A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 09
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
Wasiwasi ukazidi kuongezeka zaidi mara baada ya kujaribu tena kuipiga simu ile na kukuta ikiwa imezimwa. Akaitoa simu sikioni na kuanza kuiangalia, Bwana Boniface na Ombeni walibaki wakimwangalia, waliuona wasiwasi ambao alikuwa nao lakini hawakuelewa sababu ambayo ilimfanya kubadilika namna ile.
“Vipi?’
“Mke wangu”
“Amefanya nini?”
“Nafikiri kuna tatizo. Nampigia simu, inabaki inaita pasipo kupokelewa. Sasa hivi nimempigia, haipatikani hali inayoonyesha imezimwa” Tumaini aliwaambia.
“Kawaida tu. Si unajua wanawake watu wa kujisahau sana” Bwana Ombeni alimwambia.
“Hapana. Hii si kawaida. Ni lazima niende nyumbani Najua huyu anaweza kuwa Dominick” Tumaini alisema na kwa kasi kubwa akaondoka mahali hapo huku akiwaacha wenzake wakibaki na mshangao.
Njia nzima alikuwa akijaribu kuipiga simu ya mke wake akini hakukuwa na majibu, bado simu ilikuwa imezimwa. Akili yake ilichanganyikiwa kupita kiasi. Alitumia dakika kumi mpaka kufik nyumbani ambako akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika eneo lanyumba yake.
Hakukuwa na watu wengine zaidi ya wafanyakazi wake wa ndani ambao. Kila mfanyakazi ambaye alimuuliza, jibu lilikuwa ni kutokumuona toka alipokwenda kliniki. Maneno hayo ndio yaliyoonekana kumchanganya zaidi, masaa matatu yalikuwa yamepita tangu Edith aende kliniki.
Huku akionekana kuchanganyikiwa, akaingia garini na kisha kuanza safari ya kuelekea Kliniki. Bado akili yake haikuwa sawa kabisa, tayari wasiwasi ulikuwa umemshika moyoni.
Mara baada ya kufika kliniki, moja kwa moja akateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya mapokezi. Hakukuwa na wagonjwa wengi katika kliniki ile jambo ambalo lilioekana kumtia wasiwasi kwani alijua kama mkewe angekuwa amekwenda mahali pale angekuwa amekwisharudi nyumbani.
“Mke wangu alifika hapa?” Tumaini alimuuliza dada wa mapokezi hata kabla ya salamu
“Mmmmh! Hata salamu!”
“Samahani. Za sa hizi! Mke wangu alifika hapa?”
“Nani?”
“Ina maana mimi haunijui?” Timoth aliuliza swali lililomfanya dada yule kuanza kumwangalia katika hali ya kumchunguza.
“Aaaahh! Kumbe mheshimiwa! Samahani. Mkeo hajafika hapa” Yule dada alijibu.
“Hajafika? Mbona niliambiwa amekuja hapa Kliniki!”
“Mhh! Hapa ala sijamuona toka asubuhi” Yule dada alitoa jibu lililomchanganya sana Timoth.
**************
Dominick alikuwa akifuatilia kila kitu, ratiba ya Edith ya kwenda katika kliniki ilikuwa kichwani mwake. Kitu alichokifanya kwa wakati huo si kumfuatilia kuanzia nyumbani, alichokifanya yeye ni kwenda moja kwa moja katika kliniki ambayo Edith alikuwa akienda kila siku.
Kwa kuwa hakuja na gari lake, akaelekea katika sehemu ambayo wagonjwa walikuwa wakipumzikia. Dominick alitulia huku akiwa amevalia kofia kichwani mwake. Dominick hakuwa hivi hivi, mkononi alikuwa na kidumu cha njano ambacho ndani yake kulikuwa na petroli.
Alikaa katika sehemu ile kwa takribani dakika kumi, gari aina ya Harrier ikaanza kuingia mahali hapo. Tayari Dominick alijua kwamba lile gari lilikuwa likiendeshwa na Edith, mke wa waziri Timoth, Wala hakuonekana kuwa na haraka, aliendelea kusubiri kwa muda, Edith akateremka kutoka garini nakuanza kuelekea ndani ya jengo la kliniki ile.
Baada ya dakika arobaini na tano, Edith akatoka na kuanza kulifuata gari lake. Dominick akaanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata Edith. Mara baada ya Edith kuufungua mlango wa upande wa dereva, Dominick akaufuata mlango wa upande mwingine na kuingia huku akiwa na kidumu chake.
Edith akaonekana kushtuka, hakuelewa ni mtu gani alikuwa ameingia garini mwake. Hata kabla hajaongea kitu chochote kile, akauona mdomo wa bunduki ukiwa umemlenga mahali pale alipokuwa. Edith akaanza kutetemeka kwa hofu, tayari alijiona kuwa nusu mfu.
“Ukipiga kelele…ukiongea chochote au hata kuuliza swali lolote…roho yako halali yangu” Dominick alimwambia Edith huku akiiweka vizuri kofia yake pamoja na miwani yake myeusi.
“Unachotakiwa ni kufuata maelekezo yangu. Washa gari na moja kwa moja endesha kuelekea katika pori la Nyakipande” Dominick alimwambia Edith ambaye alikuwa akitetemeka tu.
Hakukuwa na sababu ya kuuliza swali, tayari mkwara ambao alikuwa amepigwa ulikuwa umemuogopesha kupita kawaida. Akaliwasha gari na safari ya kuelekea katika pori la Nyakipande lililokuwa Mbezi kuanza. Garini Dominick hakutaka kuongea kitu chochote kile, alikuwa makini kuangalia mbele.
Alikishikiria vizuri kidumu chake kilichokuwa na petroli tayari kwa kumchoma moto Edith mara tu watakapofika Nyakipande. Dominick hakujali kama Edith alikuwa mjauzito au la, kitu ambacho alikuwa akikijali mahali hapo ni kulipiza kisasi kwa kuteketezwa kwa familia yake.
Muda wote Edith alikuwa akitetemeka, tayari alijiona kuelekea kuuawa. Kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka kupita kiasi. Hakuwa na amani kabisa moyoni mwake, tayari aliona muda wowote ule alikuwa akielekea kuuawa.
Kutokana na foleni za hapa na pale, walitumia saa moja mpaka kufika Mbezi na kuingia katika pori hilo. Gari likaegeshwa katikati ya pori, sehemu ambayo hakukuonekana kuwa na dalili yoyote ile. Dominick akaufungua mlango na kutoka nje, akaelekea katika mlango uliokuwa katika upande wa dereva na kumfungulia Edith mlango.
Dominick akamshika Edith na moja kwa moja kumpeleka katika mti mmoja mkubwa na mrefu. Edith alikuwa akilia, hakuamini kama katika kipindi hicho alikuwa akielekea kuuawa. Tayari harufu ya petroli ilikuwa ikisikika vizuri puani mwake, hakuona kama angeweza kunusurika.
Dominick akaingiza mkono mfukoni na kutoa kamba ngumu, akamsogeza Edith mtini na kisha kumfunga. Muda wote Edith alikuwa akilia huku akipiga kelele lakini Dominick hakuonekana kuelewa kitu chochote kile. Edith alikuwa akiomba msamaha japokuwa hakujua kosa lake lilikuwa nini.
“Ni lazima nikuue kwa kukuchoma moto” Dominick alimwambia Edith na kuanza kummwagia petroli.
“Naomba unisamehe…naomba unisamehe..” Edith aliendelea kuomba msamaha
“Ni lazima nikuue. Mumeo aliiangamiza familia yangu. Na mimi ni lazima niiangamize familia yake pia” Dominick alimwambia.
“Naomba unisamehe…naomba unisamehe. Sijui chochote…” Edith alimwambia Dominick.
“Sitoweza. Mimi kama Dominick sitoweza. Nataka kuwaonyeshea kwamba sikufa, bado ninaendelea kulipiza kisasi kwa ajili ya mke wangu Christina pamoja na mtoto wangu Ibrahim” Dominick alisema huku akiungiza mkono mfukoni na kutoa kiberiti.
“Dominick….Dominick Hyera, naomba usiniue” Edith alimwambia Dominick.
Dominick akaonekana kushtuka, hakuelewa kama jina alilokuwa ameitwa aliitwa na Edith au mtu mwingine. Akayapeleka macho yake usoni mwa Edith na kuanza kumwangalia kwa makini. Dominick akazidi kusogea karibu zaidi huku macho yake yakimwangalia vizuri Edith katika hali ya kumchunguza.
“Naomba usiniue Dominick…Naomba usiniue” Edith alimwambia Dominick.
Dominick akaanza kupiga hatua kumsogelea Edith, alipomfikia na kumwangalia vizuri, Dominick akapiga magoti chini, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake, hakuamini kukutana na mtu huyo katika maisha yake. Mwili wote ulikuwa umenyong’onyea.
“Edith Philip….”
“Ni mimi Dominick…ni mimi” Edith alijibu.
*************
Kila alipokuwa akipita kwa mwanafunzi yeyote, alikuwa akichekwa kupita kiasi. Mavazi yake hayakuwa masafi hata kidogo, yalionekana kuchakaa kupita kawaida. Katika maisha yake shuleni hapo, Dominick hakuwahi kuvaa viatu, kila siku alikuwa akienda shuleni na kandambili miguuni.
Alionekana kuwa mwanafunzi wa tofauti kuliko wanafunzi wote shuleni pale. Wazazi wake hawakuwa na fedha hata kidogo, fedha ambazo walikuwa wamezipata katika biashara yao waliyoifanya ya kuuza shamba hazikuweza kumsaidia Dominick kutokana na asilimia kubwa ya fedha zile kuingizwa katika mahitaji mengine.
Shuleni alijisikia mpweke, hakuwahi kusifiwa kupendeza hata mara moja, kila siku alikuwa akionekana kituko machoni mwa wanafunzi wengine. Dominick hakuwa na marafiki shuleni, rafiki yake mkubwa alikuwa kitabu, kila alipokuwa akikaa peke yake, alikuwa akisoma jambo ambalo lilionekana kumpa faraja kubwa.
Katika mwaka wa kidato cha kwanza chote, Dominick hakuwa na marafiki wa kukaa nae na kuongea nae, wanafunzi wengi ambao walikuwa marafiki zake, walikuwa wakimsalimia mbali mbali tu. Jambo hili lilionekana kumuumiza sana Dominick ambaye hakuonekana kujali sana.
Alipoingia kidato cha pili, msichana Edith ndipo akaingia shuleni hapo. Kutokana na uzuri wake mkubwa aliokuwa nao, wavulana wengi walikuwa wakianza kumfuatilia Edith ambaye alionekana kuwa mgumu kumkubalia mvulana yeyote shuleni hapo.
Kit ambacho wanafunzi hawakuamini ni pale Edith alipoanza urafiki mkubwa na Dominick. Kila siku ilikuwa ni lazima kwa Edith kuelekea katika darasa la Dominick na kukaa nae huku wa kipiga stori hasa katika kipindi ambacho hakukuwa na walimu.
Edith akaonekana kuwa rafiki mkubwa wa Dominick, wakatokea kupendana kuliko wanafunzi wengine shuleni pale. Kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao wazazi wake, Edith akaanza kununua baadhi ya nguo kama mashati ya shule na kumpelekea Dominick ambaye alionekana kuwa na furaha kupita kiasi.
Ukaribu wao ulikuwa ukiongezeka kila siku kiasi ambacho mapenzi makubwa yakaanza kuibuka mioyon mwao. Wote walionekana kujaliana ingawa hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa radhi kumwambia mwenzake juu ya alivyojisikia moyoni
“Nakupenda Dominick” Hayo yalikuwa maneno ambayo mara kwa mara yalikuwa yakisikika kutoka mdomoni mwa Edith.
Dominick alikuwa akiogopa kumwambia Edith kitu chochote kuhusu mapenzi. Kila siku alikuwa akiyaangalia maisha yake na kisha kuyaangalia maisha ya Edith. Walionekana kuwa watu wawili tofauti hali ambayo ilimfanya Dominick kujiona kutokuwa na hadhi ya kuwa na msichana kama Edith.
Kama kulia, Edith alilia sana, na kama kubembeleza, Edith alibembeleza sana lakini Dominic hakuwa tayari kuwa na Edith. Alihitaji kuwa peke yake, maisha ya kutengwa ambayo alikuwa akiyaishi nyumbani, alijiona kutokustahili kupendwa na msichana yeyote yule.
Edith hakukoma, kila siku alikuwa akisisitiza juu ya upendo wake kwa Dominick ambaye bado aliendelea kukataa. Edith hakuonekana kuwa na raha, kila siku alionekana kuwa na maumivu moyoni, kuataliwa na Dominick kulionekana kuwa jambo kubwa na baya ambalo halikuwahi kutokea maishani mwake.
“Naomba unielewe Dominick” Edith alimwambia Dominick.
“Nafahamu Edith. Hebu jiangalie jinsi ulivyo, halafu niangalie na mimi. Hivi tunalingana kweli?” Dominick alimuuliza Edith.
“Mapenzi hayako namna hiyo Dominick. Mapenzi hayaagalii kuhusiana na mambo ya fedha. Mapenzi uangalia mioyo yetu. Nakuomba Dominick, nakuomba niwe pamoja nawe” Edith alimwambia Dominick.
Maneno hayo kila siku yalikuwa yakipita katika sikio la kushoto na kutokea sikio la kulia, Dominick hakuonekana kuelewa kitu chochote kile.
Siku ziliendelea kwenda mbele mpaka katika kipindi ambacho Dominick akaanza kuzielewa hisia za Edith juu yake. Dominick akagundua ni kwa jinsi gani Edith alikuwa amedhamiria kumpenda. Akaanglia jinsi ambvyo alijitolea kila kitu kwa ajili yake, hakuona sababu ya kumkataa.
Mapenzi yao yakaanza katika mwaka huo ambao walikuwa kidato cha pili. Kila siku walikuwa pamoja huku Edith akimtembelea Dominick nymbani kwao, Manzese Midizini.. Maisha ambayo alikuwa akiishi Dominick na wazazi wake yalimsononesha Edith ambaye kila wakati alikuwa akilia tu.
Alimpenda sana Dominick kiasi ambach hakutaka apate shida yoyote ile katika maisha yake, maisha ya dhiki ambayo alikuwa akiishi Dominick yalikuwa yakimuumiza kama alikuwa akiishi yeye. Pamoja na maisha hayo yote lakini Edith bado mapenzi yake makubwa yalikuwa juu ya Dominick.
Wakati wanaingia kidato cha tatu, baba yake Edith, mzee Philip akaamishiwa Kagera kikazi. Huo ndio ukawa mwisho wa wawili hawa kuwasiliana. Edith hakuwa na simu na wala Dominick hakuwa na simu. Kila siku waliendelea kukumbukana lakini hawakuwa na jinsi y kufanya zaidi ya kuendelea kukumbukana na kuotana ndotoni.
Baada ya mwaka mmoja, Dominick akamaliza kitato cha nne. Matokeo yake yalikuwa mazuri, akachaguliwa kujiunga na shule ya Azania. Moyo wake ambao ulikuwa ukimpenda sana Edith ukaanza kumpoteza kwa sababu akajiona kukata tamaa ya kumpata msichana huyo.
Pamoja na hayo yote Dominick hakutaka kumchukua msichana mwingine, alitamani maisha ya kuwa peke yake shuleni. Miaka miwili ikakatika shuleni na kufanya mtihani wa kidato cha sita. Matokeo yake hayakuwa mazuri sana hivyo akaamua kwenda kujiunga na chuo cha kuliia cha DSJ (Dar es Salaam School of Journalism)
Katika kipindi ambacho alikuwa akisoma huko ndipo alipokutana na msichana Christina katika sherehe moja iliyoandaliwa na wanachuo wa chuo hicho. Christina hakuwa mwanachuo wa chuo hicho, yeye alikuwa akitokea katika chuo cha IFM ila alikuja mahali hapo kama sehmu ya kusherehekea pamoja na marafiki zake.
Wakaanza kupeana namba za simu ambzo ziliwafanya kila siku kuwasiliana. Urafiki huo ukaendelea zaidi na zaidi huku wakichukua nafasi za kutoana mtoko. Wala haikupita hata miezi miwili, wakajikuta wakiwa wapenzi na kupeana ahadi mbalimbali za kuoana.
Edith hakuwepo tena kichwani mwa Dominick, mapenzi ya Christina yalionekana kumchanganya kupita kiasi hali ambayo baada ya kumaliza chuo, wakafunga ndoa na kuwa mume na mke.
************
Bado Edith alikuwa akiendelea kusoma mkoano Kagera. Kichwani mwake bado Domininick aliendelea kuwapo. Hakuona kama ingetokea siku ambayo angemsahau Dominick. Maisha yaliendelea kusonga mbele kama kawaida, akamaliza kidato cha nne na kuchaguliwa kujiunga na shule ya wasichana ya Tabora.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele, Edith akaanza kusahau maisha ya nyuma kwani hakuwa na matmaini yoyote kama angerudi jijini Dar es Salaam na kuonana na Dominick. Maisha yake yalikuwa ni kama yakianza upya, akaaua kujipanga upya.
Alipomaliza kidato cha sita, Edith akajiunga na chuo cha SAUT mkoani Mwanza. Huko ndipo alipokutana na mtoto wa Mbunge wa Mwanza Mjini, Tumaini Silikawa. Wakaanza urafiki ambao uliwanya kila siku kuonana na kutoka mitoko mbalimbali kama kenda ufukweni na hotelini.
Ndani ya mwezi mmoja, kila mtu akaingia katika mapenzi makubwa na mwenzake. Edith na Dominic wakatokea kupendana kupita kiasi. Kila siku walikuwa pamoja wakila raha za kila aina, mapenzi yao yalizidi kuchangamka kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Mara baada ya kumaliza chuo, wakaamua kufunga ndoa ya kifahari ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi Kanda ya ziwa.
Mara baada ya Bwana Silikawa kufariki, mtoto wake, Tumaini akshinda uchaguzi mdogo na kuwa Mbunge wa Mwanza Mjini. Maisha yao yakaonekana kubadilika, fedha kwao hakikuonekana kuwa jambo kubwa, wao kama mume na mke wakanunua nyumba mbili za kifahari, moja ilikuwa hapo Mwanza na nyingine ilikuwa Dar es Salaam.
Kutokana na kukaa Mwanza kwa uda mrefu, wakaamua kwenda kuishi katika nyumba yao iliyokuwa jijini Dar es Salaam. Tumaini hakuwasahau wananchi wake ambao walimfanya kuwa hapo, mara kwa mara alikuwa akielekea Mwanza na kuongea nao.
Baada ya uchaguzi mkuu kufanyika tena, Tumaini akshinda nafasi ya ubunge tena wa Mwanza Mjini. Maisha yalionekana kubadilika hasa mara baada ya rais kuchagua na kuwa waziri wa Mambo ya Ndani. Kwake ilionekana kuwa kama bahati, aliitumikia nafasi hiyo kadri ya uwezo wake.
Alimpenda sana mke wake lakini tatizo likawa moja, kupata mtoto. Kila siku maombi yake yalikuwa ni kupata mtoto. Hawakutaka kupima, kwani hawakutaka kujua ni nani alikuwa na tatizo katika mfumo wake wa uzazi. Waliendelea kubaki kama walivyokuwa kwani mapenzi ambayo walikuwa wakipeana, yalionekana kuwatosha.
Ujauzito ambao mke wake alikuwa nao ulionekana kumchanganya kupita kiasi, kila wakati alikuwa akiliangalia tumbo la mke wake, Edith uku akionekana kutokuamini kabisa kama katika miezi michache ijayo alikuwa akienda kuitwa baba.
Alizidi kumpenda mke wake kuliko kitu chochote kile huku akiitunza mimba ile kuliko kitu chochote kile. Alihakikisha mke wake anakula vizuri kutunza afya yake na ya mtoto wake wa tumboni.. Kila siku aliyaona masaa kwenda taratibu sana kwani kila siku alitamani kumuona mtoto wake akizaliwa, akijifunza kuongea na kutamka neno ‘Baba’ mbele yake.
Dominick alibaki kimya huku akiwa amechuchumaa chini, machozi ambayo
yalikuwa yakimtoka yaliloawanisha mashavu yake, Ni kweli allikuwa katika
mipango yake kabambe ya kulipiza kisasi lakini kwa Edith ambaye alikuwa mbele yake
ilionekana ngumu kufanya hivyo.
Alikumbuka mambo mengi ambayo alikuwa amefanya na Edith toka katika kipindi
cha nyuma, aliyakumbuka mapenzi mazito ambayo alikuwa nayo juu ya mwanamke
huyu, kingine zaidi ambacho alikikumbuka zaidi ni wema ambao alikuwa
amemfanyia.
Shule nzima ilikuwa imemtenga katika kipindi kile kutokana na kuwa katika
hali ngumu na uchafu ambao alikuwa nao, Edith ndiye alikuwa mtu pekee ambaye
alimsaidia kwa kila kitu katika kipindi kile kigumu, iweje leo hii amuue kwa
ajili ya kulipiza kisasi? Hii ingemaanisha nini katika maisha yake?
Ingemaanisha kuwa ameusahau wema wote ambao alikuwa amemfanyia katika kipindi
cha nyuma au alikuwa ameyasahau mapenzi makubwa ambayo alikuwa nayo shuleni?.
Kila alipokuwa akiyakumbuka mambo hayo, Dominick alibaki akiwa
amechanganyikiwa. Akabaki akiwa haelwi ni kitu gani kiilitakiwa kufanyika kwa
wakati huo. Huku akiwa na mawazo juu ya nini cha kufanya, mara simu ya Edith
ikaanza kuita, Dominick akaichukua, akapeleka macho yake katika kioo cha simu,
jina ‘My lovely husband’ lilikuwa likionekana vizuri machoni mwake.
Dominick akasikia hasira kupita kiasi, wivu mkali wa mapenzi ukawa
umemshika moyoni. Alimchukia sana
Bwana Tumaini kuliko mawaziri wote, hii ilitokana na kushiriki katika mauaji ya
kuiangamiza familia yake pamoja na kumchukua mwanamke ambaye alikuwa akimpenda.
“Nitamuua mumeo. Ni lazima nimuue” Dominick alimwambia Edith huku machozi
yakitiririka mashavuni mwake.
“Usimuue. Nakuomba usimuue…” Edith alimwambia Dominick.
“Nitamuacha vipi mumeo? Ameiangamiza familia yangu kwa kuichoma na moto
ndani ya nyumba yangu. Amebadilisha maisha yangu, nimekuwa mtu wa kutanga tanga.
Ameuumiza moyo wangu kwa kunifanya kuwa mpweke katika kipindi chote hiki.
Hakuna sababu ya kufanya afurahie maisha Ni lazima nimuue tu” Dominick
alimwambia Edith huku akiendelea kulia.
Kadri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo maisha yake ya
nyum yalivyokuwa yakijirudia kichwani mwake kama
mkanda wa filamu. Alikumbuka kila kitu, hakuona sababu yoyote ya kumuacha waziri
Tumaini hai, ni lazima amuue, tena kwa mkono wake mwenyewe.
ITAENDELEA KESHOOOOOOOOO
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

Post a Comment