MSUVA TATIZO NYOTA
Na Sweetbert Lukonge, Zanzibar
KIUNGO mshambuliji wa Yanga, Simon Msuva kweli tatizo ni nyota tu! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Taifa Jang’ombe.Yanga imepata ushindi huo katika mechi ya Kombe la Mapunduzi, jana kwenye Uwanja wa Amaan, ambapo Msuva alifunga mabao matatu na kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Masuva ambaye enzi za aliyekuwa kocha wa timu hiyo Marcio Maximo alikuwa akimtumia kama mchezaji wa akiba, alionyesha uwezo mkubwa na kuwa mwiba kwa walinzi wa Jang’ombe.Katika mchezo huo Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm alifanya mabadiliko kadhaa ya kikosi ikiwemo kumuanzisha kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ na kumuweka benchi Kelvin Yondani.
Mchezo ulianza kwa kasi ambapo iliwachukua Yanga dakika 13 tu kabla Msuva kuipatia Yanga bao la kwanza kwa kutupia wavuni mpira uliotemwa na kipa wa Jang’ombe, Kassim Abdallah, kufuatia shuti la Kpah Sherman.
Bao hilo lilionekana kuwaamsha Yanga ambao walikuwa wakishangiliwa na mamia ya mashabiki wengi waliokuwepo uwanjani hapo.Yanga waliandika bao la pili dakika ya 49 kupita kwa Msuva tena ambaye aliwazidi mbio mabeki kabla ya kufunga.
Mrisho Ngassa atajutia nafasi ya wazi aliyopoteza dakika ya 53 baada ya kupiga shuti lililogonga mtamba wa panya na kuokolewa na mabeki.Jang’ombe walifungwa bao la tatu dakika ya 64 na Msuva ambaye aliunganisha kona iliyopigwa na Coutinho.
Tambwe aliyeingia kuchukua nafasi ya Ngassa alipoteza nafasi ya wazi dakika za lala salama kabla ya Sherman kuipatia Yanga bao la nne baada ya kumalizia kazi nzuri na Msuva.
Post a Comment