MARIA - 05
Maria akainuka na kukaa kitako kitandani. Sauti za ndege zaikaanza kusikika huku mwanga ukianza kuonekana nje hali ambayo ilimuonyeshea kuwa asubuhi ilikuwa imeingia. Maria akakaa kitako, akaanza kulia tena.
Tukio ambalo lilitokea katika usiku uliopita lilionekana kumuumiza kupita kiasi. Machozi yake yakaanza kulanisha kanga ambayo alikuwa ameivaa. Akaupeleka mkono wake katika sehemu zake za siri, akajiona akwa ameumia kupita kawaida.
Akaanza kuyapeleka macho yake katika sehemu zake za siri, michirizi ya damu zilizoganda ilikuwa ikionekana katika mapaja yake. Maria akazidi kulia zaidi na zaidi, uwepo wake ndani ya kijiji hicho ulionekana kuwa mbaya katika maisha yake.
Huku akiendelea kulia, ghafla mlango ukafunguliwa na Bi Semeni kuingia. Bi Semeni akaanza kupiga hatua kumfuata Maria kitandani pale, alipomfikia, akamkumbatia.
“Pole sana binti yangu” Bi Semeni alimwambia Maria ambaye abado alikuwa akilia.
Maria hakuongea kitu chochote kile, kila alipojaribu kuongea, alijikua akilia zaidi na zaidi. Tukio lile lilimuumiza kupita kawaida. Hakutarajiwa kubakwa katika maisha yake, tena kubakwa na wavulana wengi kwa zamu.
“Nyamaza binti yangu” Bi Semeni aliendelea kumbembeleza Maria.
Maisha ya Maria yakaonekana kubadilika mpaka katika kipindi ambacho alikuja kujifungua baada ya miezi tisa kupita. Mtoto wake wa kiume alikuwa na afya nzuri ambayo mtoto alihitaji kuwa nayo. Maria akaanza kuingia katika majukumu ya kuitwa mama, alimpenda mtoto wake kuliko mtu yeyote duniani.
Tukio la kubakwa ambalo lilitokea katika kipindi cha miezi tisa iliypita bado lilikuwa likimhuzunisha, kila siku alionekana mpweke kupita kawaida hasa kila alipokuwa akilikumbuka tukio lile.
Ingawa kichwa chake kilikuwa na mambo mengi lakini hakutaka kumsahau Onesmo. Kila siku Onesmo alikuwa akiendelea kubaki kichwani mwake, alimpenda sana Onesmo na zaidi ya yote alihitaji kuwa nae ili wamtunze mtoto wao katika malezi bora.
Maria aliuona uhitaji mkubwa wa kutaka kuendelea kuishia na Onesmo hali ambayo ilimpelekea kuanza kufikiria kitu kingine akilini mwake, kutoroka kijijii hapo. Sehemu ambayo Maria alikuwa akiiamini kwamba angemuona Onesmo ilikuwa ni ndani ya jiji la Dar es Salaam tu.
Alihitaji kuondoka kijijini hapo na kuelekea ndani ya jiji la Dar es Salaam huku lengo lake hasa likiwa ni kumtafuta Onesmo na kuanza nae maisha upya. Alihitaji kumtafuta Onesmo lakini alihitaji kuwa peke yake, hali iliyomaanisha kwamba ni lazima amuache mtoto wake kijijini hapo kwa Bi Semeni.
Safari yake ilihitajika kufanyika kwa siri, hakukuwa na sababu ya kutaka kuaga kijijini hapo, alihitaji kutoroka na kumuacha mtoto wake kijijini hapo. Aliamini kwamba kama angerudi kwa mara nyingine, basi ingemlazimu kumchukua mtoto wake na kuondoka nae.
Bi Semeni alikuwa akichukua muda mwingi kukaa na mtoto wa Maria ambaye kwake alimchukua kama mjukuu wake. Alimpenda mtoto yule zaidi ya mtu yeyote kijijii pale, kila siku alikuwa akimpakata miguuni mwake huku akichukua muda mwingi kumbembeleza pale alipokuwa akilia.
“Huyu ndiye atakuwa kila kitu kwangu. Yeye ni zaidi ya wajukuu wangu wote” Bi Semeni alimwambia Maria huku akiendelea kumbembeleza mtoto yule.
Kila wakati Maria alikuwa akitabasamu pasipo kuuelezea wazi mpango wake ambao walikuwa ameupanga moyoni mwake. Kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake, alibaki akiumia sana kila alipokuwa akifikiria kwamba alikuwa akimuacha kijijini hapo siku chache zijazo.
“Ni lazima niondoke usiku wa leo” Maria alisema.
Usiku wala hakulala, macho yake yalikuwa macho huku yakiangalia juu. Muda ulizidi kwenda mbele, tayari alikuwa kitandani mwake mara baada ya kumaliza kufanya biashara ya kuuza gongo. Pembeni yake alikuwepo mtoto wake ambaye alikuwa amelala. Maria akaanza kufikiria mambo mengi ambayo yalitokea katika maisha yake ya nyuma, aliyaona maisha yake kujawa na misukosuko kuliko mtu yeyote katika dunia hii.
Maria alibaki katika hali hiyo kwa dakika kadhaa, alipoona muda wa kuondoka kijijini hapo ukiwa umetimia, akasimama na kuufunua mchago wa kitanda chake. Akachukua kitambaa kimoja ambacho alikifungua na kuchukua kiasi chote cha fedha kilichokuwa katika kitambaa hicho na kuzifunga katika kanga yake.
Maria akambeba mtoto wake na kuanza kuelekea katika chumba aichokuwa amelala Bi Semeni. Akaufungua mlango taratibu. Bi Semeni alikuwa katika usingizi mzito, Maria akamchukua mtoto wake na kumuweka pembeni mwa Bi Semeni na kisha kuondoka ndani ya chumba hicho.
“Ninaianza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa lengo moja tu la kumtafuta Onesmo” Maria alijisemea na kuondoka.
Kitendo cha kumuacha mtoto wake kilimuuma sana lakini hakuonekana kujali. Aliamini kuwa ni lazima angemuona kwa mara nyingine mtoto wake huyo, tena akiwa pamoja na Onesmo, baba wa mtoto huyo.
Ingawa katika maisha yake hakuwahi kufika ndani ya jiji la Dar es Salaam lakini Maria alipania hasa kuingia ndani ya jiji hilo. Alijua fika kuwa angeweza kupotea kutokana na ukubwa wa jiji hilo lakini hakuonekana kujali kitu chochote kile, kitu ambacho alikijali kwa wakati huo ni kumtafuta Onesmo na kuanza maisha pamoja nae.
Maria akaingia kichakani na kuanza safari ya kuelekea upande wa mashariki. Safari iliendelea kama kawaida, moyo wake ulikuwa ukimuuma kila alipokuwa akimkumbuka mtoto wake, lakini katika kipindi hicho hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima amuache mtoto wake ili apate nafasi ya kumtafuta Onesmo.
Maria aliendeleana safari yake mpaka pale alipoanza kuingia katika eneo ambalo lilikuwa na nyumba kadhaa zilizokuwa na umeme. Maria akaanza kupiga hatua za haraka haraka mpka katika nyumba moja ambayo ilikuwa na duka lililokuwa wazi.
“Samahani kaka yangu”
“Bia samahani”
“Nahitaji kulala sehemu mpaka asubuhi, sijui kuna nyumba ya wageni hapa karibu?” Maria alimuuliza muuza duka.
Muuza duka akaanza kutoa maelekezo juu ya sehemu ambayo ilikuwa na nyumba ya wageni. Baada ya kuelekezwa vya kutosha, Maria akaanza kupiga hatua huku akifuatilia maelekezo ambayo alipewa, wala hakuchukua muda, akawa amekwishafika katika nyumba hiyo ya wageni na kuchukua chumba kimoja.
****
Mara baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani, maisha ya Onesmo yakabadilika. Kila siku hakuwa akiamini kama Mungu alikuwa amemuokoa katika ajali ile ambayo ilionekana kuwa mbaya kwake. Kila wakati alikuwa akimuombea Issa ambaye alifariki siku chache baada ya kulazwa hospitalini.
Onesmo akaanza kwenda kanisani, moyo wake uliogopa kuishi nje ya wokovu, kanisa ndilo likawa jengo ambalo alikuwa akilipenda, huku Jumapili ikiwa ndio siku ambayo ilikuwa ikimfanya kuwa na furaha katika maisha yake yote.
Kila siku Onesmo alikuwa mtu wa kusali, hakutaka kufanya dhambi zozote ambazo hazikuwa n msingi kufanyika, alidhamiria kuyabadilisha maisha yake, hakutaa kuishi nje ya wokovu kwani aliamini muda wowote ule binadamu anaweza kupoteza maisha.
Maisha baada ya kifo ndio ambayo yalikuwa yakimhanganya kila siku. Hakutaka kuishi maisha ya tabu na mateso, alitamani kuishi maisha mazuri na ya milele.
Washirika wote wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Magomeni wakamzoea Onesmo ambaye baada miezi minne akapewa jukumu la kuhubiri katika ibada za vijana ambazo zilikuwa ziifanyika siku ya Jumapili jioni.
Onesmo akawa mtu mwema, mambo mengi ambayo yalikuwa yamepita katika maisha yake ya nyuma yalibaki na kuwa kama historia, hakutaka kuyakumbuka kabisa. Kila siku hakuwa mtu wa kuangalia alipotoka, alikuwa akiangalia mbele tu.
Biblia ndicho kikawa kitabu ambacho alikuwa akikipenda kukisoma katika maisha yake. Akayaona mabadiliko makubwa moyoni mwake. Akajiona kuishi maisha ya thamani na raha tofauti na kipindi kilichopita.
“Nitamtumikia Mungu hadi pumzi yangu ya mwisho” Onesmo aliwaambia baadhi ya vijana.
“Hayo ndio maisha yanayotakiwa mtumishi’
“Najua Mungu aliponitoa, kama sitomtumikia, basi yatakuwa makosa makubwa sana katika maisha yangu” Onesmo aliwaambia vijana ambao walikuwa wamekusanyika kanisani.
Miezi iliendelea kukatika, Onesmo akajiweka imara katika kumtumikia Mungu, hakutaka ujinga wowote katika maisha yake. Moyoni alijiona kuwa na jukumu kubwa la kumtumikia Mungu.
Wakinamama na viongozi kanisani wakaanza kuongea mambo mengi kuhusiana na maisha ya Onesmo. Kila mtu aliiambua kazi kubwa ya Onesmo kanisani hapo. Walifahamu fika kuwa majaribu yalikuwa mengi katika maisha ya vijana.
Kila mmoja akataka Onesmo afanye uamuzi mwingine wa kuoa. Onesmo alipopewa taarifa juu ya kile ambacho viongozi walikuwa wamejaribu kumshauri, akaanza kujifikiria kwa muda. Moyoni mwake likaja jina moja tu, Maria.
Alimkumbuka vilivyo moyoni mwake, alijua ni kitu gani ambacho mara kwa mara alikuwa akimuahidi. Alihitaji mke katika kipindi hicho lakini hakufahamu ni msichana yupi ambaye alikuwa anastahili kuwa katika maisha yake.
“Naombeni Muda. Mnajua mambo haya hatukurupuki hata kidogo, itanibidi nikae chini na kumuomba Mungu ili anipe mke mzuri na mwema” Onesmo aliwaambia.
Mambo mengi yalikuwa yakimiminika kichwani mwa Onesmo, hakujua afanye nini kwa wakati huo. Bado alitamani kumuona tena Maria lakini kwa upande wake mwingine hakukuwa na uhakika kama Maria alikuwa mke sahihi.
“Miezi mitatu imepita Onesmo. Mungu amekuonyesha chochote juu ya msichana wa kumuoa?” Mchungaji wa kanisa hilo, Samuel Mwashambwa alimuuliza Onesmo.
Onesmo hakujibu kitu chochote kwa haraka, akabaki kimya kwa muda huku akifikiria kitu. Akayapeleka macho yake chini kama kumdhihirishia mchungaji kwamba alikuwa akijifikiria kitu, baada ya sekunde kadhaa, akayainua na kumwangalia mchungaji.
“Mungu amenionyesha” Onesmo alimwambia mchungaji.
“Safi sana. Ni nani?”
“Jesca. Jesca Martin”
“Yule binti wa shemasi?”
“Ndio” Onesmo akajibu.
Akilini mwake hakuwa na mawazo na Maria tena, aliamua kuyabadilisha maisha yake kabisa, alijiona angeingia katika matatizo kama tu angediriki kurudi kijijini na kumuoa Maria. Kwanza bado alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu, suala la kuolewa lilikuwa jambo gumu kwake, hata baba yake, mzee Bwaro hasingekubali.
“Nitamuoa tu Jesca” Onesmo alijisemea huku akisimama na kuondoka.
****
Usiku Maria hakulala, kichwa chake kilikuwa kinawafikiria watu wawili katika maisha yake, wa kwanza alikuwa mtoto wake aliyemuacha kwa Bi Semeni na mtu mwingine alikuwa Onesmo. Kila alipokuwa akibimbilika katika kila upande, sura za watu hao zilikuwa zikimjia kichwani mwake.
Maria akakosa amani, alijiona kuwa miongoni mwa watu ambao hawakuwa na fraha maishani mwao. Mpaka inaingia saa kumi na moja, bado Maria alikuwa macho kana kwamba alikuwa katika kazi ya ulinzi katika benki fulani au nyumba ya bosi mmoja wa kampuni kubwa Tanzania.
Maria akainuka kutoka kitandani na kisha kuanza kupiga hatua kuufuata mfuko ambao ulikuwa na nguo kadhaa ndani yake. Tayari mwanga uikuwa umeanza kutokea, sauti za ndege mbalimbali zilikuwa zikisikika katika kila kona.
Maria hakutaka kupoteza muda wake kubaki ndani ya chumba kile, moja kwa moja akatoka na kuanza kuelekea nje. Alipoaga, safari ya kuelekea katika barabara ya lami ikaanza. Watu wanne tu waliokuwa na mizigo ndio ambao walikuwa katika kituo kidogo ambacho kilikuwa mahali hapo.
Wala haukpita muda mrefu, basi la abiria likafika mahali hapo na watu wote waliokuwa mahali hapo kupanda. Maria akaa katika kiti cha nyuma ambacho hakikuwa na watu wengi. Maria hakuufungua mdomo wake kuongea na mtu yeyote, akili yake bado ilikuwa ikimuwaza mtoto wake na Onesmo tu.
Safari ilichukua dakika sabini, basi likaanza kuingia katika kituo cha mabasi cha Ubungo. Maria alibaki akiangalia nje, idadi kubwa ya watu ambao walikuwa wakiendelea na kazi zao ilikuwa ikimshangaza.
Mara baada ya basi kusimama, moja kwa moja Maria akateremka na kuanza kuteremka. Macho yake hayakutulia sehemu moja, mara kwa mara alikuwa akiangalia katika kila upande kituoni hapo. Akaanza kupiga hatua kuelekea katika kibanda kimoja ambacho kilikuwa kikiuza vinywaji mbalimbali na kutulia.
Hakujua aanzie wapi, kila kitu ambacho kilikuwa kinaonekana mbele yake kilikuwa kigeni. Hakujua ni mahali gani ambako alitakiwa kwenda, mbele yake alijiona kuwa na safari kubwa ingawa tayari alikwishafika ndani ya jiji ambalo alikuwa akitamani kufika.
“Onesmo....” Maria alijikuta akilitaja jina hilo.
Akainuka kutoka katika kiti na kumfuata mwanamke mmoja ambaye alisimama pembeni ya kibanda hicho. Akamsalimia na wote kuanza kuangaliana kana kwamba walikuwa wakifahamiana. Maria hakujua aanzie wapi kumuulizia Onesmo.
“Samahani mama” Maria alimwambia mara baada ya kuangalia kwa sekunde kadhaa.
“Bila samahani”
“Namtafuta rafiki yangu”
“Nani?”
“Anaitwa Onesmo. Onesmo Samson” Maria alisema.
“Anakaa wapi?”
“Sijui. Ila ni hapa hapa Dar es Salaam” Maria alimwambia mwanamke yule.
“Una namba yake ya simu”
“Hapana”
“Sasa utampata vipi?” Mwanamke yule aliuliza.
Hilo lilikuwa swali gumu kwa Maria, alibaki kimya huku akiyarudisha macho yake chini, hakujua aanzie wapi kumtafuta Onesmo, tayari akaanza kujiona mjinga kwa kutokuwa na werevu wa kufanya mawasiliano na Onesmo kabla ya kuingia ndani ya jiji la Dar es Salaam.
“Kwani umetoka wapi?” Mwanamke yule aliuliza swali lililomshtua Maria kutoka katika lindi la mawazo.
“Matomboa, Morogoro” Maria alijibu.
“Haina jinsi binti, itakupasa urudi huko huko” Mwanamke yue alimwambia Maria.
“Hapana. Siwezi kurudi kijijini”
“Kwa nini?”
“Maisha ni magumu kijijini. Ni bora nikae hapa hapa mjini nitafute maisha” Maria alimwambia mwanamke yule.
“Utaanzia wapi binti?”
“Sijui nitaanzia wapi, ila acha nijaribu, mbele ya safari nitajua pa kuanzia” Maria alimwambia mwanamke yue.
Akaanza kupiga hatua za taratibu kuelekea kule kulipokuwa na geti la kutokea. Kichwa chake kilikuwa chini, mambo mengi yalikuwa yaejazana akilini mwake kwa wakati huo. Dunia aliiona ikianza kumuelemea, wakati mwingine alijuta sababu iliyomfanya kuondoka kijijini.
“Binti....” Maria alisikia akiitwa. Maria akageuka nyuma na macho yake kutua kwa mwanamke yule.
“Una pa kwenda?”
“Hapana. Nimechanganyikiwa kwa sasa, sijui nitafanya nini na wala sijui nitakwenda wapi” Maria alimwambia mwanamke yule huku machozi yakianza kumlenga.
“Usihofu. Nilikuwa na safari kesho ya kuelekea Mbeya kutafuta mfanyakazi wa ndani. Nafikiri sitokwenda huko kama utakubali twende wote nyumbani” mwanamke yule alimwambia Maria.
Maria hakuonekana kuamini, alkaanza kujiona kuwa na bahati. Akamwangalia mwanamke yule mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini. Akamsogelea mwanamke yue, alitamani kumkumbatia. Machozi ambayo yalikuwa yakimlenga katika kipindi kichache kilichopita yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
“Nashukuru mama. Niko tayari” Maria alimwambia mwanamke yule.
Safari ya kuelekea nyumbani kwa mwanamke yule ikaanza. Muda wote Maria alikuwa akionekana kuwa na furaha isiyo kifani. Kupata nafasi ya kufanya kazi ndani ya jiji la Dar es Salaam kwake ilionekaa kuwa kama bahati kubwa.
Walichukua dakika kumi kutoka kutoka Ubungo mpaka Mwenge ambako wakaingia ndani ya nyumba kubwa na nzuri ambayo ilimvutia Maria kwa kuitazama. Hakuamini kama kungetokea siku yoyote ambayo angeishi ndani ya nyumba kubwa na nzuri kama ile.
“Karibu” Mwanamke yule alimkaribisha.
“Asante” Maria aliitikia huku uso wake ukionyesha kubwa aliyokuwa nayo.
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
ITAENDELEA SIKU YA KESHO

Post a Comment