NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 5

ILIPOISHIA:
Jioni bibi alizikwa kwa sheria ya dini ya Kiislamu mimi sikwenda makaburini lakini niliambiwa siku ya pili ningepelekwa kuzuru kaburi lake.
Nilijikuta nikijawa na mawazo yasiyo na mfano juu ya matukio ya kukatisha tamaa ya maisha yangu, nikajiuliza nitawezaje kuishi peke yangu!
Nilishukuru mama Solomoni ambaye ni jirani yetu alisema angenichukua na kuishi na mimi.
SASA ENDELEA...
Niliyaanza maisha mapya kwa mama Solomoni, japo akili yangu ilikuwa mbali sana kwa kutafuta njia ya mkato ya kuondoka duniani.
Lakini mama Solomoni aliyekuwa akijua matatizo yangu kwa muda mrefu alikuwa karibu nami kwa kunifariji.
Alinionesha mapenzi makubwa kuzidi hata watoto wake wa kuwazaa, nilitakiwa kupumzika kwa kipindi kile cha majonzi ya kifo cha bibi, alitumia muda mwingi kunisahaulisha kwa kunihadithia vitu ambavyo vilinifanya nicheke.
Lakini hali ya kuzama katika dimbwi la mawazo ilikuwa ikinijia kila nilipokuwa peke yangu huku nikiwaza kwa nini nisijiue ili niepukane na tabu za dunia.
Nakumbuka siku moja nikiwa peke yangu baada ya wenzangu wote kwenda shule, nilionesha uchangamfu na kuonekana nimekubaliana na hali halisi ya mambo yote yaliyotokea.
Nilifanya kazi za nyumbani, wakati nikiosha vyombo wazo baya liliniingia kwani siku zote shetani hupenyeza ushawishi wake mbaya pale penye tatizo.
Nilipata wazo la kujiua, niliviacha vyombo nje na kuingia ndani kutafuta fedha kwa ajili ya kununulia sumu ya panya ili ninywe na kuondokana na adha za dunia.
Nilitafuta fedha sehemu zote hadi chumbani kwa mama Solomoni. Niliamini nikinywa sumu muda ule mpaka watakaporudi wangenikuta nimeshakuwa maiti.
Lakini kila kona ya nyumba sikuona hata senti tano, nilikumbuka ugumu wa maisha ya kijijini, fedha zilikuwa ni vigumu kupatikana na mtu akiipata anatembea nayo kwenye pindo la khanga yake.
Baada ya kutafuta kwa muda mrefu bila mafanikio, wakati nikitoka ndani nilipata wazo la kutumia njia nyingine ya kujiua kwa kujinyonga kwa kamba.
Japo nilikuwa mwoga kutumia njia hiyo kwa kuamini kuwa kifo chake kina mateso makubwa hasa kwa mtu kutokwa na kinyesi, ulimi kuwa nje na macho kutoka kama ngumi.
Nilichukua muda mrefu kuufikiria uamuzi huo mzito wa kujiua kwa kamba.
Niliichukua kamba na kwenda hadi chumbani ambako nilichukua meza na kupanda juu na kuifunga kamba vizuri kwenye kenchi za miti.
Ilinichukuwa muda mrefu kutengeneza kitanzi kutokana na uzoefu wangu mdogo wa kufanya jambo hilo.
Baada ya kufanikiwa kutengeneza kitanzi nilikipimisha shingoni kwanza kabla ya kukivaa. Kisha nilishuka chini na kukiangalia huku roho yangu ikisita kuchua uamuzi huo.
Kuna sauti iliniambia nijiue na nyingine ilinizuia na kuniambia kufanya kitendo hicho ni dhambi kubwa.
Niliyakumbuka maneno ya bibi kuwa mtu akijiua maisha yake yote huwa ni motoni.
Kutokana na mateso yale niliamini kabisa motoni ndiyo sehemu inayonifaa zaidi kuliko peponi.
Nilijiuliza kama kweli Mungu anayaona mateso yangu ananipa msaada gani katika maisha yangu au ndiyo hivyo vitisho wa kuishi motoni milele.
Nilijiuliza maisha ninayoishi kama yana tofauti na hayo ya motoni.
Roho mbaya ilichukua nafasi kubwa katika nafsi yangu kwa kunitaka nitekeleze uamuzi ule wa kujinyonga.
Nilipanda juu ya meza huku nikitetemeka na haja ndogo ikianza kunitoka, bado nilikuwa na ujasiri wa kutimiza kile nilichodhamiria, nilikishika kitanzi ili nikivae tayari kwa kujinyonga.
Nilishtuliwa na sauti ya mama Solomoni aliyekuwa nje akiniita huku akija kwenye chumba nilichokuwemo.
“Wee Salha uko wapi? Mbona umeacha vyombo nje vikichezewa na bata?”
Nilibakia nikijiuliza nijinyonge haraka au niache kwa kuwa kuhofia kuwa ataniwahi, pia nilipata wazo la kujificha uvunguni kwa kuamini kuwa akinitafuta na kunikosa angetoka nami kuendelea na zoezi langu.
Hilo nililiona ni wazo la kitoto kwani kama angeingia ndani na kukuta meza na kamba jinsi vilivyotengenezwa na kitanzi angejua kitu gani kilikuwa kikitaka kufanyika.
Kabla sijapata jibu la maswali yangu, mlango wa chumbani ulifunguliwa na mama Solomoni aliingia. Alishtuka kuniona nikiwa juu ya meza nimeshikilia kamba.
“Wee Salha unataka kufanya nini?”
Sikumjibu niling’aa macho kama mwanga aliyekamatwa akiwanga mchana, alinifuata na kunibeba kutoka juu ya meza na kuniteremsha chini.
“Salha mwanangu unataka kufanya nini?” Sikumjibu niliendelea kuporomosha mvua ya machozi.
“Kwa nini umekuwa na mawazo mabaya kama hayo, kwa nini unampa nafasi shetani mwanangu?” Bado nilibakia kimya huku nikijilaumu kwa kuchelewa kuchukua uamuzi wa haraka.
“Najua upo katika hali gani, lakini bado hutakiwi kumpa nafasi shetani, usimkumbatie kwani ni kiumbe kibaya sana ambaye huwa rafiki yako kabla ya kutenda, lakini ukishatenda hukuacha peke yako.”
“Nisamehe mama,” nilijikuta nikijiona mkosefu mkubwa.
“Siwezi kukuchukia hata siku moja, kuna jambo lolote baya tulilokutendea hapa nyumbani?”
“Hakuna.”
“Niambie mwanangu, kama kuna jambo lolote baya tuliokutendea au ndugu zako wamekufanya nini?”
“Hakuna kitu mama.”
“Sasa si tulishazungumza na kuelewana? Nini tena kimekukumba?”
“Nilikuwa nataka kuosha vyombo, nilikashangaa wazo la kujiua likiniijia, ndipo nilipoingia ndani nitafute fedha, nikanunue sumu ya panya ninywe. Bahati nzuri sikuiona, nikapata wazo lingine la kujiua kwa kamba, ndipo nilipotafuta na kuifunga.”
“Naelewa kichwani mwako pepo mchafu wa kifo bado anakusumbua, unatakiwa maombi. Sijajua kwenye dini yenu mnafanya nini lakini kwenye dini yetu unaombewa na pepo mchafu wa kifo anakutoka.”
“Niliwahi kusikia mtu mwenye matatizo anasomewa dua, yanaisha.”
“Lakini mwanangu pale kanisani kwetu nimewaona hata waislamu wakija kuombewa bila kuhama dini zao.”
“Basi nipeleke maana nina imani ninapoelekea ni kubaya zaidi, leo umeniwahi kesho nitafanya kitu kingine.”
Tulikubaliana jioni ya siku ile nipelekwe kanisani nikaombewe, jioni ilipofika nilifika kanisani kuombewa. Watu walikuwa wengi sana walipita mbele kwa ajili ya kuombewa matatizo yao. Mchungaji alizungumza maneno mengi kabla ya kuanza kumpitia mmoja mmoja na kumshika kwenye paji la uso huku akikemea mapepo. Kila aliyeshikwa alianguka kwa nyuma na kudakwa na wasaidizi wake mchungaji au yule ambaye pepo alikuwa mgumu kutoka alimkemea kwa sauti ya juu mpaka lilipotoka na kutulia chini baada ya muda alisimama akiwa mzima.
Katika watu waliotoka mbele, kama sikosei nilikuwa mtu wa kumi na aliponifikia alisema kwa sauti ya juu akiwa amenishika kwenye paji la uso:
“Kwa jina la Yesu, pepo mchafu ondoka ndani ya mwili wa binti huyu, mwache huru, mwache huru, toka, toka, tokaaaa.”
Baada ya kusema vile, nilijisikia kama nimepigwa shoti ya umeme na kuangukia kwa nyuma ambako kulikuwa na watu walionidaka. Nililazwa chini nikiwa sijifahamu. Baada ya muda nilinyanyuka na kuruhusiwa kwenda kukaa. Usiku mama Solomoni alinieleza:
“Sasa mwanangu umekuwa kiumbe kipya.”
“Nashukuru sana mama kwa msaada wako mkubwa.”
“Najua ulikuwa katika wakati gani, siku zote mwanadamu aliyevamiwa na shetani huwa na kiza kizito mbele yake hata ayafanyayo huwa mabaya kwa vile hajui akifanyacho kutokana na kiza kilicho mbele yake.”
“Ni kweli huwezi kuamini, sasa hivi moyo na mwili wangu umekuwa mwepesi, siwazi tena vitu vibaya zaidi ya kuyatamani maisha ambayo kwa kweli sasa ndiyo nayaona matamu.”
Baada ya mazungumzo tulikwenda kulala kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Asubuhi ya siku ya pili ilikuwa mpya kwangu kwani kila dakika niliyokuwa peke yangu, nilitubu makosa yangu kwa Mungu kwa kuamini nilichotaka kukifanya hakikuwa sahihi.
Tokea siku hiyo, nilijikuta nami nampokea Yesu taratibu, japo si kwa asilimia kubwa kutokana na dini yangu ya kuzaliwa ya uislamu, kanisani sikwenda, lakini sala za nyumbani nilishiriki ikiwemo kusali kwa kupiga magoti. Siku zilikatika, afya yangu iliimarika siku hadi siku.
Katika maisha yangu sitamsahau mama Solomoni kwa kunipa mapenzi ambayo yalinihamisha katika mawazo mabaya na kujiona nimezaliwa upya. Japo maisha yake yalikuwa ya kawaida, lakini upendo ulitawala ndani ya nyumba yake huku wanaye wakiniona kama ndugu yao wa kuzaliwa. Baada ya miezi saba kukatika nikiwa kwa mama Solomoni. Siku moja walikuja wageni ambao walikuwa ndugu wa mama Solomoni wanaokaa mjini.
Katika kuwaandalia chakula na vinywaji, ndugu yake alinishangaa kwa heshima niliyoionesha muda wote toka walipofika mpaka muda ule. Nilimsikia yule mama akiuliza kwa kilugha:
“Mama Solomoni, huyu mtoto mwenye heshima umemtoa wapi?”
“Ni habari ndefu.”
“Ya nini?”
“Salha,” mama Solomoni aliniita.
“Abee mama,” niliitikia kwa unyenyekevu.
“Hebu kamalizie vile vyombo naona ndugu zako wanafanya mchezo.”
“Hakuna tatizo.”
Nilijibu huku nikitoka nje, wakati natoka nilimsikia akisema kwa kilugha kwa kuamini siijui kwa vile hakuwahi kunisikia nazungumza toka nitoke mjini.
“Nimemtoa kijanja ili tuzungumze sipendi asikie kwani nitamtonesha kidonda ambacho naamini kimepona.”
Sikutaka kusimama kwa kuamini japo nataka kuzungumziwa mimi, lakini yalikuwa hayanihusu. Nilipofika nje, kweli niliwakuta akina Rose wanapiga stori wamesahau kuosha vyombo.
“Jamani mama kanituma niwasaidie kumaliza kuosha vyombo.”
Nami sikutaka kuosha kwa haraka, niliosha taratibu ili kuvuta muda wa mazungumzo ya ndani. Hata baada ya kumaliza kuosha, sikuingia ndani kusubiri niitwe. Baada ya nusu saa nikiwa nimekaa chini ya mti, niliitwa ndani.
“Da Salha unaitwa ndani na mama.”
Bila kujibu nilinyanyuka na kuingia ndani na kumkuta mama amekaa karibu na mama mkubwa. Waliponiona naingia, wote waligeuza sura na kuniangalia
Salha ameitiwa nini? Ili kujua, usikose siku ya kesho
Post a Comment