ad

ad

MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU - 04

   “Mbona unafanya hivi Beatrice? Nimejinyima kwa ajili yako. Nimetunza fedha zangu za shule mwezi mzima kwa ajili ya kukununulia maua. Umeyatupa? Tena katika pipa la takataka!” Simon alimwambia Beatrice huku machozi yakianza kumtoka.
   “Ulitaka nifanye nini? Niyapokee?” Beatrice aliuliza huku akionekana kukasirika.
   “Hicho ndicho nilichokitaka Beatrice”
   “Hauna nafasi kwangu. Ninakuchukia sana Simon. Kama ungejua jinsi ninavyokuchukia, usingejaribu kunifuata katika maisha yako yote” Beatric alimwambia Simon.

   Beatrice akaanza kupiga hatua kulifuata gari la Walter ambaye alikuwa akimsubiria na kisha kuingia. Akambusu Walter shavuni na kisha gari kuwashwa na kuondoka mahali hapo. Simon akabaki akilikodolea macho gari lile huku moyo wake ukizidi kumuuma zaidi.
   Simon akageuka nyuma na kutaka kuondoka mahali hapo. Macho yake yakagongana na macho ya Violeth ambayo yalikuwa yakitoa machozi. Simon akaanza kujihisi vibaya moyoni mwake, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyesababisha machozi yale kutiririka mashavuni mwa Violeth.
   Beatrice alikuwa akimuumiza moyoni mwake kila siku lakini pia yeye mwenyewe alikuwa akimuumiza Violeth kila siku. Alimuonea huruma Violeth lakini bado hakutaka kuwa nae, msichana ambaye alikuwa akimfikiria kwa wakati huo alikuwa Betrice pekee ambaye wala hakuwa akimuelewa kwa chochote kile.
   Kamwe hakutaka kukata tamaa, bado aliendelea kumfuatilia beatrice ambaye bado mapenzi yake kwa Walter yalikuwa makubwa. Mara kwa mara alikuwa akilia mbele ya Beatrice ambaye kamwe hakuhisi kuwa na mapenzi yoyote juu ya Simon zaidi ya kuendelea kumchukia mvulana huyo.
   Bado Simon alikuwa akiendelea kumletea maua Beatrice lakini maua yote hayo alikuwa akiyatupa katika pipa la takataka. Simon hakuonekana kukoma, bado alitamani kuonyesha mapenzi ya kweli kwa Beatrice, akaanza kujibana na kumnunulia kadi mbalimbali zilizokuwa na jumbe nzito za mapenzi lakini vitu vyote hivyo havikuweza kuubadilisha moyo wa Beatrice, bado aliendeea kumchukia Simon.
   Miezi iliendelea kukatika na hatimae siku ya kufanya mahafari kufika. Kila mwanafunzi alikuwa amevalia mavazi yaliyokuwa yakivutia siku hiyo. Wazazi mbalimbali walikuwa wamekusanyika katika shule hiyo ya Sekondari ya Salma Kikwete kwa ajili ya kuwazawadia watoto wao zawadi mbalimbali.
   Bi Martina alikuwa miongoni mwa wazazi ambao walikuwa wamekusanyika shuleni hapo. Kila wakati alikuwa akimwangalia mtoto wake, Simon ambaye wala hakuonekana kuwa na furaha. Simon alionekana kuwa na mawazo, hakuamini kwamba zilikuwa zimebakia wiki mbili kabla ya kutengana na Beatrice ambaye hakuwa na mategemeo kama angeweza kumuona tena.
   “Mbona hauna furaha mwanangu?” Bi Martina alimuuliza Simon.
   “Namfikiria baba. Ningetamanai nae awe mahali hapa na kuiona siku hii ambayo kwangu ni siku muhimu sana maishani mwangu” Simon alimwambia mama yake.
   “Usijali mwanangu. Kuwa na furaha, niko hapa na ninamuwakilisha pia” Bi Martina alimwambia Simon.
   Kila wakati macho ya Simon yalikuwa yakimwangalia Beatrice ambaye alikuwa amekaa sehemu moja pamoja na Walter. Simon alionekana kuchukia kupita kawaida, alimuona Walter kukaa sehemu isiyo sahihi. Alitamani amfuate Walter na kisha kumtoa na kukaa yeye karibu na Beatrice.
   “Nitakuchukia siku zote Walter” Simon alijisemea huku akiwaangalia.
   Mahafari yale yalichukua masaa manne mpaka kumaliza. Picha bado zilikuwa zikiendelea kupigwa. Alichokifanya Sion ni kupiga kumuaga mama yake kwamba anaelekea darasani mara moja na angerudi muda mchache baadae. Alichokifanya Simon mara baada ya kuruhusiwa ni kuanza kupiga hatua kumfuata Beatrice ambaye alikuwa pamoja na wazazi wake.
   “Shikamooni” Simon aliwasalimia.
   “Marahaba” Bi Imelda aliitikia.
   Simon akayageuza macho yake na kisha kuanza kumwangalia Beatrice kwa macho ambayo yalionyesha kuhitaji kufanyika utambulisho juu ya watu wale ambao walikuwa mahali pale. Beatrice akaonekana kugundua jambo hilo, alichokifanya ni kuanza kutoa utambulisho.
   “Simon. Huyu ni mama yangu. Huyu hapa ni mdogo wangu anaitwa Paula, huyu mjomba wangu na yule pale ni binamu yangu” Beatrice alitambulisha huku uso wake ukiwa na tabasamu.
   “Nashukuru kuwahamu”
   “Mama. Huyu ni mwanafunzi mwenzangu anaitwa Simon” Beatrice alimtambulisha Simon.
   “Ndiye yule kijana aliyechukua zawadi ya taaluma?” Bi Imelda aliuliza.
   “Ndio”
   “Hongera sana Simon. Ungependa kuwa nani hapo baadae?”
   “Daktari. Ningependa kushughulika na matatizo ya mifupa ya binadamu”
   “Safi sana. Mungu akusaidie kufikia malengo yako”
   “Asante” Simon alishukuru na kisha kumgeukia Beatrice.
   “Naomba tukapige picha ya ukumbusho”
   “Usijali” Beatrice aliitikia.
   Wote wawili wakatoka na kwenda darasani na kisha kumuita mpiga picha ambaye akafika mahali hapo na kisha kuwapiga picha mbili. Alichokifanya Beatrice ni kuzilipia zile picha.
   “Utazichukua zikiwa tayari. Hiyo itabaki kuwa kumbukumbu kwako kusoma na msichana mrembo kama mimi” Beatrice alimwambia Simon na kisha kuondoka.
   Simon akabaki darasani kwa muda huku akionekana kufikiria mambo mengi kichwani mwake. Maneno aliyoyaongea Beatrice yalikuwa maneno ya kawaida lakini kwa upande mwingine yalionekana kama kumuumiza. Kwa haraka haraka akachomoka darasani huku lengo lake likiwa ni kumfuata Beatrice. Alipoangalia mahali kule alipokuwa, akamuona Walter akiwa pamoja nae huku waote wakionekana kuwa na furaha.
                                                                        ***************
                                                                    Mitihani ikafanyika na hatimae wanafunzi wa kidato cha nne nchini Tanzania kumaliza elimu ya chini ya Sekondari. Japokuwa kila kitu kilikuwa kimekamilika lakini bado kuna jambo moja lilitakiwa kufanyika. Sahihi za wanafunzi zilikuwa zikihitajika katika baraza la mitihani jambo ambalo liliwapelekea wanafunzi kurudi tena shuleni kwa ajili ya kusaini karatasi hizo.
   Zoezi hilo lilitakiwa kufanyika ndani ya siku moja tu na ndo siku ambayo Simon aliiona kuwa siku maalumu ya kuendelea kumwambia Beatrice jinsi aivyojisikia moyoni mwake. Mara baada ya kusaini karatasi zile, moja kwa moja Simon akaanza kumfuata Beatrice ambaye alikuwa pamoja na Walter wakilifuata gari.
   “Beatrice” Simon alimuita na kumfanya Beatrice kugeuka.
   “Unasemaje?” Beatrice aliuliza huku akionekana kubadilika.
   “Nakupenda Beatrice. Nakuhitaji Beatrice. Najua kwamba hii inaweza kuwa siku ya mwisho kuonana nawe katika mwaka huu, ila nafikiri haitokuwa siku yangu ya mwisho kukwambia kwamba nakupenda” Simon alimwambia Beatrice huku akianza kumsogelea.
   “Kwa hiyo?”
   “Naomba unikubalie Beatrice. Kila siku nimekuwa nikisumbuka sana kwa ajili yako” Simon alimwambia Beatrice.
   Kwa mbali tabasamu likaanza kuonekana usoni mwa Beatrice, akayapeleka macho yake kwa Walter, wote wakajikuta wakianza kutoa vicheko vilivyojaa dhihaka. Vicheko vile vilimuumiza sana Simon lakini hakuonekana kujali, kitu alichokifanya kwa wakati huo ni kupiga magoti chini huku akimwangalia Beatrice kwa macho yaliyojaa huruma.
   “Nakupenda Beatrice” Simon alimwambia Beatrice.
   Wanafunzi wote ambao walikuwa wamemaliza kidato cha nne wakaanza kumwangalia Simon ambaye alikuwa amepiga magoti mbele ya Beatrice na Walter. Kila mmoja alionekana kumshangaa. Walijua fika kwamba Simon alikuwa akimhitaji sana Beatrice kuliko msichana yeyote shuleni pale, lakini waliona jambo la Beatrice kumkubali Simon lingekuwa gumu sana kutokana na fedha alizokuwa nazo Walter.
   “Mmmh..! Ana moyo wa chuma. Yaani kwa miaka miwili bado unamfuatilia msichana mmoja tu” Mwanafunzi mmoja alisikika akimwambia mwenzake.
   “Mapenzi. Simon anampenda sana Beatrice”
   “Sasa kama hamtaki si aachane nae tu”
   “Kuongea ni rahisi sana Yusto. Ila kukifanya kitendo hicho ni vigumu”
   “Mmmh! Kweli nimeamini kwamba mapenzi yameletwa duniani ili watu wengine waumizwe” Mwanafunzi mwingine aliingilia.
   Simon hakuonekana kujali macho ya watu, bado alikuwa ameendelea kupiga magoti pale chini huku akimsisitizia Beatrice kwamba alikuwa akimpenda na kumhitaji kuliko msichana yeyote shuleni pale. Beatrice nado alionekana kuwa mgumu, hakumpenda Simon hata kidogo na wala hakumbuki kama kuna siku ilitokea kumpenda mvulana yue.
   “Yaani natamani ufe Simon ili na mimi nipumzike. Kila siku unanisumbua tu” Beatrice alimwambia Simon.
   “Usiseme hivyo Beatrice”
   “Sasa wewe unataka niseme vipi? Bora ungekufa tu ili na mimi nipumzike”
   “Beatrice.....!”
   Beatrice hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo. Moja kwa moja, yeye pamoja na Walter wakaanza kupiga hatua kulifuata gari lile na kisha kuingia ndani na kuondoka mahali hapo. Simon akabaki akiwa ameumia, hakuamini kama kweli Beatrice alikuwa amemkataa kwamara nyingine tena.
   Alitamani kusimama mahali pale, alijiona kuwa mzito, akashindwa kusimama zaidi ya kuendelea kubaki mahali pale huku akiwa amepiga magoti chini. Mashavu yake yalikuwa yamekwishaloanishwa na machozi ambayo yalikuwa yakimtoka.
   Violeth akamfuata mahali pale na kisha kumuinua. Simon akasimama na kumwangalia Violeth usoni. Violeth akaonekana kuwa tofauti, nae mashavu yake yalikuwa yameloanishwa na machozi ambayo yalikuwa yamemtoka.
   “Una nini Simon? Mbona hautaki kuelewa?” Violeth alimuuliza Simon.
   Simon hakujibu kitu chochote kile, alibaki akimwangalia Violeth. Kwa mwendo wa taratibu wakaanza kupiga hatua kuelekea nje ya eneo la shule. Violeth hakutaka kumuacha Simon, alichokifanya ni kuanza kuelekea nae katika mghahawa mdogo ambao ulikuwa pembezoni mwa eneo la shule.
   “Utauumiza moyo wako mpaka lini Simon?” Violeth alianza kwa kumuuliza swali.
   “Nimechoka. Ni bora niachane nae tu. Kama alipangwa kuwa wangu, atakuwa wangu tu lakini kama hakupangwa kuwa wangu, acha aondoke” Simon alijibu kwa sauti ya kinyonge.
   “Haukutakiwa kumuomba penzi lake namna ile Simon. Kwa nini ulikuwa ukiusumbua moo wako namna ile lakini?” Violeth bado aliendelea kuuliza maswali.
   “Mapenzi. Unajua nilimpenda sana Beatrice na ninafikiri hadi sasa bado ninampenda” Simon alimwambia Violeth.
   “Hapana. Haumpendi Beatrice” Violeth alimwambia Simon ambaye alionekana kushtuka.
   “Unasemaje?”
   “Najua umenisikia vizuri kabisa”
   “Kwa nini unasema hivyo?”
   “Unajifanya kumpenda Beatrice kwa sababu tu ulisema umemuona kwenye ndoto. Si unakumbuka hata ile sauti ambayo uliisikia ndotoni?” Violeth aliuliza.
   “Nakumbuka”
   “Basi hiyo ndio sababu inayokupelekea kumtaka Beatrice. Ila nadhani huyo msichana uliyemuona ndotoni si Beatrice” Violeth alimwambia Simon.
   “Ni yeye. Nafahamu ni yeye tu”
   “Usinidanganye Simon. Ila usijali. Unachotakiwa kufanya kwa sasa ni kujipanga tu. Sahau kila kitu kuhusu Beatrice” Violeth alimwambia Simon.
   “Nitajaribu”
   “Usiseme kwamba utajaribu. Sema kwamba utamsahau”
   “Sawa. Nitamsahau”
   “Asante kwa kusikia hilo”
                                                                           **************
                                                                                
   Ukaribu kati ya Violeth na Simon ukaania hapo. Muda mwingi walikuwa pamoja huku wakifanya mambo mengi kama wapenzi isipokuwa ngono tu. Walikuwa wakitembea sehemu mbambali huku wakiwa pamoja. Walizoeana kupita kawaida huku Violeth akiitumia nafasi hiyo kuendelea kuzielezea hisia zake kwa Simon.
   Simon hakuonekana kuwa tayari kuingia katika mahusiano, akaanza kuyaogopa mahusiano kuliko kitu chochote kile. Ni kweli aliuona moyo wake ukianza kutekwa na Violeth lakini Simon hakuonekana kuwa tayari kuwa na msichana yule.
   Upande mwingine wa moyo wake bado ulikuwa ukiendelea kumpenda na kumuhitaji Beatrice ambaye alikataa kabisa kuhama moyoni mwake. Kila siku bado alikuwa akimkumbuka Beatrice huku akiamini kwamba kuna siku moja tu Beatrice angekuwa wake katika maisha yake yote.
   Ndoto ile ambayo aliiota katika miaka kadhaa iliyopita bado ilikuwa ikiendelea kumsumbua moyoni mwake. Aliikumbuka vizuri sura ya msichana yule ambaye alikuwa amemuona katika ndoto ile. Alifahamu vilivyo kwamba msichana yule hakuwa Beatrice ila alichokuwa akikifanya ni kulazimisha Beatrice awe nae kwani ndiye alikuwa msichana ambaye alitokea kumpenda katika kipindi kile alichokuwa shuleni.
   Miezi iliendelea kukatika na hatimae matokeo ya kidato cha nne kutoka. Simon alikuwa amefanya vizuri kwa kupata division one. Moyo wake ulijisikia furaha kupita kawaida. Hakuonekana kuridhika, akaanza kulitafuta jina la Beatrice. Division four ndio ambayo iikuwa ikionekana.
   Moyo wa Simon ukanyong’onyea kabisa. Hakujisikia furaha kabisa. Kutofanya vizuri kwa Beatrice kulionekana kumuumiza kwani alijua fika kwamba alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuyabadilisha matokeo yale katika kipindi ambacho alikuwa shuleni.
   Bado Simon hakuonekana kuridhika, akaanza kulitafuta jina la Walter. Matokeo ya Walter na Beatrice yalikuwa sawa. Simon akajikuta akianza akufurahia, matokeo yale ya Walter yalionekana kumfurahisha kupita kiasi.
   Simon akaanza kupiga hatua kuelekea nyumbani. Hata kabla hajafika mbali, akakumbuka kwamba kulikuwa na matokeo ya mtu fulani hakuwa ameyaangalia, alichokifanya ni kugeuka na kuurudia ubao. Akaanza kulitafuta jina la Violeth, alipoliona akaanza kuyaangalia matokeo yale.
   Violeth alikuwa amefanya vizuri kwa kuoata division two. Simon akaarijika kupita kiasi, aliona kwamba kwa aislimia kubwa yeye ndiye ambaye alikuwa amemfanya Violeth kupata matokeo yale. Mara baada ya kumaliza, akaanza safari ya kuelekea nyumbai.
   “Nashukuru” Violeth alimwambia Simon mara baada ya kufika nyumbani na kumkuta akimsubiri.
   “Usijali”
   Miezi iliendelea kukatika huku wakiendelea kuwa pamoja na kufanya mambo mengi tu. Violet alikuwa akijisikia huru kupita kawaida. Kila wakati alikuwa akihitaji kuwa pamoja na Simon. Alimpenda sana Simon kuliko mvulana yeyote.
   Shule walizotakiwa kujiunga wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao zikatangazwa. Simon akachaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Tambaza huku Vioeth akichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya wasichana ya Tabora.
   Kwa Violeth ikaonekana kuwa pigo kubwa. Hakutaka kabisa kuwa mbali na Simon, alijua ni kwa jinsi gani angeweza kumkumbuka mvulana huyo ambaye kwake alionekana kuwa kila kitu. Kila siku ambazo alikuwa akimwangalia Simon, alitamani kulia, moyo wake ulikuwa ukimuuma kupita kiasi.
   Siku ya safari ikafika, Simon akaamua kumsindikiza Violeth katika stesheni ya treni ambako alitakiwa kuianza safari yake ya kuelekea Tabora. Muda wote Violeth alikuwa akitokwa na machozi, alijisikia kuumia kupita kawaida.
   “Nakupenda Simon” Violeth alimwambia Simon.
   “Nafahamu. Uliniambia kabla na kila siku ulikuwa ukiniambia hilo” Simon alimwambia Violeth.
   “Nitahitaji uwe mume wangu Simon. Sitaki kukupoteza maishani mwangu”
   “Bado mapema sana Violeth. Cha msingi kasome kwanza, kama Mungu amepanga mimi kuwa nawe, nitakuwa nawe ila kama hajapanga, hatutakiwi kulazimisha” Simon alimwambia Violeth.
   Violeth akajisikia maumivu zaidi. Alimwangalia Simon mara mbili mbili huku akiwa haamini kama kweli bado Simon alikuwa mgumu kukubaliana nae. Ni kweli walikuwa wakionyesheana ishara nyingi za mapenzi lakini kila siku alikuwa akijiuliza juu ya sababu iliyomfanya Simon kutokumwambia neno ‘Nakupenda’
   “Unanipenda?” Violeth aliuliza huku akionekana kuwa na shauku ya kufahamu.
   “Unanionaje?”
   “Kawaida tu”
   “Nitakujibu swali lako utakapokuja Dar es Salaam. Sitaki kukuchanganya kwa sasa, kasome kwanza” Simon alimwambia ioleth.
   “Nitakupenda siku zote Simon. Hata kama nitaishi maisha gani hapo baade, ni lazima nitakutafuta. Ninakupenda sana” Beatrice alimwambia Simon.
   “Asante Violeth” Simon alimwambia Violeth.
   Honi ya treni ikaanza kusikika na abiria wote walitakiwa kuingia katika treni. Violeth akamuaga Simon kwa kumkumbatia na kumbusu shavuni na kisha kuanza kupiga hatua kulifuata treni. Siku hiyo ilikuwa ni siku iliyojaa maumivu katika maisha yake, aliona kwamba huo ndio ulikuwa mwisho wake kuonana na Simon katika maisha yake.
                                                                       *********
                                                                                  
   Matokeo yalikuwa mabaya kwa wote wawili lakini Walter hakuonekana kujali kitu chochote kile. Moyo wake haukujuta kwa nini alifeli, fedha ambazo alikuwa akizimiliki baba yake zilikuwa zimemsahaulisha na kila kitu. Hakutakiwa kuhofia kitu chochote kile kwani aliamini kwamba katika dunia ya sasa hivi, fedha ilikuwa kila kitu.
   Beatrice hakuonekana kuwa na raha, kila siku alikuwa mtu wa kujuta, alijuta kwa nini hakujishughulisha sana na masomo katika kipindi ambacho alikuwa shuleni, alijuta sababu iliyompelekea kuyaweka mapenzi mbele zaidi ya elimu.
   Walter ndiye alikuwa mtu pekee aliyekuwa akimfariji Beatrice ambaye alionekana kukata tamaa ya kuendelea kusoma. Kutokana na uwezo mkubwa wa fedha ambao ulikuwepo katika familia yake, Walter akachukua kiasi fulani cha fedha na kisha kumgawia Beatrice kwa ajili ya kuendelea kusoma katika elimu ya juu ya sekondari huku akirudia mitihani yake.
   Beatrice alishukuru kupita kawaida, hakuamini kama Walter angeweza kumsaidia namna ile. Mapenzi ambayo alikuwa nayo juu ya Walter yakaongezeka zaidi, alimpenda mara kumi zaidi ya alivyokuwa akimpenda katika kipindi cha nyuma.
   Beatrice akaanza kusoma kaika shule ya Sekondari Mbezi Beach huku Walter akiamua kusoma katika shule ya Sekondari ya Kenton. Walter hakutaka kusoma pamoja na Beatrice, alijiona kuwa na kila sababu ya kuwa mbali na binti huyo.
   Mapenzi ambayo alikuwa nayo juu ya Beatrice yalikuwa yamepungua kabisa ila kumwambia ukweli alikuwa akihofia kufanya hivyo. Alijua ni kwa kiasi gani binti huyo alikuwa akimpenda, alijua ni kwa jinsi gani binti huyo alikuwa amejitolea maisha yake kwa ajili yake.
   Kwanza alihitaji kuwa mbali nae, aliona hiyo kuwa sababu ambayo ingempeekea binti huyo kumsahau taratibu mpaka kuja kuachana rasmi. Walter alijiona kuhitaji damu mpya, alijiona kuwa na kila sabau ya kuwa na msichana mwingine mrembo ambaye angekuwa na kila vigezo vya kumkataa Beatrice.
   Katika shule hiyo ndipo Walter alipokutana na msichana mrembo, Jalia. Jalia alikuwa miongoni mwa wasichana ambao walikuwa wakivutia shuleni hapo. Mwili wake ulikuwa mwembamba huku ngozi yake nyeusi yenye kung’aa ikimfanya kupendeza katika kila eneo ambalo alikuwa akisimama au kukaa.
   Jalia alionekana kuwa msichana wa kipekee, tabasamu lake kali lilikuwa likivifanya vitundu vyake vidogo mashavuni vionekane. Us wake ulikuwa na mvuto wa hali ya juu ukiachilia mwendo wake wa kunyata ambao ndio ulikuwa chachu kubwa kwa kila mwanaume ambaye alikuwa akmwangalia.
   Jalia alijitambua kwamba alikuwa msichana mrembo ambaye alikuwa akivutia na hiyo ndio ilikuwa sababu iliyomfanya kuamua kuwa na Walter ambaye alikuwa na fedha za kutosha za kuweza kuendelea kuutunza urembo wake.
   Uhusiano wa Walter na Jalia ukaanza rasmi siku ya Jumatano, siku maalumu kwa ajili ya michezo shuleni hapo. Walter akajiona kuwa katika hali ya tofauti, uzuri wa Jalia ulikuwa ukimchanganya kupita kwaida. Hakujisikia raha hata mara moja kuwa mbali na Jalia, kila wakati alikuwa akitaka kuwa karibu na Jalia ambaye alikuwa akizidi kuongezeka uzuri kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
   “Tatizo lako hilo tu” Jalia alimwambia Walter.
   “Lipi?”
   “Ngono. Yaani kila wakati unafikiria ngono tu” Jalia alimwambia Walter.
   “Wewe ni msichana wangu Jalia, nina haki zote za kuuona mwili wako na hata kufanya mapenzi pamoja nawe. Kama hautofanya na mimi, unafikiri utafanya na nani tena? Au kuna mwingine?” Water aliuliza huku kwa mbali akionekana kubadilika.
   “Lakini mapema sana. Au unataka kufanya na mimi kisha uniache?”
   “Nikuache? Hivi kuna mvulana ambaye anaweza kuthubutu kukuacha na uzuri wako huo? Hapana Jalia, muda umefika wa mimi kufanya kitu cha tofauti na urafiki. Sisi ni wapenzi kwa hiyo ni lazima tuidhihirishie dunia kwamba sisi ni wapenzi” Walter alimwambia Jalia ambaye alibaki kimya.
   “Sawa. Ila sitaki tufanyie guest house” Jalia alimwambia Walter.
   “Hakuna hadhi huko. Tutafanyia katika hoteli moja kubwa na nzuri. Ungependa twende wapi?” Walter aliuliza.
   “Travertine Hotel”
   “Sawa” Walter aliitikia.
                                                                       ************
    Gari aina ya Harrier lilikuwa likipaki katika eneo la hoteli ya Travertine iliyokuwa Magomeni. Walter akateremka na kisha kuanza kupiga hatua katika mlango wa pili ambako akaufungua na Jalia kuteremka. Wote wakaanza kupiga hatua kuelekea mapokezini.
   Mara baada ya kukamilisha kila kitu kuhusu malipo, wakaanza kuelekea kati chumba ambacho walikuwa wameelekezwa kilichokuwa katika ghrorofa ya nne. Muda wote huo walikuwa wameshikana kimahaba. Mara baada ya kuufikia mlango, wakaufungua na kuingia ndani.
   Chumba kilionekana kuwa na mvuto kupita kawaida, kila kitu ambacho kilitakiwa kuwepo katika chumba cha hoteli ya kifahari kilikuwa ndani ya chumba hicho. Walter hakutaka kuchelewa, akavua fulana yake pamoja na suruali yake ya jinzi na kisha kujitupa kitandani.
   Muda wote Jalia alikuwa akitabasamu, kwake kuingia katika hoteli iliyokuwa na chumba kizuri namna ile ilikuwa kama ndoto ambayo kila siku alikuwa akitamani itimie. Moja kwa moja akaanza kuchojoa nguo zake.
   Walter alibaki akimwangalia kwa macho yaliyojaa matamanio, Jalia alikuwa akivua nguo zake kwa mapozi. Katika kila hatua ambayo Jalia alikuwa akipiga katika uvuaji wa nguo zake, Walter alijiona akicheleweshwa. Alitamani amfuate na kumrukia.
   “Uko tayari nije kitandani?” Jalia alimuuliza Walter
   “Muda wote. Njoo ukate kiu yangu” Walter alimwambia Jalia.
   Jalia akaanza kupiga hatua za kimapozi na kukishika kitanda kwa staili ya kuinama huku akiwa amebaki na nguo ya ndani tu mwilini mwake. Walter akajiandaa vilivyo kumpokea Jalia ambaye bado alikuwa akiendelea kumsogelea mahali pale alipokuwa.
   Huku akiwa amemfikia, mara simu ya Walter ikaaanza kusikika ikiita. Kwa haraka huku akionekana kukasirika, akaunyoosha mkono wake na kuichukua simu ile. Akayapeleka macho yake katika kioo cha simu ile, jina la Baby Beatrice lilikuwa likionekana vizuri machoni mwake.
   “Mmmmh!” Walter aliguna kimoyo moyo.
                                                                             ************
                                                                               
   Simon akaamua kusahau kila kitu ambacho kilitokea katika kipindi kile alichokuwa shuleni, hakutaka kabisa kumkumbuka Beatrice ambaye siku zote shuleni alikuwa akiutesa moyo wake na kumkosesha raha. Simon akaamua kuingia rasmi katika masomo, hakutaka kuyatamani mapenzi, aliyaona mapenzi ndio yalikuwa sababu iliyomfanya kukosa furaha shuleni.
   Simon hakutaka kumfuatilia msichana yeyote shuleni pale zaidi ya kuamua kuwa peke yake katika kipindi chote ambacho angekuwa shuleni pale. Kila alipokuwa akiwaona wavulana ambao mara kwa mara walikuwa wakiteseka katika mapenzi na ndivyo ambavyo alivyokuwa akikumbuka maisha yake ya nyuma aliyokuwa akiishi shuleni.
   Baada ya muda wa miezi sita, kila mwanafunzi akajua kwamba Simon hakuwa mvulana aliyekuwa akipenda wasichana. Siku zote alikuwa akiongea nao na kucheka nao lakini kamwe hakuwahi kuongea kitu chochote kuhusiana na uhusiano wowote wa kimapenzi.
   Simon akaonekana kujifunza. Hakutaka kuishi maisha yasiyokuwa ya furaha kama ambavyo alivyokuwa akiishi katika kipindi cha nyuma shuleni. Alijifunza mambo mengi kuhusiana na mapenzi, hakukuwa na sababu ya kuyarudia makosa kama yale ambayo alikuwa ameyafanya.
   Mara kwa mara ndoto ambayo aliiota katika miaka ile ya nyuma ilikuwa ikijirudia kichwani mwake. Sura ya msichana yule ilikuwa ikijirudia rudia kichwani mwake. Kila siku alikuwa akitamani kumfahamu msichana yule lakini haikuwezekana.
   Msichana yule ambaye alimuona ndotoni alikuwa msichana ambaye hakuwahi kumuona katika ulimwengu halisi. Alionekana kuwa msichana mzuri ambaye kwa kila mvulana ambaye angemuona basi asingesita kumwambia neno ‘nakupenda’
   Ni kweli kwamba alikuwa akimng’ang’ania sana Beatrice ingawa alijua kwamba msichana yule wala hakuwa Beatrice. Shauku yake kubwa ilikuwa ni kumuona msichana yule ambaye alikuwa amemuona ndotoni.
   Simon hakutaka kutulia shuleni, kila sikualikuwa akimtafuta msichana yule ambaye alikuwa akifanana na msichana yule aliyemuona ndotoni mwake. Simon alibahatika kuwaona wasichana wote waliyokuwa wakisoma katika shule ile ya Tambaza lakini hakumuoa msichana yeyote ambaye alikuwa akifanana na msichana yule ambaye alimuona ndotoni mwake.
   “Au ndio huyu Natasha?” Simon alijiuliza katika kipindi ambacho alikuwa akimwangalia Natasha.
   Natasha alikuwa msichana mzuri, uzuri ambao ulikuwa zaidi ya ule aliokuwa nao Beatrice. Umbo lake halikutofautiana na Beatrice, walikuwa wamefana kwa vitu vingi sana na kama kulikuwa na tofauti, basi sura pamoja na tabia havikuendana.
   Ingawa Natasha alikuwa akisifika kwa uzuri shuleni hapo lakini kamwe hakuwa na maringo. Kila mtu kwake alionekana kuwa sawa, alimsikiliza kila mtu. Wavulana kama kawaida yao hawakutaka kubaki nyuma, kila siku walikuwa wakimwambia Natasha maneno mbalimbali ya mahaba lakini hakuonekana kukubali.
   Natasha hakutaka kuwa na uhusiano na mvulana yeyote yule zaidi ya mvulana mmoja ambaye kila siku alikuwa akimvutia, Simon. Mara kwa mara Natasha alikuwa akihitaji kuwa karibu na Simon lakini Simon hakuonekana kuukubali ukaribu huo.
   Moyo wake haukutaka kuingia katika uhusiano wowote ule, bado alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kuwa peke yake japokuwa alijua fika kwamba moyo wake ulikuwa umetekwa na Violeth ambaye alikuwa shuleni mkoani Tabora.
   Natasha alikuwa akifanya vituko vingi kwa ajili ya kumtega Simon lakini hakuweza kutegeka. Simon alionekana kuwa makini katika kila hatua ambayo alikuwa akiishi shuleni pale. Hakutaka kuukaribisha ukaribu pamoja na Natasha, mara nyingi alikuwa akimkwepa.
   “Mbona unanikwepa sana?” Natasha alimuuliza Simon siku moja alipobahatika kupata nafasi ya kuongea nae.
   “Kwa sababu najua unachokitaka Natasha” Simon alimjibu Natasha huku akionekana kujiamini.
   “Kitu gani?”
   “Wewe jua kwamba najua unachokitaka. Ila naomba ujue kwamba kuna mtu amekwishawahi nafasi” Simon alimwambia Natasha.
   “Mbona unanichanganya”
   “Wala usichanganyikiwe. Ni kawaida tu” Simon alijibu na kuanza kuondoka.
   Natasha alibaki akiwa amesimama, hakuamini kama nia yake ilikuwa imejulikana na Simon. Natasha hakuonekana kukubali, bado alijiona kuwa na nafasi kubwa sana ya kumshawishi Simon mpaka kuwa mpenzi wake na kupata mapenzi ambayo kila siku alikuwa akiyalilia.
   Alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kutumia fedha. Alijua moja kwa moja kwamba Simon asingeweza kutoka nje ya himaya yake. Kila siku alikuwa akimletea Simon zawadi mbalimbali. Simon alikuwa akizipokea na kiasi cha fedha ambacho alikuwa akipewa kukitumia lakini kamwe hakumkubalia Natasha.
   Miezi iliendelea kukatika huku Simon akiendelea kuchukua masomo ya Sayansi. Bado ndoto yake ya kuwa daktari wa mifupa ilikuwa ikiendelea maishani mwake. Hakutaka kufanya mchezo, mara nyingi alikuwa akijisomea huku akiamini kwamba siku moja angekuwa daktari kama alivyotaka kuwa.
   “Naomba nafasi ya kula nawe chakua cha usiku” Natasha alimwambia Simon.
   “Hapana Natasha. Vyakula vya usiku ndivyo ambavyo vinaanzisha mambo mengine” Simon alimwambia Natasha.
   “Najua kwamba umenikatalia ombi langu la kuwa nawe, yaani hadi hili la kula nawe chakula unanikatalia. Tafadhari Simon, nakuomba” Natasha alimwambia Simon.
   Tayari machozi ya uongo yakaanza kudondoka kutoka katika macho ya Natasha. Alijioa kuwa na kila sababu ya kudondosha machozi hayo kwani aliamini kwamba ni lazima Simon angemunea huruma na kukubaliana na ombi lake. Simon alibaki akimwangalia Natasha kwa macho ya huruma, tayari machozi ambayo yalikuwa yakimtoka Natasha yakaanza kuumba huruma moyoni mwake.
   “Sawa. Ila naomba uniahidi kit kimoja” Simon alimwambia Natasha.
   “Kitu gani?”
   “Kwamba hatutofanya kitu chochote kile na wala kuniambia chochote kuhusu mapenzi” Simon alimwambia Natasha.
   “Nakuahidi”
   “Sawa” Simon alijibu na kisha kuondoka huku wakipanga kwenda kula chakua cha usiku katika baa moja iliyokuwa Kinondoni.
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

No comments

Powered by Blogger.