ad

ad

NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 11




ILIPOISHIA;
Niliamini ujauzito ni moshi ya kukaa kimya kwa kuufunika moto kwa shuka, nilimuomba Mungu kama amenibaka na kunipa ujauzito lakini aniepushe mbali asiwe ameathirika na kuniongezea zigo lingine. Lakini moyoni nilikuwa na moyo wa ujasiri na kuuapia moyo wangu kukabiliana na lolote litakalojitokeza mbele yangu kwa vile nilikuwa naishi katika dunia isiyo nihitaji.

Japo sikupenda niupate lakini niliamini kama atakuwa ameniambukiza basi hiyo ni zawadi yangu ya kuishi dunia ya peke yangu isiyohitaji furaha zaidi ya huzuni na kilio kila wakati lakini kifo nacho kikikukimbia ili uendelee kuteseka.
Usingizi mzito ulinipitia na kushtuka alfajiri wakati wa maombi, niliamka lakini sikuwa katika hali ya kawaida.
SASA ENDELEA...

Mwili wangu ulikuwa katika hali ya unyonge kama mgonjwa macho yalikuwa yamevimba kidogo na kuwa mekundu kutokana na kulia sana kila nilipokumbuka kutengana na familia niliyo izoea  kwenda kuishi sehemu nisiyoijua.
Lakini bado niliamini sikutakiwa kuogopa chochote zaidi ya kuondoka na kuwa tayari kukabiliana na lolote nitakalo kutananalo. Waliponiona waliitana na kuzungumza kwa muda kisha walikuja kwa ajili ya maombi na kunieleza jioni ya siku ile kutakuwa na kikao cha kuzungumzia matatizo yangu kwa kina.

Sikutaka kuwabishia niliwakubaliana, waliondoka na kuniacha na mama ambaye aliendelea kunitia moyo na kuamini nitayashinda yote yanayonikatisha tamaa. Nilikubaliana naye na kufanya kazi zote za muhimu za asubuhi ikiwa pamoja na kuandaa chakula cha mchana. Baada ya kuoga na kujiandaa kutoka  niliomba kwa mama nitoke mara moja.
“Ester mwanangu kwa nini usipumzike tu leo maana nakuona haupo sawa.”
“Hapana mama baada ya maombi ya asubuhi sasa hivi nipo sawa wala usihofu.”
“Umesema unakwenda wapi?”

“Kwa Suzana kuna kitabu cha maombi  alisema atanipa.”
“Basi usichelewe.”
“Sawa mama.”niliagana na mama na kuelekea ofisini kwa baba.
Nilikwenda hadi ofisini kwa baba, aliponiona alinichangamkia na kunikaribisha kwa bashasha.
“Karibu Ester.”

“Asante baba.”
“Karibu mama yangu, karibu kwenye kiti,” alisema huku akinyanyuka toka nyuma ya meza yake kwa kunikaribisha kama mgeni maalumu, ilikuwa ina tofauti na siku za nyuma nilipokwenda ofini kwa baba nilipotumwa na mama, alinikaribisha kwa heshima lakini si kwa kunyanyuka kitini na kuzunguka meza.

Alikikaribisha akionesha moyo wa upendo ambao nilijifikia jinsi ya kuachana nao, nilikumbuka mapenzi ya awali ambayo alinifanyia kiasi cha kusahau matatizo yote ya nyuma. Kosa alilofanya ni kunibaka ambalo nalo nilimsamehe lakini Mungu naye akatoa ushahidi wake wa mimi kushika mimba.

Lakini hakuwahi kunitendea kitu chochote kibaya zaidi ya kunilea kama mtoto wake wa kunizaa ndiyo maana niliamua kumsamehe aliponiomba msamaha japo historia yake ya nyuma ilionesha ana huruma ya mamba kukulia ukiwa nje ya maji ukiingia unakugeuza kitoweo.
“Za nyumbani mama?” aliniuliza kwa unyenyekevu.
“Nzuri tu baba.”
“Mmh! Sasa kwa hiyo bado una msimamo wako?”

“Baba nina imani tumeisha zungumza kinachotakiwa ni utekelezaji,” sikutaka kulegeza msimamo wangu.
“Sawa, mzigo huu hapa hesabu mwenyewe,” baba alisema huku akiweka bahasha ya fedha juu ya meza.
“Kama zipo sawa sina umuhimu wa kuzihesabu nakuamini,” nilisema huku nikichukua bahasha.
“Lakini kwa nini hukutaka tufanye zoezi dogo tu.”

“Zoezi gani?,” sikumuelewa alikuwa na maana gani.
“La kutoa hiyo mimba kwanza ni changa isingesumbua.”
“Naomba kauli hiyo uachane nayo,  labda unaona hasara fedha zako, nitaondoka hata kwa miguu bila senti tano yako na kwenda kufia mbele ya safari.”

“Hapana Ester, ni mawazo yangu tu wala si lazima.”
“Sasa baba nilikuwa na wazo jingine,” baada ya kuona msimamo wangu nilimueleza ninachowaza.
“Wazo gani?”
“Nataka nikitoka hapa nisirudi nyumbani.”
“Unakwenda wapi?”

“Ndiyo safari yangu imeanza, jioni nitapanda malori mpaka Iringa na kesho asubuhi nipande basi mpaka Dar.”
“Ulipoondoka nyumbani na mizigo yako ulimuaga vipi mama yako?”
“Sikuondoka na kitu chochote zaidi ya nilivyo hapa.”
“Amemwambiaje mama yako?”
“Nimekwambie nimefuata kitabu cha maombi kwa shoga yangu.”

“Kwa hiyo utaondoka vipi bila nguo zako?”
“Inabidi iwe hivyo kwa vile siwezi kutoka nyumbani na mzigo bila kuulizwa mswali. Kingine sasa hivi hali nyumbani imechafuka.”
“Imechafuka! Una maana gani?”
“Nimekuwa nikiulizwa maswali ya mitego na mama ambayo huenda majibu yake anayo anasubiri kauli yangu kukamilisha.”
“Una maana gani?”

“Toka siku ya kwanza mama alikuwa na wasiwasi huenda umenibaka, nilimkatalia bado alikuwa na wasiwasi na majibu yangu. Jana alinibana na maswali mazito huku akitaka niseme umenibaka nilikataa lakini bado alikuwa na mimi mpaka nilipomdanganya nitampa jibu kesho. Huoni nikirudi leo nyumbani sitakuwa na majibu ya maswali ya mama? ”
“Alisema hivyo?”
“Kuhusu nini?”
“Kuwa nimekubaka?”
“Hajasema ila ndicho anachokitaka nikiseme, amesema ana maono, ameota kuna kitu kimetendeka ndani lakini nakificha, pia kuna jambo zito la aibu linakuja na kuniomba niseme ukweli. Kuna ukweli gani zaidi ya mimi kusema kuwa umenibaka?”

“Kwa nini unang’ang’ania kubakwa, unafikiri hakuna kitu kingine anachokiwaza juu yako?”
“Kutokana na historia yako chafu ya siku za nyuma, swali la jana si la kwanza, kuna siku aliniuliza kama kweli umenibaka ungekuwa ni mwisho wa ndoa yenu.
“Amenieleza uchafu wako wa siku za nyuma hadi akalazimika kuondoka nyumbani.”
“Nimekuelewa, basi itabidi nikupe fedha ukanunue nguo za kuanzia maisha.”

“Siyo mbaya nikipata na begi kabisa.”
Baba alivuta droo na kutoa laki mbili, akanipatia.
“Kanunue nguo, ila kitu chochote kikitokea nijulishe, nitakuongeza fedha ukanunue na simu ili nijue maendeleo yako kwa vile umeondoka na damu yangu.”
“Hakuna tatizo.”

“Ukimaliza weka vitu vyako sehemu yenye usalama ili uje uniage, sawa mama?”
“Sawa baba.”
Baada ya kuniongeza fedha niliondoka hadi mjini na kununua mahitaji yangu muhimu ya nguo, simu sikuihitaji kwa vile ingekuwa chanzo cha kujiingiza kwenye matatizo hata namba ya simu ya baba sikuihitaji tena kwa vile nilipanga kwenda kuanza maisha mapya sehemu nisiyoijua, sikutaka kusumbuliwa na mtu yeyote.

Baada ya kuviweka vitu vyangu vizuri kwenye begi, majira ya saa kumi na moja na nusu jioni nilipanda gari ndogo hadi nje ya mji ili niwe na uhakika na safari yangu.
Nilifika katika mji majira ya saa kumi na mbili jioni. Mji ule ulikuwa umechangamka sana, kwa vile sikutaka watu wanizoee, nilikwenda kwenye duka moja ambalo kaka mmoja alikuwa akiuza bidhaa na kumuomba msaada wa kuwekewa begi langu ili nifanye mipango ya usafiri wa lori.

Nilimwamini kuwa asingeweza kulipekua begi langu kwa vile asingeweza kufikiria kama ndani kulikuwa na kitu cha maana.
Nilitoka hadi sehemu yanapoegeshwa  malori, nilimkuta kaka mmoja akibadilisha tairi.
“Habari kaka?” Nilimsalimia.
“Nzuri tu dada yangu,” alinijibu huku akinyanyua uso wake na kunitazama.
“Samahani kaka, wewe ni dereva?” nilimuuliza.

“Vipi, una shida gani?”
“Nahitaji msaada wa lifti mpaka Iringa.”
“Dereva amelala mpaka usiku.”
“Lakini si mnaondoka leo?”

“Ndiyo, majira ya saa nne usiku.”
“ Dereva anaamka saa ngapi?”
“Mpaka saa moja na nusu, atakuwa ameamka.”
“Basi nilikuwa naomba lifti au hata fedha naweza kulipa ili nifike Iringa.”
“Hakuna tatizo una mizigo?”

“Nina begi tu.”
“Basi nitakusaidia.”
“Nitakuwa pale dukani.”
“Hakuna tatizo dada yangu.”

Nilirudi dukani na kumuomba  yule kaka kiti ili nipumzike, nilimshukuru mwenye duka japokuwa alikuwa mwanaume lakini alikuwa na roho ya ukarimu. Majira ya saa mbili yule kaka alinifuata na kunitaka nipeleke mzigo kwenye gari.
 Nilifanya vile kwa sababu nilikuwa nimekwisha kula niliamua kukaa ndani ya gari. Majira ya saa nne usiku tuliondoka, lori lile lilikuwa linakwenda Dar es Salaam kutokana na maelezo ya dereva lakini wala sikutaka kwenda nao hadi Dar.

Niliamua kuwadanganya kuwa naishia Iringa ili niweze kuondoka na mabasi ya asubuhi yake.
Nilimshukuru Mungu tuliingia Iringa alfajiri na kwa bahati nzuri niliteremshiwa karibu na kituo cha mabasi. Niliwashukuru kwa msaada wao wa kunisafirisha bure.

Baada ya kuniteremsha wao waliendelea na safari ya Dar, kwa vile sikutaka msaada wa kila kitu niliwaacha waondoke. Sikuwa mgeni sana Iringa kwani kabla mama hajafariki niliwahi kufika naye zaidi ya mara mbili.
 Nilikwenda kukata tiketi katika basi la Upendo linalokwenda Dar.

Baada ya kukata tiketi niliingia kwenye basi na kukaa kwenye siti yangu kusubiri basi liondoke. Majira ya saa kumi na mbili na nusu basi liliondoka kituoni. Nilitulia huku nikimuomba Mungu nifike salama japo sikujua nitafikia wapi.
Niliamini kutokana na maelezo ya msichana mmoja aliwahi kurudi nyumbani baada ya kupachikwa mimba na baba mwenye nyumba na kunusurika kuuawa na mkewe baada ya kugundua mimba ilikuwa ni ya mumewe, nilijua sitapata tabu.

Maelezo yake yalinipa ujasiri jinsi alivyoweza kuingia Dar bila kuwa na mwenyeji na kuweza kupata kazi. Kwa upande wangu japo hali yangu ya ujauzito ilikuwa bado haijaanza kuonekana, nisingeweza kwenda kutafuta kazi ya ndani kwani ningekuwa mzigo.
Nikiwa nimezama kwenye mawazo nililiona basi likiacha mji wa Iringa na kuutafuta Mkoa wa Morogoro.
Moyoni nilikuwa tayari kuishi maisha yoyote na niliamini mateso yangu yalikuwa na mwisho.
Safari iliendelea huku nikimuomba Mungu nifike salama, bahati nzuri tulisafiri bila  tatizo na kuingia jijini Dar  majira ya saa kumi na moja jioni. Baada ya kushuka kwa kweli nilichanganyikiwa nianzie wapi maana jiji lilivyokuwa limejengeka tofauti kubwa na nilipotoka.
Kituoni kulikuwa na mabasi mengi na watu wengi, lakini sikutaka kuonesha ugeni kwa kuamini naweza kuibiwa kutokana na taarifa nilielezwa jiji la Dar kuna matepeli wengi.
Wakati nikiwaza nifanye nini nilimuona dada mmoja aliyekuwa na mtoto wa kike miaka minne niliyesafiri naye kwenye basi moja. Niliamini anaweza kunisaidia kwani nilikuwa nalingana naye kwa maumbile.
“Samahani dada,” nilianza kumsemesha baada ya kumsogelea alipokuwa akiweka mizigo yake vizuri.
“Bila samahani.”
“Eti dada wewe ni mwenyeji hapa?”
“Ndiyo kwani vipi?” alinijibu huku akinitazama.
“Tulikuwa kwenye basi moja, nimefika lakini nashangaa simuoni mwenyeji wangu,” nilitengeneza uongo ili nipate msaada wa kuondoka mule ndani kituo cha mabasi ambacho kilinichanganya.
“Kwani wewe umetokea wapi?”
“Mbeya, lakini safari hii nimeanzia Iringa.”
“Ndugu yako anakaa wapi?”
“Tandika,” nilijibu sehemu niliyokuwa naifahamu kwani sehemu nilizokuwa nazisikia ni Magomeni, Kinondoni, Masaki, Tandika, Mbagala na Oysterbay.
“Namba yake ya simu unayo?”
“Nimeitafuta kwenye begi siioni.”
“Jamani ndugu yangu sasa itakuwaje?” yule dada aliniuliza kwa sauti ya huruma.
“Yaani hata mimi nimechanganyikiwa mtu aniagize na kuahidi atakuja kunipokea halafu asionekane, sasa nitakuwa mgeni wa nani katika jiji hili linalotisha kwa utapeli.”
“Umeishawahi kufika hapa?”
“Ndiyo mara yangu ya kwanza.”
“Mwenyeji wako jina anaitwa nani?”
“Koleta.”
“Ni mwanamke?”
“Eeh dada! Ni rafiki yangu nilisoma naye.”
“ Anafanya kazi gani?“
“Ni baamedi.”
“Kwani na wewe umekuja kufanya kazi hiyo?”
“Hapana, mimi alinieleza kuna kazi za ndani kwa Wahindi,” nilitengeneza mazingira ya ukweli ili nipate msaada.
“Mmh! Sasa utafanya nini kwa vile muda umekwenda na mwenyeji wako haonekani?”
“Kwa kweli nimechanganyikiwa hata sijui nifanye nini?”
“Kwa nini usiende kukaa sehemu ya kupokelea wageni ili umsubiri?”
“Dada yangu kama ameshindwa kuja kunipokea kabla gari halijafika atakuja kunitafuta sehemu asiyoijua?”
“Kwa hiyo nitakusaidia vipi ndugu yangu?” aliniuliza huku akiwa na maswali atanisaidiaje.
“Nilikuwa naomba msaada wa kulala kwako leo ili kesho nijue nifanye nini.”
“Si umesema wewe ni mgeni hapa jijini?”
“Ndiyo.”
“Sasa hiyo kesho utafanyaje utarudi kwenu?”
“Ni kweli mimi ni mgeni lakini maisha nayajua, nikitulia leo kesho nitajua nifanye nini siwezi kurudi nyumbani, nimekuja kutafuta maisha.”
“Mmh! Sawa kwa vile mwanamke mwenzangu na umekuja kutafuta maisha nitakuchukua, mengine yatajulikana baadaye.”
Nilishukuru kimoyo kwa kuamini maisha ya Jiji la Dar nitayaweza kwa vile mwanzo wangu ulikuwa mzuri. Ili kumuonesha sina matatizo nilimweleza akodi teksi hadi kwake nitalipa.
“Dada unakaa wapi?”
“Keko Toroli.”
“Ni mbali kutoka hapa?”
“Siyo mbali ni daladala moja tu.”
“Kwa nini tusichukue teksi?”
“Mmh! Ni fedha nyingi.”
“Hapana dada nilitalipa mimi.”
“Mmh! Sawa.”
Alikwenda kuchukua teksi ambayo ilitubeba hadi Keko Toroli, kwa kweli mji wa Dar ulionesha umejengeka pia watu na magari yalikuwa mengi sana tofauti na nilipotoka. Tulifika nyumba aliyopanga ilikuwa chumba cha uani, chumba hakikuwa kikubwa pia hakuwa na vitu vingi, ilionesha na yeye ndiyo alikuwa akianza maisha.
Chumbani alikuwa na kitanda cha futi nne kwa sita, jiko la mafuta, la mkaa, ndoo tatu za maji, sufuria chache kwa kweli alikuwa na vyombo vichache sana.
“Karibu ndugu yangu haya ndiyo maisha yetu ya Dar,” mwenyeji wangu alinikaribisha.
“Mbona kawaida tu.”
Nilishukuru yule dada alikuwa na moyo wa upendo kwani hakunifahamu lakini alinipokea vizuri. Huo ndiyo ukawa mwanzo wangu wa kuingia Jiji la Dar na kuanza maisha mapya.

Kuyajua yote tukutane SIKU YA KESHO

No comments

Powered by Blogger.