ad

ad

VITILIVYOGO (PAPA NA MUHOGO) - 14

“Mmh! Shoga inatosha utanimalizia nyumbani.”
Betty alimaliza kinywaji chake haraka na kulipa kisha waliongozana kurudi nyumbani. Edna alikuwa na shauku ya kujua kitu gani Shaka alichomfanyia mpaka akasababisha tenki kuvunja mpaka likakauka.
                                                     ***
Majanga hayakuwa kwa Shaka na Betty tu, Stella asubuhi ilipofika kitanda kilikuwa kitamu kama nini, alijishauri mara mbilimbili juu ya kwenda shule. Alijikuta akiamua kupumzika kwani mtanange wa jana usiku ulikuwa wa kufa mtu na kumfanya achoke sana. Alikubaliana na maneno ya Diana kuwa Shaka haonjwi mara moja akakuisha hamu.
Aliamua siku ile kulala nyumbani na kusingizia kwa mama yake anaumwa tumbo baada ya kwenda kumuamsha. Diana alimpitia rafiki yake kama kawaida, alipofika alipokelewa na mama yake.
“Shikamoo mama.”
“Marahaba Diana.”
“Vipi shosti wangu ameshatoka?”
“Hapana, leo anaumwa.”
“Nini tena mama?”
“Tumbo, anasema limemuanza toka usiku.”
“Ngoja nikamuone ili niwahi shule.”
Diana alikwenda moja kwa moja chumbani kwa Stella, alimkuta amepitiwa usingizi. Alimsogelea kitandani na kumtikisa huku akimwita.
“Stella... Stella.”
“Abee,” Stella aliitika huku akigeuka kumtazama Diana.
“Vipi?”
“Mbona hivyo tatizo nini?”
“Mmh! Wee acha tutazungumza jioni ukirudi, nimechoka sana.”
“Nini Tena?”
“Mmh! Shaka temea chini.”
“Ndio ukanifanya nini kunigandisha nikaliwa na mbu.”
“Shoga yangu nisamehe, sasa hivi utachukua elfu kumi juu ya meza, lakini jioni nitakulipa fidia, naomba ukamwambie dereva akuwahishe shule.”
“Mmh! Hongera mwaya.”
Diana aliondoka huku roho ikimuuma kwa kitendo cha kugandishwa wakati mwenzake akila raha ambazo kwake alikuwa amezikosa kwa muda mrefu. Lakini moyoni alifarijika kwa kuamini siku ile utawala ungekuwa wake kutokana na Stella kutoenda shule na yeye kuwa na Shaka na jioni ya siku ile naye angepata raha alizosikosa kwa muda mrefu.
Baada ya kumueleza dereva maagizo ya Stella, alimchukua na kumuwahisha shule mara moja.
Lakini alipofika shule alijikuta akikosa raha na kuiona siku ile mbaya baada ya kumkosa Shaka aliyetegemea kumkuta shuleni. Kwa vile shule ilimtumbukia nyongo naye alisingizia ugonjwa na kurudi nyumbani.
                                                      ***                   
Siku ya pili Shaka na Stella wote walikuja shule kama waliambizana. Diana alijikuta kwenye wakati mgumu. Shida yake kubwa ilikuwa kuzungumza na Shaka kwa nafasi bila Stella kuona. Alimvizia Shaka alipokwenda msalani alimfuata ili kumuuliza. Walisubiri wakati anatoka msalani ndipo alipomsimamisha na kumuuliza:
“Shaka vipi, mbona unanitesa?” Diana alilalamika.
“Kivipi?”
“Mbona sikuelewi?”
“Kivipi?”
“Ina maana na mimi sina hamu na wewe?”
“Tatizo nini?”
“Yaani naona kila siku wewe na Stella, mimi lini jamani?”
“Stella ndiye mwenye mali.”
“Shaka nionee huruma nami nina hamu na wewe.”
“Basi kesho.”
“Jamani kesho mbali kwa nini isiwe leo? Shaka nionee huruma yaani nina hamu kama mjamzito na embe mbichi kila nikikuona mate ya uchu yananijaa mdomoni.”
“Ngoja niangalie mambo yatakavyokuwa.”
“Shaka au hunipendi? Mapenzi niliyokupa hukuyapenda?”
“Hujui jinsi gani nilivyo na usongo na wewe, niache kazi hiyo nitakujulisha hata leo jioni.”
“Yaani nitafurahi ile mba...”
“Diana, Stella huyo,” Shaka alimshtua Diana baada ya kumuona Stella akija kwa mbali.
“Mungu wangu, sijui atajua?” Diana alisema kwa sauti ya chini.
“Wewe niachie wala usioneshe wasiwasi wowote.”
“Sawa.”
Baada ya muda Stella alifika na kusimama pembeni yao. Aliwaangalia wote usoni na kumuuliza Diana.
“Diana unazungumza nini na mpenzi wangu?”
“Jamani kuna ubaya gani kuzungumza na shemeji yangu?”
“Stella tatizo nini?” Shaka aliingilia kati mazungumzo.
“Kwani huyu nani yako?”
“Shemeji yangu.”
“Sehemu hii mnazungumza nini wawili?”
“Huyu si shoga yako?”
“Ndiyo, lakini simuamini.”
“Kwa hiyo nikitaka kumtuma kwako nisimtume.”
“Mtume, lakini si kusimama muda wote huo.”
“Sawa mama.”
“Haya nimekuja mwenyewe niambie.”
“Nilikuwa namwambia jioni ukitoka unisubiri,” Shaka alitengeneza uongo.
“Yaani hata mimi nilikuwa na hamu na wewe, japokuwa juzi ulinipa kipigo cha pweza, leo ilikuwa lazima nikuambie ukanizimue. Kila ninapokuona mate ya uchu yananijaa mdomoni lakini leo baba taratibu kesho nije shule.”
“Wewe tu mama, ndiyo maana nilikuwa namtuma Diana aje akutaarifu mapema ili ujiandae usiseme nimekushtukiza.”
“Mimi na wewe hata ukiniamsha usiku wa manane huniishi hamu.”
“Basi mi’ natangulia darasani.”
Shaka alirudi darasani na kuwaacha Stella na Diana wakienda msalani. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na haja ya kujisaidia bali waliingia msalani kutimiza wajibu.
Stella  alishtuka baada ya kutoweka kwa Shaka na Diana kwa pamoja darasani, siku zote hakumuamini shoga yake kutokana na kauli tata.
Alijikuta akiingiwa na wasiwasi kitu kilichomfanya atoke darasani na kuanza kumtafuta Shaka. Bahati aliwaona kwa mbali karibu na msalani wamesimama wakizungumza.
Mtoto wa kike presha ilimpanda na kwenda kama mbogo. Lakini majibu ya Shaka ya kumtaka jioni ilimfurahisha kwani ndicho kitu alichokitaka jioni ya siku ile baada ya kipigo cha juzi yake.
Diana roho ilimuuma baada ya nafasi yake ya kupunguza mateso kuchukuliwa tena na Stella. Alimshangaa Shaka kubadili kitu walichokipanga kwa jioni ya siku ile. Lakini bado alijipanga kuzungumza na Shaka kabla muda wa kutoka shule.
Shaka naye aliamini njia aliyotumia ndiyo iliyosaidia bila hivyo Stella angewasha moto kwa vile hakuwa na simile anapopandisha hasira. Alipanga kuonana na Diana siku inayofuata.
Jioni ilipofika Shaka aliondoka na Stella kwenda kula raha na kumuacha Diana akikasirika kwa kupinda mdomo kama pindo la jamvi bovu. Hata Stella alipomuomba amsindikize alikataa kwa kusingizia kuwa Sam mpenzi wake ametuma ujumbe amsubiri. Stella alikodi gari na kuondoka wawili na mpenzi wake Shaka bila kujua kaharibu mpango wa watu.
Lakini Shaka kabla ya kuondoka alimpa Diana ujumbe wa siri uliosema: Usiumie kesho zamu yako nitazimaliza hamu zako zote. Ujumbe ule  ulimfanya Diana atabasamu kidogo.
Siku ile mchezo ulikuwa wa kawaida na kuwafanya wote wawahi nyumbani.
                                     ***     
Siku ya pili wote walikuja shuleni kama kawaida kitu kilichozidi kumuudhi Diana ambaye alitegemea shoga yake kupata kipigo cha pweza mkaidi na kumfanya asije shule.
Kwa vile siku ile Stella alikuja shule Diana ilibidi awe mbali na Shaka, lakini alikuwa katika wakati mgumu wa kumfikia Shaka bila Stella kujua. Muda wa mapumziko kama kawaida Stella alikuwa karibu na Shaka muda wote kama kawaida yake hakutaka kumpa nafasi baada ya kuugundua utamu wake.
Kipindi cha mapumziko, muda wote alikuwa karibu hakutaka msichana yeyote ajipendekeze, kitu kilichofanya kila msichana shuleni kumwita Shaka shemeji.
Wakiwa wamekaa kwenye bustani ya shule wakipata vinywaji, Diana alikuwa akihangaika kama kuku anayetaka kutaga kufikisha ujumbe kwa Shaka japokuwa kuna wakati alimkonyeza na Shaka kuishia kutabasamu tu. Shida yake kubwa ilikuwa kumfikishia Shaka ujumbe kuhusiana na ahadi yao ya kukutana siku ile jioni ya siku ile kama walivyokubaliana jana yake.
Alipoona muda wa kurudi darasani unakaribia, alijifanya anakwenda msalani, alipofika aliandika ujumbe kwenye karatasi: Sasa leo itakuwaje? Si unajua zamu yangu.
Baada ya kuandika alirudi na kukaa pembeni yao. Alimtegea Stella anatazama pembeni, akakirusha kile kikaratasi ambacho kilidondoka pembeni lakini Shaka alishindwa kukichukua, alitegea wakiondoka akiokote ajue nini kimeandikwa katika kile kikaratasi.
Kengele ilipolia wakati Stella akinyanyuka alikiona kile kikaratasi na kukifungua, Diana na Shaka wote walishtuka lakini waliondoka bila kuangalia nyuma kusubiri.
Stella alikifungua na kukisoma hakukielewa alikitupa na kumfuata Diana aliyekuwa ameshusha pumzi nzito baada ya kuona kile kikaratasi kimetupwa na Stella kuelekea alipokuwa bila kuonyesha amegundua kitu kwenye kile kikaratasi.
“Shaka mpenzi,” Stella alimwita Shaka.
“Niambie.”
“Jana nimeinjoi sana mapenzi yaani nimelala swaafi, leo nataka tena maana hamu zangu bado zipo juu kila nikikuona, ikiwezekana wiki hii yote uwe unanipa mbili za mkwezi au mguu wa jini.”
“Hakuna tatizo baby,” Shaka alijibu huku akimtazama Diana aliyekuwa amevimba kwa hasira.
Walielekea darasani, walipofika Shaka alitoka kujifanya anakwenda msalani ili arudi kukichukua kile kikaratasi. Alichepua mwendo haraka kuwahi eneo kilichopo kikaratasi na kukichukua. Stella alitoka darasani kuelekea ofisini alishangaa kumuona Shaka akitokea kwenye eneo walilokuwa wamekaa.
Alijiuliza Shaka pale alifuata nini, alijikuta machale yakimcheza na kurudi eneo lile ambapo Shaka alikuwa ameshaondoka na kuingia darasani. Kilichomshtua Stella ni kukikosa kikaratasi kile, aliachana nacho kwani aliamini huenda ni wasiwasi wake tu.
Shaka alipofika darasani alikifungua kile kikaratasi kwa siri na kukutana na ujumbe wa Diana wa kumtaka kuwa naye kwa siku ile. Alijiuliza atafanyaje kumkwepa Stella ambaye alikuwa na hati miliki ya kummiliki na tayari alikuwa amemkubalia wakati huohuo Diana alikuwa akijua ndiyo siku yake.
Lakini aliamini kama hatamdanganya basi atamtoroka na kwenda kumpa raha Diana kwani naye alikuwa na manjonjo yake ndani ya kumi na nane ambayo aliyamisi.
Wakati Shaka akiwaza yale Diana kwenye dawati alikuwa katika wakati mgumu baada ya shoga yake kurudi alipokidondoshea kipande cha karatasi.
 Wasiwasi wake ulikuwa kuulizwa na Stella lakini baada ya kurudi hakuonesha wasiwasi wowote. Naye alikaa kimya kuogopa kujiingiza mwenyewe kwenye mtego.
Akiwa kwenye dawati lake muda mwingi aliwaza jinsi ya kupata jibu la Shaka ili ajue moja atapata au atakosa.
Wakati akiwaza yale Stella aliitumwa kupeleka madaftari ofisini, alipotoka nje ya darasa alichepua haraka mpaka kwa Shaka aliyekuwa ameinama akisoma daftari.
“Shaka vipi?” alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Poa.”
“Ujumbe umeupata?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo?”
“Kawa kawa.”
“Shaka muongo!”
“Kweli.”
“Na Stella.”
“Kazi hiyo niachie mimi, wee kaa mkao wa kula.”
“Poa.”
Diana alirudi haraka kwenye dawati lake kabla ya Stella hajarudi.
                                                                ***
Diana baada ya kupata uhakika wa kuwa na Shaka jioni ya siku ile  alipanga kutoka mapema kwa kisingizio cha ugonjwa wa tumbo. Alitengeneza uongo kwa shoga yake ili akiondoka asiwe na wasiwasi.
“Stella nasikia tumbo linaniuma,” Diana alisingizia ugonjwa.
“Limeanza saa ngapi?”
“Mmh! Muda lakini sasa hivi nasikia kama kuendesha.”
“Kwani usiku umekula nini?”
“Chipsi mayai.”
“Basi yatakuwa mafuta tu.”
“Wacha niwahi msalani.”
“Shoga nenda peke yako, sikusindikizi,” Stella alijifanya kuchoka.
“Haya shoga wala nisikusumbue, si unajua matatizo ya kuendesha kazi yangu nitakuwa kama konda wa daladala kwenda na kurudi kila dakika.”
“Pole shoga, siku nyingine uwe makini na machipsi yenu.”
Diana hakujibu alijifanya kukimbilia msalani, alifurahi mpango wake kwenda kama ulivyopangwa. Baada ya kwenda kama mara tatu Stella aliamini shoga yake ni mgonjwa kweli.
“Shoga tumbo leo silielewi bora nikapumzike.”
“Kapumzike shoga yangu.”
Diana aliondoka na kicheko moyoni huku akimng’ong’a shoga yake  ambaye aliamini shoga yake kweli anasumbuliwa na tumbo. Diana baada ya kuondoka alikwenda zake kwenye nyumba ya wageni waliyokwenda siku ya kwanza kula raha zao huku akijipanga kumpiku shoga yake kwa machejo ya kwenye sita kwa sita.
                                                          *** 
Muda wa kutoka shule, Shaka alikwenda hadi kwa Stella ambaye alijua atamkuta wapi. Alipofika alijifanya mwenye wasiwasi mwingi.
“Shaka vipi mbona kama haupo sawa?” Stella alimuuliza huku akishika glasi ya juisi.
“Wakati nakuja nimekutana na mwalimu John kanieleza kuwa baba alikuja na kutoa maagizo nikitoka shule nisipite popote, mama anataka kunituma.”
“Mmh! Sasa itakuwaje?”
“Yaani nimechanganyikiwa najuta kupitia eneo la ofisini,” Shaka alijifanya kujilaumu.
“Siyo mbaya basi tufanye kesho.”
“Hakuna tatizo.”
“Basi kunywa juisi uwahi nyumbani,” Stella alimbembeleza Shaka anywe juisi.
Shaka alikunywa juisi harakaharaka kama mtu mwenye haraka ya kweli, Stella alimpa fedha ya kukodi teksi awahi kwao.
“Basi mpenzi wangu wahi nyumbani msalimie mama mkwe.”
Stella alimpa shilingi elfu ishirini ya nauli.
“Mpenzi itakusaidia kwa nauli.”
“Asante,” Shaka aliipokea na kutoa pochi mfukoni ili aweke fedha aliyopewa.
Kumbe wakati anatoa pochi karatasi ya ujumbe wa Diana ilidondoka bila kujua, Stella aliimana kuiokota. Wakati ananyanyuka Shaka naye alikuwa akigeuka kwa haraka alikitupia kwenye begi  la madaftari na kutulia. Shaka aliagana na Stella na kuwahi kwenye miadi yake na Diana aliyetangulia machinjioni.
Baada ya Shaka kuondoka, Stella alikitafuta kile kikaratasi lakini hakukiona, alipanga atakwenda kukitafutia nyumbani. Kwa vile shoga yake aliondoka anaumwa aliamua kupitia kwao kumjulia hali. Alikwenda hadi nyumbani kwao na Diana lakini alielezwa hajaonekana toka alipotoka asubuhi alipokwenda shule.
Kwa vile alikuwa akimjua vizuri shoga yake alijua alikwenda kwa mwanaume tu. Aliamua kurudi kwao bila kuwaeleza lolote juu ya taarifa za kuumwa kwa shoga yake kuogopa kumchongea. Akiwa njiani kwenda kwao alimshangaa shoga yake kuwa msiri kiasi kile kushindwa kumwambia anakwenda wapi.
Alipofika nyumbani baada ya shughuli zake alikumbuka kuna kikaratasi alichoangusha Shaka na kukitupia kwenye mfuko wa madaftari. Alijikuta akipandwa na shauku kutaka kujua kikaratasi kile kina nini.
Aliuchukua mfuko wa madaftari na kumimina madaftari yote kitandani na kuanza kutafuta kwa kupekua ukurasa mmojammoja kwa umakini na kushangaa kukikuta kwenye kitabu cha hadithi.
Kabla ya kurudisha vitu vyake ndani ya begi alikifungua kile kikaratasi, alishtuka kukiona kile kikaratasi na ujumbe ambao aliuona asubuhi na kuudharau. Kilichomshtua kukikuta kwa Shaka aliyerudi sehemu alipokitupia, wazo la haraka lilimjulisha kuna siri nzito kati ya Shaka na Diana na kuona kabisa shoga yake alikuwa akimzunguka.
Alijilaumu kuchelewa kukisoma kile kikaratasi kwani lazima angewafumania, aliamini kabisa Diana hakuwa akiumwa bali kumtoroka ili akamzunguke na kura raha zake. Hata taarifa za Shaka kuitwa nyumbani aliamini hazikuwa za kweli bali uongo uliotengenezwa ili waende wakakutane.
Stella alijikuta akikosa raha kabisa usiku ukawa mbaya sana kwake na kupanga kumtia adabu shoga yake hata ukiwezekana kuuvunja kabisa kwa vile hakuwa mtu sahihi kuwa naye. Kama vile tu anamchukulia mpenzi wake vipi akiolewa anaweza kumchukulia hata mumewe.
Siku hiyo alilala kwa shida sana huku akiomba siku ya pili ifike haraka ili akamtie adabu shoga yake mnafiki. Wasiwasi wake wa siku za nyuma aliamini kuwa Diana anatembea na Shaka ulikuwa na ukweli japo Shaka alimbana kutokana na yeye kuonekana ndiye aliyeuza siri ya utamu wake, hivyo kumfanya shoga yake aingie kichwakichwa.
Lakini aliapa kesho yake moto atakaomuwashia Diana hakutakuwa na wa kuuzima, akajiapiza kuwa tayari kwa lolote hata kufukuzwa shule lakini lazima amtie adabu shoga yake anayemlamba kisogo pamoja na msaada mkubwa wa kimaisha anaompa lakini hakuridhika na kumchukulia mpenzi wake.
                                               ***
Siku ya pili kama kawaida Stella alikwenda shuleni akiwa na shauku ya kuonana na shoga yake amueleze ukweli jana alikwenda wapi. Hata hamu ya masomo hakuwa nayo zaidi ya kutaka kupata ukweli ya mambo yaliyotokea jana. Diana naye siku ile alijitahidi kumchangamkia shoga yake baada ya kujua jana kama mali zake ziliibwa:
“Jamani shoga pole,”  Diana alimpa pole Stella iliyomshtua.
“Pole ya nini shoga?” Stella alishtuka.
“Nilisikia jana ulikuja nyumbani kunitazama ukanikosa.”
“Wewe si umeondoka ukiwa unaumwa?”
“Ndiyo shoga.”
“Uliniaga unakwenda wapi?”
“Nyumbani.”
“Sasa mbona hukurudi nyumbani?”
“Sikuweza kurudi nyumbani kwa kuogopa kuboreka home kwa muda mrefu.”
“Ulikwenda wapi?”
“Kwa shemeji yako.”
“Nani?”
“Jamani kuna mwingine zaidi ya Bonny, nilipofika nilikunywa dawa na kujilaza mpaka jioni aliporudi shemeji yako akanirudisha  nyumbani.”
“Mmh! Sawa, unaendeleaje?”
“Niko poa.”
“Mmh! Sawa.”
Stella alijikuta akibakia njia panda na kujiuliza ule ujumbe katika karatasi Shaka aliandikiwa na  nani japokuwa mwandiko ulikuwa kama wa Diana. Alijikuta akirudi nyuma kwanza ili kufanya uchunguzi wa kina. Baada ya Diana kuruka kimanga Stella alipanga kumbana Shaka kuhusiana na kile kikaratasi alichokidondosha.
Aliamini kama atamuuliza swali jepesi atalipangua lakini kama atapeleka tuhuma za moja kwa moja lazima atamchanganya na kujua ukweli. Siku hiyo hata hamu ya masomo hakuwa nayo alitaka kujua nani aliingiza mkono kwenye mzinga wake na kulamba asali yake tamu kwa Shaka.
Alipanga kuonana na Shaka mapumziko huku aliapa moyoni kumshikisha adabu  yeyote akayemjua kumchukua mpenzi wake na kuwa radhi hata kufukuzwa shule lakini amshikishe adabu. Shaka naye akiwa darasani hakujua kipi kinaendelea wala kukikumbuka kikaratasi alichopewa na Diana kama kimo mfukoni au kimepotea.
Stella alimtoka Diana amwite Shaka kwenye darasa lililokuwa halina wanafunzi, Shaka alikwenda bila wasiwasi bila kujua anaitiwa nini.
Hali ya shuleni ilikuwa ya kawaida kila mwanafunzi alisimama popote kwani walimu walikuwa wamefuata mshahara benki. Alipoingia darasani alimkuta Stella ametulia darasani peke yake,
“Niambie mpenzi?” Shaka alijifanya kuchangamka.
“Poa,” Stella alijibu kwa sauti ya unyonge kitu kilichomshtua Shaka.
“ Shaka sasa hivi umekuwa si muaminifu.”
“Una ushahidi kwa hayo uyasemayo?”
“Ninao Shaka.. ninao,” Stella alijikuta akidondosha chozi mbele ya Shaka.
 “Ushahidi gani?”
“Shaka nitakupa leo jioni.”
“Ushahidi wa nini?”
“We si unabisha utauona.”
“Haya tusubiri hiyo jioni.”
“Kwa hiyo leo itakuwaje?”
“Stella naomba leo unisamehe kwa vile nilipata mualiko wa shangazi nilishindwa kukataa,” Shaka alitengeneza uongo kwa vile jioni ya siku ile alikuwa na kazi na Betty.
“Sasa mbona hukumtuma mtu kunieleza kuwa amepata mwaliko?”
“Hilo ndilo kosa langu.”
“Au Shaka umeshanichoka maana kila kukicha vituko haviishi.”
“Stella unakwenda wapi huko, lini nimekufanyia hivi?”
“Unajua Shaka! Ila mi  sitaki kusema,” Stella alisema huku akifuta machozi.
“Basi mpenzi nisamehe nakuahidi sitakuumiza tena.”
 “Sawa Shaka nitafanyaje nami nakupenda wewe nifanyie vituko lakini mwisho wa siku utajua mwenye mapenzi ya kweli ni mmoja tu,  mimi Stella wengine wote wezi na matapeli.”
 “Nimekuelewa mpenzi wangu lakini wasiwasi wako tu, mimi ni wako peke yako.”
“Shaka naomba unyamaze usinichefue.”
“Haya mama nimenyamaza.”
“Jioni ya leo nina kazi na wewe, tena nataka maelezo ya kina bila hivyo leo nitamtwanga mtu, siwezi kuliwa kisogo huku najiona.”
“Stella mbona kila dakika huishi lawama.”
“Utasema hivyo lakini leo jioni utaujua ukweli.”
“Haya mama jioni tutajua mbivu na mbichi.”
“Baby nimeshikika ngoja niwahi msalani.”
“Poa, ukitoka huko urudi hapa.”
Shaka alikwenda msalani, wakati anarudi alikutana na Diana naye anatoka msalani.
“Mambo mpenzi?”
“Poa.”
“Jana umenipa burudani ya kufa mtu.”
“Aah! Kawaida tu.”
Kumbe wakati wakizungumza Stella aliwaona kwa mbali na kuja kasi alipokaribia Shaka alikuwa wa kwanza kumuona.”
“Stella huyo.”
“Yupo wapi?” Diana alipogeuka alikutana na uso wa Stella uliojaa shari, Stella alikuja na kazi moja kumtia adabu shoga yake baada ya kuona akilamba asali yake kwa siri na kumgeuza babu jinga inama ufikiri mali yako inaliwa.
Stella aliyekuwa na hasira alikwenda moja kwa moja kumvaa Diana, kitu kilichomfanya ashtuke na kuhoji.
“Stella vipi?”
“Diana kwa nini unanizunguka?”
“Mimi?” Diana alijifanya kushangaa.
“Unafanya nini msalani na Shaka?” Stella alimuuliza kwa sauti ya juu.
“Jamani mbona makubwa, imeanza lini?” Diana alijifanya kushtuka.
“Stella leo umekuwaje?” Shaka naye aliungana na Diana kushtuka huku akitaka kumtenganisha na Diana.
“Niache nimshikishe adabu,” Stella alitumia nguvu kumkunja Diana.
“Stella hapa ni shule mambo hayo hayafai tutafukuzwa shule,” Shaka alimtahadharisha Stella.
“Acha nikufuzwe lakini nimshikishe adabu.”
“Leo una tatizo gani, kusimama na Stella nimeanza leo? Umemtuma kwangu mara ngapi? Muda si mrefu ulimtuma kwangu, umenitanguliza naye sehemu mara ngapi?” Shaka alijifanya kuja juu.
“Shaka mnanila akili,” Stella alilalamika huku akiangua kilio.
“Naomba unisikilize,” Shaka alimbembeleza Stella aliyekuwa amepandwa na hasira.
“Utaniambia nini Shaka wakati nina ushahidi?”
“Ushahidi gani Stella?”
“Najua mtaumbuka siamini kama Diana angenilamba kisogo,” Stella aliendelea kulalamika huku akitokwa machozi.
“Stella jamani, Shaka ni shemeji yangu kuna kosa gani kusimama naye kwani limeanza leo?” Diana alijitetea.
“Jamani hebu tuwe wastaarabu, kama kuna tatizo tutazungumza jioni baada ya masomo.”
“Edna una bahati leo ningefukuzwa shule kwa ajili yako,” Stella alimwambia shoga yake kwa hasira.
“Jamani tusambae mkuu wa shule anakuja huku,” Shaka aliwashtua walipogeuka walimuona mkuu wa shule akielekea upande ule.
Shaka na Stella walielekea msalani na Diana alirudi darasani akiwa na maswali lukuki sababu ya Stella kumbadilikia ikiwa asubuhi walikuwa wakicheka pia hata kusimama na Shaka haikuchukua hata dakika mbili kusema aliwaona kwa muda mrefu akajua wanatongozana.
Hali ya shoga yake kipenzi kumkunja shati huku akiwa amekasirika na kuwa tayari kwa lolote.  Alijikuta akiwa na maswali juu ya kukutana jana yake kwa siri na Shaka huku ikiwa hakuna mtu aliyewaona kwani kila mmoja alikwenda kivyake kwa hilo aliamini hujui lolote huenda ni wasiwasi wake tu lakini hakuwa anajua lolote juu ya kukutana na Shaka jana yake.
Kutokana na kuwa na mawazo mengi alijikuta amepita darasa mpaka alipoitwa na mwanafunzi mwenzake ndipo aliposhtuka na kurudi darasani mwake. Muda wote alikuwa ajiuliza jioni itakuwaje kikao chake na shoga yake kipenzi aliyegeuka mbogo na kutaka kumpa kipigo cha mbwa mwizi.
Alijiuliza huo ushahidi anaotaka kuutoa ni upi? Picha? Alikataa na kuamini hajawahi kupiga picha na Shaka pia hata kukutana kwao mazingira hayakuwa rahisi kuwatilia mashaka na mtu. Alijipa moyo kusubiri jioni ifike ili atoe ushahidi unaoonesha yeye na Shaka ni wapenzi.
Shaka na Stella wakiwa wanaelekea msalani Stella alimwita Shaka.
“Shaka.”
“Unasemaje?”
“Ukitoka msalani nisubiri.”
MTUNZI: DK. AMBE
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
Website: www.2jiachie.com
ANGALIZO: ITAENDELEAMPAKA MWISHO HAPA KAMA SHARE ZITAFIKA 3,000 NA COMMENT 2,000 VINGINEVYO MTAMALIZIA KATIKA KITABU

ITAENDELEA SIKU YA KESHO

No comments

Powered by Blogger.