RAIS OBAMA ATHIBITISHA KIFO CHA KASSIG
Rais Barack Obama amethibitisha kifo
cha mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada la Marekani Abdul-Rahman
Kassig, ambaye ameuawa kwa kukatwa kichwa na kuonyeshwa katika video
iliyorushwa na kundi la Islamic State (IS).
Bwana Obama amekitaja
kitendo hicho kuwa "uovu uliopitiliza" na kutoa salaam zake za
rambirambi kwa familia ya Bwana Kassig, aliyekuwa na umri wa miaka 26,
ambaye alitekwa nyara nchini Syria mwaka jana.
Video hiyo ambayo
imethibitishwa na Ikulu ya Marekani, inamwonyesha mtu aliyejificha uso
akiwa amesimama juu ya kichwa cha Bwana Kassig.
Pia inaonyesha kukatwa vichwa kwa raia 18 wa Syria waliotambuliwa kama maafisa wa jeshi na marubani.
Rais
Obama amempongeza Bwana Kassig kama mtu wa kutoa msaada kwa watu
wengine na kusema " alichukuliwa kwetu katika kitendo cha uovu wa
kupitiliza uliofanywa na kikundi cha kigaidi ambacho ulimwengu
unakihusisha na unyama".
"leo tunatoa sala zetu na rambirambi kwa
wazazi na familia ya Abdul-Rahman Kassig, ambaye pia tulimjua kwa jina
la Peter," amesema.
Kauli ya Bwana Obama imekuja wakati akirejea
Marekani kutoka Australia ambako alikuwa akihudhuria kikao cha viongozi
wa nchi za G20.
Kikundi cha IS, ambacho kinadhibiti sehemu kubwa ya Syria na Iraq, mpaka sasa kimewaua mateka watano kutoka nchi za magharibi.
Wengine ni Waingereza Alan Henning na David Haines, na waandishi wa habari wa Marekani James Foley na Steven Sotloff.
Mauaji
hayo yalitekelezwa na mtu anayeaminika kuwa Mwingereza. Ndevu za mtu
huyo zinafanana na wapiganaji walioficha nyuso zao wakiwa wamepigwa
picha ya video wakimwonyesha Bwana Kassig.
Tofauti na video zilizotolewa
siku za nyuma na kundi la IS, video hii mpya inaonyesha sura za
wapiganaji wengi wa jihad na wanaonyesha sehemu yake kuwa ni Dabiq
katika jimbo la Aleppo nchini Syria.
Bwana Kassig alikuwa askari wa zamani wa Marekani ambaye alitumikia jeshi la nchi hiyo nchini Iraq.
Baadaye
alifundishwa kama mtaalam wa matibabu ya dharura na kuanzisha shirika
la kukabiliana na matukio ya dharura na msaada (Sera), likisaidia
kusambaza misaada katika makambi yaliyo katika pande zote mbili za mpaka
wa Syria.
Alikuwa akiandaa mradi kwa ajili ya shirika lake la
Sera alipotekwa mwezi Oktoba 2013 wakati akisafiri kuelekea mashariki
mwa Syria.
RAIA WA MAREKANI AKATWA SHINGO NA IS
Peter Kassig mda mchache kabla ya kukatwa shingo na wapiganaji wa IS
Kanda hiyo pia ina picha za watu kadha waliouawa ambao wanasemekana
kuwa wanajeshi wa Syria waliokuwa wametekwa nyara.Marekani imesema kuwa
inafanya juhudi za kubaini chimbuko la kanda hiyo.Bwana Kassig ambaye anajulikana kama Peter alitekwa nyara mwaka uliopita.Mnamo mwezi Octoba kanda nyengine ya video ya kifo cha mfanyikazi mwengine wa misaada kutoka Uingereza Alan Henning iliisha huku Kassig akitishiwa.
(Chanzo: BBC)

Post a Comment