NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 4

“Hata najua! Kwani nani alinileta hapa?”
“Polisi wa doria.”
“Mungu wangu! Walinikuta wapi?”
“Kwa maelezo yao wakati wanapita waliuona mwili wako ukiwa umelala pembeni mwa barabara huku ukinyeshewa na mvua. Wao walijua umefariki.
Sasa endelea...
walikuchukua mpaka hapa na kutaka upelekwe mochwari lakini mganga mkuu alikataa na kusema huwezi kupelekwa chumba cha maiti bila kufanyiwa uchunguzi.
Ndipo ilipogundulika kuwa hujafa bali umepoteza fahamu.”
“Mungu wangu!” nilishika mdomo baada ya kusikia habari hiyo mbaya.
“Mdogo wangu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa mwili wako tulikutana na michirizi ya damu sehemu za siri, tulipoichunguza ilionesha umetolewa mimba vibaya.”
“Jamani, mbona niliambiwa kutoa ni rahisi?”
“Sasa mdogo wangu nina imani baada ya kupata ufahamu unatakiwa kupata kifungua kinywa nimekununulia maziwa na chapati.”
“Nashukuru dada.”
Nilipatiwa maziwa na chapati, kwa kweli nilimshukuru sana yule dada kwa roho yake ya kibinaadamu. Wakati napata kifungua kinywa aliingia askari mmoja mwenye nyota moja na kukaa pembeni ya kitanda changu.
“Hujambo binti?”
“Sijambo, shikamoo.”
“Marahaba na pole sana.”
“Asante.”
“Maliza kula tuzungumze.”
Nilipomaliza, nilisogea karibu yake, ajabu sikuwa na maumivu ya tumbo kama niliyokuwa nayo baada ya kutoka kwenye ule mtaro na kunisababishia kushindwa kusimama.
Baada ya kuniacha nitulie kwa muda yule askari alianza kwa kuniuliza jina langu.
“Unaitwa nani binti?”
“Salha.”
“Salha nani?”
“Sina baba.”
“Mama?”
“Pia sina.”
“Unaishi na nani?”
“Bibi.”
“Unaishi sehemu gani?”
“Kijijini.”
“Umefikaje huku?”
Nilimweleza jinsi nilivyopata mimba na kuletwa mjini na mpenzi wangu kwa ajili ya kuitoa.
“Mpenzi wako anaitwa nani?”
“Samweli.”
“Anaishi wapi?”
“Kijijini.”
“Anajishughulisha na nini?”
“Anauza chipsi.”
“Hiyo sehemu uliyopelekwa kutoa mimba unaijua?”
“Naikumbuka sehemu yenyewe lakini nyumba ipo ndani kidogo sijui kama nitaikumbuka.”
“Unaweza kwenda kutuonesha?”
“Nitajitahidi.”
Baada ya kusema vile yule askari alinyanyuka na kutoka nje, baada ya muda alirudi na daktari.
“Hujambo binti?”
“Sijambo, shikamoo.”
“Marhaba, unaendeleaje?”
“Sijambo kiasi.”
“Unaweza kutembea?”
“Nitajaribu.”
Nilinyanyuka kitandani na kujaribu kutembea niliweza, nilipewa nguo za kuvaa, zilikuwa hazitamaniki kwa tope na damu. Tulitoka hadi nje ya hospitali, nikatambua kumbe nilikuwa hospitali ya mkoa, niliingizwa kwenye gari na kuwapeleka sehemu niliyonyofolewa ujauzito wangu.
Nilijitahidi kuikumbuka njia tuliyopita ili niweze kufika katika ile nyumba bila kupotea.
Tulipofika tulikuta nyumba imefungwa, lakini askari walikwenda kwa mjumbe na kuuliza ni shughuli gani zilifanyika pale.
“Kwa kweli mimi najua nyumba ya mtu, sijui kazi nyingine.”
“Kama hujui tunaomba kuingia ndani kwa kuvunja mlango na wewe ukiwepo.”
Baada ya kuvunja niliwaelekeza hadi katika chumba nilichoingia, tulikuta kuna vifaa vya hospitali vya kutolea mimba na baadhi ya dawa.
Vitu vyote vilichukuliwa na mimi kurudishwa hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi ikiwemo kusafishwa uchafu baada ya kutolewa ujauzito vibaya.
Siku ya tatu nilitolewa hospitali na kupelekwa kijijini pamoja na askari ambao walimfuata mpenzi wangu aliyekuwa akikabiliwa na kosa la kinyama la kukusudia kuua akisaidiana na mganga aliyenitoa ujauzito wangu.
Tulipofika kijijini niliwapeleka moja kwa moja kwa Samweli lakini hatukumkuta, waliulizia na kuelezwa kuwa alipotea zaidi ya siku nne. Niliposikia vile nilijua kuwa amekimbia baada ya kujua ameua.
Baada ya kumkosa nilipelekwa nyumbani kwa bibi. Nilishangaa kukuta nyumba ikiwa katika hali iliyoonesha kuwa haijapitishwa ufagio, hata vyombo vilikuwa vichafu. Nilijiuliza bibi alikwenda wapi!
Niliingia ndani na kuwaacha nje wale maaskari ili nimwite bibi, hali ya ndani ilitawaliwa na kimya kitu kilichonishtua na kujiuliza kama bibi alikuwa amekwenda shamba. Lakini mawazo yangu yalipingana, kama angekuwa amekwenda shamba basi hata uani kungekuwa kusafi kwani bibi alikuwa anapenda sana usafi kiasi cha kuniambukiza na mimi.
Niliingia ndani huku nikimwita kwa sauti.”
“Bibi...bibi...upo wapi?”
Sikupata jibu lolote, kwa vile nilikuwa nimetoka kwenye mwanga, giza la ndani lilinifanya nisione vizuri ndani. Nikiwa natembea kuelekea chumbani nilijikwaa na kuangukia, kumbe nilipoangukia ilikuwa juu ya mwili wa bibi. Nilimshika bibi alikuwa amepoa kama vile alikuwa kwenye jokofu.
Nilimtikisa huku nikimwita lakini hakujibu chochote, pembeni ya bibi kulikuwa na harufu kali ya kinyesi.
Nilijiuliza iweje bibi afikie hatua ya kujisaidia bila kujisafisha, pamoja na kuumwa lakini hakuwa kwenye hali ya kujisaidia ndani. Nilimtingisa kwa sauti lakini hakushtuka.
“Bibi, mimi mjukuu wako nimerudi,”
nilitamka kwa sauti lakini hakukuwa na jibu, nikatoka nje walipokuwa askari na kuwaomba msaada. Waliingia ndani na kuutazama mwili wa bibi. Mmoja aliniuliza:
“Mna ndugu wengine zaidi yako?”
“Hapana, tupo wawili.”
“Kuna majirani watu wazima mnaofahamiana nao?”
“Ndiyo.”
“Basi wafuate uje nao.”
“Kwani bibi kafanya nini?”
“Hebu fanya haraka,” askari alisema kwa sauti kali kidogo.
Nilikimbia kwa jirani yetu, mama Solomoni, aliponiona alishtuka na kuniuliza:
“Wee Salha ulikuwa wapi?”
“Nilienda mjini mara moja.”
“Mlikwenda pamoja na bibi yako.”
“Nilikwenda peke yangu.”
“Sasa na bibi yako kaenda wapi, kila nikipita simuoni, nilijua labda wote hampo.”
“Mbona bibi yupo.”
“Mmh! Kama yupo mbona sijamuona, kwani hata hali ya kwenu ilionesha hakuna mtu.”
“Mama Solomoni unatakiwa nyumbani mara moja.”
“Kuna nini?”
“Twende mara moja.”
Niliongozana na mama Solomoni, tulipofika yule askari ambaye alionekana ndiye kiongozi wao alimwita pembeni na kuzungumza naye kwa muda, niliwaona wakiongozana kuingia ndani.
Mama Solomoni alitoka na nguo alizokuwa amevaa bibi.
Baada ya usafi niliitwa kuelezwa ukweli kuwa bibi yangu amefariki. Naapa kuwa tangu nizaliwe mpaka nitakapoingia chini ya ardhi sitalia tena kama nilivyolia baada kuelezwa bibi amefariki.
Nitaendelea kumuomba mwenyezi Mungu anisamehe kwani kilio nilicholia siku ile nilifikia hatua ya kukufuru.
“Jamani huu ni mkosi, eeh Mungu hata hiki kidogo umekichukua unataka niishi kwenye dunia gani? Kwa nini huniui? Kwa nini unazuia mauti yangu? Nina faida gani ya kuendelea kuishi? Sina mama wala baba, sina bibi wala ndugu! Nitaishi dunia ipi jamani? Mungu hebu nioneshe dunia yangu, naamini kabisa hii si dunia ninayopaswa kuishi.”
Walijaribu kunibembeleza lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kuninyamazisha. Maumivu niliyoyasikia hayakuwa tofauti na mtu aliyepasuliwa moyo kwa kisu butu, tena bila ya ganzi.
“Wee Salha acha kumkufuru Mungu.”
“Simkufuru, sijasema hata moja la uongo, hivi mimi naishi dunia gani ya mateso kiasi hiki? Kila kukicha nimekuwa miye, ina maana watu wa mateso wamekwisha mpaka niwe mimi peke yangu?”
“Wee binti hebu mrudie Mungu wako, kifo ni kitu cha kawaida kwa wanadamu, muombee bibi yako apokelewe na kupumzishwa mahali pema peponi.”
“Jamani naomba nikamuone bibi yangu.”
“Hapana Salha, utamuona baadaye.”
“Jamani naomba nimuone bibi yangu, maskini bibi nimekuacha ukiwa na siri nzito moyoni, kwa nini bibi usiniambie.”
“Hebu mpelekeni akamuone bibi yake,”
alisema mkuu wa polisi. Niliingizwa ndani na kumkuta bibi amelazwa kitandani akiwa amefunikwa shuka. Bado sikuamini kama bibi amekufa, nilimfunua na kumuona kama amelala. Nilianza kumtikisa taratibu huku nikimwita:
“Bibi amka nimerudi,” lakini bibi hakuwa na jibu, alikuwa amelala.
“Bibi jamani ni kweli wasemayo kuwa umekufa? Umeniacha na nani? Bibi unajua kabisa sina baba wala mama, kwa nini unaniacha peke yangu? Najuta kukuacha peke yako. Bibi amka usife, nionee huruma mimi bado mdogo, maisha siyajui... bibi.. bibiiiiiiiii,” nilipiga kelele huku nikimtikisa kwa nguvu aamke, kitu kilichofanya wanishike kwa nguvu kunitoa baada ya kumkumbatia bibi yangu kwa nguvu zote huku nikilia kwa sauti.
Baada ya kutolewa nje, nilijikuta nikihema kwa shida na kujiona kama nakufa. Dunia niliiona ikizunguka, ghafla nilianguka chini na kupoteza fahamu.
Niliposhtuka nilikuta wanakijiji wamejaa nyumbani wakipanga taratibu za mazishi, nilichukuliwa na akina mama wa kijijini ambao walinibembeleza kwani kila dakika nilimtaja bibi huku nikilia kwa sauti.
Jioni bibi alizikwa kwa sheria ya dini ya Kiislam, sikwenda makaburini lakini nilielezwa kuwa siku ya pili ningepelekwa kuzuru kaburi la bibi. Nilijikuta nikijawa na mawazo yasiyo na mfano juu matukio ya kukatisha tamaa ya maisha yangu, nikawa najiuliza nitawezaje kuishi peke yangu.
Nilishukuru jioni ile mama Solomoni alisema atanichukua na kuishi na mimi.
Itaendelea SIKU YA KESHO
Post a Comment