JINI LA DARAJA LA SALENDA - 18

ILIPOISHIA:
Alijikuta akipatwa na kigugumizi, alijifikiria amjibu nini Balkis aliyekuwa akimtazama usoni huku machozi yakimtoka. SASA ENDELEA...
“Muddy nipo hapa toka saa tano usiku baridi lote limeniishia nikijua haupo mbali, kumbe umekwenda kwa wanawake zako,” Balkis alijiliza kiuongo.
“Nisamehe Ba..Ba..lkis,” Muddy alijitetea baada ya kujua kuwa ameumbuka.
“Niambie ukweli ulikuwa wapi?”
“Nilikufuata kwenu.”
“Kufanya nini, wakati niliondoa kwako hukuniambia kitu?”
“Nililipenda jumba lenu nilitaka kuliona kwa macho yangu nikiwa kwa nje.”
“Si ungenieleza unataka kupajua kwetu ili nikupeleke kuliko kunichunguza au huniamini?”
“Nakuamini lakini basi tu, yaani nimechanganyikiwa, jumba kama lile sikuwahi kuliona hata mchana huwa silioni maeneo yale.”
“Narudia tena, kwa nini usiniulize jumba letu lilipo? unaweza kulitafuta mwaka mzima na usilione.”
“Naomba unisamehe kwa yote yaliyojitokeza.”
“Muddy nilishakusamehe tangu siku ya kwanza nilipokuona ukipasuliwa moyo wako kwa kisu butu bila ya ganzi na mkeo wa bandia, niliamini mtupo uliotupwa haukujua ungeangukia wapi na muanguko wako ungekuwa mkubwa sana na usingesimama tena.”
“Nashukuru Balkis kwa kuyaokoa maisha yangu, nisamehe kwa yote, siyo kwamba sikuamini la hasha, bali nilipenda kuuona utukufu wa utajiri wa familia yako. Bado nipo njia panda kujiuliza jumba zuri kama lile limejengwa lini maeneo yale.”
“Maeneo gani?”
“Si pale pembeni ya njia panda ya kuelekea Masaki.”
“Nataka nikutaadharishe kitu kimoja, yaani usije tena maeneo yale kwani baba yangu akikuona anaweza hata kukutoa uhai.”
“Atanijuaje?”
“Mbona anakujua, aliponiuliza nilimdanganya, sasa kama atakuona tena maeneo yale lazima atajua namdanganya na atakufanyia kitu kibaya.”
“Je, akinikuta kwenu?”
“Kwa sasa baba yupo, hivyo hutuwezi kwenda tena mpaka tutakapooana.”
“Kwa hiyo utakuwa unakuja kulala hapa?”
“Ndiyo maana yake.”
“Si umesema nyumba hii itapigwa bei itakuwaje?”
“Usiwe na wasiwasi kila kitu niachie mimi, ukitoka mahakamani nitakupeleka kwenye nyumba yako mpya.”
“Nitashukuru mpenzi wangu.”
Balkis baada ya kuingia ndani aliisikia nyumba ukinuka sana, aliogopa kusema kwa kuhofia kumuudhi mpenzi wake. Alitafuta mbinu ya kumuondoa Muddy ili afanye usafi ndani mle.
Alimtuma kitu ambacho alijua hawezi kukipata karibu, alijua nafasi ile ingempa fursa ya kuwaita wajakazi wake kufanya usafi kwa muda mfupi. Alimuomba samahani kabla ya kumtuma:
“Samahani mpenzi wangu.”
“Bila samahani.”
“Najua umechoka lakini naomba nikutume kitu.”
“Nitume tu mpenzi wangu.”
“Kwa vile nataka kufanya usafi, naomba kaninunulie udi sehal”
“Upo sehemu gani?” ”Kwenye maduka wanayouza manukato utaupata.”
“Hakuna tatizo wacha niwahi.”
“Nioneshe ufagio.”
Baada ya kumpa ufagio Muddy alitaka kuondoka na gari lakini Balkis alimkataza alijua akitembea kwa miguu atachukua muda mrefu kurudi kuliko akitumia gari.
“Unaweza kuupata karibu wala usitumie gari.”
“Hakuna tatizo.”
Muddy aliondoka na kumwacha Balkis akijifanya anafagia, baada ya kuondoka tu, aliacha kufagia na kujishika kwenye paji lake la uso. Haikuchukua sekunde wajakazi kumi walikuwa mbele yake wakiwa wamepiga magoti.
“Rabeka mwana wa mfalme una shida gani?” Waliuliza kwa pamoja.
“Nataka mfanye usafi wa nyumba yote, sitaki kusikia harufu mbaya kama hii.”
Mara moja wajakazi walianza kusafisha nyumba nzima, ilikuwa ajabu waliondoka vitu vyote vya ndani na kuviweka vipya na vyenye thamani kwa muda mfupi, ndani pakabadilika, pakapendeza na kuvutia kila kona ya nyumba ilinukia kwa harufu nzuri.
Muddy alijikuta akitembea umbali mrefu kutafuta udi sehal, kila alipouliza watu hawakuujua. Alijikuta akikata tamaa na kuamua kurudi kumweleza Balkis kuwa udi wenye jina hilo kila alipouliza watu hawakuujua. Kutokana na kwenda umbali mrefu ilibidi wakati wa kurudi apande gari, jasho likimvuja kwa kutembea.
Alipofika nyumbani aliingia ndani lakini alishtuka kukuta nyumba yake ikiwa imebadilika na kupendeza sana, aliviona vitu tofauti kiasi cha kuamini kuwa alikuwa amekosea, hakukuwa kwake. Alitoka nje ili akaitafute nyumba yake lakini mlangoni alikutana na Balkis akiwa amebeba siagi na jam.
“Vipi mpenzi mbona nimekuona umeingia na unatoka?”
“Ha! Hapa ni kwangu?” Alishtuka.
“Eeh! Kwako, kwani vipi?”
“Umefanya usafi mkubwa hivi kwa muda gani?” ”Usinione nipo hivi mimi ni mwanamke wa shoka.”
“Na mbona kuna vitu vipya?”
“Sasa kipi cha ajabu, yote haya nimeyapanga kwa muda mrefu, nilipokuwa nakuja kulala hapa. Nilimtuma mtu avilete vitu hivi, wakati unaondoka vilikuwa vinaingia.”
“Sasa nyumba ikiuzwa?”
“Achana na wazo hilo hebu nenda kaoge ufungue kinywa.”
Muddy hakujibu kitu alichukua taulo na kwenda kuoga, nyumba ilikuwa ikinukia kama ujinini kwa akina Balkis. Muddy alipotoka kuoga alikuta chai imeshatayarishwa juu ya meza, ilikuwa tamu ambayo Muddy aliwahi kuinywa nyumbani kwa akina Balkis tu.
Pamoja na kuisifia chai lakini Muddy kila alipomuangalia Balkis moyo wake haukuamini kama alikuwa na mwanamke mzuri kama yule tena tajiri mwenye mapenzi ya dhati kwake.
Usikose kusoma katika Gazeti la Risasi Jumamosi.
ILIPOISHIA:
Muddy hakujibu kitu, akachukua taulo na kwenda kuoga huku nyumba ikinukia kama kwa kina Balkis. Alipotoka kuoga alikuta tayari kifungua kinywa kipo juu ya meza. Kifungua kinywa kilikuwa kitamu ambacho Muddy aliwahi kukiona nyumbani kwa kina Balkis tu. Kila alipomuangalia bado moyo wake haukuamini kuwa na mwanamke mzuri kama yule, tena tajiri na mwenye mapenzi ya dhati kwake. SASA ENDELEA...
“Muddy nihakikishie kuwa huwezi kurudiana na Ashura?”
“Nakuhakikishia kukupenda siku zote na kamwe sitarudiana na yule mwanamke muuaji.” “Muddy unayosema yanatoka moyoni au mdomoni?”
“Yanatoka moyoni mwangu?”
“Ukinigeuka?”
“Nifanye lolote.”
“Muddy kama unayosema ni kweli basi kitu nilichotaka kukifanya naachana nacho.”
“Kipi hicho?”
“Nilitaka kusimamia kesi yako kuhakikisha hawachukui kitu chochote.”
“Kwa nini usifanye hivyo?”
“Naacha ili maisha yako yakiwa mazuri mtu yeyote asikuguse.”
“Kwa hiyo nitakuwa na maisha mazuri zaidi ya haya?” Muddy aliuliza.
“Mara kumi ya haya.”
“Usiniambie!”
“Kwangu fedha si tatizo, ninachokitaka kutoka kwako ni mapenzi ya kweli, sihitaji kitu kingine.”
“Nakuahidi utayapata hapa.”
“Basi tegemea kuishi maisha ya raha mpaka kufa kwako.”
“Asante mpenzi wangu,” Muddy alisema huku akimkumbatia Balkis.
***
Muda ulipofika Muddy aliitwa mahakamani na hukumu ilikuwa ile ile ya kugawana mali. Kwa vile alishaelezwa na Balkis maisha yake baada ya hukumu, hakuchanganyikiwa baada ya kuelezwa yale. Baada ya hukumu ile, Muddy pia alitakiwa kumlipa fidia ya fedha ambayo ilimfanya asipate kitu katika mali zitakazouzwa, vikiwemo gari na nyumba.
Ashura alishangaa kumuona Muddy pamoja na pigo zito yupo katika hali ya kawaida. Baada ya hukumu Muddy alitoka nje ya mahakama na kwenda moja kwa moja kwa Balkis aliyekuwa akimsubiri. Muddy alishtuka kumuona Balkis akiwa pembeni ya gari la kifahari.
“Karibu mpenzi.”
“Asante.”
“Pole na masaibu yote.”
“Asante,” walikumbatiana, kitendo kile hakuna aliyekiona zaidi ya Muddy peke yake.
“Nina imani mambo yamekwenda kama nilivyokueleza?”
“Yaani umekuwa kama wewe ndiye uliyeyapanga yote, hakuna hata kimoja kilichokwenda kinyume.”
“Basi huyo ndiye Ashura ambaye pia hilo si jina lake halisi.”
“Una maana gani kusema hivyo?”
“Nitakueleza, kila mwanaume aliyemchezea mchezo huu anamjua kwa jina hili lakini jina halisi anaitwa Shuuna.”
“Ina maana hata hayo majina aliyotumia kwa hao mabwana wa awali unayajua?”
“Nayajua.”
“Alikuwa anaitwa nani?”
“Twende kwanza nyumbani ukapumzike, mengine tutazungumza tukifika.”
Muddy aliingia kwenye gari na kuondoka, kabla ya kuingia kwenye gari Ashura alishtuka kumuona Muddy na mwanamke mrembo aliyejitambulisha kuwa ndiye mkewe siku aliyokwenda kwake kumuonya.
Alijikuta akikosa raha na kujiona wamefanya kazi bure sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Waliona kama hawakufanya kitu na kujikuta akimuuliza mwanaume wake.
“Yule mwanamke mwenye fedha Muddy kamtoa wapi?” Ashura aliuliza.
“Hata mimi nashangaa, ni wazi wameanza uhusiano kipindi mkiwa wote.”
“Ndiyo maana hata ilipotolewa hukumu hakushtuka.”
“Hata mimi nilishangaa kuona anakubali kila kitu.”
“Kwa hiyo tutakuwa tumefeli?”
“Hapana, hatujafeli kwani tulivyovitaka tumevipata, ila kuna biashara nyingine nzuri,” mwanaume wa Ashura alisema.
“Biashara gani?”
“Tukafungue mashitaka ya kudai kuhujumiwa penzi lako lililosababisha muachane na mumeo wakati bado unampenda.”
“Aisee, wazo zuri sana! Kweli wewe bwana mipango, sasa mpango huo tuufanye lini?”
“Kwanza tupajue wanapoishi ili tufanye mpango wa kufungua mashitaka.”
“Hilo wazo, mbona mwaka huu tutatengeneza fedha mpaka zitukimbie.”
“Hiyo ndiyo kazi yetu.”
“Lakini Mussa kuna jambo nimekumbuka.”
“Jambo gani hilo?”
“Unakumbuka yule mwanamke alivyotuonya kuhusu tabia yetu kuwa itatutokea puani?”
“Sasa wewe unamuogopa, atatufanya nini mwanamke yule?”
“Mmh! Nashangaa moyo unanienda mbio nilipomkumbuka.”
“Si kwa vile amekuchukulia mumeo.”
“Yule si mume wangu nilikuwa naye kibiashara zaidi.”
“Basi mpango wa haraka ni kudili na Muddy kuhakikisha anaokota makopo.”
Wakati wakipanga kuchukua fedha za Balkis, muda huo Muddy alikuwa akikaribishwa kwenye jumba la kifahari.
“Karibu mpenzi wangu hapa ndipo kwako ishi kwa furaha na mapenzi ya kweli,” Balkis alimkaribisha kwa sauti tamu.
“Ha! Siamini.”
“Hata lile gari ni lako.”
“Usiniambie!” Muddy alizidi kupigwa na butwaa.
“Ukweli ni huo, leo usiku kutakuwa na sherehe fupi ya kufunga ndoa yetu ili uweze kunitumia kihalali kama mkeo.”
“Hakuna tatizo, asante sana mpenzi.”
Muddy alishukuru kwa kupiga magoti huku machozi yakimtoka na kujiuliza bila ya Balkis maisha yake yangekuwaje baada ya kufanyiwa utapeli na Ashura.
****
Ashura na mwanaume wake baada ya kutoka mahakamani waliongozana na madalali kwenda kuuza mali za Muddy zikiwemo gari na nyumba siku ile ile, kutokana na mipango iliyopangwa mapema. Baada ya kufanikiwa kuuza gari na nyumba waliendelea kufurahia mafanikio yao kufuatia kazi yao ya utapeli na kujipanga kwa ajili ya kupambana na Balkis kuhakikisha wanapata fedha kupitia kwa Muddy.
Pamoja na kupata vitu walivyovitaka kutoka kwa Muddy, bado Ashura moyo wake ulikosa raha, alijiuliza atamtazamaje Muddy siku wakikutana kutokana kuonekana ameingia kwenye maisha mazuri tofauti na awali walipokuwa pamoja.
Baada ya kumuacha Muddy na kuonesha kuchanganyikiwa, alitegemea kusikia amejinyonga. Kufuatia kupona kifo hicho, Ashura alitegemea siku ya hukumu angemuona Muddy akitoka mahakamani na kuanza kuokota makopo, lakini ilikuwa ni kinyume na mategemeo yake.
Wasiwasi wake Muddy lazima angelipa kisasi, wazo lake lilikuwa kumuwahi kabla hajawahiwa yeye. Akiwa amekaa na mwanaume wake, Ashura alimueleza jambo:
“Mussa nina jambo linaniumiza akilini mwangu.”
“Lipi tena mpenzi?”
“Nina wasiwasi na Muddy kutulipizia kisasi.”
“Ni kweli hata mimi nilikuwa na wazo hilo.”
“Sasa tufanye nini kabla hajafanya lolote, maana akitulia atajipanga na yule dada anaonekana ana fedha hivyo anaweza kutufanyia kitu kibaya.”
“Ondoa hofu hawawezi kutufanya lolote zaidi ya sisi kuwamaliza wao.”
“Hayo ndiyo maneno.” Ashura alipata faraja.
***
Wakati Ashura na Musa wakipanga mipango yao, usiku wa siku ile ufukweni mwa Bahari ya Hindi maeneo ya Daraja la Salenda kulikuwa na sherehe kubwa ya harusi kati ya Balkis na Muddy. Katika kundi la watu wote waliokuwepo kwenye sherehe ile Muddy peke yake ndiye aliyekuwa mwanadamu, lakini waliobakia walikuwa majini.
Lakini hakuwajua kwa vile walikuwa katika maumbile ya kibinadamu, Muddy alimuoa rasmi Balkis na kuwa mkewe wa halali. Ilikuwa sherehe kubwa kuwahi kutokea katika maisha ya Muddy. Baada ya harusi walilala kwenye kitanda cha bembea kilichowabembeleza mpaka kunakucha.
*****
Taarifa ya ndoa ya Balkis ilifika chini ya bahari kwa Mfalme Barami Hudirud, kitendo kile kwake alikiona kama ni dharau kutoka kwa mwanaye kufunga ndoa na mwanadamu. Alimfuata mkewe aliyekuwa amekaa kwenye bustani akibembea kwenye kiti.
“Mama Balkis,” alimwita kwa sauti ya juu iliyomshtua.
“Mtukufu Mfalme wa chini ya bahari, mbona sauti kali, kuna usalama?”
“Mwanao ananitafuta nini?”
“Kwani kafanya nini tena mtukufu mfalme?”?”Tunamkataza nini na anafanya nini?”
“Amefanya nini?”
“Anaweza kuvunja amri yangu?” Mfalme Barami alisema huku akipiga ngumi kifuani kwa hasira.
“Mume wangu, lakini si bado anaendelea kuleta vizazi vya wanawake?”
“Kwa nini ameolewa na mwanadamu?”
“Ha! Ndiyo kafanya hivyo!” Malkia Huleiya alishtuka.
“Eeh! Tena nasikia watwana na vijakazi walikuwepo kwenye harusi hiyo.”
“Usiniambie!”
“Kwa jinsi alivyovunja amri yangu, wote waliohudhuria harusi ile watakutana na adhabu kali,” alisema kwa hasira mpaka povu likamtoka mdomoni.
“Mume wangu usimguse mtu yeyote ni wewe uliyempa amri mwanao kwa watwana na vijakazi juu ya kuheshimu amri zake.”
“Basi kama sivyo hivyo nitamtuma mtwana mkuu Muhuru akammalize huyo mwanaume.”
“Bado hujatumia busara, kumbuka kosa lako lolote litatugharimu, kitendo cha kukataa kumuondoa mwanaume wa kwanza huku kilizua patashika na ulipotaka kumuua ulisikia alichosema mwanao. Hivi umuue huyu aliyefunga naye ndoa itakuwaje?”
“Sasa kuna haja gani kuendelea kuleta vizazi vya wanawake wakati ameishajiamulia kuolewa na mwanadamu?”
ITAENDELEA KESHOOOOOOOOOOO
Post a Comment