MKOA WA KAGERA WACHUKUA TAHADHARI DHIDI YA EBOLA
Mkuu
wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe akitoa ufafanuzi namna
Serikali livyojipanga kukabiliana na ugonjwa wa Ebola mkoani humo kwa
kuongeza vifaa kinga na kuwawezesha kielimu wataalam wa afya wanaofanya
kazi ya uchunguzi wa dalili za ugonjwa huo walioko katika vituo vya
ukaguzi mpakani.
Afisa Afya wa Kituo cha Ukaguzi cha Kabanga, mpakani mwa Tanzania na
Burundi Bw. Amos Mangaluke akipitia fomu zilizojazwa na raia kutoka nje
ya nchi wanaotumia mpaka huo kufuatia zoezi la uchunguzi wa dalili za
awali za ugonjwa wa Ebola linalofanyika kituoni hapo.
Ofisi ya Uhamiaji ya Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Kizuizi cha magari katika mpaka wa Kabanga unaotenganisha Tanzania na Burundi, wilayani Ngara.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO
31/8/2014, Kagera
MKOA
wa Kagera umechukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa kuongeza
nguvu katika udhibiti na ukaguzi wa raia wa kigeni kutoka nchi za
Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoingia
nchini Tanzania kupitia vituo vya mpakani vya mkoa huo.
Akizungumza
katika mahojiano maalum wilayani Ngara, Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali
mstaafu Fabian Massawe amesema kuwa kufuatia hali hiyo serikali kupitia
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeongeza vifaa kinga na kuwawezesha
kielimu wataalam wa afya walioko katika hospitali za mkoa huo na vituo
vya ukaguzi mpakani.
Amesema kuwa mkoa huo kijiografia unapakana
na nchi tatu zikiwemo Uganda kwa upande wa Kaskazini, Rwanda na Burundi
kwa upande wa magharibi na kuongeza kuwa mkoa kupitia kamati za Afya na
wataalam wa afya walioko maeneo yote ya vituo vya ukaguzi wanafanya kazi
zao ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa kila anayeingia nchini kupitia vituo
hivyo anachunguzwa dalili za Ebola.
“Mkoa wa Kagera kama
tunavyojua unapakana kwa karibu sana na nchi za Burundi, Rwanda na
Uganda, kuna mwingiliano mkubwa sana wa watu kutoka eneo moja kwenda
jingine hapa lazima tuchukue tahadhari kubwa , ninawahakikishia wananchi
kuwa tumejipanga vizuri katika kuimarisha uchunguzi kupitia kamati
zetu za afya” Amesisitiza.
Amesema kufuatia uwepo wa ugonjwa huo
katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uongozi wa
mkoa kupitia kamati ya Afya na ile ya Ulinzi na Usalama unaendelea
kuwaelimisha wananchi kupitia vituo vya mbalimbali vya radio vya mkoa
huo kuhusu dalili za ugonjwa huo , namna ya kujikinga na namna ya kutoa
taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini mtu mwenye dalili za ugonjwa
huo.
Kwa upande wake Afisa Afya wa Kituo cha ukaguzi cha
Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi Bw. Amos Mangaluke
akizungumzia hali ya ukaguzi wa raia wanaoingia nchini kupitia mpaka huo
amesema kuwa zoezi la uchunguzi wa dalili za awali za ugonjwa wa Ebola
linafanyika kwa ufanisi mkubwa kufuatia kituo chake kuwa na vifaa kinga
vinavyomsaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema
takribani watu 500 wanaotumia mpaka huo wa Kabanga huchunguzwa afya zao
kwa siku ambapo hujaza fomu maalum ya taarifa ambayo hutumiwa na
wataalam wa afya kituoni hapo.

Post a Comment