MARIA SEHEMU - 07 (YA MWISHO)
Moyoni alijisikia maumivu makali hata zaidi ya kuchomwa na msumari wa moto.
“Unasemaje Onesmo?” Maria aliuliza kwa mshtuko.
“Sahau kila kitu Maria. Mungu ameyabadilisha maisha yangu. Mimi ni Onesmo mpya” Onesmo alimwambia Maria.
Maria akajiona akiishiwa nguvu za miguu, akakaa chini, machozi yalikuwa yakimtoka, hakuamini kama kukutana kwake na Onesmo kungekuwa kama vile, alitarajia furaha lakini furaha yote akaiona ikitoweka. Onesmo alikuwa ameuumia moyo wake kupita kiasi.
“Usilie Maria. Itakubidi ukubaliane na ukweli” Onesmo alimwambia Maria maneno ambayo yalimuumiza zaidi.
“kweli gani Onesmo? Ukweli huu wa kunisaliti? Ukweli wa kukataa kuishi nami ili tumlee mtoto wetu? Ukweli gani nikubaliane nao Onesmo?” Maria aliuuliza huku akiendelea kulia kwa chngu.
Onesmo akaonekana kushtuka, maneno ambayo aliyaongea Maria katika kipindi hicho yalionekana kumshtua kupita kawaida. Neno mtoto ndio ambalo lilionekana kumshtua zaidi. Akamuinua juu Maria, akaanza kumwangalia usoni.
“mesemaje? Mtoto? Mtoto gani?” Onesmo aliuliza huku akionekana dhahiri kushtuka.
“Mtoto wetu Onesmo. Nilikimbia kijijini baada ya kugundulika kuwa nina ujauzito wako Onesmo. Nimejifunga salama. Nimemacha kijijini Onesmo” Maria alimwambia Onesmo.
Onesmo akaonekana kuishiwa nguvu, akamwachia Maria, akapiga hatua kurudi nyuma. Maneno yale yalionekana kumshtua. Mbele yake tayari aliona giza, hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya. Hakuelewa kama harusi ile ingekuwepo au la. Maria alioekana kanza kuvuruga kila kitu.
“Maria. Kwa nini haukuniambia?”
“Ningekwambia vipi? Ulipoondoka kijijini ulirudi tena? Ulitegemea ningekwambia vipi?” Maria aliuliza.
Onesmo akakosa jibu la kumwambia Maria, alibaki kimya hku akiona mwili wake ukifa ganzi. Hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati huo. Kichwani alijihisi kuchanganyikiwa zaidi.
Huku akiwa katka lindi la mawazo, simu yake ikaanza kuita. Akaitoa kutoka mfukoni na kuangalia kioo cha simu. Jina ‘Wifey’ ndio ambalo lilikuwa likionekana. Kabla hajaipokea, akayapeleka macho yake usoni mwa Maria.
“Inabidi tutafute muda wa kuongelea suala hili Maria” Onesmo alimwambia Maria.
“Sitaki Onesmo. Acha tu nimtunze mtoto wangu mwenyewe, sitaki ushiiki kwa chochote kile. Kama unataka kuoa, wewe endelea tu, niache na maisha yangu” Maria alimwambia Onesmo huku akiendelea kulia.
Maria hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, akapiga hatua kuelekea barabarani. Mwendo wake ulikuwa wa taratibu, uso wake alikuwa ameuelekezea chini. Hakuamini kama Onesmo yule aliyekuja kijijini na kufanya nae mapenzi ndiye yule ambaye alikuwa ameamua kumfanyia mambo kama yale.
Moyo wake ulijawa na maumivu makali. Kitu zaidi ya msumari wa moto alikihisi kikiwa kimeuchoma moyo wake. Maria aliendelea kulia kama mtoto, akafika mpaka kituoni, akaingia ndani ya daladala na kuchagua kiti kimoja cha peke yake na kutulia.
“Sitaki kumuona tena. Ameuumiza moyo wangu...” Maria alijisemea.
****
Jina Maria ndio ambalo liliendelea kuwepo moyoni mwa Onesmo, kila siku alikuwa akimuwaza Maria ambaye kwa mara ya mwisho alikutana nae kanisani. Alijitahidi kumtafuta lakini jitihada zake zote ziligonga mwamba, hakuweza kumuona.
Alijua fika Maria alikuwa ameumia kutokana na kile ambacho alikuwa amemfanyia, lakini kwa wakati hu Onesmo hakutaa kuangalia nyuma kwani vitu vyote vilivyotokea aliamini kuwa ni historia.
Baada ya wiki moja, Onesmo akafunga harusi kanisani na msichana Jesca, harusi haikuwa na kipingamizi chochote kile japokuwa mara kwa mara Onesmo alionekana kuwa na hofu kuwa Maria angeweza kuwa kipingamizi kwake.
Maisha ya ndoa pamoja na Jesca yaliendelea kama kawaida. Onesmo hakutaka kuficha kitu chochote kile, alimueleza mkew, Jesca kila kitu kilichotokea katika maisha yake ya nyuma. Hakumficha kuhusu mtoto ambaye alizaa pamoja na Maria, kila kitu alikiweka wazi.
Miezi sita baadae Onesmo akaamua kusafiri na mkewe, Jesca kuelekea Matombo kwani aliamini kuwa mtoto wake angekuwepo huko.
“Nimekuja kwa ajili ya kitu kimoja tu mzee wangu” Onesmo alimwambia mzee Bwaro ambaye alikaa akimsikiliza.
“Kitu gani tena kijana wangu? Unahitaj mizigo mingine?” Mzee Bwaro alimuuliza.
“Hapana mzee wangu, nimemfuata mtoto wangu” Onesmo alimwambia mzee Bwaro ambaye alionekana kushtuka.
“Mtoto wako? Mtoto yupi?”
“Niliyezaa pamoja na Maria” Onesmo alimwambia.
Mzee Bwaro akabaki kimya, mkewe, Bi Sara akainamisha kichwa chini na machozi kuanza kutiririka mashavuni mwake. Onesmo hakuelewa kitu chochote kile, alibaki akiwaangalia kwa zamu.
“Kumbe wew ndiye uliyesababisha haya yote? Kufuta ndoto za binti yangu?” Mzee Bwaro aliuliza huku akionekana kukasirika.
“Huo ndo ukweli. Nilifanya vile pasipo kufahamu kuwa nilichokuwa nakifanya kilikuwa ni upumbafu. Katika hili ninahitaji msamaha wenu. Najua Maria hataki kuniona tena, lakini naamini mtoto wangu atakuwa na hamu kubwa ya kuniona mimi” Onesmo Alisema.
Bi Sara akashindwa kuvumilia kubaki mahali pale, akainuka na kuanza kuelekea chumbani huku machozi yakiendelea kumtoka.
“Umemtonesha kidonda chake?” Mzee Bwaro alimwambia Onesmo.
“Nani?”
“Mke wangu”
“Kivipi?”
“Kwa kumtajia jina la Maria”
“Kivipi?”
“Maria alifariki. Alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alietwa kijijini hapa na mwanamke mmoja ambaye alikuwa pamoja na mtoto wake. Tulimzika katka makaburi ya hapo nyuma” Mzee Bwaro alimwambia Onesmo.
“Unasemaje mzee! Maria alifariki?” Onesmo aliuliza huku akionekana kutokuamini.
“Huo ndio ukweli”
Mzee Bwao akasimama na kuanza kuelekea nje mpaka katika chumba cha nyumba nyingine. Onesmo alibaki akiwa ameinamisha kichwa, hakuamini kama maneno yale yalikuwa na ukweli wowote ule. Moyo wake bado ulikuwa ukimpenda Maria japouwa alikuwa na mke kwa wakati huo.
Mzee Bwaro wala hakuchukua muda mrefu, akarudi mahali pale huku akiwa na mtoto wa kiume. Onesmo akaanza kumwangalia mtoto yule, kwa mbali alifanana nae japokuwa baadhi ya vtu alifanana na Maria.
Onesmo akamchukua mtoto yule na kumpakata. Kila alipokuwa akimwangali, picha ya Maria ilikuwa ikimjia kicwani. Onesmo aliumia kuliko kawaida lakini wakati mwingine alifarijika mara baada ya kumkuta mtoto wake akiwa mzima wa afya.
“Huyu atakuwa ukumbusho wangu kwa Maria” Onesmo alijisemea moyoni huku akimwangalia mtoto wake.
Hawakukaa sana mkoani Morogoro, siku iliyofuata, Onesmo na mkewe, Jesca wakaanza safari kurudi Dar es Salaam. Njia nzima Onesmo alikuwa na majonzi lakini kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake, wakati mwingine alijisikia kufarijika.
“Kila kitu kilichotokea katika maisha yangu ya nyuma kitabaki na kuwa historia. Historia ambao kamwe haitoweza kujirudia” Onesmo alimwambia mkewe na kumkumbatia.
****
Mara baada ya kuondoka kanisani, Maria hakutaka kumuona tena Onesmo. Moyo wake tayari ulikuwa umejeruhiwa, maumivu makali yalikuwa yameupata moyo wake. Akaanza maisha mapa huku akijitahidi kumsahau Onesmo.
Miezi ilikatika zaidi na zaidi mpaka pale ambapo hali yake ilipoanza kuwa mbaya. Akaanza kutapika ovyo, mwili wake ukaanza kupata vipele vya ajabu huku afya ikianza kudhoofika. Maria akabadilika kabisa, alikonda kupita kiasi.
Baada ya miezi kadhaa, Bi Lilian akaamua kumpeleka Morogoro katika kijiji cha Semakwede kumtafuta Bi Semeni ambaye ndiye Maria aliyajitambulisha kuwa ni mama yake. Kutokana na umarufu mkubwa aliokuwa nao Bi Semeni, wala Bi Lilian hkaupata tabu, akafika nyumbani hapo huku akiwa na Maria aliyekuwa hoi.
Bi Lilian alijitambulisha. Kila mwanakijiji aliyemuona Maria alibaki akihuzunika, hali yake iliwatisha kupita kiasi.
“Kuna vijana nao wana ugonjwa kama huu. Mungu wangu! Ugonjwa huu utamaliza kijiji hiki” Bi Semeni alisema huku akimwangalia Maria.
Wala hazikupta dakika nyingi, kijana mmoja akaingia mahali hapo. Akamfuata Maria pale alipokuwa amelazwa na kumwangalia kwa makini. Machozi yakaanza ktiririka mashavuni mwa kijana yule ambaye nae hali yake ilikuwa kama ya Maria.
“Nisamehe Maia” Kijana yule alimwambia Maria.
“Mtula. Kuna nini tena?” Bi Semeni aliuliza huku watu wakiwa wameanza kuingia ndani ya nyumba ile kumwangalia Maria.
“Mimi ndiye chanzo, na mimi ndiye ambaye nilimwambukiza Maria ugonjwa huu” Mtula alimwambia na watu wote waliokuwa mahali pale kushtuka.
“Nilitoka na ugonjwa huu Dar es Salaam. Nilipojijua nimeathirika, nikaamua kurudi kijijini. Sikutaka kufanya mapenzi na msichana yeyote kwa kuogopa kuua kiumbe kisichokuwa na hatia” Mtula alieleza hali iliyowafanya watu wote ndani ya ile nyumba kunyamaza.
“Kuna siku vijana wa hapa kijijini walitaka kumbaka Maria, sikutaka kitu kile kitokee na ndio maana nilijitahidi kuingana nao. Kwa kuwa walikuwa wengi, nikashindwa, ikanibidi nikubaliane nao” Mtula aliwaambia.
“Ingawa nilijua kuwa ningemsababishia matatizo Maria lakini pia nilitaka kuwaua vijana wale kwa kutaka kufanya kitendo cha kinyama kama kile. Nikaanza kumbaka Maria, nikamwachia ugonjwa huu na wote waliofuatia baada yangu, nao wakaambukizwa ugonjwa huu” Mtula alielezea huku machozi yakiendelea kumtoka.
“Nisamehe Maria. Sikufanya hivi kukuangamiza wewe. Nilifanya hivi kwa nia ya kuwaangamiza vijana wale waliokuwa na nia mbaya” Mtula alimwambia Maria.
“Nim..ek.usam..eh..e...” Maria aliongea kwa sauti ya chini huku akimwangalia Mtula.
Mtula hakutaka kubaki mahali hapo kwani machozi yaliongezeka zaidi na kilio cha kwikwi kuanza kusikika. Watu wote waliokuwa mahali pale wakaanza kulia, kila mmoja alionekana kuumia.
“Nitampeleka nyumbani kwao” Bi Semeni alimwambia Bi Lilian.
“Kwani hapa sio nyumbani kwao?” Bi Lilian aliuliza.
“Hapana. Kwao Matombo”
“Lakini aliniambia kuwa hapa ni kwao, na wewe ni mama yake”
“Huwa amezoea kuniita hivyo. Ila bado namchukulia kama mwanangu” Bi Semeni alisema.
****
Siku iliyofuata Bi Semeni akakodisha baiskeli tatu kwa ajili ya kuelekea katika kijiji cha Matombo ambacho wala hakikuwa mbali sana kutoka katika kijiji cha Semakwede. Baiskeli moja ilimbeba Maria, ya pili ilimbeba Bi Lilin na ya tatu ilimbeba yeye mwenyewe huku akiwa amembeba mtoto wa Maria.
Safari iliwachukua zaidi ya dakika arobaini njiani na ndipo wakaanza kuingia katika eneo la kijiji kile. Mara baiskeli ziliposimamishwa, Bi Semeni na Bi Lilian wakaanza kuelekea katika baiskeli ambayo ilimbeba Maria na kumteremsha.
Kutokana na kanga ambazo alikuwa amevalishwa mwili mzima hakukuwa na mwanakijiji yeyote ambaye alifahamu kama mtu yule alikuwa Maria. Wote wakamshika Maria katika upande wa kushoto na kulia na kisha kuanza kuelekea katika nyumba ambayo walikuwa wameelekezwa.
Bi Sara alikuwa nje akiendelea na shughuli zake kama kawaida, ghafla akashtukia ugeni wa watu watatu wakianza kuingia ndani ya eneo la nyumba ile. Bi Sara akaacha kazi ambayo alikuwa akiendelea nayo, moja kwa moja akaanza kupiga hatua kuufuata ugeni ule.
“Kuna nini jamani? Huyu ni nani? Bi Sara aliuliza maswali mawili mfululizo huku akionekana kuanza kuchanganyikiwa kwa hofu.
“Maria. Huyu ni Maria” Bi Semeni alijibu.
“Huyu ni Maria? Maria binti yangu! Mungu wangu! Kuna nini tena? Mbona yuko hivi?” Bi Sara aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alijibu swali lolote alilouliza Bi Sara, wote walibaki kimya. Wakaendelea kupiga hatua mpaka wakaingia katika sebule ya nyumba ile. Tayari wanakijiji walikwishaanza kujaa nje ya nyumba hiyo, kila mmoja alitamani kumfahamu mtu yule ambaye alikuwa ameshikwa pande zote mbili.
“Mbona binti yangu yuk hivi?” Bi Sara aliuliza swali jingine lakini nalo halikujibiwa.
Mzee Bwaro akaitwa mahali hapo na ndipo Bi Semeni akaanza kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha ya Maria tangu kipindi ambacho aliingia ndani ya kijiji cha Semakwede. Bi Semeni alichukua dakika tano, zamu ya Bi Lilian ikafika ambaye nae akaelezea kila kitu kuhusu Maria tangu kipindi ambacho aliingia ndani ya jiji la Dar es Salaam.
“Mmesema kuwa alijifungua salama?” Mzee Bwaro aliuliza.
“Ndio”
“Mjukuu wangu yuko wapi sasa?”
Swali lile likamfanya Bi Semeni kusimama na kutoka nje ambako moja kwa moja akaanza kupiga hatua kumfuata mwendesha baiskeli mmoja na kumchukua mtoto yule na kuanza kuelekea nae ndani. Bi Sara akainuka na kisha kumchukua mtoto yule.
“Mungu wangu! Mjukuu wangu!” Bi Maria alisema huku akimwangalia mtoto yule.
Bi Semeni na Bilian hawakutaka kukaa sana, wakamuacha Maria nyumbani hapo na wao kurudi katika kijiji cha Semakwede.
Hali ya Maria ilizidi kuwa mbaya kadri siku zilivyozidi kwenda mbele, kila siku alikuwa mtu wa kujikuna tu huku mdogo wake, Agness akimsaidia kumlisha chakula na kumvalisha nguo. Kila mwanakijiji aliyetamani kumuona Maria, hakudiriki kutaka kumuona tena, Maria alionekana kutisha.
“Huu ugonjwa mbaya sana. Nasikia aliupata hapo Semakwede baada ya kubakwa” Kijana mmoja aliwaamba wenzake.
“Kumbe aliupatia hapo jirani! Unasema kweli au unatania?”
“Huo ndio ukweli. Ugonjwa huu kwa sasa haupo Dar es Salaam tu, umeingia mpaka vijijini, tuweni macho jamani” Kijana yule aliwaambia wenzake.
Baada ya wiki moja Maria hakufumbua macho yake. Kama ambavyo alivyolala usiku na ndivyo ambavyo alitarajiwa kulala milele. Huo ndio uawa mwisho wa Maria, historia ya maisha yake ikaishia katika hali ambayo hakukuwa na mtu aliyeamini ingeishia namna hiyo.
Maria akazikwa katika eneo la makaburi kijijini hapo. Kila mtu ambaye alikuwa akiliangalia kaburi, taswira ya picha ya Maria ilikuwa ikimjia kichwani mwake. Urembo na mvuto wake viliwafanya watu kutokumsahau katika maisha yao.
“Pumzika kwa amani dada. Wewe umetutangulia, amini kuwa nasi tuko nyuma yako kukufuata” Hayo yalikuwa maneno yaliyosikika kutoka kwa Agnes kila alipokuwa akiliangalia kaburi la dada yake, Maria.
MWISHO

Post a Comment