A JOURNALIST IS BACK (MWANDISHI AMERUDI) - 05
“Yaani bado walikuwa na kisasi na maisha yangu mpaka wakaiangamiza familia yangu?” Dominick aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Edmund...Edmund...yaani watu hawa ndio waliiangaliza familia yangu? Ni lazima niwaue, ni lazima niangamize familia zao pia kama walivyoiangamiza yangu. Tena nitaziangamiza kwa kuzichoma moto na kisha kuwaua wao wenyewe. Ni lazima Edmund. NI LAZIMA……!!!” Dominick alimwambia Edmind huku akilia kama mtoto. Mwili wake ukabaki ukitetemeka kwa hasira, kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kutetemeka kwa hasira.
“NI LAZIMA NIWAUE….” Dominick alisema kwa hasira huku akiondoka mahali hapo kwa mwendo wa kasi kuelekea kule walipolipaki gari.
**********
5
Dominick hakuonekana kuwa na raha kabisa, huzuni ambayo alikuwa nayo katika kipindi cha nyuma ilikuwa imeongezeka zaidi. Kitendo cha kuwafahamu wabaya wake kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Hakuamini kama wale mawaziri ndio ambao wangeweza kumfanyia kitu kama kile.
Kila siku mawaziri wale walikuwa wakijifanya kuwa karibu na waandishi wa habari lakini kumbe walikuwa ni watu hatari ambao wala hawakutakiwa kusogelewa. Kila siku ambazo Dominick alikuwa akiwaona wakiongea katika vipindi mbalimbali vya televisheni, alibaki akiumia tu.
Akaamua kujipanga, alitaka kutekeleza kila kitu pasipo wasiwasi wowote wala kujulikana na mtu yeyote. Hakuona sababu ya watu wale kuendelea kuishi na wakati walikuwa wamemuumiza kwa kuiteketeza familia yake kwa kuichoma moto.
Alipanga kuwaua wote, tena si wao tu, angeanza na familia zao na kisha kuwaua wao wenyewe. Alitaka sana nao kwanza waanze kuumia kabla ya kuwamaliza. Alitamani wayaonje maumivu ambayo alikuwa ameyasikia hata kabla hawajaonja mauti.
“Nitaanza na nani sasa” Dominick alibaki akijiuliza.
“Walijiita BoT, nami nitaanza na majina yao kama jinsi yalivyo, ni lazima niwaue” Dominick alisema kwa hasira huku akijifunika shuka na kulala.
Siku iliyofuata Dominick akaanza kufanya maandalizi ya kazi yake ambayo alikuwa ameipanga kuifanya, alitamani kuifanya haraka sana hata kabla hakijaharibika kitu chochote kile. Hakuonekana kuwa na pupa, alitaka kuifanya taratibu lakini kwa umakini mkubwa sana.
Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuchukua kitabu kikubwa cha simu za mezani na kuanza kuziangalia namba za simu za ofisini mwao, alipozipata, akaziandika sehemu. Dominick hakuridhika, akaangalia na namba za simu za mezani za nyumbani kwao, nazo akaziandika pembeni pia.
“Nitahitaji unisaidie kitu kimoja” Dominick alimwambia Edmund.
“Kitu gani tena? Kukusaidia kazi yako?”
“Hapana. Kazi hii wala haihitaji msaada wa mtu yeyote, nataka kuifanya mimi mwenyewe”
“Sasa unataka nikusaidie nini?”
“Nahitaji mafuta ya petroli ya lita ishirini”
“Hilo si tatizo. Kuna jingine?”
“Labda na kiberiti pamoja na gari lako. Ile bunduki yako si unayo?” Dominick alimuuliza.
“Ninayo. Nayo pia unaitaka?”
“Ndo maana nikaiulizia”
Edmund akainuka na kwenda chumbani kwake ambako akamletea bunduki pamoja na kiberiti. Akachukua pochi yake na kutoa kiasi kilichotosha cha kununua petroli ya lita ishirini na kisha kuondoka kuelekea katika kituo cha kuuzia petroli.
Wala hakuchukua muda mrefu, akarudi, akamgawia Dominick mafuta yale na kisha kumkabidhi ufunguo wa gari lake. Dominick hakutaka kupoteza muda kubaki mahali hapo, moja kwa moja akatoka nje mpaka katika sehemu ya maegesho ya magari na kuchukua gari la Edmund.
“Nitachukua miezi mingi mpaka kurudi hapa. Nitahakikisha kazi inaanza kwa mmoja baada ya mwingine” Dominick alimwambia Edmund.
“Usijali. Kazi njema” Edmund alimwambia Dominick.
Dominick akaondoka na kuelekea katika hoteli ya La Vista Inn na kuchukua chumba. Hakutaka kuendelea kuishi nyumbani kwa Edmund katika wakati ambao atakuwa akiendelea na kazi yake ya kuuridhisha moyo wake. Huko hotelini ndipo sehemu ambayo alipanga kila kitu, namna ya kuanza kazi mpaka kuimaliza.
“Nitaanza na huyu waziri wa wa Utalii na Mali asili, Boniface Akwaiziwe. Nitaanza kuiangamiza familia yake kwanza, ili achanganyikiwe na aje Dar es Salaam kutokea Bungeni” Dominick alijisemea.
Tayari muda ulikuwa umekwenda sana. Saa ya ukutani wala haikuonekana kwenda tofauti na saa yake ya mkononi, zote zilikuwa zikimuonyesha kuwa tayari saa moja na nusu usiku. Akatoka chumbani na moja kwa moja kuanza kushusha ngazi mpaka chini ambako akaingia katika mghahawa wa chakula hapo hotelini na kuagizia chakula.
Kofia kubwa ya Malboro pamoja na miwani ambayo alikuwa ameivaa wala haikumfanya kujulikana. Alionekana kuwa mgeni kwa kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia. Alipomaliza kula chakula pale mghahawani, akarudi chumbani kwake kuendelea na kazi ya kupanga mbinu mbalimbali za mauaji.
“Nitaanza rasmi kesho. Ila dereva ndiye mtu wa muhimu sana kupatikana” Dominick alijisemea.
Siku iliyofuata ndio ilikuwa siku ambayo alitaka kuanza kazi. Alichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika nyumba ya waziri Boniface ambako akakaa mbali kidogo na geti lile huku macho yake yakiangalia getini. Wala hazikupita dakika nyingi, akamuona mtu mmoja akipiga hodi katika geti lile.
Dominick akayapeleka macho yake katika saa yake, ilikuwa ikimuonyeshea kwamba tayari ilikuwa saa kumi na mbili na robo asubuhi. Hakuwa na shaka kwamba yule aliyekuwa akigonga hodi alikuwa dereva, mtu ambaye alikuwa akimtaka kwa udi na uvumba.
Dominick akaliwahsa gari lake na kuanza kusogea kule geti lilipokuwa, alipomfikia, akateremka na kuanza kumsogelea huku kofia na miwani vikiwa vimemkaa vizuri.
Dereva yule bado alikuwa akisubiri geti lifunguliwe ili aingie ndani, achukue gari na kumpeleka mtoto wa Waziri shuleni. Mara akashtukia kitu kikiwa kimemgusa kisogoni, alipogeuka, akakutana na mdomo wa bunduki.
Dereva akaonekana kushtuka kupita kiasi, mdomo wa bunduki ulimfanya kumuogopesha. Akayapeleka macho yake usoni mwa mtu aliyemnyooshea bunduki, hakumfahamu kabisa kutokana na kofia pamoja na miwani ambayo alikuwa ameivaa.
“Ingia ndani ya gari langu haraka” Dominick alimwambia dereva ambaye bila kubisha, na kwa nidhamu zote, akaingia huku akitetemeka.
“Shikilia usukani. Nataka uendeshe gari wewe mwenyewe” Dominick alimwambia dereva ambaye kwa haraka sana, akashikilia usukani.
“Endesha moja kwa moja kuelekea nyumbani kwako” Dominick alimwambia dereva yule.
“Kwa nini kwangu lakini? Nimekufanya nini mkuu?” Dereva aliuliza huku akitetemeka.
“Nisikilize. Sihitaji maswali, fanya kile ambacho ninakuamuru kukifanya. La sivyo, nitatawanyisha ubongo wako sasa hivi” Dominick alimwambia dereva maneno ambayo yalizidi kumtetemesha zaidi
Hakuwa na jinsi zaidi ya kuwasha gari na safari ya kuelekea nyumbani kwake kuanza. Njia nzima alikuwa akitetemeka kwa hofu, kila alipokuwa akiuangalia mdomo wa bunduki, alizidi kutetemeka. Tayari nguo zake zilikuwa zimekwishaloana kwa sababu ya jasho ambalo lilikuwa likimtoka, amani yote ilikuwa imemtoka.
Aliendesha kwa makini sana huku akitii kila kitu ambacho alikuwa akiambiwa. Gari likasimama nje ya nyumba moja ambayo ilikuwa katika ujenzi wa kuuzungushia ukuta. Dereva akasimamisha gari na kumwangalia Dominick kwa wasiwasi.
“Tu..mekw..ish..afik..a” Dereva alimwambia Dominick huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Liingize gari katika eneo la nyumba yako” Dominick alimwambia dereva yule ambaye akatii amri.
“Hautakiwi kuonyesha wasiwasi wowote. Japokuwa haunifahamu, jifanye mimi ni rafiki yako wa muda mrefu. Ukifanya vingine, nitakuua wewe pamoja na familia yako. Umenielewa?” Dominick alimalizia kwa kwa kuuliza swali.
“Nimekuelewa mkuu”
Dominick akaiweka bunduki yake kiunoni na kuifunika na fulana yake. Hakutaka mtu yeyote ajue kama alikuwa na bunduki. Dereva akatulia kama alivyoamrishwa, akaufungua mlango na kuingia ndani. Akaanza kumuita mkewe, ambaye baada ya muda, akafika sebuleni hapo.
“Mbona umerudi tena?” Mkewe, Bi Amina alimuuliza huku akionekana kushangaa.
“Nimekutana na rafiki yangu, nimeamua kuja nae hapa” Dereva, Omari alimwambia mkewe.
“Sawa. Karibu mgeni”
“Asante”
Omari akakaa kochini na kuanza kuangaliana na Dominick ambaye muda wote uso wake ulikuwa umetawaliwa na tabasamu pana. Bi Amina akaondoka mahali hapo na kwenda jikoni kuandaa chai. Omari hakujua ni kitu gani ambacho kilitakiwa kuendelea, akazidi kumuangalia Dominick katika hali ya kutaka kuuliza swali.
“Tumekwishafika. Kuna kingine?”
“Ndio. Nataka uende kwa bosi wako. Ninawataka watoto wake wawili pamoja na mkewe uje nao hapa. Hakikisha unakuja nao” Dominick alimwambia Mrisho.
“Sasa nitawezaje kuja nao wote?. Kwa watoto sawa. Ila kwa mkewe sijui kama itawezekana” Omari alimwambia Dominick.
“Itawezekana tu. Wewe nenda, kama haitowezekana, basi acha nimuue mkeo” Dominick alimwambia Omari ambaye akaonekana kushtuka.
“Umuue mke wangu?”
“Ndio. Sasa si utakuwa umeshindwa kazi. Ni lazima nimuue kama hautoweza kuniletea wote ambao ninataka kuwaona mahali hapa” Dominick alimwambia Omari huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikiongea.
Omari hakuwa na jinsi, akamuita mkewe na kumuaga. Akaondoka mahali hapo huku akimuacha Dominick nyumbani hapo. Njia nzima Omari alionekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama Dominick angeweza kumuacha mkewe kama tu asingekifanya kile ambacho alitaka kifanyike. Akajiapiza ni lazima awachukue wote ambao walihitajika. Hakuonekana kuwa tayari kumpoteza mkewe.
Dominick hakutaka kuendelea kubaki mahali pale, alichokifanya ni kumuaga mkewe Omari kwa kumwambia kuwa alikuwa akielelekea sehemu fulani na baada ya muda angerudi. Dominick akatoka nje ambako akachukua gari lake na kuondoka mpaka hotelini, akaliacha na kurudi nyumbani kwa Omari kwa miguu huku kidumu cha petroli cha lita tano kikiwa mkononi mwake.
Dominick akafika na kukaribishwa tena na Amina, akatulia kochini na kuanza kunywa chai. Hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule hali ambayo Amina hakumtilia shaka hata kidogo. Kila wakati Dominick alikuwa akiiangalia saa yake, muda ulizidi kwenda lakini wala Omari hakurudi.
“Au atakuwa amekwenda polisi? Hapana hawezi kufanya hivyo” Dominick alijiuliza na kujijibu.
Wala haukuchukua muda mrefu sana, muungurumo wa gari ukaanza kusikikanje ya nyumba. Dominick akachungulia na alipoona ni gari la waziri Boniface, akatoka nje. Kwa haraka sana akaanza kulifuata, alipolifikia, Omari akateremka na Dominick kuingia ndani.
“Kazi nzuri sana. Mkeo yuko salama” Dominick alimwambia Omari huku akiingia garini na Omari akiteremka.
Kitu cha kwanza Dominick akayapeleka macho yake katika kiti cha nyuma, watoto wawili wa kike waliokuwa na sare za shule walikuwa nyuma pamoja na mama yao walikuwa wametulia. Mke wa waziri Boniface, Bi Upendo akaonekana kushtuka, tayari wasiwasi ukaanza kumuingia.
Hakujua sababu iliyompelekea Omari kuteremka na kumwachia gari mtu mwingie ambaye wala hakuwa akimfahamu. Akataka kuufungua mlango na kutoka nje, tayari milango yote ilikuwa imepigwa roki. Akateremsha kioo na kumwangalia Omari kwa uso uliojaa hasira.
“Ndio unafanya nini Omari?. Huyu ni nani na kwa nini unamuachia gari? Haujui kama hili gari ni la mtu mkubwa?” Bi Upendo aliuliza maswali manne mfululizo.
“Nimefanya hivi kwa ajili ya mke wangu mama. Kama nisingefanya hivi basi ni lazima ningempoteza mke wangu” Omari alimwambia Bi Upendo ambaye alionekana kushangaa.
Hata kabla hajauliza swali jingine, gari likaondolewa mahali hapo kwa mwendo wa kasi. Dominick hakutaka kuulizwa swali lolote lile, akaanza kuendesha gari kwa mwendo wa kasi. Lengo lake lilikuwa ni kufika katika ufukwe wa Coco kwani aliamini kwa asubuhi hiyo ya saa moja, kusingekuwa na watu wengi.
Bi Upendo alikuwa akiuliza maswali mengi huku akionekana kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa lakini Dominick hakujibu lolote, alikuwa kimya huku akionekana kuwa na hasira. Picha ya familia yake ikaanza kuonekana kichwani mwake, nyumba ambayo ilikuwa ikiteketea ikaanza kujirudia kichwani kama mkanda wa filamu.
Taswira ya miili ya familia yake ambayo ilikuwa imeteketezwa kwa moto ikaanza kuonekana kichwani mwake. Machozi yakaanza kumtoka, hasira ikazidi kumpanda, akaanza kupaona ufukweni mbali, alitamani gari liwe na mabawa, lipae na kutua ufukweni.
“Nyamazaaaaa….!” Dominick alimwambia Bi Upendo kwa sauti ya kelele iliyojaa hasira.
“Ni lazima niwaue. NI LAZIMA” Dominick alijisemea huku akiyauma meno yake kwa hasira
********
Kundi la BoT likaonekana kujipongeza. Kila siku ilionekana kuwa ya furaha kwao. Walipongezana kwa kazi nzito ambayo walikuwa wameifanya. Taarifa za uongo walizoletewa juu ya kifo cha Dominick na kifo cha Saida zilionekana kuwafurahisha kupita kiasi.
Waliambiwa na vijana wale kuwa walimfuata Saida nyumbani kwake ambako wakakutana na Dominick ambaye wakaamua kuondoka nae mpaka porini, na huko ndipo walipoamua kuwaua wote wawili. Taarifa ile ya uongo ilionekana kuwa ya faraja kwao, hakukuwa na mtu ambaye alionekana kubisha na wakati mpaka picha za kutengenezwa walikuwa wamekabidhiwa.
Kila siku kwao ilionekana kuwa kama sikukuu. Walikunywa na kufurahia pamoja. Kila siku muda wa Bunge ulipokuwa ukimalizika, walikuwa wakikutana katika mghahawa ulioitwa Matimya ambao ulikuwa katikakati ya mkoa wa Dodoma na kufurahia pamoja.
Walionekana kukamilisha kazi ndefu ambayo ilikuwa ikiwasumbua vichwa vyao, walijiona kuwa na amani sasa. Glasi zao zilikuwa hewani, wakazigonganisha na kisha kuanza kunywa huku wakiongea maneno mbalimbali yaliyojaa dhihaka juu ya Dominick.
“Kiko wapi sasa? Alijifanya anajua sana” Mzee Boniface aliwaambia wenzake.
“Tusimlaumu jamani. Hakujua kama analeta mzaha kwa watu walio na mikono mirefu” Waziri Ombeni aliwaambia na wote kuanza kucheka.
“Cheeeeerrs! Kwa ajili ya marehemu Dominick na Saida” Waziri Tumaini alisema huku akinyanyua glasi juu.
“Cheeeeerss….! Bwana Ombeni na Boniface waliitikia.
********
Dominick akaingia katika eneo la ufukwe na kulipaki gari lile. Kutokana na wakati kuwa asubuhi sana, hakukuwa na watu ufukweni. Kwa haraka haraka huku akionekana kuwa na hasira akateremka huku mkoni akiwa na kidumu cha mafuta ya petroli.
Bi Upendo akabaki akipiga kelele za kuomba msaada, hali tayari ikaonekana kuwa ya hatari. Alipiga kelele sana lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alizisikia kelele zile. Dominick akaanza kulimwagia petroli gari lile. Kila kitu ambacho alikifanywa kwa wakati huo alikifanya kwa haraka haraka.
Alipomaliza kulimwagia petroli kwa nje, akafungua mlango na kuanza kuwamwagia petroli Bi Upendo pamoja na watoto wake. Wote walikuwa wakilia ndani ya gari lakini wala Dominick hakuonekana kujali. Machozi yalikuwa yakimtoka kwa hasira.
Taswira ya nyumba ambayo ilikuwa ikiteketea ikaanza kumjia kichwani, hasira zaidi zikampanda kiasi cha kujuta kwa kuja na lita tano, aliziona ndogo sana. Alipomaliza, akachukua kiberiti na kuliwasha moto gari lile. Kelele za Bi Upendo na watoto wake zikazidi kusikika zaidi.
Kila Bi Upendo alipojaribu kuufungua mlango kwa ajili ya kutoka nje, milango ilikuwa imepigwa roki. Harufu za nguo zlizokuwa zikiungua kwa moto ikaanza kusikika kunuka na hatimae harufu ya miili iliyokuwa ikiteketea ikaanza kunuka pia.
Kutokana na upepo kuwa mkubwa ufukweni pale, moto ule ukaonekana kuchochewa. Mara milio ya vitu vitatu vilivyoonekana kupasuka vikasikika kutoka garini, hivyo vilikuwa vichwa ambavyo vilikuwa vimepasuka kutokana na kuteketezwa sana na moto.
Kuteketea kwa gari lile kukawafanya watu waliokuwa mbali kabisa kuanza kuuona moto mkubwa, wakaanza kukimbilia kule ambako moto ule ulipokuwa. Dominick hakuwepo mahali pale, tayari alikuwa amekishaondoka huku moyo wake ukionekana kuridhika kiasi.
Kila mtu aliyefika mahali pale alibaki akishangaa, watu wote walibaki wakiwa wameduwaa tu, hawakujua wafanye nini na wakati gari lilikuwa likizidi kuteketea kwa moto. Baada ya muda watu wakaonekana kurudiwa na akili zao, wakaanza kuchukua maji baharini na kuanza kuuzima moto ule. Moto ukazimika, wakasubiri bodi lipoe ili kuangalia kama kulikuwa na mtu yeyote garini.
Mlango wa gari ukavutwa, kijana mmoja akachungulia garini, kile ambacho alikiona alishindwa kuvumilia, akatoka huku akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa. Kila alipokuwa akiulizwa aliona nini, hakuongea kitu chochote kile, alikwenda pembeni na kuanza kutapika.
“Kuna nini? Umeona nini?” Kijana mwingine alimuuliza.
“Nendeni mkaangalie wenyewe. Inatisha”
“Inatisha? Inatisha nini?”
“Nyie kaangalieni tu”
Vijana wengine wakaelekea katika gari lile na kuchungulia ndani. Miili mitatu ilikuwa ikionekana vizuri huku ikiwa imeteketea kwa moto na huku ikitoa moshi. Simu zikaanza kupigwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay ili kuwaomba mapolisi kufika mahali hapo haraka iwezekanavyo.

Post a Comment