USIKU WA KIGODORO - 11
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
ILIPOISHIA:
“Kwanza unatakiwa urudi mapokezi, uliona bosi amekuja huku ina maana amekupigia simu sana mapokezi hukupokea.”
“Mh! Huo ni mtihani mwingine,” alisema Lina akionekana ana wasiwasi kupita kawaida.
Baada ya nusu saa akiwa bado kwenye jiko, alisikia simu ya mapokezi inaita…
SASA JIACHIE…
“Mh! Naitwa sasa,” alisema Lina huku akijishika kifuani kama ishara ya kuogopa.
Alitoka hadi mapokezi, akapokea…
“Haloo bosi.”
“Njoo uchukue vitu vyako.”
Lina alikata simu, akatembea kwenda chumbani huku moyoni akisema…
“Liwalo na liwe tu, sasa nitafanyaje? Kwanza ni afadhali ajue ili hili zigo linitue, nitaishi kama mkimbizi hadi lini sasa?”
Lina aliingia kwenye ofisi ya bosi wake huyo akapata mshtuko kutomuona James…
“Chukua vyombo vyako bwana,” alisema bosi wa Lina huku akiwa ametumbulia macho vyombo hivyo. Lina alitamani sana kumuuliza aliko mgeni, lakini kwa sababu ya cheo alishindwa. Akatoka haraka mpaka jikoni…
“Nikwambie kitu mama angu, sijamwona James kule kwa bosi,” alimwambia mama wa Chai…
“Mh! Ina maana ameondoka au?”
“Sidhani, nahisi amekwenda chooni.”
Dakika tatu mbele wakasikia watu wakitoka huku wanaongea…
“Hao wanatoka sasa,” alisema Lina.
Ni kweli, bosi wa Lina alikuwa akimsindikiza James huku wakiongoea mambo mbalimbali ya biashara.
Lina alipotoka, alisimama mapokezi na kumwona James akiishia na gari lake huku bosi wake akirudi…
“Lina,” aliita bosi huyo.
Lina moyo ukamlipuka lip!
“Abee bosi.”
“Unamfahamu mtu anaitwa James?”
Lina alitaka kuanguka chini, alihisi haja ndogo lakini akajikaza…
“Ni yupi huyo bosi?”
Lina alipojibu hivyo, bosi wake alikaa kwenye kiti cha wageni lakini kabla hajasema neno akasimama akimwambia…“Hebu twende ofisini kwangu kwanza.”
Lina alisimama, bosi wake alitangulia mbele, yeye akafuata nyuma. Alijua ishu imeshasanuka, ameshagundulika ni muongo, tapeli mkubwa.
“Karibu,” alisema bosi huyo.
“Asante.”
Bosi huyo alimwangalia kwa muda Lina kisha akaanza…
“Humjui James?”
“Yupi huyo bosi?”
“We unamjua James yupi?”
“Mimi namjua James kijana mmoja anakujaga hapa.”
“Leo kaja?”
“Sina hakika.”
“Huna hakika? Kwani maziwa ulimletea nani?”
“Bosi, nilipoleta maziwa nilimkuta mgeni anasoma gazeti la Daily News, wala sikumwona sura. Nilipofuata vyombo sikumkuta, labda alikuwa chooni. Kwa hiyo sijamwona.”
“Oke. James huyo unayemsema wewe ni nani yako?”
Lina alikaa kimya kwa muda akijiinamia…
“Bosi ni stori ndefu.”
“Kama ipi Lina? Mbona una hatari wewe msichana?! Yaani na uzuri wako wote unakuwa tapeli wa mapenzi?”
“Nimekosa bosi.”
“Umekosa nini sasa?”
“Nimekuwa mwongo kweli.”
“Mimi nilikuwa sijui lolote, leo ndiyo kaniambia unajua mimi nimefunga ndoa ya Lina? Nikamuuliza Lina gani? Akasema Lina mfanyakazi wako. Nilishtuka sana. Mimi ninavyojua wewe umefunga ndoa na Semi, sasa kusikia umefunga na mwanaume mwingine da..!
“Nikamuuliza unaishi naye? Akasema ndiyo, ila kasafiri kwenda kwao Korogwe, Tanga mama yake ni mgonjwa. Kidogo niseme yupo na nikuite mbele yake lakini nikajua kuna siri imefichwa, ndiyo maana kumbe hukai mapokezi ulimwona akiingia, si ndiyo?”
Lina alikubali kwa kutingisha kichwa juu kwenda chini na kurudi tena juu kuashiria amekubali alichoambiwa.
“Hebu niambie, nini kilitokea?” aliuliza bosi huyo huku akijiweka vizuri.
Lina naye alikaa sawa, akamwangalia bosi wake huyo kisha akaangalia ukutani. Aliporudisha macho kwa bosi wake akafunguka kuanzia mwanzo wa kukutana na James kazini hapo, ndoa hadi siku hiyo ambayo James alimwambia yeye yupo Korogwe...
“Mh! Lina, mbona una hatari wewe halafu mambo yenyewe mazito. Sasa unadhani nini kitatokea mbele?” aliuliza bosi huyo huku akimkazia macho Lina…
“Hata sijui bosi. Lakini nimeamua kukwambia ukweli wote ili kama unaweza kunisaidia ufanye hivyo.”
“Mh! Cha kukusaidia sina Lina, naamini ni wewe kujisalimisha kwa James na kumwambia ukweli maana yeye ndiyo hana ndoa na wewe na si Semi…”
“Je, nikimwita mbele yako nikatubu kwake?”
“Unahisi itawezekana? Hilo ni suala la kijamii zaidi tena kifamilia. Kulizungumzia ofisini si sahihi, mbaya zaidi kitendo hicho kinaichafua kampuni.”
Lina alijiinamia kwa muda akitafakari jambo huku akiwa hana la kusema na bosi wake huyo alikuwa akimwangalia tu huku akipangapanga vitu mezani kwake japokuwa havikuwa katika mpangilio mbaya.
“Unamjua nani katika marafiki wa James?” aliuliza bosi huyo.
“Hakuna.”
“He! Kweli? Mbona ni tatizo kubwa sana. Yeye anamfahamu nani kwenye ukoo wako?”
“Hakuna.”
“Mh!”
Wakati wanaendelea kuzungumza, mara mlango uligongwa, bosi akauliza nani?
“James.”
“Mh!” aliguna kwa mshtuko Lina lakini kwa sababu alishamweleza bosi wake kila kitu ikabidi bosi huyo aamue kwa busara kumchukua Lina na kumwingiza chooni mwake kisha akafungua mlango kumkaribisha James...
“Vipi bwana James?”
“Nimesahau ile kadi ya namba za kule Marekani.”
“Oooh, hii hapa,” alisema bosi huyo akiwa ameufungua mlango kwa uwazi mkubwa, James akaingia kuichukua kadi hiyo, akaondoka lakini safari hii hakusindikizwa.
Bosi alimfuata Lina, akamtoa chooni…
“Unajua kwa nini niliamua kukuingiza chooni ili usionane na James?”
“Naamini hukupenda niumbuke.”
“Hilo ni mojawapo lakini pia sababu kubwa umeniambia kila kitu, nikajua akikuona humu ndani inaweza kuwa balaa zito,” alisema bosi huyo akiwa amekaa.
Lina alikosa amani ya moyo, alijikuta akiwa mdogo kuliko inavyotakuwa kuwa. Aliamini uzuri wake ndiyo kisa cha yote, akajichukia ghafla.
“Nashukuru sana bosi, lakini sijajua nitamalizaje hili tatizo.”
“Mtegemee Mungu litaisha, lakini ikiwa tu kama ndani ya moyo wako utakiri kwamba ulichofanya sicho.”
“Nakiri hata sasa bosi kwamba nilichofanya sicho kabisa.”
“Basi kaendelee na kazi.”
Lina alisimama huku bosi wake akimwangalia kwa macho makavu kabisa, akaenda kwenye eneo lake la kazi, alikaa kwa hali ya wasiwasi, lakini aliamini anaanza kupata mwanga wa tatizo.
“Lakini lazima James atakuwa amejua kitu, haiwezekani asinipigie mpaka kunakucha halafu tena mpaka saa hizi, si kweli, amesikia kitu,” alisema Lina. Mara palepale simu ikaingia, James alipiga…
“Mh! Hatajwi,” alisema…
“Haloo baby?” alipokea Lina…
“Yes d, nimekususa leo.”
“Nimeshangaa, nikasema huyu mume wangu vipi tena,” alisema Lina huku akisimama kwenda jikoni. Alijua lazima atamuulizia mama…
“Vipi mama anaendeleaje?”
“Kidogo nafuu.”
“Nipe nimsalimie.”
Lina alishamminya mama wa chai, akampa simu naye akaigiza. Walizungumza kwa sekunde kama kumi na tano kisha James akaomba kuongea tena na Lina, simu ikarudishwa…
“Sasa unarudi lini, si kazini uliomba ruhusa ya siku chache tu?”
“Nitarudi kesho.”
“Oke, halafu leo nilikwenda kazini kwenu, nikamkuta yule mmamamama, sijui anafanyaga kazi gani?”
“Ee, mama yetu huyu bwana, anapikaga chai,” alisema Lina lakini akashtuka kwamba ameongea kitu cha kujikamatisha kule kusema ‘mama yetu huyu’ wakati yeye yuko mbali na ofisi, angesema ‘mama yetu yule’.
Baada ya kukata simu alimwambia yule mwanamke alichozungumza na James. Pia alimwambia alichomsimulia bosi wao.
***
Lina alikuwa nyumbani kwake usiku, mumewe alisharudi. Wakiwa sebuleni wamekaa, mumewe akasema…
“Yule rafiki yangu Kindaundau anasema ana shida sana na mimi. Sijui ana shida gani maana namuuliza ni nini anasema mpaka tukutane laivu.”
“Mh!” Lina aligunia moyoni, alijua kumekucha sasa…
“Kwani mna dili lolote kwa sasa?” aliuliza Lina akiwa anaangalia chini.
“Hatuna. Halafu yule ana kawaida moja, akiwa na tatizo anasema nashangaa hili anasema si la kuongea kwenye simu.
Kesho yake ilikuwa sikukuu, Lina aliwasiliana na James akamwambia ndiyo anapenda gari Korogwe kurudi Dar, James akamuuliza ataingia saa ngapi ili akampokee…
“Kwenye saa nane,” alidanganya Lina…
“Basi linaitwaje?”
“Burudani.”
“Basi utanikuta stendi Ubungo.”
“Sawa baby.”
***
Saa saba mchana, Semi alimwambia mkewe Lina waende wakale Mlimani City. Lina alitaka kuchomoa lakini akahisi mumewe hatamwelewa kwani ni kawaida yao sikukuu kutoka kwenda kupata lanchi au dina mahali.
Walifika Mlimani City, wakaa kwenye meza ya peke yao kabla hawajasikilizwa, Semi alimpigia simu Kindaundau na kumwambia kama yupo jirani aende hapo. Akamjibu ampe dakika kumi na tano tu.
***
Saa nane kamili, James alifika Ubungo stendi bila kumpigia simu Lina. Alitaka akishafika ndiyo ampigie.
Aliegesha gari mahali, akashuka na kutembeatembea huku sasa simu ikiwa sikioni akimpigia Lina.
Lina akiwa na mumewe, Semi alipata mshtuko mkubwa sana kuona simu ya James, akakumbuka kwamba alimwambia atafika Dar saa nane.
Kwa upande wake, James alishangaa kupiga simu ya Lina mara tatu bila kupokelewa. Mara, akaliona basi la Burudani likiingia, akalifuata.
ITAENDELEA SIKU YA KESHO

mbona picha tu?
ReplyDelete