MARIA - 01
Jina la mzee Michael Bwaro halikuwa geni masikioni mwa wanakijiji waliokuwa wakiishi katika kijiji cha Matombo mkoani Morogoro. Mzee Bwaro alisifika sana kutokana na umiliki wake mkubwa wa mashamba makubwa yaliyokuwa sehemu mbalimbali kijijini hapo.
Kila mtu alikuwa akimheshimu mzee huyu ambaye alijizolea sifa mbalimbali kutokana na ucha Mungu wake. Mzee Bwaro hakuwa mchoyo, kila siku alikuwa akiwasaidia wanakijiji mbalimbali ambao walikuwa katika maisha magumu. Kila alipopata mazao katika kipindi cha mavuno, kiasi fulani alikiuza huku kiasi fulani akiwasaidia watu kadhaa kijijini hapo.
Sifa za mzee Bwaro zilikuwa zikiongezeka kila siku, machoni mwa watu alionekana kuwa mtu mwema kuliko mtu yeyote kijijini pale. Mzee Bwaro hakutaka kujivunia mali alizokuwa nazo, kila siku alikuwa akiwathamini watu wale ambao walikuwa na matatizo katika maisha yao.
Kupitia fedha zake nyingi alizokuwa akizipata, mzee Bwaro akaanzisha miradi mbalimbali na baada ya mwaka mmoja, akaweka mradi wa maji kijijini hapo. Tatizo la maji likaonekana kubaki kama historia katika kijiji cha Matombo.
Nyumba ya mzee Bwaro ndio ikawa nyumba ya kwanza kuwekwa umeme kijijini hapo huku watu wengine nao wakitumia nafasi hiyo kuvuta umeme katika nyumba zao. Mzee Bwaro akaonekana kuwa ndiye kiini cha mabadiliko kijijini hapo.
Mzee Bwaro akatoa wazo la kuanzishwa kwa shule za sekondari na msingi hapo kijijini. Wazo lake hilo likaonekana kuwa zuri, hakukuwa na mtu yeyote ambaye alileta kipingamizi chochote kile. Michango ikaanza huku mzee Bwaro akiwa ndiye kiongozi katika michango hiyo.
Ujenzi wa shule hizo ukaanza mara moja. Ujenzi ulikuwa ukienda kwa kasi kubwa kiasi ambacho ndani ya mwaka mmoja kila kitu kilikuwa tayari. Wanafunzi ambao walikuwa wakisoma katika shule za mbali wakaamishiwa ndani ya shule hizo, walimu wazuri wakaajiriwa katika shule hizo huku mishahara yao ikitolewa na wanakijiji kijijini hapo.
Pamoja na kuwa na utajiri mkubwa na heshima ya hali ya juu lakini mzee huyo hakutaka kabisa mabinti zake wawili, Maria na Agness wachezewe. Kila siku alikuwa akiwawekea ulinzi mkubwa, wao ndio walionekana kuwa furaha yake katika maisha yake.
Aliwalea katika mazingira ya dini, kila siku ambazo walikuwa wakihitajika kanisani, aliwataka kuwa huko. Maria na Agness wakajiunga na kwaya ya kanisa hilo la Praise And Worship lililokuwa kijijini hapo. Kila mvulana aliogopa kuwasogelea mabinti hao, heshima na ukali wa baba yao ulionekana kumuogopesha kila mtu.
Mpaka wanafikia umri wa miaka kumi na nane, Maria na Agness hawakumjua mwanaume yeyote yule, walikuwa bikira. Hawakutaka kufanya mapenzi na mvulana yeyote yule, waliuthamini usichana wao kuliko kitu chochote kile katika maisha yao.
Maria na Agness wakajizolea sifa nyingi kijijini hapo kwa kuwa walikuwa wasichana ambao walitulia katika maisha yao. Hawakutakiwa kupata tabu katika maisha yao na ndio maana walipewa kila kitu maishani mwao, walipatiwa elimu nzuri kutoka katika shule za kijijini hapo.
Kila siku walikuwa wakisoma kwa bidii kwani waliamini kuwa elimu ndio ilikuwa urithi wao mkubwa katika maisha yao. Hawakuzitamani mali za wazazi wao, kila siku walitamani kupata mali zao wenyewe. Hali hiyo ikawafanya kufanya vizuri katika masomo yao, wakaanza kuongoza darasani katika kila somo.
“Hivi ndivyo ninavyotaka” Mzee Bwao aliwaambia alipokuwa akiziangalia ripoti zao.
Ripoti zao zilikuwa zikiridhisha. Walikuwa wamefanya vizuri katika masomo yote kwa Maria kushika nafasi ya kwanza na Agness kushika nafasi ya pili.
Maisha yaliendelea kama kawaida. Kila siku walikuwa wakisomewa risala, walitakiwa kuwa kama walivyokuwa, kila mtu alitamani kutimiza ndoto zake ambazo alikuwa amejiwekea kaika maisha yake. Mama yao, Bi Sara ndie ambaye alikuwa nao karibu zaidi, aliwafundisha kuwa na maadili mema maishani mwao, kumheshimu kila mtu.
Walifundishwa mambo mengi kuhusu mahusiano mpaka njia ambazo wavulana wengi huzitumia katika kufanikisha kile wanachokitaka kutoka kwa wasichana mbalimbali. Maria na Agnes wakaonekana kuwa makini katika kila kitu ambacho walikuwa wakiambiwa, hawakutaka kupotoshwa na mvulana yeyote yule.
“Ningependa kuwa mfanyabiashara” Agness alimwambia mzee Bwaro.
“Na wewe Maria”
“Ningependa kuwa sista” Maria alijibu.
Maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida, kila mmoja alikuwa akisoma huku kichwani akiwa na malengo yake. Agness akaonekana kuvutiwa sana na masomo ya bishara, kila siku alikuwa akishinda na kalkuleta, masomo ya biashara yalionekana kumteka akili.
Maria alionekana kuwa tofauti na Agnes, muda mwingi alikuwa akiutumia kwenda kanisani, kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea kanisani, Maria alihusika vilivyo. Biblia ndicho kilikuwa kitabu alichopenda kukisoma katika maisha yake, ndoto za kutaka kuwa sista zilionekana kuitawala akili yake.
“Nitataka kuwa bikira maisha yote. Sitomruhusu mvulana yeyote autoe usichana wangu” Hayo ndio yalikuwa maneno ambayo alikuwa akiyazungumza Maria kila siku alipokuwa akisoma Biblia Takatifu.
**********
Biashara bado zilikuwa zikiendelea kufanyika. Wafanyabishara mbalimbali waliokuwa wakitoka katika sehemu mbalimbali Tanzania walikuwa wakikusanyika katika kijiji cha Matombo na kuchukua mazao mbalimbali na kuyapeleka miji kwenda kuyauza.
Kati ya wavulana ambao walikuwa wakifanya kazi ya kwenda kuchukua mazao kijijini Matombo mkoani Morogoro alikuwa kijana Onesmo Samson. Kila wiki Onesmo alikuwa akitembelea katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchukua mazao na kuyapeleka katika kampuni ya WALEO CO. LIMITED iliyokuwa jijini Dar es Salaam.
Ingawa kazi ile ilikuwa ikimchosha kupita kawaida lakini hakutaka kuiacha. Kila wiki alikuwa akisafiri kuelekea katika vijiji mbalimbali. Alijitolea kufanya kazi katika maisha yake ili mladi tu, maisha yake yawe kama vile ambavyo aliyataka kuwa.
Mara baada ya kufika katika kijiji cha Matombo, Onesmo akaanza kuelekea katika moja ya shamba la mzee Bwaro kwa ajili ya kuchukua mahindi. Gari lao aina ya Canter lilikuwa likipita katika njia ambayo ilikuwa na mabonde mabonde hali iliyowapelekea kuendesha taratibu.
“Hii kazi ngumu kweli Issa” Onesmo alimwambia rafiki yake aliyekuwa ndani ya gari pamoja nae.
“Unafikiri tukiacha kazi hii tutafanya kazi gani? Au kuza mitumba Tandale” Issa alimwambia Onesmo.
Walichukua dakika kumi kutoka katika barabara ya lami mpaka kufika katika moja ya mashamba ya mzee Bwaro. Wafanyakazi walikuwa wamejaa katika shamba hilo huku wakiendelea na kazi yao ya uvunaji. Onesmo akasimamisha gari na moja kwa moja wote kuteremka.
“Mnataka gunia ngapi kwa leo?” Mfanya kazi mmoja aliwauliza.
“Kama kawaida yetu. Wekeni magunia sitini” Onesmo alimwambia mfanya kazi yule.
Kazi ya kupakia magunia ikaanza mara moja. Kutokana na kuwa na gari moja tu mahali hapo, wafanya kazi wote walikuwa wakipakia magunia hayo huku Onesmo na Issa wakiwa wamekaa pembeni wakiangalia kazi ilivyokuwa ikifanyika.
“Huwa haturuhusiwi kupokea malipo. Malipo hupokea mzee mwenyewe” Kijana mmoja aliwaambia.
“Mzee mwenyewe yuko wapi?”
“Leo hajisikii vizuri”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Twendeni niwapeleke nyumbani kwake” Kijana yule alisema.
Wote wakaingia garini na safari ya kuelekea nyumbani kwa mzee Bwaro kuanza. Barabara haikuwa nzuri, gari bado liliendelea kupita katika mashimo mashimo huku magunia yakiwa yamefungwa vizuri kwa kamba. Walitumia muda wa dakika kumi tu, wakawa wamekwishaingia katika eneo la nyumba ya mzee Bwaro.
“Mzee tumemkuta?” Kijana yule aliuliza.
Mara baada ya kujibiwa kuwa yupo ndani, wote watatu wakaingia na kukaa sebuleni. Alipopewa taarifa kuwa wateja walikuwa wamefika nyumbani kwake kwa ajili kufaya malipo, mzee Bwaro akaoka sebulei pale.
“Magunia sitini” Kijana yule alimwambia mzee Bwaro na kisha Onesmo kutoa kiasi cha fedha na kumlipa mzee Bwaro.
“Ninyi ni wafanyabiashara wangu wazuri na waaminifu sana. Mtakapokuja kwa mara ya pili, nitawaongeza japo gunia moja” Mzee Bwaro aliwaambia.
“Tutashukuru sana mzee. Tunaweza kupata maji?” Onesmo alimwambia mzee Bwaro.
“Kwa nini isiwe soda?” Mzee Bwaro aliuliza.
“Nafikiri haitoweza kukata kiu niliyokuwa nayo” Onesmo alijibu.
Mzee Bwaro akaagiza maji yaletwe mahali pale kutoka kwa binti yeke yeyote. Huku wakiendelea kuongea sebuleni pale kuhusu mambo yao ya kibiashara, mara Maria akatokea mahali hapo huku akiwa ameshika jagi lililokuwa na maji pamoja na bilauri mbili.
Moyo wa Onesmo ukalipuka kwa mshtuko mara baada ya macho yake kutua usoni mwa Maria. Akamwangalia mara mbili mbli huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akikiona kwa wakati huo. Maria akaonekana kumvutia kupita kawaida, akamwangalia vizuri zaidi, uzuri wa Maria ulikuwa ukionekana wazi.
“Karibuni” Maria akawakaribisha huku akitoa tabasamu.
Tabasamu lile ndilo ambalo liliongeza msisismko mwilini mwa Onesmo, akaonekana kuchanganyikiwa, mvuto wa Maria ukaonekana kumteka kupita kiasi. Vishimo vilikuwa vikionekana mashavuni mwake hali ambayo ilizidi kumchanganya Onesmo.
Mpaka wanaondoka mahali hapo, Onesmo alikuwa amechanganyikiwa kupita kiasi. Maria akaonekana kumteka kuliko msichana yeyote. Alijua kwamba aliwaona wasichana wengi jijini Dar es Salaam, wasichana wazuri na wanaovutia, ila kwa Maria ilionekana kuwa tofauti, alionekana kuvutia zaidi kuliko wasichana wale aliowaona Dar es Salaam.
“Umemwona mtoto yule?” Onesmo alimuuliza Issa huku wakiwa wameanza safari ya kurudi Dar es Salaam.
“Yupi?”
“Aliyetuletea maji”
“Yule binti wa mzee Bwaro?”
“Huyo huyo. Umemuonaje?”
“Mzuri sana. Ila sikutaka kumwangalia sana, si unajua wazee wengine nuksi” Issa alimwambia.
“Nimevutiwa sana na mtoto yule. Ni lazima nirudi tena?” Onesmo alimwambia Issa.
“Sawa. Ila kuwa makini, nasikia mzee nuksi kweli kwa mabinti zake. Anaweza hata akakuua japokuwa ni mlokole kupita kiasi” Issa alimwambia Onesmo.
Onesmo akajikuta akiingia katika ulimwengu mwingine, ulimwengu wa mapenzi. Mapenzi yakaonekana kumteka, kila wakati akili yake ilikuwa ikimfikiria Maria tu. Uzuri wa Maria ulikuwa umemchanganya kupita kiasi, kila siku maisha aliyaona yakienda taratibu sana, alitamani mizigo wa mahindi ambayo walikuwa wameileta Dar es Salaam iishe na kwenda kuchukua mizigo mingine.
Siku ziliendelea kukatika, masaa yaliendelea kusonga mbele kama kawaida mpaka kufika kipindi ambacho mzigo ambao walikuwa wameuleta kuisha. Walitakiwa kurudi mkoani Morogoro kwa ajili ya kuchukua mzigo mwingine haraka iwezekanavyo kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu amao walikuwa wakiyahitaji mahindi.
Kwa Onesmo kila kitu kilionekana kuwa shwari, kurudi tena Morogoro kwake ilionekana kuwa kama nafasi ambayo alikuwa akiisubiria kwa hamu kubwa. Usingizi haukupatikana kirahisi kama siku nyingine, kila wakati mawazo yake yalikuwa yakimikiria Maria. Alipanga mbinu nyingi za kuhakikisha Maria anakuwa wake katika kipindi hicho.
Siku iliyofuata, safari ya kuelekea Morogoro ikaanza. Onesmo bado alikuwa akijifikiria ni kwa jinsi gani alitakiwa kufanya ili kumuingiza binti huyo katika mikono yake. Akilini zilikuja mbinu nyingi ambazo alikuwa na uhakika ni lazima Maria angeingia katika mikono yake.
Kwa mwendo ambao walikuwa wakiutumia, walitumia masaa matatu mpaka kufika morogoro ambako safari nyingine ya kuelekea Matombo kuanza. Shauku kubwa ya kumuona Maria ikazidi kuongezeka moyoni mwa Onesmo kadri gari lilivyozidi kusonga mbele.
Kutokana na mvua ambazo zilikuwa zikiendelea kunyesha, walitumia dakika ishirini mpaka kufika katika kijiji cha Matombo. Moja kwa moja wakateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika nyumba ya mzee Bwaro. Hawakutaka kuelekea moja kwa moja mashambani kutokana na Onesmo kushinikiza kwenda nyumbani kwa mzee huyo kwa ajili ya kumuona Maria tu.
“Tutahitaji gunia mia moja” Onesmo alimwambia mzee Bwaro.
“Hizo nyingi sana. Hatuwezi kuvuna kwa siku moja tena kwa shamba moja. Kitu nitakachokifanya ni kwenda katika mashamba yangu yote kwa ajili ya kutafuta mahindi yatakayotosha kwa gunia zote hizo” Bwana Bwaro aliwaaambia.
“Kwa hiyo itawezekana kufanyika kwa siku moja mzee wangu?” Onesmo aliuliza.
“Haiwezekani. Mtatakiwa mkae hapa Morogoro hata kwa siku mbili” Mzee Bwaro aliwaambia.
“Sijui kama itawezekana mzee. Hatukutarajia kulala huku Morogoro, kwa hiyo hatuna hata fedha za kulala gesti” Onesmo alimwambia mzee Bwaro huku Issa akiwa kimya akiwasikiliza.
“Msihofu, nitawaandalia chumba hapa nyumbani kwangu kwa kipindi mtakachotumia kusubiri mizigo yenu” Mzee Bwaro aliwaambia.
Onesmo akaonekana kushtuka, hakuonekana kukiamini kile ambacho alikisikia kutoka kwa mzee Bwaro. Akamwangalia mara mbili mbili, kulala kijijini hapo ilionekana kuwa nafasi kubwa kwake kumpata Maria. Jakukuwa na mtu aliyekataa, wote wakakubali kulala kijijini hapo.
Moja kwa moja wakapelekwa chumba ambacho walitakiwa kukitumia katika kipindi ambacho mizigo ya mahindi ilipokuwa ikipakiwa garini mwao. Bado Onesmo alijifikiria mambo mengi kuhusu Maria, hakutaka kuipoteza nafasi hiyo aliyopewa ambayo kwake aliiona kuwa kama nafasi ya bahati.
Kila alipokuwa akitoka nje, hakuwa akimuona Maria. Alijitahidi kumtafuta zaidi na zaidi lakini Maria alionekana kuwa adimu kuonekana katika macho yake. Onesmo hakutaka kukata tamaa, kila wakati alizidi kumtafuta Maria kimya kimya pasipo kushtukiwa na mtu yeyote yule, Maria bado hakuonekana kwake.
Ilipofika saa kumi alasiri, Onesmo akaonekana kushtuka mara baada ya macho yake kumuona mtu ambaye alikuwa aihitaji kumuona kwa kipindi kirefu, Maria. Onesmo akamwangalia Maria mara mbili mbili huku akiwa haamini kama amefanikiwa kumuona msichana huyo.
Alivalia sketi yake ya shule iliyokuwa na rangi ya kijivu pamoja na shati jeupe. Machoni mwa Onesmo, Maria alionekana kupendeza kupita kawaida, uzuri ambao alikuwa nao katika kipindi kile alipomuona kwa mara ya kwanza ukaonekana kuzidi zaidi na zaidi.
Mara kwa mara Onesmo alikuwa akijionyesha kwa Maria kitu ambacho alihitaji kuzoeeka machoni mwa msichana huyo. Kila wakati Onesmo alikuwa akimkonyeza Maria ambaye hakuonekana kujali kitu chochote kile zaidi ya kuachia tabasamu pana lililomchanganya Onesmo.
Onesmo hakutaka kuonekana kushindwa, nje ndio yalikuwa makazi yake kwa siku hiyo. Ingawa kulikuwa na wanakijiji wengi lakini hakukuwa na mwanakijiji yeyote ambaye aliona jinsi Onesmo alivyokuwa akitumia muda wake kumkonyeza Maria.
“Samahani dada” Onesmo alimwambia Maria katika kipindi ambacho jua lilianza kuzama.
“Bila samahani”
“Ningependa kuongea nawe mara moja” Onesmo alimwambia Maria ambaye alichukulia kila kitu kawaida.
“Sasa hivi? Kuhusu nini?” Maswali mawili mfululizo yalimtoka Maria.
“Baadae kidogo. Nafikiri saa moja hivi”
“Maongezi kuhusu nini?”
“Utayajua tu kama utanipa nafasi ya kuongea nawe” Onesmo alijibu.
“Sawa. Labda kule karibu na uwanja muda huo” Maria alimwambia Onesmo na kondoka.
Onesmo alijiona kupata ushindi wa mapema zaidi, kitendo cha Maria kumuahidi kuonana nae, tena katika sehemu ambayo ilikuwa na kificho ilionekana kumfurahisha zaidi. Akajiona kuwa mwanaume aliyekuwa na bahati maishani.
Muda ulizidi kusonga mbele lakini kwa Onesmo dakika zilionekana kwenda taratibu zaidi ya ambavyo alikuwa akiona kabla. Kila wakati macho yake yalikuwa katika saa yake, mshale wa dakika ulionekana kwenda taratibu sana.
“Ngoja nianze kwenda” Onesmo alijisemea mara baada ya saa moja kutimia
INAENDELEA HAPA HAPA

Post a Comment