ad

ad

AHADI YA NDOTONI - 02


ILIPOISHIA:
“Akikuuliza mama yako mweleze ni ya kijana mmoja konda wa daladala.”
“Sawa baba.”
“Ila kesho nina safari ya kikazi kwa wiki nzima nikirudi tutaitoa, ila naomba iwe siri yako”
“Sawa baba.”
ILIPOISHIA WIKI JANA
Siku ya nne toka ingundulike mimba ya Jeska, maswali ya wanafunzi wenzake juu ya hali yake yalimnyima raha, wapo waliodiriki kumwambia.
“Jeska tuna wasiwasi huenda wewe ni mjamzito.”

Maneno yale yalimchanganya na kumnyima raha, alijikuta akiona siku haziendi muda alioelezwa na baba Edna amsubiri unachelewa. Wazo la haraka lililoingia kichwani mwake ni kwenda kuitoa ile mimba kwa vile pesa za kutolea alikuwa nazo.

Jeska baada ya maneno ya chini chini kuhusiana na ujauzito aliokwanao, alipanga siku ya pili wakati wa mapumziko atoroke kwenda kuutoa. Siri ilibakia moyoni mwake kwa kuogopa kuwashirikisha watu wengine. SASA ENDELEA..
***
Usiku ulikuwa mgumu kwa Jeska alifikiria mengi katika maisha yake, aliamini mkosi ndiyo uliokuwa sehemu kubwa ya maisha yake. Familia yake ilifariki akiwa hajui lolote, mali aliyoachiwa na wazazi wake nayo ndugu wa baba yake waliihodhi yote na mwisho walimfukuza huku wakimtishia kumuua.

Hata aliyeonekana mwokozi wake, mwisho kumbaka na kibaya kampatia ujauzito. Shuleni nako maneno ya chini chini yaliishaanza juu ya hali yake ambayo wazoefu walianza kujua ni ujauzito. Wasi wasi wake ulikuwa mwisho kuchukuliwa na kupelekwa kupimwa.

Aliamini kama angepelekwa kupimwa na kugundulika mjamzito na kusimamishwa shule. Kitendo kile kingemuathiri kisaikolojia hata shule ingemshinda kusoma baada ya kujifungua.
Aliona kumsubiri mzee Ezekiel baba yake Edna ni kuongeza tatizo juu ya tatizo.

Msimamo ulikuwa ule ule siku ya pili baada ya mapumziko atoroke na kwenda kutoa ujauzito. Kutokana na taarifa za juu juu utoaji wa mimba changa hauchukui muda mrefu, mtu wa mfano ilikuwa kwa msichana Fatuma aliyejulikana mjamzito lakini alitoa mimba siku moja na siku ya pili alikuja shuleni kama kawaida.

Usingizi ulimchukua usiku wa manane, hata alfajiri alipoamka bado kichwa kilikuwa kizito kwa kuchelewa kulala. Siku hiyo alionekana mtu mwenye mawazo mengi japo alijitahidi kuchangamka, lakini kuna muda hujisahau na kurudia mawazo yake.

Baada ya kuamka na kujiandaa na shule, Edna aliiona ile hali alijitahidi kumchangamsha shoga yake.
“Jeska vipi mbona unanitia ukiwa, si kila kitu kimekubaliwa hata kama baba wa mtoto humjui lakini wazazi si wamejitolea kukulea wewe na mtoto wako hata elimu wamesema watampa?”

“Ni kweli, lakini ujauzito huu umenivurugia kila kitu katika maisha yangu.”
“Lakini Jeska ni wewe ulikuwa mstari wa mbele kunishauri juu ya kujikinga na mapenzi kipindi hiki cha masomo au ndiyo kinyozi hajinyoi.”

Kauli ile ilimfanya Jeska atokwe na machozi huku akiamini kabisa Edna angejua kilichomsababishia kuwa katika hali ile asingesema yale. Machozi ya Jeska yalimtisha Edna na kujutia kauli yake.
“Basi samahani kwa kauli yangu sina nia mbaya kwako, naomba unisamehe sana.”

“Edna, najua hujui na ukijua utanionea huruma na kuamini kauli yangu ya kukatisha maisha yangu ungeiunga mkono.”
“Nisijue nini wakati mama alinieleza kila kitu.”

“Edna wewe na mama yako hamjui kitu, nitaumeza mfupa huu mpaka hapo Mungu atakapochukua maisha yangu.”
“Jeska, kuna nini mbona unanitisha au umeathirika?”

“Mara mia moja ningeathirika ningeshangilia kwa vile siku hizi watu wanatumia dawa ya kupunguza makali na kufuata ushauri na kuishi maisha marefu kuliko hata wasio athirika.”

“Jeska shoga yangu kuna siri gani tena ambayo hutaki niijue? Kumbuka wewe ni zaidi ya ndugu maisha yetu tumekuwa tunashirikiana kwa kila kitu. Kwa nini leo unanificha siri ambayo nina uwezo hata kuwashawishi wazazi wangu kuitatua kama mimi itanishinda.”

“Edna, nina imani ukijua ukweli ninaweza kukuharibia mudi yako ya masomo.”
“Kuhusu nini?”
‘Ujauzito huu.”

“Kwani una nini?”
“Kumjua mwenyewe.”
“Mwenyewe, si konda au kuna mwingine?”
“Yupo, wala si konda ila mwenyewe alinieleza nimueleze mama kuwa ujauzito ni wa konda.”

“Jeskaaaa! U...una...taka kuniambia konda si mwenye ujauzito huu?”
“Ni kweli ila ipo siku mwenye ujauzito utamjua au usimjue kabisa, nina imani nikimtaja mbele yenu huenda nikautua mzigo lakini huenda nikamtwisha mwingine jambo ambalo sipendi litokee.”

Mzee Ezekiel na mkewe walikubaliana Jeska asiguswe kwa lolote bali apate msaada kama sehemu ya familia.
Baada ya makubalino yale, Edna alimueleza mama yake uamuzi mzito aliotaka kuuchukua. Mama Edna alishtushwa na habari zile, alimfuata Jeska aliyekuwa chumbani amejilaza akilia.

“Jeska...Jeska mwanangu amka mama.”
Jeska alinyanyuka huku macho yakiwa yamemvimba kwa kulia, mama Edna alishtuka na kuamini uamuzi mbaya wa Jeska yeye ndiye muhusika kwani alionesha kumtenga toka walipotoka hospitali bila kumpa majibu muhusika.

Mama Edna alishtuka hali aliyomkutanayo Jeska ilimshtua sana.
“Jeska mwanangu mbona hivyo mama?”
“Hapana kawaida?”
“Unaumwa?”
“Hapana.”
“Sasa nini?”
“Kawaida tu mama.”

“Hapana Jeska mwanangu najua jinsi gani nilivyokukosea.”
“Hujanikosea mama.”
“Si kweli Jeska, nakiri kufanya kosa, kwanza naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea.”
“Mama hujafanya kosa lolote.”

“Ni vigumu kuliweka wazi lililokusibu moyoni mwako, naweza kusema baada ya kutoka hospitali mimi kama mzazi nilijikuta nachanganyikiwa na kushindwa kuamini nilichoambiwa hospitali na jinsi nilivyokuwa nakuamini.”
“Ni kweli mama, mimi ndiye mkosefu kwa tukio lililotokea wa kuomba msamaha ni mimi.”

“Hapana Jeska, napenda kukueleza kitu kimoja, sisi ni wazazi na wajibu wetu ni kuwatunza ninyi. Hivyo lazima tukasirike mnapokosea kuonesha jinsi gani tusivyokubaliana na yaliyotokea. Lakini mwisho wa yote ni kukusamehe kwa vile imeisha tokea.”

“Sawa mama nimekusikia, lakini nimeisha yatia doa maisha yangu.”
“Hapana Jeska, kukosea ni sehemu ya kujifunza. La muhimu ni kumtafuta huyo mwenye mzigo huo ili tujue nini majaliwa baada ya mtoto. Ila malezi yako na hali yako bado itabakia mikononi mwetu.”
“Sawa mama.”

“Nani mwenye mzigo huu?”
“Konda wa daladala”
“Mmh, haya...yupo wapi?”
“Siku hizi simuoni wala hajui kama siku tulipokutana aliniachia ujauzito huu.”
“Umekutana mara ngapi.”

“Mara moja ilitokea kama ajali, yaani najuta,” Jeska alisema kwa sauti ya kilio ambayo ilionesha kweli anajua. Lakini alifunika kombe mwana haramu apite.
“Sawa, basi tuliza mawazo tutailea mimba na mtoto akizaliwa vile vile tutamlea na ukijifungua tutaendelea kukusomesha.”
“Nitashukuru mama.”

“Basi mama naomba usilie na kujiona umefanya kosa kubwa, la muhimu ni kujifunza kutokana na makosa. Usifanye chochote kibaya cha kujizuru, sawa mama.”
“Sawa, nitafanya hivyo mama yangu.”
“Basi twende ukale.”

“Sijisikii kula mama.”
“Hapana nyanyuka mwanangu mzuri.” Mama Edna alimbembeleza Jeska huku alimshika mkono na kunyanyua, Jeska naye hakutaka kumbishia mama yake alinyanyuka na kutoka naye nje.

* * *
Siku zilikatika huku Jeska akiendelea kumeza mfupa wa siri nzito juu ya ujauzito aliopewa na baba Edna. Alijitahidi kuzuia hali yake kila akiwa shuleni ili wasimgundue kama mjamzito kutokana na kusinzia kila wakati na kichefuchefu.

Siku ya nne toka ingundulike mimba ya Jeska, maswali ya wanafunzi wenzake juu ya hali yake yalimnyima raha wapo waliodiliki kumwambia.
“Jeska tuna wasiwasi huenda wewe ni mjamzito.”
Maneno yale yalimchanganya na kumnyima raha, alijikuta akiona siku haziendi muda alioelezwa na baba Edna amsubiri unachelewa. Wazo la haraka lililoingia kichwani mwake , kwenda kuitoa ile mimba kwa vile pesa za kutolea alikuwa nazo.

Jeska baada ya maneno ya chini chini ya kumfikiria mjamzito, alipanga siku ya pili wakati wa mapumziko atoroke kwenda kutoa ujauzito. Siri ili ilibakia moyoni mwake kwa kuogopa kuwashirikisha watu wengine.
Baada ya kufika alikutana na daktari ambaye walikubaliana kiasi cha pesa kwa ajili ya kazi ile. Jeska alipanda kitandani kwa ajili ya kutolewa mimba, daktari alianza mara moja kufanya kazi yake ya kumsaidia Ziraili mtoa roho kutoa roho ya kiumbe kisicho cha hatia.

Katika utoaji wa mimba mambo hayakwenda kama alivyozoea damu ilimtoka nyingi sana. Mganga alichanganyikiwa hali ya Jeska ilikuwa mbaya sana, cha kwanza kukifanya kilikuwa kufanya kazi ya ziada ya kuzuia damu ambayo ilitokana na makosa ya utoaji mimba.

Baada ya kufanikiwa kuzuia damu hali bado ilikuwa mbaya sana kutokana na kupoteza damu nyingi. Daktari alimuhamishia katika chumba kingine ili kumpumzisha akipata nguvu aende kwao. Dokta alifanya siri ikiwemo kumpelekea chakula cha kumpa nguvu, Jeska alikula kwa shida baada ya kula alimdunga sindano ya usingizi ili apumzike kwa muda kabla ya kiza kuingia ili aende kwao.

Majira ya saa mbili dokta alimtoa Jeska ambaye afya yake haikuwa nzuri alitembea kama mtu aliyelewa. Alimkodia gari hadi kwao na kumueleza dereva akiisha mshusha tu asisubiri kitu atimue zake kukwepa ushahidi. Jeska alipofikishwa kwao baada ya kuteremka kwenye gari, gari liliondoka bila kujua kama amefika salama. Jeska alitembea kizunguzungu kikiwa kikubwa sana hakuweza kufika mbali alianguka chini.

Wapita njia ndiyo waliomuona amelala chini pembeni ya geti la nyumba moja. Watu walimshangaa binti mwenye nguo za shule ambaye alionekana akitokwa na damu kwenye miguu hata siketi yake nayo ilikuwa imelowa damu. Kila mmoja alisema lake wengi waliamini huenda amebakwa.

Mmoja kati ya wale watu alimtambua Jeska na kuwaeleza yule ni msichana wa nyumba iliyokuwa mbele yao. Mmoja wa watu waliokuwa pale walikimbia kwenda kugonga mlango na kuwaita waliokuwa ndani. Wa kwanza kutoka alikuwa Edna, baada ya kupewa taarifa zile alikimbilia kwenye kundi la watu waliokuwa wamemzunguka Jeska aliyekuwa hajitambui.

Hata bila ya kumtambua vizuri nguo na viatu alijua ni Jeska, aliangua kilio kilichowashtua waliokuwa ndani. Mama Edna alifika kwenye tukio na kukuta Jeska amelala chini hajitambui damu zikimtoka chini kuonesha kuna kitu kibaya kafanyiwa.

Kwa haraka walimbeba juu juu na kuchukua gari mara moja alikimbizwa hospitali.
Alipofikisha uchunguzi wa haraka ulionesha alifanyiwa zoezi la utoaji mimba uliofanyika vibaya na kusababisha kutokwa na damu nyingi sana zilizosababisha kupoteza nguvu.

Ilifanyika huduma ya haraka kuyaokoa maisha ya Jeska kwa kuongezewa damu na kutibiwa majeraha aliyopata wakati wa kutoa mimba.
Mama Edna alitaka kujua kama zoezi alilofanya Jeska la utoaji wa mimba lilifanikiwa.
“Eti baba alifanikiwa kuitoa mimba?”

“Ndiyo mama, vipimo vinaonesha mimba imetoka.”
“Mungu wangu mbona mtoto huyu ana mazito hivi, nilimuonya asiitoe japo baba yake hakumjua lakini sijui shetani gani aliyemvaa na kufanya mauaji ya kiumbe kisicho na hatia.”
“Poleni sana.”

“Hatujapoa baba na hospitali iliyofanya hivi lazima tuishitaki.”
“Nafikiri kuna umuhimu wa kufanya hivyo.”

Daktari aliwaomba warudi nyumbani wakapumzike kwani hakukuwa na madhara zaidi waliamini damu atakayo ongezwa itamsaidia kumrudisha katika hali yake ya kawaida. Ila walishauriwa kumpima virusi vya Ukimwi kwa usalama zaidi wa afya yake.

Baada ya kutolewa wasiwasi mama Edna na Edna walirudi nyumbani huku wakizidi kumuombea dua ili atoke salama. Njiani Edna tukio la Jeska alilimsukasuka moyoni kiasi cha kumfanya akose raha, maneno ya Jeska kukanusha ujauzito ule siyo wa konda ina mtu ambaye hakutaka kumtaja ulimsumbua sana. Itaendelea Siku zote.

No comments

Powered by Blogger.