NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 12

ILIPOISHIA;
Chumbani alikuwa na kitanda cha futi nne kwa sita, jiko la mafuta na mkaa, ndoo tatu za maji na sufuria chache kwa kweli alikuwa na vyombo vichache sana.
“Karibu ndugu yangu haya ndiyo maisha yetu ya Dar,” mwenyeji wangu alinikaribisha.
“Mbona kawaida tu.”
Nilishukuru yule dada alikuwa na moyo wa kiutu japokuwa alikuwa hanifahamu. Huo ndiyo ukawa mwanzo wangu wa kuingia katika Jiji la Dar na kuyaanza maisha mapya.
SASA ENDELEA...
Kwa vile nilikuwa na malengo yangu niliamini kama nami nitatoa msaada wa chakula kwa mwenyeji wangu, ingenisaidia kujipanga hata kujua anajishughulisha na nini kitu ambacho kitanisaidia kujua cha kufanya.
“Samahani dada yangu,” nilimweleza usiku tukiwa kitandani kabla ya kulala.
“Bila samahani.”
“Nina imani una mtu.”
“Una maana gani?”
“Mwanaume anayekusaidia kupunguza ukali wa maisha.”
“Ndugu yangu yaani maisha ya mjini naishi kiujanjaujanja tu, huyu mtoto hata baba yake simjui.”
“Ulimpataje?”
“Ndugu yangu kazi zetu za kuzunguka ovyo kutafuta riziki.”
“Kazi gani hiyo?”
“Kwanza nilipofika nilikuwa mfanyakazi wa ndani, maisha yalikuwa magumu kwani mshahara ulikuwa mdogo lakini kazi nzito ndipo nilipompata shoga yangu mmoja niliyetoka naye kijijini na kunivuta kwenye kazi ya ubaamedi ambayo kidogo ilinisaidia.”
“ Nimeshasikia kuwa mshahara wake ni mdogo tofauti na kazi yenyewe ya kupigwa na baridi usiku?”
“Ni kweli lakini hao mabaamedi wanajenga kupitia kazi hiyo hiyo.”
“Wanajenga? Wanajenga vipi?”
“Kazi ile unaweza kupata bwana wa kukuoa au kukuhonga fedha nyingi, wengine tunatumia ujanja kuwazidishia bili wateja au kupewa ofa za bia ambazo hatunywi bali tunachukua fedha na maisha yanasonga.”
“Mmh! Mimi nina aibu sana kazi hiyo nitaiweza?”
“Utaiweza tu, hata mimi nilikuwa hivyo hivyo lakini njaa mbaya inakufanya mtu usichague kazi.”
“Hivi nikiwa na fedha kidogo ninaweza kufanya biashara gani ya kuweza kunipatia riziki?”
“Kama shilingi ngapi?”
“Laki mbili.”
“Mmh! Unaweza kufanya biashara ya kununua nguo na vipodozi na kuvikopesha.”
“Wateja wapo?”
“Wapo, unajua mara nyingi wanawake wa uswahilini huwa hawawezi kulipa mara moja, lakini ukiwapa walipe baada ya mwezi wanaweza kudunduliza na kukulipa.”
“Nilikuwa na wazo la kukuomba tuifanye kazi hiyo pamoja ili tuachane na kazi ya baa,” niliamini huenda kazi hiyo ikatukomboa.
“Hakuna tatizo.”
Tulikubaliana kuifanya biashara ile ambayo niliamini kidogo ina heshima tofauti na ile ya ubaamedi.
Kwa vile usiku ulikuwa umekwenda sana tulilala kuitafuta siku ya pili.
***
Nilianza kwa kuyabadili maisha ya shoga yangu kwa kufanya biashara ya kukopesha vipodozi na nguo za kike.
Nilimshukuru Mungu kutokana na hali ya ukaribu aliyonifanyia shoga yangu aliyekuwa akiitwa Salome au mama Konso.
Kutokana na ucheshi wangu niliweza kuzoeleka haraka mtaani, kila mmoja alinipenda.
Nilijikuta na wakati mgumu wa kuamua niishi katika dini gani, wazo lilikuwa kurudi katika dini yangu ya zamani. Kwa vile mwenyeji wangu alikuwa muumini mzuri wa Kikristo niliamua kubaki katika dini yangu hiyo mpya.
Pamoja na kuwa nilikuwa na fedha nyingi lakini sikutaka kujionesha wala kuzitumia kwa fujo.
Niliamua tuhame nyumba ile ya zamani na kwenda kukaa sehemu nyingine, kutoka Keko Toroli tukaenda kukaa Temeke kwa Sokota.
Tulihamia kwenye nyumba ambayo ilikuwa na umeme na kununua vitu vya ndani ambavyo viliweza kutuweka katika watu wenye maisha yenye unafuu tofauti na awali nilivyomkuta shoga yangu.
Nilimshukuru Mungu biashara yetu ilikwenda vizuri mpaka siku moja shoga yangu aliponieleza kuwa amepata bwana wa kukaa naye.
Japo jambo lile lilikuwa zuri lakini kwangu lilikuwa pigo, hasa kwa kuzingatia kuwa tumbo langu nalo lilikuwa likikua siku hadi siku.
“Ester si kwamba nakukimbia la hasha nami nataka kuishi maisha yangu, hata wewe huwezi kukaa hivi siku zote lazima kuna mtu atajitokeza na kukutaka utaishi naye, kama ulivyonieleza dereva teksi anavyokubembeleza kukuoa na kuwa tayari kuilea mimba yako.”
“Sasa ndugu yangu ni heri ungekuwa unakaa karibu, Gongo la Mboto nikishikika itakuwaje?”
“Usiombe mabaya, ukijisikia tu nijulishe, nitakuja mara moja ndugu yangu.”
Sikuwa na jinsi, Salome alihamia Gongo la Mboto kwa bwana’ake ambaye alikutana naye katika biashara zake. Katika vitu alivyonishukuru shoga yangu ni kumbadilisha kutoka katika kutoheshimika mpaka maisha ya kuonekana mtu mbele za watu na hatimaye kupata bwana aliyekubali kukaa naye kama mke na mume.
Kwa vile nilikuwa nimeshakuwa mwenyeji maeneo yale, nilipata msichana wa kazi wa kunisaidia kazi ndogondogo za ndani. Ujauzito nao ulianza kuniendesha na kunifanya niwe nyumbani muda mwingi. Kwa vile Salome pamoja na kuwa kwa mumewe alikuwa akifuata biashara na kuzigawa.
Siku moja usiku baada ya kazi zangu za asubuhi nilisikia maumivu makali ya tumbo, ukali wa maumivu ulisababisha nipoteze fahamu.
Niliposhtuka nilijikuta hospitali na pembeni yangu alikuwepo shoga yangu Salome na msichana wangu wa kazi. Nilipopepesa macho niliona chupa ya damu pembeni yangu niliyokuwa naongezewa.
Nilishtuka na kuvuta kumbukumbu zangu baada ya kufanya usafi wa chumbani kwangu na kushikwa na maumivu makali ya ghafla ya tumbo. Baada ya maumivu makali, sikuelewa kilichoendelea mpaka nilipojikuta hospitali. Nikiwa katikati ya lindi la mawazo, Salome alinisemesha kwa sauti ya chini.
“Vipi Ester, unajisikiaje?”
“Hata sijui nini kinaendelea kwani vipi?” Nilijikuta nauliza kwa vile sikuelewa nilifikaje hospitalini tena nikiwa naongezewa damu.
“Nilipigiwa simu na Mere kuwa umeanguka ghafla na huzungumzi huku ukitokwa na damu nyingi. Nilichanganyikiwa na kuja mbio, huwezi kuamini mshtuko nilioupata kutokana na Mere alivyokuwa akizungumza huku akilia, nilichokumbuka ni pochi ya fedha na kuwahi kuja huku. Nilikodi bodaboda mpaka hapa, viatu na khanga nimechukulia kwako.
“Shoga kuna kitu gani ulichofanya?”
“Kitu gani! Una maana gani kusema hivyo?” nilishindwa kumuelewa anamaanisha nini.
“Damu niliyokuta imekutoka utafikiri umechinja mbuzi.”
“Mungu wangu!” nilishtuka kusikia vile.
“Mbona unashtuka?”
“Sasa damu zinitoke kama kumechinjwa mbuzi nimefanya nini?”
“Kwani ilikuwaje?”
Nilimwelezea hali iliyonipata muda mfupi baada ya kumaliza usafi wa chumbani kwangu.
“Mmh! Sasa kutokwa na damu nyingi kiasi kile, tena inanuka sana kunatokana na nini?”
“Kwani daktari anasemaje?”
“Kwa kweli muda mwingi alikuwa akikushughulikia, sikupata muda wa kumuuliza.”
“Kwani muda huu ni saa ngapi?”
“Saa kumi jioni.”
“Mmekula?”
“Mbona unauliza kula badala ya afya yako?”
“Nina imani toka asubuhi mpo na mimi hospitali?”
“Ni kweli, lakini la muhimu ni afya yako.”
Mara aliingia daktari na kuja moja kwa moja kwenye kitanda changu.
“Pole,” aliniambia kwa sauti ya chini huku akinishika begani.
“Asante.”
“Unaendeleaje?”
“Naweza kusema sijambo, japo sijajua hali yangu kwa vile bado nimelala kitandani.”
“Kwa jinsi ulivyokuja na sasa ulivyo hujambo sana.”
“Kwani daktari tatizo kubwa ni nini?”
“Tumbo.”
“Nasikia damu zimetoka nyingi, ujauzito wangu una usalama?”
“Upo salama.”
“Ooh! Afadhali maana nilikuwa na wasiwasi huenda umetoka.”
“Vipi chakula mmemletea?” daktari alimgeukia Salome.
“Ndiyo, tumefanya kama ulivyotuagiza.”
“Basi mpeni ale kisha apumzike, kesho nina imani atatoka.”
Baada ya kusema vile aliondoka na kutuacha chumbani, Salome alikuwa ameniletea mtori.
“Mmh! Shoga mtori huu umetengeneza saa ngapi?”
“Nimenunua hotelini.”
“Mmh! Mzuri sana, wanajitahidi,” nilisema baada ya kupiga vijiko vitatu vya mtori.
“Lakini unajisikiaje?” wakati nikiendelea kula Salome aliyekuwa amekaa pembeni yangu aliniuliza akiwa anachezea nywele zangu.
“Najiona nipo sawa.”
“Pole sana shoga yangu.”
“Asante sana, yaani nashukuru sana kwa kuwahi kuja, sijui bila wewe ningekuwaje?”
“Yote mipango ya Mungu, tushukuru kwa yote aliyoyafanya kwa ajili yetu.”
Baada ya kula chakula nilidungwa sindano na kupumzika na kuwaacha Salome na msichana wangu wa kazi wakirudi nyumbani.
Siku ya pili kabla ya kuruhusiwa kutoka niliitwa ofisini kwa daktari, baada ya kuingia na kutulia, daktari alikuwa akiandika kitu kwenye karatasi kisha akaniita jina langu.
“Ester.”
“Abee.”
“Pole sana.”
“Ahsante.”
“Umeolewa?”
“Hapana.”
“Nani mwenye ujauzito?”
“Mimi mwenyewe.”
“Japo inaonesha hupendi mambo yako kujulikana, nilikuwa nataka kukueleza jambo ambalo lingekuwa vizuri uwe na mwenzako.”
“Ni kweli ujauzito wangu hauna baba.”
“Umekuja kwa njia ya roho mtakatifu?”
“Nilibakwa,” niliamua kukata shauri.
“Ooh! Pole sana.”
“Ahsante.”
“Sasa napenda nikueleze kuwa ujauzito wako umetoka.”
“Eti?” nilishtuka.
“Pole sana najua itakuuma lakini inaonekana ulikuwa na tatizo la muda mrefu ambalo hukuliwahisha hospitali.”
“Mmh! Nimeamini wa moja havai mbili.”
“Lakini kwa upande wangu naona mshukuru Mungu kwa kukuondolea kitu ambacho kama kingekuwepo kingekuongezea maumivu ya kubakwa.”
“Ni kweli, lakini bado mwanangu angekuwa hana hatia na wala nisingeweza kuwaza kubakwa zaidi ya kumlea, niliamini yeye ni zawadi yangu kutoka kwa Mungu.”
“Basi imekuwa bahati mbaya nina imani Mungu atakupatia mwanaume wa halali na watoto wa halali.”
“Mmh! Sina budi kukubaliana na yote yaliyotokea nina imani kila kitu ni mapenzi ya Mungu.”
“Kwa vile afya yako tokea jana imeendelea vizuri, baada ya matibabu yaliyokwenda vizuri nitakuruhusu ila kama kuna tatizo lolote usisite kurudi hapa haraka, kadi nitakayokupa itakusaidia kukuonesha kuwa ni mteja wetu.”
“Ahsante.”
“Kwa hiyo sasa hivi unakaa na nani?”
“Peke yangu.”
“Huna mzee?”
“Sina, nipo peke yangu.”
“Na jamaa aliyekulipia matibabu ni nani yako?”
“Nani kanilipia?” nilishtuka kusikia kuna mtu kanilipia gharama zote za matibabu.
“Anaitwa Victor.”
“Aah! Kumbe ni Victor?” nilishtuka kumsikia ni yeye, kweli yule kaka alikuwa amepania pamoja na kumwekea vikwazo vya kutokuwa pamoja naye, bado alikuwa karibu yangu.
“Unamjua?”
“Ndiyo.”
“Ni nani yako?”
“Ni rafiki yangu wa kawaida.”
“Kwa hiyo upo singo?”
“Ndiyo.”
“Huna mtu?”
“Sina, mbona maswali mengi?”
“Jamani mti wenye matunda si ndiyo unaopigwa mawe.”
“Ni kweli, lakini kwa sasa sihitaji mtu.”
“Basi ukihitaji nipo Dokta Hashimu.”
“Sawa dokta japo sihitaji kwa sasa.”
“Hata baada ya miaka kumi, jina langu naomba ulipe upendeleo maalum.”
“Tumuombe Mungu.”
Baada ya kuruhusiwa nilirudi nyumbani kwa teksi ya Victor aliyekuwa yupo jirani na hospitali.
Nilipofika sikuwa na budi kumshukuru Victor kwa ubinaadamu wake.
“Ahsante Victor kwa yote uliyonifanyia.”
“Kawaida tu Ester, yote nayafanya kwa ajili ya kukuonesha jinsi gani ninavyokuthamini.”
“Mungu atakuzidishia.”
“Ahsante.”
Baada ya kuachana na Victor na Salome kurudi kwake nikiwa kitandani nimejilaza, niliwaza mambo mengi juu ya matukio yote ninayokutana nayo, nilijikuta nikiungana na Dokta Hashimu kuwa ni heri mimba ile imetoka kwa vile sikuitarajia.
Moyoni niliamini huenda ndiyo maisha yangu mapya baada ya mateso ya muda mrefu.
Kutoka kwa ujauzito hakukuniuma sana, niliona kawaida japokuwa majirani walinipa pole huku wakiniombea kwa Mungu anipatie mtoto wa kuziba pengo lile.
Kwa vile Victor alionesha mapenzi ya dhati nilikubali kumkabidhi moyo wangu na kuwa mwanaume wangu wa kwanza nikiwa Dar.
Nini kilitokea? Usikose kusoma siku ya keshoooooo
Post a Comment