A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 12
MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
Matukio haya yaliyofuatana yakatengeza historia kubwa nchini Tanzania ya kuwapoteza viongozi wawili ndani ya miezi kumi na moja tena huku wote wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi. Hakukuwa na amani tena katika maisha ya viongozi, wasiwasi mkubwa ukawa umeongezeka katika maisha yao.
Hawakutakiwa kumuamini mtu yeyote katika maisha yao ya kila siku. Walitakiwa kuishi maisha ya peke yao na familia zao. Mauaji yale yalionekana kuendelea kama mfululizo wa filamu za tamthilia.
Upelelezi bado ulikuwa ukiendelea kufanyika lakini hakuna kitu ambacho kilipatikana, muuaji hakupatikana japokuwa kila mtu alijua kwamba muuaji huyo alikuwa akiishi miongoni mwao.
*******
Bwana Tumaini alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika na mauaji yote ambayo yalikuwa yametokea. Hakutaka kujiuliza kitu chochote kile, jambo ambalo aikuwa amedhamiria ni kuwaeleza mapolisi kwamba Dominick ndiye ambaye alikuwa amehusika katika kila kitu.
11
Hakujali maswali ambayo angeulizwa baada ya kutoa maelezo yale, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kuwaeleza mapolisi tu kwani aliona kwamba ilikuwa bora kufanya hivyo kuliko zamu yake ya kuuawa itakapofika.
Alidhamiria kweli kwenda kuwaeleza mapolisi ukweli wote kwamba kila mauaji ambayo yalikuwa yakitokea yalikuwa kama kisasi kutoka kwa Dominick ambaye waliiteketeza familia yake. Muda wote alikuwa na presha, alitaka mazishi ya Bwana Boniface yamalizike haraka haraka ili aelekee katika kituo cha polisi na kueleza kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
Siku zikaanza kukatika huku mazishi yakiwa yamelizika. Bwana Ombeni akajipanga vilivyo kwenda kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea toka siku ile ambayo walikuwa wamewatuma vijana wao kwenda kuiteketeza familia ya Dominick.
Hakutaka kuuawa kama wengine walivyouawa, alitaka kuinusuru roho yake haraka iwezekanavyo. Moja kwa moja akatoka kutoka ndani ya chumba chake na kuingia garini huku lengo lake likiwa ni kuelekea katika kituo cha polisi cha Oysterbay kwa ajili ya kuelezea kila kitu.
Garini, akili yake wala haikutulia, muda wote alikuwa akimfikiria Dominick. Alitamani kufika katika kituo cha polisi haraka iwezekanavyo na kuelezea kile ambacho kilikuwa kikimsumbua moyoni mwake. Safari iliendelea kama kawaida mpaka akaanza kuingia katika eneo la kituo cha polisi cha Oysterbay. Kwa haraka haraka akateremka na kuanza kuelekea ndani ya kituo kile.
“Karibu mzee” Poisi ambaye alikuwa kaunta alimkaribisha.
“Asante” Bwana Ombeni aliitikia.
Mapolisi wote ambao walikuwa nje wakaingia ndani kwa ajili kumsikiliza Bwana Ombeni ambaye alikuwa ameingia ndani ya kito kile. Kila mmoja akajua kwamba Bwana Ombeni alikuwa na kitu kizito moyoni ambacho alikuwa akitaka kuielezea polisi.
*************
Bwana Ombeni alionekana kuchanganyikiwa. Tayari alikuwa katia kituo cha polisi kwa wakati huo. Hakuwa na nguvu za kuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku akiwaangalia mapolisi tu. Alikuja hapo akiwa na nguvu kabisa za kuwaeleza mapolisi kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake pamoja na njama zote ambazo alikuwa amezifanya katika kuiteketeza familia ya Dominick na kutaka kumuua Dominick mwenyewe.
Kwa wakati huo alikuwa akijutia uamuzi ambao alikuwa ameuchukua, alijuta kwa kushirikiana na wenzake katika kutekeleza kile kitu ambacho kwa wakati huo alikiona kuanza kukilipia. Hakutaka tena kujificha, alitamani aendelee kuishi kuliko kuendelea kuficha kitu kile ambacho alikiona ni lazima akilipie kwa yeye mwenyewe kuuawa.
“Nimekuja……” Bwana Ombeni aliwaambia mapolisi ambao walikuwa kimya wakimwangalia.
“Ndio mzee. Tumekuja hapa kukusikiliza” Mkuu wa kituo hicho, Hussein alimwambia.
“Nimekuja kueleza ukweli. Kila kitu na njama zote ambazo nilizifanya katika maisha yangu kushirikiana na wenzangu” Bwana Ombeni aliwaambia.
“Ndio mzee tunakusikiliza”
“Nimefanya mambo mabaya sana kwa kushirikiana na wenzangu. Sisi ndio tuliiangamiza familia yake” Bwana Ombeni aliwaambia na kunyamaza kwa muda.
“Mliiangamiza familia yake? Nani?”
Bwana Ombeni akabaki kimya kwa muda, akaanza kujifikiria kama ingekuwa vizuri kumtaja Dominick mahali pale. Alijua fika kwamba angewekwa chini ya ulinzi hapo hapo kabla ya mambo mengine kufuata.
“Nani mheshimiwa?” Hussein aliuliza.
“Familia ya……” Bwana Ombeni alisema lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, simu yake ya mkononi ikaanza kuita.
Kwa haraka haraka akaichukua kutoka katika mfuko wake wa suruali na kisha kuangalia kioo cha simu, namba ambayo ilikuwa ikiingia katika muda huo ilikuwa ngeni simuni mwake. Kwa haraka haraka akaipeleka sikioni.
“Halloooo….” Bwana Ombeni aliita.
“Hallooo…!” Sauti ya upande wa pili iliitikia.
“Naongea na nani?” Bwana Ombeni aliuliza.
“Mwandishi wa habari wa gazeti la Mambo leo”
“Sawa. Nikusaidie nini?”
“Tumezipata taarifa zote kuhusu wewe na wenzako ambao mlifanya mauaji kwa kuiangamiza familia ya mwandishi mwenzetu, Dominick. Kila kitu tumeambiwa na ushahidi umekamilika. Hapa ninapoongea na wewe nipo ofisini mwangu nikiandaa gazeti kwa ajili ya kuitoa taarifa hiyo gazetini kesho” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
Bwana Ombeni akaonekana kushtuka kupita kiasi. Akaonekana kuanza kutetemeka huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Hakuamini kama mambo yale ambayo walikuwa wameyafanya na kuwa kama siri tayari yalikuwa yameanza kutapakaa.
Alijua kwamba kama taarifa ingetolewa gazetini basi ingekuwa hatari zaidi. Wananchi wote wangeshtuka na kuitaka serikali kumchukulia hatua kali kwa kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela au kunyongwa.
Kwa haraka haraka akatoka pale kaunta alipokuwa na moja kwa moja kuelekea garini mwake huku akionekana kutetemeka. Mapolisi wote wakabaki wakishangaa, hawakuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kikiendelea kwa mzee huyo kwa wakati huo.
“Umesemaje?” Bwana Ombeni aliuliza mara baada ya kuingia garini.
“Ndio hivyo mzee. Nilifanya uchunguzi wa muda mrefu. Nimeweza kugundua hayo, na sasa ndio ninaandaa gazeti. Kesho, kila Mtanzania ataweza kugundua uovu wako ulioufanya” Mwandishi yule ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake kiusalama alimwambia.
“Nimekusikia. Naomba unielewe kitu kimoja. Nikweli nimefanya uovu huo ila kwa sasa ninahitaji sana kitu hiki kutokujulikana. Nakuomba, nakuomba sana kama itawezekana tukutane na kuweza kuinunua habari hiyo kwa kiasi chochote cha fedha” Bwana Ombeni alimwambia mwandishi.
“Hauwezi kuinunua habari hii. Hivi unajua kuwa kama nikiiweka habari hii gazetini nitaweza kupata zaidi ya milioni ishirini? Hii ni habari yenye fedha sana” Mwandishi wa habari alimwambia Bwana Ombeni.
“Nakuomba sana. Nitainunua hata kwa milioni hamsini” Bwana Ombeni alimwambia.
“Haitowezekana kabisa. Ni lazima niiuze kama hautoongeza kiasi kikubwa zaidi” Mwandishi alimwambia.
“Nimekuelewa. Nitakupa milioni mia moja. Najua ni fedha nyingi sana, ila ninachokitaka ni kwamba kitu hicho kiwe siri kati yangu na wewe tu. Nakuomba unisaidie, nina milioni mia moja mwandishi” Bwana Ombeni alimwambia mwandishi huyo.
“Sawa. Njoo na fedha hizo hapa Caspian Hotel. Chumba namba 18. Kuwa mwangalifu asikugundue mtu yeyote yule” Mwandishi yule alimwambia.
“Usijali. Ninakuja na fedha hizo”
“Kama ukichelewa. Hautonikuta”
“Usijali, nitafanya haraka iwezekanavyo” Bwana Ombeni alisema na kisha simu kukatwa.
Hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo tena, moja kwa moja akaliwasha gari lake na safari ya kuelekea benki kuanza. Alihitaji kufanya kila kitu kuhakikisha jambo lile linakuwa siri ambayo hatoweza kuitambua mtu yeyote yule.
Mara baada ya kufika benki, moja kwa moja akaelezea shida yake na kisha kupelekwa katika chumba maalumu ambako huko akakabidhiwa kiasi cha fedha ambacho alikuwa akikihitaji kwa muda huo na safari ya kuelekea katika hoteli ya Caspian kuanza.
Garini, kichwa chake hakikutulia kabisa. Muda wote alikuwa akimfikiria mwandishi yule wa habari pamoja na habari ambayo alikuwa nayo juu yake. Ni kweli hakutaka Mtanzania yeyote afahamu juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake.
Hakujali kama alikuwa akilipa kiasi kikubwa cha fedha kwa wakati huo kwa ajili ya kuinunua habari ili, ila kitu ambacho alikuwa akikijali ni kuifanya habari ile kuendelea kuwa siri tu. Hakutaka kupata aibu yoyote ile na hiyo ndio maana alihakikisha kufanya kila kitu kuwa siri.
Mara baada ya kufika katika eneo la hoteli ya Caspian, moja kwa moja akateremka na kisha kuanza kuelekea sehemu ya mapokezi. Alipofika, akaelekezwa kwenda katika chumba ambacho alitakiwa kwenda na kuanza kwenda kule.
Mara baada ya kukifikia, akaanza kupiga hodi na kukaribishwa. Mwandishi alikuwa bafuni, hivyo moja kwa moja akatulia kitandani huku brifukesi yake akiiweka pembeni. Bwana Ombeni alibaki kuwa na mawazo mahali pale, alitaka mwandishi yule atoke bafuni na kumkabidhi habari ile haraka iwezekanavyo na yeye kuondoka mahali pale.
Mlango wa bafuni ukafunguliwa na mwandishi kutoka. Bwana Ombeni akaanza kumwangali mwandishi yule kuona kama alikuwa akimfahamu. Hakuweza kuuona vizuri uso wake kutokana na mwandishi yule kutumia taulo kuufuta uso wake.
“Mungu wangu! Dominick!” Bwana Ombeni aliita kwa mshtuko mara baada ya kuona uso wa mwandishi yule.
“Umeshtuka sana?” Dominick alimuuliza Bwana Ombeni huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Usishtuke. Wewe ni rafiki yangu mkubwa sana. Mara zote nilikuwa nikiandika habari zako gazetini. Au umesahau?” Dominick alimuuliza.
Bwana Ombeni hakujibu kitu chochote kile, alibaki akimwangalia Dominick kwa macho yaliyojaa mshtuko. Hakuamini kama yule mtu ambaye alikuwa akimwangalia mbele yake kwa wakati huo alikuwa Dominick, mwandishi ambaye walikuwa wameiangamiza familia yake.
“Nataka tuongee tu leo. Wewe ni rafiki yangu mkubwa. Au umesahau hilo?” Dominick aliuliza.
“Sijasahau” Bwana Ombeni alijibu huku akitetemeka, tayari kijasho kikaanza kumtoka.
“Kila siku nilikuwa nakufagilia katika magazeti na kukufanya kujulikana zaidi nchini hapa. Unakumbuka hilo?” Dominick aliuliza.
“Nakumbuka” Bwana Ombeni alijibu.
“Wewe ni rafiki yangu Ombeni, wala hautakiwi kuogopa lolote. Umekumbuka kuja na fedha zangu?” Dominick alimuuliza.
Bwana Ombeni akaanza kuliangalia brifukesi lake ambalo alikuja nalo mahali pale na kisha kulichukua na kumkabidhi Dominick ambaye tayari alikuwa ameufunga mlango kwa ufunguo. Dominick akaifungua brifukesi ile na kisha kuanza kuziangalia fedha zile, akatabasamu.
“Lakini kumbuka kwamba ulinisaliti. Yaani upendo wote ule niliokuonyeshea, malipo yake yakawa ni usaliti. Unakumbuka kama ulinisaliti?” Dominick aliuliza huku tabasamu pana likionekana usoni mwake. Bwana Ombeni hakujibu kitu chochote kile, alibaki kimya huku akimwangalia Dominick.
“Swali gumu hilo, inaelekea haukumbuki kitu chochote kile” Dominick alimwambia Bwana Ombeni.
“Nakumbuka” Bwana Ombeni alimwambia Dominick.
“Safi sana. Unakumbuka kwamba ulinisababishia kidonda kikubwa maishani mwangu?” Dominick aliuliza, tayari uso wake ukabadilika, tabasamu lote ambalo lilikuwa likionekana kabla likapotea.
ITAENDELEA SIKU YA KESHO

Post a Comment