AHADI YA NDOTONI - 05
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com
ILIPOISHIA
Jeska alikwenda hadi chumbani na kuiweka pesa yake chini ya mto kisha alitoka sebuleni alipomuacha mgeni. Lakini sebule ilikuwa nyeupe mgeni hakuwepo, alipotoka nje pia hakumkuta pamoja na gari lake. Sasa Endelea...
Alijiuliza mgeni ametoka vipi kwa muda mfupi bila kuaga wala gari lake kutoa muungurumo wakati wa kuondoka.
Hakutaka kuumiza akili yake zaidi ya kurudi sebuleni na kujitupia kwenye kochi na kujikuta akivuta taswira ya mzee Ezekiel na mipango yao kabambe ya kufunga ndoa na kuyabadili maisha yake kwa kumjengea jumba na kumnunulia gari la kifahari.
Moyo ulimuuma na kujikuta akilia peke yake kwa sauti ya chini huku akipiga mikono kwenye sofa na kusema kwa sauti.
“Haiwezekani kila baya kwa nini liwe kwangu, nimefiwa na wazazi nimedhurumiwa mali nimebakwa na mwisho niliyekuwa namtegemea amekufa kuna faida gani kuendelea kuishi bora nife.
”
Wazo la haraka lililomujia Jeska ni kujiua, alinyanyuka alipokuwa amekaa na kuelekea chumbani kwake, chini ya kitanda kulikuwa na kamba ya kuanikia nguo ndani wakati wa mvua. Aliichukua na kutoka nje ili aelekee kwenye mti ajiue.
Ajabu ya mwaka aliyokutananayo kidogo apige kelele ya woga baada ya kumuona mgeni akiwa amekaa kwenye sofa akimtazama.
“Ha!” Jeska alishika mkono kifuani kwa mshtuko.
“Mbona umeshtuka?” Mgeni alimuuliza huku ameachia tabasamu pana.
“Ha..a..a..pa..na,” Jeska alijibu kwa kubabaika.
“Hiyo kamba ya nini?”
“Aa..aa. ya kawaida.”
“Unajua kutaka kujiua ni kuingilia kazi ya muumba kwa vile lazima ufe.”
“Umejuaje?”
“La muhimu si kujua nimejuaje zaidi ya kukuonya tena usiingilie kazi ya muumba.
”
“Lakini wewe nani?” Jeska alimuuliza.
“Jeska hata ukinijua si muhimu zaidi ya kujipanga kwa maisha mapya na si kukimbilia kujiua.
”
“Ulikuwa wapi mbona nilitoka muda mfupi hukuwepo?”
”Nilikuwa nimeondoka kwa vile nilikuwa na haraka nisingeweza kukusubiri, lakini uso wako ulionesha una dhamira mbaya moyoni mwako kitu kilichonifanya nirudi kabla hujachukua uamuzi mbaya.”
“Nina faida gani ya kuendelea kuteseka kila siku.”
“Nimekueleza nitakusaidia unataka msaada gani zaidi ya huo?”
“Basi nisamehe, nimechanganyikiwa na maisha.”
“Nimekusamehe naomba unisindikize, ila nakuomba usirudie kufanya ujinga wowote, sawa?”
“Sawa.”
Walitoka hadi nje ambapo mgeni aliingia kwenye gari lake Jeska alimfungulia geti na mgeni aliondoka na kumpungia mkono. Jeska alilisindikiza gari lile kwa macho mpaka likapotea huku akijiuliza mtu yule ni nani mbona kama anaonekana wa ajabu ajabu. Lakini aliamini yale ni mawazo yake kutokana na kuchanganyikiwa na maisha.
Jeska alirudi ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwake na kujilaza chali macho alitazama juu ya dali.
Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi juu ya yule mwanaume msamaria mwema. Alijiuliza ni mtu wa aina gani, bado alipingana na akili yake pengine kuchanganyikiwa ndiko kulikomfanya hata alipotoka hakumuona. Lakini kama hakumuona sebuleni hata gari lake. Bado alibakia njia panda asijue ukweli ni upi.
Kingine kilichomchanganya mtu yule kujua mambo yake mengi, wazo la kuwa mtu yule labda jini hakuwa nalo zaidi ya kuamini mtu yule alikuwa akimjua vizuri kuliko alivyojifahamu yeye mwenyewe. Akiwa amejilaza akitazama juu kwenye dari hakuona faida ya kuendelea kuishi hata kama yule mwanaume angeamua kumsaidia bado asingeweza kuyamudu maisha.
Bado shetani mbaya hakuwa mbali naye ufumbuzi mkubwa katika maisha yake ilikuwa ni kuyakatisha maisha yake. Jeska aliamini hakuna mtu wa kumsaidia tena katika maisha yake. Wazo la kujinyonga bado halikuwa mbali naye alikurupuka na kwenda kuchukua kamba aliyoirudisha chumbani na kutoka nayo tena kwa kujiamini ili akajinyonge.
Alitoka mpaka nje kabla ya kuchukua uamuzi ule mzito alimtuma mfanyakazi wake wa ndani sehemu ambayo aliamini mpaka atakaporudi atamkuta ameisha jinyonga. Hata mlinzi vilevile alimtuma mbali ili tu awe huru kutekeleza mpango wake wa kujinyonga.
Baada ya kukagua eneo lilo na kuliona lipo katika hali ya utulivu, alichukua kamba yake na kuzunguka nyuma ya nyumba kwenye miti na kuifunga kwa kupanda kwenye mti. Alikumbuka alisahau sturi ya kupandia. Alirudi ndani kuchukua kwa haraka kabla hawajarudi wafanyakazi wake.
Alipofika ndani alichukua sturi na kuzunguka nayo nyuma ya nyumba ili atimize dhamira yake ya kujinyonga.
Wakati anatoka ndani alikutana na mfanyakazi wake wa ndani.
“Dada mbona una kisu mkononi?”
“Wewe Sara mbona umewahi kurudi?” Jeska alimuuliza kwa hasira.
“Dada ulichonituma nimekipata hata kabla ya kufika uliponituma tena kwa bei nafuu.”
“Sikiliza Sara kukutuma kule nilikuwa na maana yangu nakuomba urudi upesi kachukue pesa ndani uwahi haya mafuta siyataki,” aliyapigiza mafuta ukutani kwa hasira, chupa ilipasuka na mafuta kutawanyika.
“Sasa dada mbona ni kitu kile kile tu.”
“Sara siku hizi tumekuwa tunabishana?”
“Dada siwezi kurudi roho inaniuma.”
“Kwa nini?”
“Kwa uamuzi unayotaka kuchukua.”
“Uamuzi gani?”
“Ya kutaka kuyakatisha uhai yako.”
“Wewe Sara umejuaje?” Jeska alishtuka kusikia vile.
“Nijueje? Wakati uso wako unaonesha una dhamira mbaya ya kutoa uhai wako.”
“Aah!” Jeska alipigwa na bumbuwazi mpaka kisu kikamponyoka.
“Lakini dada kwa nini usimsikilize mgeni?”
“Mgeni, mgeni gani?”
“Eeh, yule kaka aliyekuleta mchana.”
“Alisemaje?”
“Si alisema atakusaidia kila kitu.”
“Basi Sara nimekuelewa.”
Jeska alisema huku akigeuka arudi ndani, alishtuka kumuona mlinzi akiwa anatokwa machozi.
“Ha! Mnyalu umerudi saa ngapi?”
“Sijaenda popote bosi.”
“Kwa nini hujaenda popote na kwa nini unalia?”
“Sijaenda kwa kuhofia nikiondoka utajiua na ninalia kwa vile ukifa nitafanya wapi tena kazi.”
“Umejuaje dhamira yangu.”
“Inajionesha usoni kwako.”
Kauli ile ilimshtua sana Jeska na kujiuliza uso wake unaonesha vipi dhamira iliyokuwa moyoni mwake. Alipanga akienda ndani akajitazame usoni ili aione dhamira yake usoni kwake inaonekana vipi.
“Mnyalu si unajua maisha magumu unafikiri baada ya kufa mzee mimi nitawezaje kuyahimili maisha haya. Kwa sasa hivi nina uwezo lakini huko mbele mambo yatakuwa magumu sana, nitatakiwa nilipe kodi ya mwaka milioni mbili na laki nne kazi sina nitazipata wapi.
“Bado mshahara wenu kula yetu mnafikiri Jeska mimi nitafanya nini, Mnyalu wewe si mgeni kwangu nimeisha kueleza siri yangu ya maisha. Umeona jinsi mikosi inavyoniandama unafikiri mwisho wake nini?”
“Lakini mbona mgeni alisema atakusaidia?”
“Mnyalu umejuaje?”
“Ma mdogo Jeska si muhimu kujua nimejuaje ila kumsikiliza mgeni alivyokuonya asiyakatishe maisha yako pia yupo tayari kukusaidia.”
Maneno ya Sara na Mnyalu yalizidi kumchanganya Jeska na kukubaliana na ombi la wafanyakazi wake kuwa asiyakatishe maisha yake. Aliamua kurudi ndani huku moyo ukimuuma kwa uamuzi wa kijinga wa kutaka kuitoa roho yake bila sababu.
Aliingia hadi chumbani kwake na kupiga magoti mbele ya kitanda kumuomba Mungu amsamehe kwa yote aliyoyataka kufanya. Baada ya kuomba toba ya majuto huku akilia alijikuta akilala kwenye zuria bila kujijua. Alishtushwa na sauti ya Sara.
“Dada...dada.”
Kabla ya kuitikia alijiangalia alipokuwa amelala kwenye zuria pembeni ya kitanda. Alijinyanyua alipokuwa amekaa kwenda kufungua mlango, alikutana na Sara akitweta huku jasho likimtoka.
“Vipi Sara mbona hivyo?”
“Samahani dada nilikuta foleni kubwa.
“Ya nini?”
“Si uliponituma.”
“Kukutuma nini tena?”
“Dada si ulinituma nikufuatie mafuta.”
“Mafuta! Mbona sikuelewi si uliishaleta.”
“Dada nimeleta saa ngapi na mimi sasa hivi ndio nafika.”
“Sara mbona sikuelewi unafika vipi wakati mafuta umeishaleta.”
“Dada utakuwa anachanganyikiwa, umenituma mafuta na kunieleza nisinunue popote zaidi ya uliponituma na sasa ndiyo narudi.”
“Sasa haya ni maajabu, sasa Sara aliyeniletea mafuta ni Sara gani?”
“Kwani kuna mtu kakuletea mafuta?”
“Sio mtu bali wewe Sara, hebu acha kunichezea akili.”
“Kweli dada mimi ndiyo nafika.”
“Mmh, mbona nazidi kuchanganyikiwa aliyekuja na kunikataza nisijiue ni Sara gani?”
“Ha! Dada ulitaka kujiua?”
“Ha..ha..a..pana.”
Wakati akiwa bado yupo njia panda mlinzi wake aliingia.
“Ma mdogo Jeska ulichonituma nimezunguka kila kona nimekosa.”
“Mmh, Mnyalu na wewe unataka kunichezea akili kama Sara au mmepanga kunitania?”
“Kivipi Ma mdogo?”
“Wewe si uliniambia hukuondoka baada ya kugundua nataka kujiua?”
”Mungu wangu! Mamdogo ulitaka kujiua?”
“Jamani mbona unanichezea akili?”
“Dada kwani vipi mbona kama umechanganyikiwa?” Sara alimuuliza Jeska ambaye aliamini walikuwa wakimchezea akili.
“Jamani hebu acheni kunichezea akili ni kweli ndio mnafika?”
“Dada tokea lini nikakudanganya, sijui kaka Mnyalu.” Sara alijitetea.
“Hata mimi sijawahi kukutania, unasema kuna mtu kama mimi alikuja kukueleza usijiue labda malaika hakutaka kuona unaukatisha uhai wako.”
“Hata siamini bado hayajaniingia kichwani.”
“Dada kwa upande wangu ndio nafika toka uliponituma nitawezaje kwenda kule na kisha niwepo hapa kwa wakati mmoja?”
“Sawa hamkuwepo ni nani anayefanana na wewe na mwingine na Mnyalu waje kwa wakati mmoja kwa umbile na mavazi yenu?”
“Dada labda ulikuwa umelala ukaota lakini mimi sikiwepo,” Sara alizidi kujitetea.
“Hata mimi,” Mnyalu naye alikana kuwepo.
“Mmh, sawa.”
“Lakini dada kwa nini ulitaka kujiua?” Sara alitonesha kidonda.
“Jamani naomba mniache kwanza.”
“Tutakuacha tu dada, lakini kwanini unataka kututia ukiwa?” Mnyalu naye aliuliza.
“Jamani nimechanganyikiwa mwenzenu na maisha,” Jeska alijitetea baada ya kubanwa sana.
“Ma mdogo Jeska kujiua bado si suruhisho la matatizo kwa vile kila kiumbe kina haki ya kufa, kuingilia kazi ya Mungu ni kujiongezea matatizo.”
“Basi jamani nimekosa nisameheni sirudii tena kuchukua uamuzi kama huo.”
“Sawa dada.”
Walimuacha Jeska akirudi chumbani kwake kupumzika na kila mmoja alikwenda kuendelea na kazi yake. Jeska akiwa kitandani amejilaza alijikuta akijawa na mawazo mengi juu ya kile kilichomtokea cha Sara na Mnyalu kuonekana wakimsihi asijiue na baadaye kuonekana katika sura nyingine kila mmoja akikana hakuwepo muda ule.
Bila kujielewa usingizi ulimpitia, aliposhtuka alishangaa kujikuta amelala kwenye nyumba ngeni kwake. Lakini chumba kilikuwa kizuri sana kilichokuwa na mapambo na harufu nzuri hewa yake ilikuwa nzuri sana. Pembeni yake alikuwa amelala yule bwana msamalia mwema aliyemuahidi kumsaidia.
Yule bwana alikuwa kwenye usingizi mzito, Jeska alijiuliza pale ni wapi na amefikaje. Alijikuta akiwa na shauku ya kutaka kumuamsha yule bwana amuulize pale ni wapi na amefikaje.
Kabla hajamshika upepo mwanana mzuriii wenye harufu nzuri ya manukato ulimpiga usoni na kujikuta ukipatwa na usingizi na kujilaza pembeni ya yule bwana. Jeska alishtuka siku siku ya pili na kujikuta amelala kitandani kwake.
Alikurupuka kitandani na kutoka hadi nje ya chumba chake.
Milango ilikuwa bado imefungwa kuonesha hakuna aliyeingia wala kutoka. Alitamani kuita lakini ajabu aliyetaka kumwita hakumfahamu jina. Alikwenda msalani na bafuni lakini hakumuona mtu.
Alijiuliza mtu yule aliyekuwa naye usiku yupo wapi?
Bado hakuamini alitoka hadi kwa mfanyakazi wake wa ndani kumuuliza.
“Sara.”
“Abee dada.”
“Mgeni umemuona?”
“Mgeni gani?”
“Si yule kaka wa jana.”
“Wala sijamuona.”
Hakuongeza neno aliondoka hadi getini kwa mlinzi.
“Mnyalu kuna mgeni yoyote?”
“Hataa.”
“Mnyalu ina maana gari la mgeni wa jana mchana hukuliona?” ”Sijaona gari wala mtu.”
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?” aliuliza swali bila kujua anayemuuliza hajui lolote.
“Nani?”
“Ok, basi.”
Jeska aligeuka kurudi ndani huku akiamini kabisa mgeni alilala naye chumba kimoja, kingine kilichomchanganya ni sehemu aliyokuwa amelala kwenye chumba chenye hewa na uzuri wa ajabu. Jeska aliamini alichokiona hakikuwa ndoto bali kitu cha kweli.
Kilichomshangaza zaidi kidoleni pete yake ya uchumba aliyovalishwa na mzee Ezekiel haikuwepo, kila dakika alijikuta akizidi kuchananyikiwa na kila kilichokuja mbele yake. Alizidi kuingiwa na wasiwasi na kujiuliza yule mgeni ni nani ni mtu wa kawaida au jini. Lakini bado hakukubaliana na mawazo yake, alijikuta akiwa na shauku kuonana na mgeni kutaka kumuuliza mambo yanayomtatiza juu yake.
Asubuhi kama alivyoelezwa na mgeni alikwenda chini ya mto na kuzitoa fedha alizopewa na mgeni za matumizi. Alifunua mto na kuzitoa zile fedha ambazo alinunua vitu muhimu kwa ajili ya chakula cha siku ile. Wazo lilikuwa kumpikia chakula mgeni kama atakuja mchana, lakini hakujua mgeni anakula chakula gani.
Baada ya kuzigawa pesa kwa ajili ya matumizi ya siku ile, alioga na kufungua kinywa kisha alifanya usafi wa kitanda. Ajabu wakati akiondoa mto ili atandike alishtuka kuzikuta tena noti mpya za elfu tano tano kama alizozitoa asubuhi zipo chini ya mto.
Alijiuliza zile pesa alichukua au vipi, alitandika na kuzirudisha chini ya mto, alipanda kitandani na usingizi haukuchelewa ulimchukua.
Nini kitaendelea? Kuyajua yote tukutane SIKU YA KESHO HAPA HAPA.
TOA MAONI YAKO JUU YA SIMUIZI HII HAPACHINI
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com

Post a Comment