ad

ad

TANESCO LAWAMANI, YAKATA UMEME BILA TAARIFA

Dar. Tatizo la kukatika kwa umeme, imekuwa kero katika maeneo mbalimbali ya nchi na lawama nyingi zimekuwa zikielekezwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Maeneo mengi yamekumbwa na kero hiyo tangu wiki iliyopita mpaka jana huku wahusika wakishindwa kutoa taarifa ya nini kinachosababisha kero hiyo ya kukatika kwa umeme.

Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yaliyopo eneo la Ubungo juijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba 
Hali hiyo imesababisha adha hata katika vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea kwenye Ukumbi wa Karimjee,
Dar es Salaam.
Hali hiyo, ilisababisha Wajumbe wa Kamati kushindwa ama kuendelea na shughuli zao au kukatisha majadiliano yao na viongozi wa taasisi mbalimbali.
Wajumbe wa kamati hizo walionekana kuangaika kwa kufungua madirisha na milango na wengine waliegesha viti kwenye milango ili kupata hewa, baadhi wakitoka nje mara kwa mara na wengine wakitumia makabrasha yao kujipepea kutokana na joto kali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge (PAC, Deo Filikunjombe aliyekuwa akiongoza kikao, ilibidi amwombe radhi Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Philimon Luhanjo kutokana na kuchelewa kuanza kwa kikao kulikosababishwa na kukatika kwa umeme.
“Pole sana mzee nimekuona umewahi kweli kufika lakini shughuli zetu hapa zimekwamishwa na umeme, kwa utaratibu ulivyo ni lazima majadiliano yanayoendelea kwenye vikao vyetu yarekodiwe kwa ajili kumbukumbu.
“ Hata hivyo nawapongeza kwa kupata hati safi tofauti na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kimekuwa kikipata hati chafu kila mwaka licha ya kwamba vyuo vyote vinatakiwa kuwa mfano mzuri kwa sababu ndiyo vinazalisha wataalamu wetu,” alisema Filikunjombe.
Luhanjo ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, aliwasili katika ofisi ndogo za Bunge jijini hapa akiwa ameongozana na Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Gerald Monela saa 2 asubuhi na kuingia kwenye kikao cha PAC kilichoanza saa 5.30.
Maofisa wa kitengo cha umeme wa ofisi hiyo walijikuta wakihangaika na kukosa amani wakidhani ni hitilafu iliyosababishwa na miongoni mwa vifaa vinavyotumika katika jengo hilo kabla ya kubaini kuwa umeme ulikuwa unakatika na kuwaka.
“Samahani nahisi kama hii AC yako ndiyo inasababisha umeme kuzima mara kwa mara, ngoja tuizime japo dakika 10,” alisikika mmoja wa maofisa hao akizungumza na mfanyakazi mwenzake.

Wafanyabiashara walia
Wafanyabiashara wa barafu, samaki, nyama kwenye bucha na katika baadhi ya maeneo ya jiji na mikoani, wamefunga biashara zao kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika.
Mmoja wa wafanyabiashara wa bucha katika maeneo ya Gongo la Mboto alisema analazimika kununua nyama kidogo ili aweze kuiuza yote kuhofia isiharibike.
Chanika
Kwa takribani majuma mawili sasa, maeneo ya Chanika yaliyo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, umeme umekuwa ukikatika kila mara bila kuwapo na taarifa yoyote kutoka Tanesco.
Mfanyabiashara wa chipsi na vinywaji baridi Chanika mwisho, James Mwanry alisema umeme hukatika kwa zaidi ya saa 6 mpaka 10 kila siku.
“Ni kama kawaida sasa, mfano siku ya Ijumaa hukatika jioni na kurudi usiku kati ya saa sita na wakati mwingine hadi asubuhi,” alisema.
Hali hiyo imewafanya baadhi ya wakazi kuhisi kuwa kuna mgawo wa kimya kimya.
Christopher Thadei, Mkazi wa Chanika kwa Singa alisema ni bora Tanesco wakawaweka wazi wananchi kama kuna mgawo ili wajue badala ya mtindo huu unaoendelea sasa.
Temeke
Eneo la Mbagala Rangi Tatu wilayani Temeke, ni kati ya maeneo yanayokumbwa na adha hiyo.
Imeelezwa kuwa eneo hilo hukatiwa umeme kila jumapili kwa saa 12.

“Ni kawaida kukatika mara kwa mara umeme na kuna siku unakatika hata mara nne kwa siku bila,” alisema Wivu Jamal mkazi wa Mbagala.
Alisema: “Si ajabu wakazi wa Mbagala kuacha kuwasha vitu hata umeme unaporudi kwani hauchukui dakika tano unakatika tena...hali hiyo inajirudia mara kwa mara na wakati mwingine huunguza baadhi ya vifaa vya umeme.”
Ilala
Maeneo mbalimbali ya Tabata wilayani Ilala pia yamekumbwa na adha hiyo.
Eneo la Tabata Segerea, kwa majuma mawili mfululizo sasa kumekuwa na katizo la umeme lisilo na ratiba maalumu.
“Siku za hivi karibuni umeme umekuwa ukikatika mara nyingi tofauti na hapo awali. Unaweza kukatika asubuhi saa tatu asubuhi ukarudi baada ya saa mbili au tatu hivi na wakati mwingine zaidi.
“Kwa mfano, jana saa mbili usiku hadi usiku wa manane ulikatika, ukarudi usiku wa manane hata sikumbuki saa ngapi…nasikia ilikuwa hadi Kinyerezi,” alisema Said Rashid, Mkazi wa Tabata Segerea.
Maeneo ya Tabata Kisiwani kumekuwa na hali kama hiyo juzi usiku kuanzia saa 12: 00 jioni hadi saa 5:00 usiku huku baadhi ya wakazi wakionekana kuitupia lawama Tanesco.
Kariakoo
Kero ya kukatika kwa umeme imekuwa ikiwakumba wakazi wa eneo la Kariakoo na vitongoji vyake kwa takriban miezi miwili sasa.
Katika maeneo hayo, kumekuwa na kelele za jenereta katika baadhi ya maduka huku wafanyabiashara wengine wakifanya biashara ya jenereta kwa kasi.
Mmoja wa wakazi wa Mitaa ya Twiga na Jangwani, Amina Seif aliliambia gazeti hili kuwa umeme ulikatika tangu Jumanne ni miezi miwili sasa tatizo hilo lipo.

“Hii hali kwa kweli siyo nzuri...inahatarisha maisha na mali zetu kwa sababu umeme unavyokatika na kurudi, kama mtu hayupo nyumbani na ameacha baadhi ya vitu vinawaka si vinaweza kuungua...sasa tunajiuliza huu ni mgawo wa kimya kimya,” alihoji Seif.
Buguruni
Maeneo ya Buguruni pia ni tatizo na imeelezwa kuwa vibaka hutumia nafasi hiyo kupora watu.
Kinondoni
Kwa upande wa maeneo ya Kinondoni inadaiwa kuwa hali hiyo imedumu kwa wiki nzima sasa.
“Kama Tanesco wameamua kugawa umeme watuambie, badala ya kufanya siri,” alisema Gabriel Julius mkazi wa Kinondoni Mkwajuni na kuongeza:
“Tunaomba watuarifu wananchi kama ilivyokuwa zamani...umma una haki ya kufahamishwa kuhusu hali hii.”
Mburahati
Maeneo ya Mburahati na vitongoji vyake katika wilaya Kinondoni, yamekuwa yakikosa umeme mara kwa mara na kusababisha adha kwa wananchi.
Mkazi wa eneo hilo Aziza Abdallah alisema katika eneo lao umeme hukatika kila baada ya siku moja kwa zaidi ya saa 12 na kusababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.
Ubungo
Katika maeneo ya Ubungo, baadhi ya wakazi walisema imekuwa mazoea kwao kukumbwa na katizo la umeme kila siku.
ENDELEA KUSOMA HAPA

No comments

Powered by Blogger.