UNAAMBULIA MAUMIVU KILA UKIPENDA? JIFUNZE HAPA
HAPAWENGI sana wanaumizwa penzini, wanakutana na mtu na kutupa mapenzi yao yote lakini ndani ya muda mfupi wanaambulia maumivu.
Wanasema labda siyo bahati yao, wanahamia kwingine lakini nako pia wanakuta yaleyale hapo ndipo baadhi yao wanapoanza kusema; oooh, mimi sina bahati, oooh labda sijapangiwa kuishi na mume au mke kwani anaona umri unazidi kuyoyoma pasipo kumpata mwenza wa maisha.Ndugu zangu, kuna kitu cha kujifunza katika eneo la uhusiano ili kuepuka maumivu ya kila siku.
Achana na dhana zisizokuwa na kichwa wala miguu, yakupasa ujifunze kudumu penzini ili ikiwezekana huyo uliyenaye mfikie hatua ya kuwa mume na mke.
Kuanzisha uhusiano, kuujengea mizizi na mkazoeana inahitaji kila mmoja wenu ajitoe haswa kwa mwenzake. Mnapoanzisha uhusiano kila mmoja wenu anakuwa na tabia zake tofauti, uvumilivu unatakiwa katika kusomana tabia.
Yawezekana mwenzako akawa na tabia ambayo labda haikufurahishi, usikimbilie kuachana naye, tumia busara kumbadilisha mwenzako. Pigana mpaka dakika ya mwisho kulinda penzi ulilonalo.
Ukitumia ukali kumbadilisha mwenzako, yawezekana naye hapendi ukali, anakuacha. Utakubali kuachana naye kwa kusingizio kwamba eti utampata mwingine, nani kakuongopea huko nako utaambulia maumivu ambayo hukuyategemea kwani huwezi jua kwamba unayemfata naye ataweza kuvumilia lugha ya ukali.
Mbaya zaidi, kutokana na watu wengi kuumizwa kwa sasa, wameamua kuwa watu wa kucheza na akili za wenzao. Hawana mapenzi ya kweli. Tatizo hili limekuwa likiwatesa zaidi wasichana, wanaingia katika mapenzi na vijana ambao wameshaamua kucheza na hisia za wenzao bila kujali kwamba kuna wakati naye atahitaji kuwa na familia yake.
Maumivu ya kila siku ndiyo ambayo yanasababisha vijana wengi kwa sasa kufata yale maneno ya ule wimbo wa Lady Jaydee usemao; “Namaliza leoleo tu…hakunaga mapenzi yale, kupendana ni zama za kale.”
Wanapendana leo na kuachana siku hiyohiyo, eti hakuna haja ya kuendeleza penzi siku inayofuata. Tunajiongopea, utakuwa na kazi ya kubadilisha mpenzi kila kukicha? Faida yake ni nini sasa!
Tunapaswa kuepuka papara katika kuanzisha uhusiano. Hakikisha unamsoma mwenzako vizuri kabla ya kuingia naye penzini. Kaa chini utafakari kabla ya kuanzisha uhusiano mpya, jipe muda wa kumtafakari huyo mtu ambaye unaona yupo mbioni kuwa mpenzi wako.
Usipokuwa na papara, yawezekana ukagundua mapema vitu vingi viovu kutoka kwa mwenzako ukaona haina haja hata kuingia penzini.Jifunze kupitia penzi lako la awali. Jiulize ni kitu gani kilisababisha muachane na mpenzi wako wa awali. Ukitulia na kutafakari kwa makini utagundua tu wapi ulikosea au pengine mwenzako alikosea.
Kwa kulitambua hilo litakusaidia pale utakapoanzisha uhusiano mpya kwani utalibaini tatizo mapema kwani umeshajifunza tatizo kupitia mapito yako ya penzi la awali.
Zitambue sifa za mume au mke mwema, ikiwezekana jifunze kupitia wakubwa waliokutangulia. Jifunze kupitia bibi, babu au hata wazazi wako. Mume au mke bora ana sifa tofauti kabisa na mabinti viruka njia au wanaume ‘mabitozi’.
Ukijifunza hilo basi utakuwa makini katika kuchagua mume au mke mwema.
Kubwa na la muhimu kuliko yote ni kumtanguliza Mungu. Mtangulize katika suala mume au mke mwema. Kwa imani yako, muombe Mungu akuoneshe mke au mume mwema.
Kwa macho yetu ya tamaa za kibinadamu huwa ni vigumu sana kumtambua.
Utadanganyika kwa kigezo cha uzuri pasipo kujua tabia zake, utaambulia maumivu. Tumuombe yeye, hakika hatatuangusha!
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Post a Comment