ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 23




ILIPOISHIA;
Walitoka huku wakiamini mzee Njiwa Manga uwezo wake wa kutibu umepungua ndiyo sababu ya kushindwa kuwasaidia kupambana na Balkis.
SASA ENDELEA...

BAADA ya kutoka kwa mganga wakiwa ndani ya gari lao walianza kujadiliana kuhusiana na maneno ya mzee Njiwa Manga.
“Sasa tutafanya nini?”
“Kwa nini tusiachane naye?”

“Mmh! Lazima atatufanyia kitu kibaya, si umemuona ametokwa na machozi ya damu kwa hasira, anaweza kutufanya kitu kibaya.”
“Sasa tufanyeje?”

“Lazima tutafute njia nyingine, unajua mzee yule nimemtoa akili, shida yake ni fedha na si kutaka kujua tutafanya nini.”
“Tena namshangaa anajifanya hataki fedha wakati anafanya kazi ile ili kusukuma maisha yake,” Ashura aliongezea.
“Ooh! Nimekumbuka kuna sehemu moja kuna mtaalam mmoja nina imani anaweza kutusaidia. ” Tonny alisema.

“Kama ni hivyo tusirudi nyumbani tupitie huko huko maana bado simuamini yule mwanamke amenitisha sana, lakini Tonny asiwe kama mzee Chujio tukaumbuka?”
“Namuamini ameshawahi kunifanyia mambo mengi ambayo sikuwahi kukushirikisha, y ule mzee huwa haulizi ukimueleza chochote hata kuua anafanya,tena anapenda kuua kama nini.”


“Tena huyo ndiye mzuri sana, lakini tutafika salama?” Ashura alikuwa na wasiwasi.
“Sifa ya yule mganga ukiwa na wazo la kwenda kwake kuanzia hapo unakuwa salama hakuna kitu cha kukuzuia.”
“Tena huyo anafaa, kwa nini hukusema mapema?”
“Nilimuamini babu yule baada ya kujua ana sifa ya kutatua matatizo ya majini.”

“Basi tuelekee, leo hatuna kazi nyingine zaidi ya kuujua mwisho wa Balkis.”
Safari ilielekea kwa mganga mwingine, njia nzima ilikuwa ni mitihani mingi kutokana na gari kuteleza bila utelezi na kuona mambo ya kutisha lakini safari iliendelea. Matukio hayo yalimtisha sana Ashura kufikia hatua ya kumuomba mwanaume wake wasitishe safari yao.
“Tonny kwa nini tusirudi huoni safari yetu imejaa matukio ya kutisha tunaweza kupata ajali mbaya na kufa?”

“Shuuna hivi ni vitisho vya Balkis baada ya kugundua tunakwenda kwa mganga mwenye uwezo wa kumuangamiza. Hawezi kutufanya lolote ni kuhangaika kwake kwa mfa maji tu.”
“Mmh! Yaani naogopa kuna kipindi niliona mti wa ajabu umetokea ghafla barabarani, nilijua tunakufa na kufumba macho, nilipofumbua nilishangaa kuona tumevuka salama.”

“Shuuna hizo ni hila za majini, ule si mti ni kiini macho tu ukiukwepa tu umeumia lazima gari litapinduka.”
“Jamani! Ningekuwa mimi ningeukwepa.”
“Lazima ungepinduka, barabara hii umepita mara ngapi?”
“Mara nyingi tu.”

“Huo mti uliwahi kuuona?”
“Sijawahi kuuona.”
“Basi mimi nimepasua katikati ya mti ule hakuna kitu kilichoizuia gari kupita.”
“Mmh! Kweli yule mwanamke ni jini.”

“Awe jini mara ngapi?”
“Tukipata dawa itatusaidia sana.”
“Hesabu tumemkomesha, yule bwana alisema katika dunia hii hawezi kurudisha roho ya mwanadamu tu, kwa vile ni kazi ya Mungu peke yake. Lakini chochote kinachowezekana kwa mwanadamu kwa uwezo wa Mungu anakifanya kwa ukamilifu.”

Baada ya kufanikiwa kuvuka vizingiti vya Balkis walifika Vingunguti walikata kushoto njia ya kuingia Jeti Rumo, waliifuata njia ile mpaka maeneo ya Kijiwe Samli. Tonny alisimamisha gari mbele ya duka moja  ambapo pembeni yake kulikuwepo na vijana wakicheza drafti.
“Tumefika,” Tonny alisema huku akizima injini ya gari.
“Mbona yupo kwenye makazi ya watu?” Ashura aliuliza.

“Siku hizi huduma zimewafuata watu, hakuna waganga wa kizamani kuwa kijijini nyumba za majani. Waganga wa siku hizi wanakwenda na wakati hata mavazi yao si kaniki na ngozi na shanga kibao.”
Baada ya kufunga gari na kuliacha katika hali ya usalama aliifuata njia ya uchochoro kati ya nyumba ya duka na ya kawaida na kutokea mtaa wa pili walikata kulia kuelekea kwa mganga.

“Tonny huku umepajuaje?”
“Kuhangaika, unafikiri kama tungekuwa tunamtegemea mzee Chujio peke yake ingekuwaje?”
“Mmh! Na kweli, ona kama alivyotutoa nishai yule mzee sijui kunguru, baada ya kifo cha mzee Chujio tungekwenda wapi?”
“Atajijua mwenyewe kama anaitwa Njiwa au bundi, mzee yule kanichefua hana lolote kumbe sifa za uongo.” Tonny alimkandia mzee Njiwa Manga.

“Nashangaa mganga kupanga cha kumchanjia mgonjwa, mwenye tatizo ni yeye au sisi?”
“Waganga wengine miyeyusho tu, tumefika,” Tonny alisema huku akiingia kwenye uzio wa nyumba moja ya kifahari.
“Sweet hapa kwa mtu au kwa mganga?”
“Nikueleze mara ngapi si wote wanatumia makazi ya kisasa.”

“Karibuni,” walikaribishwa na dada mmoja aliyeonekana yupo kwenye meza iliyokuwa na simu ya mezani.
“Asante,” walijibu kwa pamoja.
“Mzee yupo?”
“Yupo na wateja, mnaweza kumsubiri.”

Walikaa kwenye sofa kama vile wanataka kuingia kwenye hospitali za kifahari, hali ile ilizidi kumchanganya Ashura.
“Sweet, mbona sielewi, hapa ni kwa mganga au hospitali?”
“Kwa mganga.”
Wakiwa  katika ya mazungumzo, msichana aliyekuwa mapokezi aliwashtua.

“Sahamani, sasa mnaweza kwenda kuonana na mzee.”
“Hakuna tatizo,” alinyanyuka na kuingia katika chumba alichokuwemo mganga.
“Karibuni,” mganga aliwakaribisha.

Alikuwa tofauti na waganga wengine, alikuwa yupo kwenye chumba chenye kiyoyozi na kukaa kwenye kiti cha kifahari nyuma ya meza iliyonakshiwa kwa vitu vya thamani. Moyoni Ashura aliona yule si mganga bali mjanja wa mjini anayekula fedha za watu kiujanjaujanja na si kwa huduma za kweli.

Hakuamini hata siku moja kama kuna mganga wa dawa za asili hajifungi kaniki na chumba kujaa vikapu na chupa za dawa. Swali lake alipanga kumuuliza mpenzi wake baada ya kutoka mle ndani.
“Ooh! Mr Tonny za siku mbili tatu?” mganga alimsalimia Tonny kuonesha wanafahamiana.

“Nzuri mkubwa.”
“Karibuni sana.”
“Asante, nimekuja tena.”
“Karibu, halafu Tonny ile kazi niliyokufanyia hakurudisha majibu.”
“Nilikuwa nije kesho kukueleza, imekwenda kama ulivyonieleza.”

“Umepata kile ulichotaka?”
“Yaani wewe kiboko, sijawahi kuona mtu kama wewe.”
“Tatizo mnakuwa hamuamini, pia nikiwaeleza malipo mnaona kama nawakamua lakini hamjui na mimi natafuta kama nyie. Mimi si mganga anayesema eti nipe sadaka wakati maisha yake yanamkimbiza mchakamchaka.

Nataka kukueleza kitu kimoja Mr Tonny, nimepewa uganga ili niwasaidie watu matatizo yao, pia mimi mnipunguzie makali ya maisha. Hebu fikiria mtu nilimtengenezea dawa akaenda machimboni na kupata zaidi ya milioni hamsini, nikiomba milioni mbili mnaona nyingi.

Mwingine ameshinda kesi ya ufisadi zaidi ya milioni 150, kunilipa milioni mbili zangu imekuwa shida, mtu kama huyo utamuweka kwenye kundi gani?”
“Kweli ubinadamu kazi.”
“Tuachane na hayo, mmh! Mna tatizo gani?”

“Kuna jini mmoja anatusumbua,” Tonny alisema.
“Jini! Huyo jini mmemjuaje?”
Tonny alimueleza kisa kizima cha Balkis, baada ya kumsikiliza kwa makini mganga Kakakuona alisema:
“Nimewaeleweni, kazi itafanyika mnavyotaka, malipo yake ni milioni mbili.”

“Mbona nyingi?” Tonny alishtuka.
“Nyingi? Uhai wa mzee Chujio kutokana na maelezo yenu nani kaulipa, familia yake sasa hivi inateseka kwa ajili yenu.”
“Punguza kidogo.”

“Haipungui, kazi ya kupambana na jini yule ni kumbwa, heri upambane na jini kisirani, siku zote majini mapole huona yameonewa na vita yake ni kubwa.”
“Sawa tutalipa kwa hiyo utatufanyia kazi gani?”
“Ninyi mnataka nini?”

“Umuue,” alisema Ashura.
“Noo, nasikia majini yana fedha, tunataka kinga ili tuipate mali yake?”
“Kupata mali yake ni vigumu kwa vile inatumika kijini na si kibinadamu.”
“Sasa utatusaidia vipi?”

“Vyovyote lakini tofauti na hilo.”
“Basi fanya kama alivyosema mwenzangu.”
“Hakuna tatizo, tangulizeni milioni kesho njooni na iliyobaki ili tumalize kazi.”
“Tuna laki tano tu kwenye gari.”

“Leteni hizo nyingine kesho.”
Wakati Tonny akienda kwenye gari Balkis alikuwa pembeni ya nyumba ya mganga, moyo wake kila dakika ulijaa hasira na kuona hakuna haja ya kuwaonea huruma. Kila alivyokuwa akimuangalia Tonny alitamani kumvaa lakini kila alipomsogelea alipoteza uwezo wake. Roho ilizidi kumuuma na kuona  kama anafanya mzaha ambao ungemletea madhara mwishowe.

Baada ya kurudi na mkoba wa fedha walizoombwa na mganga,  Balkis aliendelea kufuatilia mazungumzo ya kina Ashura na mganga, aligundua kuwa mganga alikuwa amekubali kuwapa kinga pia mganga alikuwa na dhamira mbaya ya kuua.

Ile ilimfanya akose raha na kutokwa na machozi, alipata wazo la kuwahi chini bahari kabla uchawi wa kuua haujafanywa. Lakini alikumbuka ana deni na baba yake la kuachana na Muddy, mwanaume aliyepanga kuachana naye baada ya kumpa ujauzito....
ALIJIKUTA akiuapia moyo wake kuwa atapigana mpaka tone la mwisho la damu yake lakini hatarudi chini ya bahari. Akiwa amesimama pembeni ya nyumba kwenye mti wa jirani katika umbile la njiwa, alijiuliza atafanya nini ili aweze kujiokoa na hatari ile.

Alishuhudia Ashura akitoa laki tano  kwenye mkoba na kumpatia mganga ambaye alinyanyuka ili akachukue vifaa vya kutengengeneza dawa ya kummaliza. Balkis juu ya mtu alijikuta akipoteza uwezo wake wa kawaida baada ya kuamini wakati wowote anaweza kufanyiwa kitu kibaya.

Alijua waganga wengi huwavuta majini kwa dawa na kuwamaliza, akiwa ametota kwa jasho kwenye manyoya yake kwa hofu ya kifo. Alimuona mganga akitoka uani kwake na kumwita mkewe aliyekuwa akizungumza na wanawake wenzake.  
“Mke wangu,” alimsikia akimwita mkewe kwa sauti ya juu kidogo.

“Abee mume wangu,”  alimuona mkewe aliyekuwa amevalia nguo na vito vya dhahabu kila kona kuonesha kwamba wanaishi maisha ya kifahari.
“Hebu nenda dukani kaniletee ile kiboko ya majini.”

“Kuna mtu ana jini nini?” Alimuuliza huku akipokea fedha.
“Kuna jini mmoja anawakosesha raha wateja wangu.”
“Sasa unataka kumfanya nini, unataka kumtia kwenye chupa nini?”

“Namuulia mbali, unajua jini ukilifungia kwenye chupa likitoka linaweza kukumaliza. Dawa yake sasa hivi ni kulimalizia mbali, itakuwa wakijua wanakuja Kakakuona watakuwa wanakimbia wenyewe.”
“Ngapi nichukue?”

“Kwa vile nammaliza kazi kabisa nichukulie tano na ndimu kumi na nne na sindano kumi na nne.”
“Mmh! Mbona nyingi sana leo umepania.”
“Nimemuona ana kiburi, pia ana mchezo wa kutaka ushindani, nikimfunga anaweza kutoka, si unajua siku hizi watu wakikuta kitu lazima wakifungue.”

Kauli ile ilimshtua Balkis ambaye aliamini siku ile ndiyo ilikuwa ni mwisho wa maisha yake, wazo la haraka lilikuwa ni kurudi kwao na kuwa tayari kukubaliana na matakwa ya baba yake ya kuachana na Muddy ili awe salama.
“Mmh! Haya kazi kwenu,” mkewe mganga alisema huku akitokea mlango wa nyuma kwenda duka la dawa za asili.

Balkis alimuangalia mke wa mganga na kumuona ni mweupe asiye na kinga imara ya kuzuia nguvu za majini, kutokana na kukataa kuchanjwa na mumewe. Kwa vile mumewe alimpata baada ya kuja kutibiwa kutafuta dawa ya kuolewa na kigogo mmoja na mganga akamgeuzia kibao cha kutengeneza dawa ambayo ilimfanya yule mwanamke ampende mganga badala ya mtu aliyemkusudia.

Baada ya kufanikiwa kumpata, ilibidi akubaliane na mkewe ambaye hakutaka kuishi kiganga zaidi ya maisha ya kifahari ya kujirusha kwa kutembelea gari. Kutokana na uwezo wa mganga wateja wake wengi walikuwa watu wenye uwezo hivyo kumfanya asiwe na shida ya fedha ndogo ndogo.

Pamoja na mkewe kutoishi kama mke wa mganga na muda wote kuvaa nguo na vito vya thamani, bado alikuwa akijua baadhi ya dawa ambazo zilikuwa zikitumiwa na mumewe.
Hata pale mumewe alipokuwa safarini alielekezwa jinsi ya kuzitengeneza na kuwapa wateja lakini mumewe alipokuwa nyumbani yeye aliendelea na maisha yake ya kujiachia.

Balkis aliona ile ndiyo nafasi yake ya kufanya kitu kitakachomfanya mganga asifanye lolote juu yake. Alikurupuka kutoka juu ya mti kama njiwa na kumgonga kichwani mke wa mganga ambaye alikwenda juu na aliporudi chini  hakuomba hata maji.

Waliokuwepo pembeni walimuona njiwa mweupe akimgonga kichwani na kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Kelele na kilio cha mtu aliyeingia kwa mganga zilimshtua mganga aliyekuwa ameanza kuandaa vifaa vya kummaliza Balkis. Aliacha na kutoka na kukutana na mfanyakazi wake wa mapokezi.

“Vipi?” alimuuliza baada ya kumuona amechanganyikiwa.
“Mama.”
“Amefanya nini?”
“Ame....”

“Yupo wapi?” aliuliza huku presha imempanda.
“Yupo nje ya nyumba.”
“Kafanya nini?”
“Si...sijui.”

Mara alisikia sauti za vilio vya mashoga wa mkewe ambao walikuwa wakizungumza naye muda mfupi uliopita, vilio vile vilizidi kumtisha na kumchanganya.
“Jamani kuna nini?” Aliuliza tena macho yakiwa yamemtoka pima.
Nini kitaendelea? Tukutane siku ya kesho:::

2JIACHIE.COM Tunawatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya wasomaji wetu.
2jiachie wanapenda kuwataarifu wasomaji wake anayetaka kuweka picha yake kwenye tovuti yetu akionyesha akiwa amejiachia kwa mwaka mzima na habari ya 2jiachie atume picha.

Tutatuma picha kuanzia leo Desemba, 25 - January 5,  2015 kama sehemu ya kuwa pamoja na wasomaji wetu.

 Picha zitumwe kwenye emailhii 2jiachie@gmail.com au WhatsApp +255 654 50 42 66 

No comments

Powered by Blogger.