ad

ad

MATAJIRI NDANDA WACHAPANA LIVE


Dar es Salaam.
Matajiri wa Ndanda FC wameshindwa kujizuia na kujikuta wakichapana makonde hadharani kwenye mechi ya timu yao dhidi ya JKT Ruvu iliyochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Vigogo hao wakitwangana makonde sekunde chache baada ya kipenga cha mwisho wakati Ndanda ikikubali kipigo cha mabao 2-0.

Vibopa hao ambao mmoja alifahamika kwa jina la Maarifa na mwingine Mamu, ambaye pia ni mkurugenzi wa timu hiyo walianza vurumai kipindi cha pili cha mchezo huo huku wakionekana kurushiana vijembe vya chinichini wakiwa jukwaani.

Baada ya mchezo kumalizika, Maarifa alinyanyuka na kumfuata Mamu kisha kuanza kumshambulia kwa makonde ambayo yalimpata sawia mkurugenzi huyo wa Ndanda, ambaye alijibu mashambulizi hayo kabla ya kuamuliwa na baadhi ya wadau wa timu hiyo akiwamo mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara (Mtwarefa).

Licha ya kuamuliwa, vigogo hao wa Ndanda waliendelea kutoleana maneno huku Mamu akimpiga Maarifa na chupa yenye maji iliyompata sawia usoni kabla ya mashabiki wa timu hiyo kumtoa Maarifa uwanjani.

Baada ya mchezo huo, gazeti hili lilimfuata mkurugenzi wa Ndanda kujua chanzo cha ugomvi huo, na alisema: “Siwezi kulizungumzia suala hili, wewe andika kama ulivyoona kwani si ulikuwepo.”
CHANZO: MWANANCHI

No comments

Powered by Blogger.