A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 11
MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
Nitakusaidia. Anaishi hotelini kwa sasa” Dokta Pius alimwambia Bwana Boniface.
“Unaijua hoteli yenyewe?”
“Naifahamu. Huwa ninawasiliana nae mara kwa mara. Na sasa anataka kukua wewe na kisha kumuua Bwana Ombeni” Dokta Pius alimwambia Bwana Boniface.
“Mungu wangu! Yupo hoteli gani?”
“La Vista Inn pale Magomeni”
“Sawa. Inatubidi twende. Naomba unisaidie kumuua. Ninakuahidi kukupa kiasi chochote ukitakacho” Bwana Boniface alimwambia dokta Pius.
“Sawa. Kajiandae. Nitakusaidia kila hatua” Dokta Pius alimwambia Bwana Boniface ambaye akanyanyuka na kuanza kuelekea chumbani kwake.
Dokta Pius akabaki sebuleni pale huku akionekana kuwa na mawazo. Mara baada ya kutulia kwa sekunde kadhaa, akainuka na kisha kuanza kuelekea ndani ya chumba cha Bwana Boniface ambako alikuwa amekwenda kujiandaa. Dokta Pius alionekana kuwa mtu mwema ambaye alidhamiria kumsaidia Bwana Boniface.
Kila siku Dominick alikuwa akiwaza jinsi ya kufanikisha pango wake wa kuwaangamiza wabaya wake ambao walimpa majeraha moyoni mwake. Hakutaka kuwaacha wakiwa hai, alijiona kukosa amani kila alipokuwa akijifikiria kuwaacha.
Kitu alichokifanya Dominick kwa wakati huo ni kuanza kutafuta urafiki na dokta Silyvester wa zahanati ya St’ Maria iliyokuwa Magomeni. Kila siku alikuwa akifika hospitalini hapo huku akionekana kubadilika kupita kawaida. Kichwa chake hakikuwa na nywele kabisa, alivaa ndevu za bandia ambazo ilikuwa ni jambo gumu sana kumgundua.
Siku ziliendelea kwanda mbele huku ukaribu wake na dokta Silyvester ukizidi kukua kila siku. Ndani ya mwezi mmoja tu, wakawa wamezoeana kana kwamba walikuwa wamefahamiana kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Dominick akawa akitumia muda mwingi sana kuonana na dokta Silyvester ambaye alikuwa akimkaribisha sana katika zahanati yake. Hakuwa na hofu kabisa na Dominick na wala hakufahamu kwamba kulikuwa na kitu ambacho Dominick alikuwa akikihitaji kutoka kwake.
Kitu ambacho alikuwa akihitaji Dominick ni mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo tu. Hakuwa na shida ya kutafuta koti la daktari kwani aliamini kama angetumia koti lolote la muuza nyama buchani basi ilikuwa ni lazima mtu yeyote afahamu kwamba alikuwa daktari wa hospitali fulani.
“Nataka unifundishe mengi kuhusu udaktari” Dominick alimwambia dokta Silyvester.
“Kama kipi Pius?”
“Kwanza hii mashine. Unajua inaonekana kuwa mashine ya kawaida sana lakini kwa mtu kama mimi inaweza kuwa tofauti na ninavyodhani” Dominick alimwambia dokta Silyvester ambaye akaanza kumulekeza Dominick kuhusiana na mashine ile.
Dominick alijifanya kuwa msikivu wa hali ya juu. Dokta Silyvester aliendelea kumuelekeza kila kitu kuhusiana na mashine ile. Dokta Silyvester hakumfundisha kuhusiana na mashine ile tu bali aliendelea kumfundisha na mambo mengine pia.
“Hivi inauzwa?” Dominick aliuliza.
“Ndio. Hasa katika maduka makubwa ambayo yanauza vifaa mbalimbali vya hospitalini” Dokta Silyvester alimwambia.
Dominick hakuona ugumu wowote ule, tayari akawa na matumaini ya kuweza kuipata mashine ile. Akaulizia kuhusu gharama ya mashine ile na kisha kutaka kufahamu maduka ambayo yalikuwa yakiuza mashine zile. Alipopata maelekezo ya kutosha, kesho yake akapaelekea kununua.
Akarudi katika chumba ambacho alikuwa amepanga na kutulia. Akaanza kuangalia mashine ile pamoja na koti, vitu vyote hivyo alikuwa amevinunua kutoka katika maduka ya vifaa vya madaktari katika duka moja kubwa lililokuwa Mwenge.
Dominick akachukua simu yake ya mkononi na kuchukua line ya simu mpya, akaingiza salio na kisha kupiga namba za Bwana Boniface. Simu ikaanza kuita, iliita kwa zaidi ya dakika moja, wala haikupokelewa. Hakukata tamaa, aliendelea kupiga zaidi na zaidi, baada ya muda, simu ikapokelewa.
“Unasemaje?”
“Ndio hivyo mzee. Yaani nimeshtuka sana aliponiambia” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Habari zako zimenishtua sana, naomba tuonane ili tuweze kuliongea hili” Bwana Boniface alimwambia huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Haitowezekana kuonana na mimi. Nina majukumu mengi ya kazi. Nimejaribu kukwambia ili tu ujue jinsi gani utaweza kujilinda” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Nahitaji msaada wako. Najua kutakuwa na mambo mengi unayafahamu. Naomba tuonane. Nakuomba kukuona dokta Pius” bwana Boniface alimwambia Dominick.
“Kila kitu fedha. Kila kitu fedha mzee wangu”
“Nalifahamu hilo. Naomba tuonane, kuhusu fedha si tatizo kwangu. Ninachotaka ni kuonana nawe tu” Bwana Boniface alimwambia Dominick.
“Sawa. Kama kuonana, nitahitaji kuonana nawe usiku, kwa mchana haitowezekana kabisa kutokana na ubize wa kazi” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Unafanya kazi katika hospitali gani?”
“Amana”
“Sawasawa. Nitamtuma mtu akufuate hapo muda wowote ule”
“Sawa. Mwambie aje saa tatu usiku. Ila atakapofika, hatakiwi kuteremka kutoka garini. Sitohitaji wafanyakazi wanione nikiongozana na mtu kuelekea katika gari lake.Nitakachokifanya nitawasiliana nae, cha msingi nitumie namba yake ya simu” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Usijali. Nitakutumia sasa hivi” Bwana Boniface alisema na simu kukatika.
Dominick akabaki katika hali ya mawazo. Kwa kiasi fulani akajiona kuanza kupata mafanikio juu ya kile ambacho alikuwa amepanga kukifanya. Akajilaza kitandani huku akianza kufikiria ni kwa jinsi gani angefanikiwa kufanya kile ambacho alikusudia kukifanya.
Kwanza akainuka kutoka kitandani na moja kwa moja kuanza kuelekea katika droo ya kabati na kisha kutoa bunduki yake, akaanza kuiangalia kwa muda fulani na kisha kuirudisha na kwenda kitandani.
*********
Simu ya Dominick ambaye alikuwa katika eneo a hospitali ya Amana ikaanza kuita. Akitoa simu ile na kuanza kukiangalia kioo cha simu ile, namba ilikuwa ngeni, hivyo akaonekana kumjua mtu ambaye alikuwa akimpigia muda huo.
Alichokifanya ni kuanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka kuelekea nje ya eneo la hospitali ile huku akiwa na koti refu jeupe pamoja na mashine ya kusikilizia mapigo ya moyo ambayo alikuwa ameizungushia shingoni mwake. Mara baada ya sekunde kadhaa, akafika nje ya eneo la hospitali ile.
Akaanza kuangalia huku na kule, gari aina ya Range ilikuwa imepaki pembeni kabisa. Hakuwa na wasiwasi nalo kwani alikuwa na uhakika kwamba gari ile ndilo ambalo alihitajika kuingia kwa wakati huku. Akaanza kupiga hatua za haraka haraka kulifuata.
“Karibu dokta Pius” Mwanaume mmoja ambaye alionekana kuwa na mwili uliojazia alimwambia Dominick huku akimfungulia mlango.
“Asante” Dominick alijibu huku akiingia ndani ya gari lile na safari ya kuelekea katika nyumba ya Bwana Boniface kuanza.
**************
Dominick akakigusa kitasa cha mlango wa chumba cha Bwana Boniface na kuufungua mlango. Bwana Boniface alikuwa akijiandaa tayari kwa ajili ya kwenda kumuua Dominick ambaye alikuwa katika hoteli ya La vista Inn. Tegemeo lake kubwa kwa wakati huo lilikuwa kwa dokta Pius ambaye alikuwa amemuacha sebuleni.
Kichwa chake kikaguswa na mdomo wa bunduki. Akaonekana kushtuka kupita kiasi, akaanza kugeuka nyuma, macho yake yakatua katika uso wa dokta Pius. Bwana Boniface akabaki akishangaa pasipo kuelewa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo.
Alimwangalia dokta Pius usoni, macho yake yalikuwa mekundu huku machozi yakiwa yanamlenga. Bwana Boniface hakuelewa ni kitu gani kilikuwa kinaendelea mpaka dokta Pius kumnyooshea bunduki. Bwana Boniface akabaki akitetemeka tu.
“Dokta! Vipi tena?” Bwana Boniface aliuliza huku akionekana kuhofia.
“Unachokiona ndicho kinachoonekana” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Kwa nini unataka kufanya hivi?”
“Kwa sababu ya kisasi. Hiki ndicho kitu nilichokuwa nikikihitaji kwa kipindi kirefu” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Sijakuelewa. Nimekuita hapa kwa sababu ya kunisaidia…lakini kwa nini unataka kunigeuka? Au Dominick amekutuma?” Bwana Boniface aliuliza.
*********
Bado Dominick alikuwa akitokwa na machozi, kila alipokuwa akimwangalia Bwana Boniface ndivyo ambavyo mambo mengi ya nyuma yalivyokuwa yakimiminika kichwani mwake. Alikumbuka vilivyo siku ambayo nyumba yake ilikuwa ikiteketezwa kwa moto na mkewe mpendwa pamoja na mtoto wake kuuawa siku hiyo.
Alijiona kuwa na sababu zote za kumuua Bwana Boniface kama kisasi cha familia yake. Hakutaka kumuacha katika usiku huo, hiyo ilionekana kuwa nafasi kubwa katika maisha yake juu ya kuendelea na zoezi lake lile. Aliendelea kumwangalia Bwana Boniface kwa macho yaliyojaa hasira.
“Ninakuua…ninakuua kwa mkono wangu mwenyewe” Dominick alimwambia Bwana Boniface ambaye muda wote alikuwa akishangaa.
“Dokta Pius….mbona unanifanyia hivi?” Bwana Boniface aliuliza.
Dominick akabaki akimwangalia kwa muda, akaitoa miwani yake na kuiweka katika mfuko wa koti lake na kisha kuzitoa zile ndevu za bandia. Bwana Boniface akabaki akimwangalia Dominick, sura yake wala haikuwa ngeni machoni mwake.
“Najua umekwishawahi kuniona kabla ya hapa” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Hapana. Hii ndio mara ya kwanza kukuona. Sikuwahi kukuona kabla ya hapa” Bwana Boniface alimwambia Dominick.
“Niangalie vizuri. Hauwezi kusema kwamba haunifahamu. Nitazame vizuri” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
Bwana Boniface akabaki akimwangalia Dominick. Ni kweli sura yake haikuwa ngeni machoni mwake lakini kila alipojaribu kukumbuka mahali ambapo alikuwa amekwishawahi kuiona sura ile, alikosa jibu.
“Wewe ni nani?” Bwana Bonifac aliuliza.
“Muuaji nisiyekuwa na huruma. Mimi ni mwandishi ambaye nimerudi tena kutoka kaburini” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Dominick! Mungu wangu! Dominick!”
“Ndio mimi. Nimekuwa nikiisubiri nafasi hii kwa muda mrefu sana. Nimekuwa nikiangaika maishani mwangu. Nilikuwa na furaha katika kipindi chote, mkataka kunipa huzuzni maishani mwangu, nawapongeza kwa kuwa mlifanikiwa kwa asilimia mia moja” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
“Dominick. Dominick……” Bwana Boniface alijikuta akiita jina la Dominick pasipo kuongea kitu chochote kile.
Alimwangalia Dominick mara mbili mbili, hakuamini kama Dominick angeweza kutumia njia ile kuingia ndani ya nyumba yake. Alitamani kuleta ubishi ili apate kujiokoa kutoka katika mikono ya Dominick lakini kila alipokuwa akiuangalia mdomo wa bunduki ile akabaki akiogopa kufanya hivyo.
Dominick akaanza upiga hatua mpaka kitandani ambako akauchukua mto wa kulalia na kuuweka mbele ya mdomo wa bunduki ile huku lengo lake kubwa likiwa ni kuuzia mlio wa risasi ile usisikike kwa sauti kubwa.
“Wote mtaelekea kule mlipoipeleka familia yangu” Dominick alimwambia Bwana Boniface.
Wala hazikupita hata sekunde kumi, milio kadhaa ya risasi ikasikika kwa mbali kabisa. Dmu zilikuwa zikimtoka Bwana Boniface. Akabaki chini huku akirusha miguu yake huku na kule. Kifua chake kilikuwa kimetobolewa na risasi kadhaa.
Dominick akaiangalia ile maisti ya Bwana Boniface. Hakuonekana kuridhika kabisa, akaifuata ale chini na kuanza kuiongezea risasi kadhaa. Kila alipokuwa akiiangalia maiti ile na ndivyo ambavyo hasira zilivyozidi kumpanda.
Mara baada ya kuridhika, akairudisha miwani yake pamoja na ndevu zake za bandia na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea nje ya chumba kile. Akayafuta macho yake ambayo yalikuwa yakitokwa na machozi na kujiweka katika hali ya kawaida, alipomaliza, akatoka nje ya nyumba ile na kuingia garini.
“Tayari dokta?” Mwanaume yule aliyekuwa na mwili wa kujazia alimuuliza Dominick.
“Tayari. Nirudishe hospitalini” Dominick alimwambia mwanaume yule na kisha kuanza kumudisha hospitalini ambako baada ya kufika Amana akateremka na kumzuga dereva kwamba alikuwa akielekea katika hospitali ile.
Alipoona gari lile limeondoka mahali pale, moja kwa moja akaanza kulifuata garil lake na kisha kuanza kuelekea katika hoteli ya La Vista Inn.
********
Hali ya hewa ikachafuka zaidi, viongozi wa Serikali wakachanganyikiwa zaidi, mauaji ambayo yalikuwa yametokea katika usiku uliopita yakaonekana kuwachanganya. Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama Bwana Boniface angeweza kuuawa ndani ya nyumba yake iliyokuwa na ulinzi wa kutosha.
Kitu walichokifanya mapolisi ni kumuita mwanaume yule ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kumuendesha Bwana Boniface katika gari lake la kifahari aina ya Range. Moja kwa moja mwanaume yule akaingizwa katika chumba zcha mahojiano.
“Unaitwa nani?” Polisi aliuliza.
“Bakari Omari” Mwanaume yule alijibu.
“Ulikuwa wapi katika kipindi ambacho Bwana Boniface alikuwa akiuawa?” Polisi aliuliza.
“Kama ni yule dokta ndiye aliyefanya mauaji hayo, basi naweza kusema kwamba nilikuwa nje ya nyumba yake ila kama si yeye basi sikuwapo katika eneo la nyumba yake” Bakari alijibu.
“Ninahitaji kufahamu mengi kuhusiana na huyo dokta” Polisi alimwambia Bakari.
“Mzee alinipigia simu nyumbani na kunieleza kwamba kuna daktari ambaye nilitakiwa kwenda kumchukua katika hospitali ya Amana ifikapo usiku. Nilichokifanya kwa wakati huo ni kwenda katika hospitali hiyo na kumchukua na kisha kuanza kwenda nae nyumbani kwa marehemu” Bakari alielezea na kukaa kimya.
“Anaitwa nani?”
“Dokta Pius”
“Sawa. Endelea”
“Kwa jinsi nilivyokuwa nikiwaangalia wote kwa pamoja, niliweza kugundua kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba walikuwa wakifahamiana, naweza kusema hivi kwa kuwa muda mwingi walikuwa wakionyesheana tabasamu katika nyuso zao. Mara baada ya muda fulani, wakaingia ndani” Bakari alisema.
“Inamaanisha ulibaki nje?”
“Ndio”
“Kwa nini?”
“Mzee hakutaka niingie kitu ambacho nilijua kwamba walikuwa na kitu cha siri walitaka kuongelea ambacho sikutakiwa kukifahamu” Bakari alielezea.
“Sawa. Endelea”
“Ilichukua muda kama wa dakika ishirini, dokta Pius akatoka ndani ya nyumba ile na kisha moja kwa moja kuingia garini. Alinitaka niondoke mahali hapo na kumrudisha kazini kwake, katika hospitali ya Amana. Nilipomfikisha huko, nikaondoka zangu” Bakari alielezea.
Maelezo yote ambayo alikuwa ameyatoa yalikuwa yameandikwa katika faili maalumu na kisha kuruhusiwa. Walichokifanya mapolisi kwa wakati huo ni kuondoka kituoni hapo na moja kwa moja kuelekea katika hospitali ya Amana.Kitu ambacho walikuwa wakitaka kukifahamu katika wakati huo ni juu ya uwepo wa dokta Pius ambaye hadi muda huo ndiye alikuwa akionekana kuwa muuaji. Mara baada ya dakika kadhaa, wakafika katika hospitali ile na moja kwa moja kuelekea ndani ya jengo lile.
Kitu ambacho walikuwa wakikitaka katika muda huo ni kuonana na dokta mkuu ambaye angewapa maelekezo kuhusiana na dokta Pius ambaye kila mmoja alikuwa na wasiwasi nae. Mara baada ya kuelekezwa mahali ilipokuwa ofisi ya dokta mkuu, wakaanza kuelekea huko.
“Inashangaza sana” Dokta mkuu, Bwana Samuel aliwaaambia mara baada ya kuongea kwa muda.
“Kwa nini?”
“Katika hospitali hii wala hakuna dokta mwenye jina hilo” Dokta Samuel aliwaambia huku akitoa faili ambalo lilikuwa na majina ya wafanyakazi wote wa hospitali ile na kuwagawia.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, hawakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Ni kweli kutokana na maelezo ya Bakari, dokta Pius alitoka ndani ya jengo lile la hospitali na kisha kuelekea katika gari lile ambalo alikuja kumpokea, sasa kwa nini dokta yue hakuwa na mmoja wa wafanyakazi katika hospitali ile?
Kila walipokuwa wakifikiria, hawakupata jibu, hai ilionekana kuwashangaza kupita kawaida, hawakuelewa ni kitu gani ambacho kilitakiwa kufanyika kwa wakati huo. Kitu walichokifanya ni kuondoka katika hospitali ile na kuelekea ofisini huku wote wakionekana kukasirika kupita kawaida.
Bado hali haikutulia mitaani, magazeti ambayo yalikuwa yameandika taarifa ya kifo cha Bwana Boniface yalikuwa yakinunuliwa kuliko magazeti yote. Kila mtu kwa wakati huo alitaka kufahamu sababu halisi ambazo zilimfanya Bwana Boniface kuuawa.
Wananchi hawakuelewa juu ya matukio yale ya mauaji kutokea. Kila mtu mitaani alikuwa akisema lake, wengine walidiriki hata kusema kwamba vyama pinzani ndio ambavyo vilikuwa vikifanya mauaji yae.
Matukio haya yaliyofuatana yakatengeza historia kubwa nchini Tanzania ya kuwapoteza viongozi wawili ndani ya miezi kumi na moja tena huku wote wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi. Hakukuwa na amani tena katika maisha ya viongozi, wasiwasi mkubwa ukawa umeongezeka katika maisha yao.
Hawakutakiwa kumuamini mtu yeyote katika maisha yao ya kila siku. Walitakiwa kuishi maisha ya peke yao na familia zao. Mauaji yale yalionekana kuendelea kama mfululizo wa filamu za tamthilia.
Upelelezi bado ulikuwa ukiendelea kufanyika lakini hakuna kitu ambacho kilipatikana, muuaji hakupatikana japokuwa kila mtu alijua kwamba muuaji huyo alikuwa akiishi miongoni mwao.
*******
Bwana Tumaini alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika na mauaji yote ambayo yalikuwa yametokea. Hakutaka kujiuliza kitu chochote kile, jambo ambalo aikuwa amedhamiria ni kuwaeleza mapolisi kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika katika kila kitu.
ITAENDELEA SIKU YA KESHO
MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

Post a Comment