AHADI YA NDOTONI - 06
ILIPOISHIA;
Baada ya kuzigawa pesa kwa ajili ya matumizi ya siku ile, alioga na kufungua kinywa kisha alifanya usafi wa kitanda. Ajabu wakati akiondoa mto ili atandike alishtuka kuzikuta tena noti mpya za elfu tano tano kama alizozitoa asubuhi zipo chini ya mto.
Alijiuliza zile pesa alichukua au vipi, alitandika na kuzirudisha chini ya mto, alipanda kitandani na usingizi haukuchelewa ulimchukua.
SASA ENDELEA....
Aliposhituka alitaka kuhakiki alichokiona ni kweli au alikuwa akiota alifunua tena mto na kuzikuta pesa zipo kweli. Alizitoa na kuzihesabu, hesabu yake ilikuwa ile ile noti mpya nne za elfu tano. Alijikuta akishtuka na kujiuliza iweje pesa zile azitoe kisha alipoangalia alizikuta zipo vilevile.
Wasiwasi ulianza kumjaa huenda kaka yule si mtu wa kawaida, lakini kilichomshangaza ni upole na ucheshi wake ambaye alionekana ni mtu mwenye huruma sana.
Alijinyanyua kitandani na kwenda bafuni kuoga alipomaliza kulirudi sebuleni kuangali vipindi kwenye runinga, kengele ya mlangoni ilimfanya ananyuke kwenda kufungua. Alipofungua mlangoni alikutana na kaka msamalia mwema ambaye hakuwahi kumuuliza jina japo yeye alikuwa akilifahamu lake.
“Ha! Karibu,” Jeska aliachia tabasamu pana.
“Asante,” ilikuwa tofauti na alivyomzoea akiwa mtu mwenye tabasamu na bashasha muda wote huku akizungumza kwa sauti ya chini na upole. Lakini uso wa mgeni ulikuwa imejaa hasira kitu kilichomtisha Jeska na kutaka kujua kulikoni.
“Karibu kaka mwema,” Jeska alimkaribisha kwa mashaka kidogo.
Mgeni aliingia bila kujibu neno na kutembea taratibu mikono nyuma na kumpa mgongo Jeska aliyekuwa akimshangaa baada ya kuketi kwenye kochi alitembea taratibu mikono nyuma na kichwa amekiinamisha kuonekana mtu mwenye maweazo mengi.
Jeska alikosa la kusema na kuendelea kumsindikiza kwa macho huku akiwa hajui kuna nini, alikwenda kusimama mbele ya ukuta na kutazamana nao bila kugeuka alimwita Jeska.
“Jeska,” sauti nzito ambayo hakuwahi kuisikia masikioni kwake ilimwita.
“A..a..be..e..e.” Jeska alijibu kwa kubabaika huku mapigo ya moyo yakimwenda kwa kasi kutokana na hofu iliyomshika moyoni.
“Kwanini hunisikii?” Mgeni alimuuliza akiwa bado amempa mgongo.
“Sa..sa..sa..mahani.”
“Jeska kwa nini unataka kujiua?”
“Sa..sa..mahani... kaka.”
“Hujanijibu, unaniomba samahani ya nini?”
“Nina matatizo yasiyokwisha.”
“Una matatizo gani?”
“Sina mtu wa kuyaongoza maisha yangu toka kifo cha baba nimebakwa na niliyekuwa namtegemea amefariki.”
“Jeska.”
“A..a..be.”
“Nilikuambia nini?”
“Nisijiue.”
“Hapana Jeska la kwanza kabla ya kukueleza hili?”
“Utanisaidia.”
“Sasa kwa nini unakaidi ninachokueleza?”
“Nisamehe nimekosa sirudii tena,” Jeska alimfuata mgeni na kupiga magoti nyuma yake kwa vile uso wake alikuwa ametazama ukutani.
“Nimeniomba msamaha mara ngapi?”
“Najua nimekosa mimi ni kiumbe dhaifu nahitaji kusamehewa.”
“Jeska ni matatizo gani umeyapata baada ya kifo cha mzee Ezekiel?”
“Sijapata ila ni wasiwasi wa moyo tu.”
“Au hupendi msaada wangu nikuache ujiue?”
“Hapana kaka, wewe ni kiumbe muhimu maishani mwangu naomba usiniache.”
Mgeni aligeuka na kumnyanyua Jeska aliyekuwa amepiga magoti kuomba msamaha.
“Basi nyanyuka,” ajabu sauti ile ilibadilika na kuwa sauti aliyoizoea ya chini yenye upole.
Jeska alishtuka kuuona uso wa mgeni umejaa machozi na fulana yake imelowa kwa machozi.
Mgeni alimvutia kifuani kwake huku mikono yake laini ikimpigapiga taratibu mgongoni na kumfanya Jeska asisimke.
“Pole sana Jeska najua umekata tamaa lakini nakuhakikishia kukusaidia na kukulinda kama nilivyokuahidi awali.”
“Nashukuru kaka mwema , samahani lakini wewe ni nani?”
“Kwa nini ya muhimu hutaki kufanya unataka kunijua?”
“Kutokana na matukio ninayo kutananayo naomba uniweke wazi ili nijue niliyenaye si wa ndotoni bali wa kweli.
Matukioni ninayokutananayo huona kama nipo ndotoni yasiyo na ukweli.”
“Kwa jina naitwa Lakashi.”
“Mmh, jina zuri sana.”
“Asante, ningependa nawe siku moja uitwe Lakashina.”
“Jina zuri lakini mbona kama la Kihindi?”
“Kwani mimi Mhindi?”
“Ila kwa mbali kama mpemba vile?”
“Ni kweli nina asili ya arabuni, unajua maana ya majina hayo?”
“Hata.”
“Lakashi ni mume mwenye huruma.”
“Na Lakashina?”
“Mke msikivu.”
“Kwa hiyo unataka kunioa?”
“Itabidi nifanye hivyo ili kukuondolea mawazo najua shetani wa kifo bado hachezi mbali na wewe kitu kimenifanya nisicheze mbali na wewe kuyaokoa maisha yako.”
“Asante Lakashi nakuahidi sitakusaliti nakupenda sana Lakashi.”
“Nashukuru Lakashina.”
Walikumbatiana kwa nguvu huku kila mmoja akionesha mapenzi mazito kwa mwenzake.
Siku ile Lakashi alishinda na kulala pale wakiwa kama wapenzi wa muda mrefu kwa jinsi walivyokuwa. Furaha ya Jeska ilirudi upya na kujikuta akifurahia maisha na kusahau tabu zilizomkabili.
Usiku wakiwa kitandani wamejilaza kila mmoja alilalia mto wake, Lakashi alimwita Jeska.
“Lakashina.”
“Abee.”
“Napenda uniitikie rabeka saidi yangu.”
“Rabeka saidi yangu.”
“Swadakta, ni hivi japo hatujakaa pamoja muda mrefu sikupenda tutengane kwa sasa.”
“Kwa nini unasema hivyo mpenzi?”
“Muda wangu wa kukaa na wewe ulikuwa bado kwa vile nina safari ya mbali ambayo itaniweka mbali nawe kwa muda mrefu.”
“Lakashi safari gani hiyo? Na unasafiri lini?”
“Usiku huu natakiwa nisafiri, kilichonifanya leo niwe karibu ni kutokana na dhamira yako mbaya. Nimerudi kukuhakikishia kuwa nipo kwa ajili yako na kila nililokuahidi kukusaidia nitafanya hivyo.
Japo sitakuwepo lakini nakuhakikishia kukurudishia vyote vilivyochukuliwa na baba zako wadogo.”
“Lakashi mpenzi wangu wewe ni nani, mwanasheria au mpelelezi?”
“Mimi ni mtu wa kawaida ila ni mtetezi wa haki za watu.”
“Sasa utaipataje?”
“Hiyo kazi niachie ila kuna kitu nilisahau kukuambia kuhusu mama Edna, sasa hivi hali yake ni salama.”
“Lakashi umejuaje?”
“Lakashina huu si wakati wa kuulizana ni kukujulisha usichokijua, ila nakuonya kitu kimoja usiende kwa kina Edna kufanya hivyo ni kosa kubwa ambalo utalijutia maishani kwako.”
“Kwa nini Lakashi?”
“Unajua vizuri kuliko mimi.”
Majibu ya Lakashi yalimfanya Jeska abakie kimya asihoji lolote, Lakashi aliongeza kusema;
“Lakashina unafahamu kabisa kifo cha mzee Ezekiel kinatokana na yeye kutoka kwako, uongo?”
“Kweli.”
“Sasa unataka kwenda kufanya nini? Pia unakumbuka ulipokutana na Edna alipokuelezea ukamuone mama yake alikuwa mahututi hukuonesha ushirikiano kama kweli familia ile ilikulea. Leo ukienda utawaambia nini?”
“Basi Lakashi nimekuelewa.”
“Tuachane na hayo la muhimu usiku huu ni kufunga ndoa ya mimi na wewe kuwa mke na mume.”
“Lakashi tutafungaje ndoa ya watu wawili bila shehe wala padri?”
“Lakashina unakubali mimi niwe mumeo?”
“Hilo halina shaka.”
“Hujajibu, nakuuliza tena unakubali Lakashi kuwa mumeo?”
“Nakubali.”
”Lakashina hujanijibu vizuri, ngoja nikufundishe, mimi Lakashina nakubali Lakashi kuwa mume wangu.”
“Mimi Lakashina nakubali Lakashi kuwa mume wangu.” Jeska alirudia kama alivyoelekezwa na Lakashi.
Lakashi alirudia kumuuliza Jeska mara tatu naye Jeska alijibu mara tatu, baada ya hapo usingizi ulimpitia Jeska.
Usiku wa manane Lakashi alimuamsha Jeska kumuaga.
“Mahabuba amka nikuage muda huu ni muafaka wa kuondoka, ila sijui lini nitarudi lakini nakuhakikishia ukiwa na shida na mimi, utaniota ndotoni nami nitatokea na kukufariji kwa lolote utakalo.”
“Lakashi ndotoni utanitokea vipi nawe haupo?”
“Niamini kwa hilo, kesho kuna mtu atakuletea pesa za matumizi”
“Mmh Haya! Nakutakia safari njema.”
“Asante, ila nakuomba kitu kimoja kuanzia tulipofunga ndoa jina lako ni Lakashina usikubali kuitwa Jeska na wewe sasa hivi ni Muislamu.”
“Jamani nitaweza masharti ya dini?”
“Si ngumu utayaweza tu, kuanzia leo vaa nguo za heshima usinywe pombe.”
“Nitajitahidi.”
“Kwa heri mpenzi.”
“Nikusindikize.”
‘Hapana usiku ni mkubwa wee lala.”
Jeska alimvutia kifuani Lakashi kwa muda machozi yalimtoka kisha alimtazama usoni na kusema;
“Kwa heri mume wangu, nakuomba uwahi kurudi nina imani wewe ndiye mwanaume wangu sahihi. Kwa nini hukusubiri urudi ili tufanye hili?”
“Ni kweli usemacho dhamira yako mbaya ndiyo iliyosababisha yote haya, la muhimu zingatia, nikirudi nakuhakikishia kukupa maisha nusu ya peponi.”
“Kwa heri mpenzi wangu, nakuahidi kufanya kila ulilonieleza.”
Lakashi alimuaga Jeska na kutoka nje, Jeska alibakia amekaa kitandani hata usingizi ulivyompitia hakujua. Aliota yupo kwenye harusi kubwa ambayo hakuwahi kuiona katika maisha yake yote. Yeye akiwa bibi harusi aliyepambwa na kupambika na Lakashi akiwa bwana harusi. Katika harusi hiyo alivishwa pete ya almasi na mkufu wa dhahabu wenye jina la Lakashina.
Alipozinduka asubuhi alijikuta amelala kitandani kwake shingoni kulikuwa na mkufu wa dhahabu na mkononi pete ya almasi alishtuka.
Jeska aliishangaa pete ya almasi na mkufu wa dhahabu wenye jina la Kashina, alijiuliza ndoa ile kaifunga saa ngapi, mbona alikuwa kwenye njozi na kuota yupo kwenye ndoa lakini ajabu asubuhi kajiona akiwa na vitu alivyoviona ndotoni.
“Mmh, hii ina maanisha nini? Au? Hapana bwana huyu huenda ni Jini haiwezekani. Mungu wangu kama nimefunga ndoa na jini itakuwaje...Eeh Mungu nisaidie mimi.” Jeska alisema kwa sauti ya chini huku mkono mmoja kashikilia kifuani.
“Mmh, kama kweli sijui nitakuwaje?...Mbona kaniaga sijui anakwenda wapi na atarudi lini? Na...na...na nini hatima ya maisha yangu...Mmh! Ngoja tuone!”
Jeska alijinyanyua kuelekea bafuni kuoga, alijimwagia maji kujitoa uchovu baada ya kuoga alisimama mbele ya kioo kikubwa kujitazama. Juu ya ziwa la kushoto alishangaa kuona kuna maandisha rangi ya dhahabu yenye kumeremeta yaliyokuwa yameandikwa Lakashina.
Ilikuwa ajabu ya mwaka kuona maandishi yakimeremeta kama ndani ya mwili wake kuna taa. Alijaribu kufuta kwa mkono sehemu iliyokuwa na maandishi, vidole navyo vilianza kumetameta na hatimaye alijiona mwili mzima ukimetameta na sehemu yenye jina likimeta zaidi.
Kwa mshtuko alijikuta akianguka chini na kupoteza fahamu, aliposhtuka alijikuta amelala kitandani. Alijishangaa na kujiuliza maswali yasiyo na majibu juu ya kilichomtokea, pete ilikuwa kidoleni na mkufu ulikuwa kwenye droo ya kitanda. Aliiangalia pete iliyokuwa na uzuri wa ajabu lakini hakujua ni madini gani.
Alipotupa jicho pembeni lilitua kwenye mkufu uliokuwa na jina lake, aliubeba na kuutazama na kulisoma jina na kuurudisha kwenye droo ya kitanda. Alikwenda tena bafuni kuoga ili aende mjini kwa sonara kuulizia ile pete ni ya madini gani na mkufu una thamani gani.
Baada ya kuoga alisimama tena mbele ya kioo kuangalia alichokiona kilikuwa kweli au ndoto. Jibu lilikuwa lile lile kwenye ziwa la kushoto kuna jina lililoandikwa kwa maandishi ya dhahabu yenye kumetameta. Hakutaka kuhangaika nayo, alirudi chumbani na kubadili nguo ili awahi mjini.
Kutokana na maandishi yale aliona aibu kuvaa nguo alizozizoea za mikanda na matiti nje. Ilibidi avae za kujistiri mwili ili kuogopa watu kumuona kituko. Alipotoka sebuleni alikutana na mfanyakazi wake wa kike akiwa katika gauni lililonakshiwa uzi wa halili.
Alipomuangalia alishtuka, lakini Sara hakuonekana kushtuka.
“Za asubuhi Sara?”
“Nzuri tu dada Lakasina.”
“Wee Sara umeniitaje?”
“Lakashina au ulitaka nikuite Mrs Lakashi.”
“Nani kakutajia jina hilo?”
“Dada wewe mwenyewe jana kwenye harusi ulitueleza tusikuite tena Jeska bali Lakasina.”
“Mmh! Haya.”
“Safari ya wapi asubuhi asubuhi?”
“Nafika mjini mara moja.”
“Ni kweli shemeji amesafiri jana usiku?”
“Ni kweli wewe umejuaje?”
“Dada Lakashina mbona kila kitu kwako kigeni au jana ulikuwa unatutania si jina lako?”
“Ni kweli langu.”
“Sasa tatizo nini au tuendelee kukuita ulilolizoea la Jeska?”
“Hapana, kama umeweza kulishika hili jipya ni vizuri.”
Jeska wakati anajiandaa kutoka kengele ya mlango ililia, alimruhusu aingie alikuwa mlinzi wa mlangoni aliyekuwa amevaa suruali nyeupe na shati jeupe lenye maua shingoni, mikononi na pembeni.
Juu alivalia kikofia kidogo chenye maua kama ya kwenye shati na suruali, miguuni alivaa makubazi.
“Mnyalu leo umevaaje?”
“Dada si unajua tumerudi muda mbaya kutoka kwenye sherehe, nikaona niendelee na kazi zangu baadaye nitabadili.”
Maneno ya Mnyalu yalizidi kumchanganya na kujiuliza hiyo harusi wao waliijuaje wakati yeye muolewaje ameifunga kwenye njozi. Hakutaka kumshangaa sana, aliona kushangaa kumemchosha kila aliposhangaa walimshangaa yeye.
“Vipi Mnyalu ulikuwa unasemaje?”
“Kuna mgeni.”
“Anatoka wapi?”
“Sijamuuliza ila alitaka kukuona.”
“Mwanamke au mwanaume?”
“Mwanaume.”
“Mwambie apite ndani.”
Mnyalu alitoka na baada ya muda alirudi na mgeni aliyekuwa amevalia nguo kama za Mnyalu zilifanana kwa kila kitu hata makubazi aliyovaa. Wazo la haraka alijua ndugu yake Mnyalu.
“Karibu.”
“Asante, habari za hapa?” Mgeni alimsabahi huku akimpa mkono Lakashina (Jeska).
“Nzuri,” Lakashina alimtazama mgeni aliyekuwa amekaa kwenye kochi ameshikilia mfuko mdogo.
“Pole na pilikapilika za jana usiku?”
“Nn...nn...nzuri,” kauli ile ilimshtua na kujikuta ni yeye peke yake aliyehudhuria ndoa yake kwenye njozi tofauti na wote waliohudhuria kama kawaida.
“Mbona kama hujiamini?”
“Aa...aa...kawaida.”
“Nina imani una taarifa yangu?”
“Ipi?”
“Kutoka kwa Lakashi”
“Yupo wapi?” Lakasina alishtuka kumsikia Lakashi.
Itaendelea siku ya kesho...
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com

Post a Comment