akichambua mboga za majani, mama alitoa kauli ambayo ilinishtua sana, ilibaki kidogo sufuria la mchuzi linibinukie. Alisema kwa sauti ya kawaida lakini maneno kwangu yalikuwa makali moyoni mwangu.
“Unajua nini?” alivyosema vile kulinifanya nigeuke nimtazame bila kusema kitu.
“Yaani asubuhi Martha aliponiita nilijua labda umebakwa.”
“Nimebakwa?” Kauli ile ilinishtua.
“Eeh.”
“Na nani?”
“Na baba yako.”
“Mamaa maneno gani hayo?” nilizidi kushangaa moyoni na kukataa mdomoni.
“Unajua mwanangu, wewe umeshakuwa msichana mkubwa ambaye unaweza kubeba ujauzito, uongo?”
“Kweli.”
“Hapa kwangu nilikataa kuwa na wafanyakazi wa ndani kabisa, hata ndugu zangu wa kike siku za nyuma sikutaka walale hapa wakija kunitembelea.”
“Kwa nini mama?” nilimuuliza huku nikiacha kukaanga nisije kuingiza mkono.
“Unajua baba yenu siku za nyuma alikuwa mlevi na mzinzi sana, tabia yake ilikuwa kutembea na wasichana wa kazi. Nimemfumania zaidi ya mara mbili, kutokana na kauli zao, huanza kwa kuwabaka na kuwatishia kuwafukuza kazi, wakikaa kimya anawageuza mke wa pili.”
“Mmh!” niliguna.
“Usigune mwanangu, hata ndugu zangu wasio wastaarabu alitembea nao, kwa kweli nilikuwa kwenye wakati mgumu sana. Lakini Yesu siku zote aliniongoza na kunitia moyo, lakini yalipozidi nilirudi kwetu ambako nilikaa mwaka mzima, kila alipokuja kuniomba msamaha nilikataa. Kupitia wazee wa kanisa niliweza kumkubalia kurudi kwa angalizo kuwa siku akirudia basi ndiyo siku ya kuachana kabisa.
“Na kuanzia siku hiyo sikutaka msichana wa kazi, hata ndugu zangu wote wa kike walikuja na kuondoka, sikukubali walale. Lakini taratibu naye alimrudia Yesu japo sina uhakika sana, lakini tabia zake za kuacha pombe na kuwahi nyumbani vilinifanya niamini kweli ni kiumbe kipya.
Lakini leo nilipoitwa nilikumbuka alivyombaka mfanyakazi mmoja aliyekuwa bado msichana, akiwa hajakutana kimwili na mwanaume. Huwezi kuamini, pamoja na kosa la mume wangu, tulishirikiana kulimaliza kwa kutoa fedha ili liishie ndani kwani kwa tendo lile baba yako angefia gerezani. Basi leo ilikuwa hivyohivyo, nilipokuja nilikuwa nimejiandaa kuondoka, wala asingeniona labda maiti yangu.”
Mmh! Yalikuwa maneno mazito yaliyonisisimua sana, nikamshukuru Mungu kuificha siri ile. Japokuwa iliniumiza, niliamini ilileta amani ndani ya familia ile kwani kama ningesema kilichotokea, kauli yangu ingekuwa sawa na kijiti cha moto ambacho kingetua ndani ya tenki la mafuta na kuisambaratisha familia.
Lakini nilijiuliza kama ndiyo tabia yake ya mtu akinyamaza anamgeuza mke mdogo na kwangu angefanya hivyo?
NIKIWA katikati ya mawazo mama alinishtua kwa mazungumzo yake...
“Usinione hivi nilikuwa mnene, si unaona picha zangu za sebuleni? Vituko vya baba yenu vimeumaliza mwili wangu, nilikuwa mtu wa kulia kabla ya kupelekwa kwa Yesu aliyegeuka kuwa mfariji wangu. Nilikonda kama mgonjwa wa kifua kikuu, wengi walijua nitakufa wakati wowote,” mama alisema.
Kwa kauli ile ilionesha jinsi gani mama Mather alivyomvumilia mumewe kwa matendo machafu na kufikia kipindi cha kusema liwalo na liwe. Siku iliisha vizuri huku nikielewa nini kilisababisha awe vile.
Kwa kauli ya mama Mather ilionesha kumbe tabia ya mzee Sifael ya kuwabaka wanawake ilikuwa ya asili, moyoni niliapa kutorudia tendo lile hata kama ataniahidi kunipitia kitu cha thamani! Moyoni nilimsamehe na kuamini kujutia makosa yake mpaka machozi kumtoka mtu mzima, ilionesha jinsi alivyoumizwa na vitendo vyake viovu.
Kilichoniumiza ni alivyokuwa akiongoza sala ya asubuhi kwa kumtaja Mungu kinafiki huku kila mmoja aliyekuwepo pale akiamini kabisa mzee Sifael alikuwa msafi mbele ya Mungu, mtu aliyeokoka, kumbe bado ni makazi ya shetani kwa kushindwa kuzuia tamaa za mwili.
Niliamini tabia ile kama aliifanya ndani akijua kosa lile linaweza kuivunja ndoa yake, basi nje ilikuwa ndiyo imeota mizizi.
Baada ya kuandaa chakula, nilimuaga mama na kwenda chumbani kwangu kupumzika ili nipate muda wa kuwaza yote niliyoelezwa na mama Mather.
Muda wote mama alinionea huruma kutokana na hali yangu, baada ya kufanya kila kitu cha muhimu nilimuacha akijiandaa kusoma Biblia yake ambayo alipokuwa peke yake alipenda kusoma.
Baada ya kuachana naye niliingia chumbani kwangu na kujilaza kitandani na kuanza kurudisha kumbukumbu zangu nyuma.
Sikuanza kubakwa usiku ule, ni tangu mkasa wangu wa kukataliwa na baba na kuhukumiwa kwa kosa ambalo sikulifanya. Baada ya kutoka kwa baba nikaja kwa Samweli, mvulana aliyenipa mimba na kunitupa akiamini nimekufa!
Mwisho nilimalizia kukumbuka nilivyobakwa usiku na mzee Sifael, mtu niliyemheshimu na kuamini ndiye mkombozi wa maisha yangu.
Tabia yake ya kutembea na wanawake mchanganyiko, tena bila kinga wakiwemo ndugu wa damu wa mkewe na kuwabaka wasichana wa kazi, ilinikera sana.
Ilionesha kabisa alitumia fedha zake kuwanyamazisha wote aliowabaka wa nje ya familia na hata wale tulioishi nao pale nyumbani.
Nilijikuta nikifuta heshima yake kanisani kama mmoja wa wazee wa Kanisa wenye heshima kubwa waliokuwa wakitegemewa kuliongoza Kanisa. Nilijiuliza kama mzee wa Kanisa ana tabia mbaya kama ile waumini wa kawaida watakuwa katika hali gani.
Niliwachukia wazee wote wa Kanisa, nikihisi wote wana tabia kama ya mzee Sifael. Kwa upande mwingine sikutakiwa kumhukumu mtu kwa kosa la mwingine. Wazo lililokuja haraka akilini mwangu ni kuamini uamuzi wangu wa kubadili dini haukuwa sahihi kwa kuamini hakuna mtu mwenye uhakika wa kuingia peponi hasa ukizingatia nguvu za shetani ni kubwa kwa watu wenye mioyo dhaifu kama mzee Sifael.
Nilijiuliza, ingekuwaje kama ningewaeleza nimeamua kurudi kwenye dini yangu ya zamani ya uislamu, lakini pia sikuelewa wangenichukulia vipi.
Niliamini kama ningetaka kufanya uamuzi mzito kama ule ambao hakuna ambaye angeupenda, kungenijengea chuki japokuwa wasingejua sababu ya mimi kurudi kwenye dini yangu.
Ukweli ni kwamba, sababu hasa ni baada ya mtu niliyemheshimu tena mwenye sifa kubwa kanisani kunifanyia kitendo cha kinyama kama kile.
Jambo kama lile sikutakiwa kukurupuka, nilitakiwa kujipanga ili likikamilika niondoke bila kuaga. Wasingejua nitakapoelekea, nilipanga kuwaachia ujumbe wa kuwashukuru na kuwaomba wasinitafute kwa kuamini ni kiumbe ninayelazimisha maisha mazuri wakati maisha yangu ni ya tabu na mateso.
Pamoja na kupata wakati mgumu juu ya uamuzi mzito niliotaka kuuchukua, niliamini ule ndiyo ufumbuzi wa kuiokoa ile ndoa baada ya kupata maelezo ya mama Mather kuwa msichana akibakwa na kukaa kimya, basi lazima angegeuzwa nyumba ndogo.
Mwisho wa yote ni kuvunja ndoa ya watu ambayo ilionekana imeshikwa na uzi wa buibui iliyosubiri wa kuigusa ipatikane sababu na kulaaniwa na mama mtu mzima aliyeniamini kama binti mwenye heshima.
Ingekuwa aibu sana kwa namna ambavyo ananichukulia, kusikia natembea na mume wake, tena siku aliyosikia nikipiga kelele nilikuwa naye chumbani.
Nilijiuliza nitaweka wapi uso wangu, japo sikutakiwa kufunua kombe kabla mwana haramu hajapita! Nilijikuta nipo njia panda!
Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya kesho.
Post a Comment