AHADI YA NDOTONI - 14, MWISHO WA HII SIMULIZI

ILIPOISHIA;
“Nilikusamehe toka nilipojua udhaifu wako, ila ndoa yetu iliisha siku uliponirudishia pete yangu.” SASA ENDELEA...
“Nisamehe Lakashi.”
“Nataka nikueleze kitu kimoja, siku zote kiburi si maungwana, nilikupenda na kuwa tayari kukusamehe kwa lolote. Lakini ulivuka mipaka, tulipoachana sikutaka kuchukua kila nilichokukupa. Uliyoyafanya ndiyo yaliyopoteza mali yako pombe na nyama ya nguruwe ndiyo iliyochoma.”
“Najua Lakashi naomba unisamehe.”
“Msaada wangu ni mmoja kukupa maisha mazuri, lakini ukifanya kosa lingine utageuka nguruwe milele.”
“Nipo tayari kuyafanya yote utakayo yataka.”
“Hakuna kitakacho badilika zaidi ya kuwa kama nilivyokueleza tukiwa pamoja.”
“Nitashukuru Lakashi.”
“Hakuna maisha mazuri kama mtu kujiheshimu na kuwaheshimu waliokuzunguka. Changua maisha yanayomfurahisha Mungu ndiyo uyafanye siku zote.”
“Nimejifunza Lakashi, nisamehe.”
“Basi rudi nyumbani kwako.”
“Nyumbani kwangu wapi?”
“Kwani ulikuwa unakaa wapi?”
“Nyumba yangu si iliungua?”
“Nani aliyekuambia imeungua?”
“Niliona mwenyewe”
“Nimekuambia rudi nyumbani kwako.”
“Sawa.”
“Haya rudi,” baada ya kusema vile aliitupa kamba chini iliyogeuka nyoka ambaye aliingia kwenye majani na kupotea. Jeska alitoka kwenye majani na kurudi nyumbani kwake kwa miguu.
Njiani lilipita gari iliyompa lifti mpaka nje ya geti la nyumba yake, alishangaa kukuta nyumba yake ipo kama kawaida hakuamini na kujiuliza iliyoungua ilikuwa nyumba ipi. Alipoingia ndani alishangaa kukuta kila kitu kipo hata mlinzi wake alikuwepa kama kawaida.
Aliyazungukia magari yake yalikuwepo kama kawaida hakuna lililoungua.
“Dada,” mlinzi alimwita.
“Abee.”
“Za siku?”
Swali lile lilimshtua na kujikuta akichukua muda kumjibu, alijiuliza ni mlinzi gani aliyempigia simu kuwa nyumba inaungua? Kabla mlinzi ajamshtukia alimjibu.
“Nzuri tu.”
“Naona safari hii umeondoka bila kutuaga?” mlinzi alimuuliza huku akimshangaa vazi alilokuwa amevaa.
Kabla ya kufanya lolote alimuacha mlinzi bila kujibu kitu na kwenda ndani, hali ya ndani ilikuwa kama alivyoiacha ilikuwa katika hali ya usalama, ila hali ya hewa ilikuwa nzito kama kuna kitu kimeoza mle ndani. Alikwenda kuoga na kubadili nguo. Akiwa amekaa sebuleni sauti ilimjia akilini:
“Naomba utoe uchafu wako wote uliouweka humo ndani mara moja.”
Bila kujibu alinyanyuka na kwenda kumwita mfanyakazi wake kuondoa vitu vyote alivyokatazwa na Lakashi. Baada ya kuondoa chupa za pombe na vipande vya nyama na mifupa ya nguruwe haikuchukua muda hali ya hewa ilibadilika mle ndani na kuwa nyepesi tena yenye manukato aliyoyazoea.
Hali ile ilimshangaza sana Jeska na kujiona kama mtu aliyezaliwa upya, akiwa bado haamini kilichotokea simu yake iliita alipopokea ilitoka kwa msichana wa dukani kwake:
“Dada upo wapi?”
“Nyumbani?”
“Umerudi lini?”
“Leo.”
“Jamani dada mbona ukutuaga, mali zimekwisha wateja wanatusumbua sana.”
“Jamani poleni, naomba jioni mje wote nyumbani.”
“Huwezi kuamini tumefurahi kukuona.”
Jeska alikata simu na kubaki akiwa katika dimbwi la mawazo na kujiuliza kilichomtokea kilikuwa ni ndoto au kiini macho. Alinyanyuka na kwenda kuangalia gauni alilopewa na Lakashi hospitali lilikuwa lilelile. Hakutaka kuamini mara moja, alikwenda moja kwa moja kwenye hospitali aliyolazwa baada ya kuokotwa na Lakashi.
Majibu yalikuwa yale yale alipelekwa pale baada ya kuokotwa na msamaria mwema aliyesema kuwa amemkuta amelala pembeni ya gari lake lililokuwa limeungua moto, pia alieleza kuwa ameunguliwa na nyumba pamoja na duka. Kilichowashangaza ni muonekano mwingine wa nguo za heshima alizokuwa amevaa siku ile na kumsikia daktari kwa mbali akimuelezea muuguzi wake:
“Huyu ndiye Lakashina ninaye mfahamu.”
Kauli ile ilimuumiza sana moyo wake na kujua kabisa alikuwa amekosea njia, aliondoka na kurudi nyumbani. Alipofika alilia sana na kujutia yote aliyoyafanya, alitamani kumuomba radhi Lakashi na kuwa tayari kumsubiri kwa muda wowote hata miaka kumi.
Baada ya kulia sana mpaka sauti ikamkauka, alipitiwa usiungizi. Hakuchukua muda Lakashi alitokea mbele yake.
“Jeska unalia nini?” Lakashi alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Naomba unisamehe Lakashi,” Jeska alipiga magoti mbele yake.
“Nyanyuka Jeska wa kupigiwa magoti ni Mungu peke yake,” Lakashi alimnyanyua Jeska na kumketisha kitandani.
“Lakashi najua nimekukosea, Nipo chini ya miguu yako pamoja na yote niliyoyafanya sikuwahi kuisaliti ndoa yetu. Nakuahidi kuwa mke mwema na muaminifu pia nipo tayari kukusubiri hata miaka miamoja. Nimegundua wewe ndiye mume wa maisha yangu...Nakupenda Lakashi umekuwa msaada na kinga ya maisha yangu...nakuomba usiniache....nirudishie pete yangu. Kumbuka mimi ni mwanadamu niliye na upungufu mwingi, kukosa ni sehemu ya maisha ila nimejifunza kutokana na makosa.
Umekuwa kiumbe wa ajabu pamoja na kukufanyia yote mabaya lakini bado umekuwa ukinijali na kunilinda. Nisipo yathamini hayo, mimi sifai tena kuishi chini ya jua kwa vile sina tofauti na viumbe vilivyomuudhi Muumba na kuviteketeza kwa gharika.
Nakuahidi mbele ya Muumba tusiyemuona lakini yupo mbele yetu kuwa sitakuumiza tena, nitayashika yote uliyonifundisha ili niwe mke mwema katika maisha yangu yote.”
“Jeska...Jeska...Jeska.”
Jeska alishtuka usingizini baada ya kuitwa huku akitikiswa begani, alipofumbua macho alijishangaa kuona amezungukwa na familia yake. Alitulia kwa muda akiwaangalia waliomzunguka na kujiuliza alichokiona mbele yake ni kweli au aliota.
Familia yake yote ilikuwa mbele yake, alijitahidi kunyanyua mdomo wake amwite mama yake.
“Ma..a..ma,” aliita kwa sauti ya upole huku michirizi ya machozi ikiwa pembeni ya macho yake.
“Abee mwanangu,” mama yake alimuitikia kwa upole.
“Ni wewe mama au naota?”
“Huoti mwanangu ni mimi mama yako.”
“Baba yuko wapi?”
“Alisafiri lakini atarudi leo.”
“Mbona mmenizunguka?”
“Toka ulipolala jana jioni mpaka usiku huu ndiyo unashtuka, kwani ulikuwa unaota nini mwanangu maana umetoa ahadi nzito ya ndotoni?”
“Mama nampenda sana Lakashi najuta kumkosea.”
“We Jeska, Lakashi ni nani?”
“Mama mwanaume wa pekee aliyeonesha kunijali pamoja na kumfanyia makosa bado kanisamehe.”
“We Jeska, utakuwa mwendawazimu huyo Lakashi anaishi wapi?”
“Hata sijui mama.”
“Hebu nyanyuka kwanza hapo kitandani.”
Mama Jeska alimnyanyua mwanaye aliyekuwa akiendelea kulia.
Baada ya kuoga, Jeska aligoma kula mpaka amuone Lakashi.
“Jeska una nini mwanangu mbona sikuelewi, Lakashi ni nani?”
“Ni mwanaume wa pekee aliyenipenda kwa dhati.”
“Mbona familia yako hatumjui?”
“Lakini mama mbona kama sielewi.”
“Huelewi nini mwanangu?”
“Inawezekana nilikuwa naota!”
“Uliota nini mwanangu?”
Jeska alimueleza mama yake jinsi alivyokutana na Lakashi, baada ya kumsikiliza mama yake alicheka na kusema:
“Kumbe ndoto! Ona sisi wazazi wako na familia yote tupo hai.”
“Mama, pamoja kuwa na ndoto maishani mwangu nitaolewa na mwanaume kama Lakashi.”
“Kwa hiyo upo tayari kubadili dini?”
“Nipo tayari, nakiri kumpenda Lakashi mpaka kufa.”
Jeska aliamini katika maisha yake ile haikuwa ndoto bali maisha kamili na kuamini siku moja Lakashi atamtokea na kumuoa. Aliishi kwa kuzingatia yote aliyomuahidi Lakashi ndotoni.
MWISHO.
Post a Comment