ad

ad

She is too young to die - 9



Msomekela  katika zahanati yake maeneo ya Sinza ambaye baada tu ya kumwona mtoto na kumsikiliza kifuani aliwaambia hapo hapo kwamba mtoto wao alikuwa na tatizo liitwalo PDA! Wakakutwa na mshtuko, ilikuwa ni mara ya kwanza wao kusikia jina hilo.
Je, nini kitaendelea? Maisha ya mtoto huyo pekee wa Salome na Gilbert yataokolewa? SONGA NAYO…

Gilbert na mke wake walikuwa wakitetemeka,  hofu kubwa ilikuwa imewapata, katika maisha yao hakuna hata mmoja kati yao aliyewahi kusikia neno hilo! Lilikuwa geni,   picha iliyowajia kichwani ni  kwamba huo ulikuwa ni ugonjwa mkubwa tena mpya kama ilivyokuwa kwa  magonjwa kama Homa ya Bonde la Ufa au Ebola. Waliendelea kumshuhudia daktari akimpima Faith kitandani, aliponyanyuka kuwaangalia kwa mara ya pili swali lao lilikuwa ni lile lile,  PDA ulikuwa ni ugonjwa gani.
“Ni maelezo marefu kidogo, kaeni kwenye kiti ili niwafahamishe!”
“Una tiba?” Gilbert aliuliza, hakuna kitu alichotaka kukifahamu  zaidi ya kupona kwa mtoto wake.
“Tulia Gilbert niwaelezeni, usiwe na haraka, tutafika tu huko!”

Wote wawili wakaketi kwenye viti vya mbao maarufu kama ‘office chair’ vilivyokuwa mbele ya  meza ya Dk. Msomekela ambaye usoni kwake wala hakuonyesha wasiwasi wowote,  tabasamu lilikuwa vile vile na sauti yake ya upole iliendelea kumtoka taratibu akiwaondolea wasiwasi. Ilikuwa ni kawaida ya madaktari kutoonyesha mshtuko hata kama mgonjwa alikuwa na hali mbaya kiasi gani, lakini kwa uzoefu wake Gilbert macho ya Dk. Msomekela yalimwonyesha wazi kwamba tatizo la mtoto wao lilikuwa kubwa.
“Tumetulia daktari tueleze sasa!”
“Kabla mtoto hajazaliwa, akiwa tumboni mwa mama yake huwa ana mfumo wake wa damu ambao hauchanganyiki kabisa na mfumo wa mama! Damu huwa inakutana kwenye kondo la nyuma tu ambako damu ya mtoto huja kuchukua hewa safi, chakula na kuacha hapo uchafu ili utolewe nje na mama! Hii inamaanisha kwamba kwa sababu hewa safi hutoka kwenye damu ya mama, mapafu ya mtoto huwa hayafanyi kazi…mnanisikia?”
“Ndio daktari tunakusikia!” Gilbert  aliitikia akimsikiliza daktari kwa makini,  Salome  wala hakusema chochote, machozi yalikuwa yakimbubujika na kulowanisha nguo zake! Alijisikia  miongoni mwa binadamu wenye bahati mbaya, tayari alishapoteza mfuko wake wa uzazi,  alishapoteza baba yake na sasa mtoto pekee ambaye angekuwa naye maishani ndiye  huyo aliyekuwa katika hali mbaya bila matumaini ya kupona.
“Salome!” Daktari aliita.
“Bee daktari!”
“Unanisikia?”
“Nakusikia daktari, lakini  napenda kufahamu kama mwanangu atapona!”
“Sikiliza kwanza, nataka mnielewe vizuri…!”
“Sawa!”  Salome aliitikia akijifuta machozi, muda huo huo Faith alianza kulia tena kwa sauti ya juu, akanyanyuka kwenda kumchukua kutoka kwenye kitanda alipomlaza na kuketi naye mikononi akijaribu kumpa titi ili anyonye lakini hakuwa tayari.
“Moyo una vyumba vinne,  viwili juu vinavyoitwa Atriums  na vya chini vinaitwa Ventricles, katika mwili wa binadamu mkubwa vyumba vya juu  husukuma damu kwenda kwenye vyumba vya chini kupitia kwenye valvu ziitwazo Bicuspid na Tricuspid, damu ikiwa  kwenye  chumba cha chini upande wa  kushoto husukumwa kuingia kwenye mshipa uitwao Pulmonary Vein kwenda kwenye mapafu kuchukua hewa safi na   iliyopo  kwenye chumba cha  chini kulia  ambayo huwa imetoka kwenye mapafu kuchukua hewa husukumwa kuingia kwenye mshipa uitwao Aorta kwenda sehemu mbalimbali za mwili! Mmenielewa?”
“Ndio daktari!”
“Sasa   hiyo ni kwa mtu mzima kama mimi na ninyi lakini  kwa mtoto mdogo mapafu huwa hayafanyi kazi, hivyo damu inayosukumwa kutoka kwenye chumba cha chini kushoto badala ya kwenda kwenye mapafu huingia kwenye mshipa wa Aorta, kupitia kwenye tundu liitwalo Ductus arteriosus na kupelekwa sehemu mbalimbali za mwili wa mtoto! Tundu hili hutakiwa kuziba muda mchache tu baada ya mtoto kuzaliwa na kulia ambapo mapafu huanza kufanya kazi, hivyo damu kuanza kupita kwenye mshipa wa Pulmonary Vein kwenda kwenye mapafu kuchukua hewa ya oksijeni, kwa bahati mbaya kwa baadhi ya watoto tundu hili huwa linagoma kuziba, ndipo PDA hujitokeza, PDA ni kifupi cha neno PATENT DUCTUS ARTERIOSUS, nikimaanisha tundu lililogoma kuziba, mmenielewa?”
“Ndio,  kwa hiyo mtoto wetu ana tundu lililogoma kuziba?”
“Dalili zote zinaonyesha hivyo,  hata hivyo itabidi nifanye kipimo kiitwacho ECG ili niweze kuona namna moyo unavyofanya kazi!”
“Ugonjwa huo una tiba?”
“Ni mpaka upasuaji!”
“Hapa nyumbani inawezekana?”
“Sio rahisi, lazima msafiri kwenda India tena haraka iwezekanavyo!”
“Mungu wangu!” Salome alijishika kichwani.
Daktari aliandika kwenye faili na kuagiza mtoto alazwe kwenye  chumba cha wagonjwa mahututi wakati vipimo vikifanyika, huko aliwekewa hewa ya oksijeni na mpira wa kula chakula kupitia puani huku akipewa dawa za kuuongeza moyo wake nguvu ya kufanya kazi! Masaa ishirini na nne  baadaye, Gilbert akiwa bado yuko nje ya wodi, majibu ya vipimo vyote yalitoka na kuonyesha alichokisema daktari kilikuwa sahihi, Salome aliposikia hivyo moyo wake ulianza kwenda mbio, akamtaarifu mume wake ambaye bila kuchelewa alimwambia daktari, akapimwa mapigo na kuonyesha yalikuwa yameshuka mpaka kufikia tisini chini ya sitini!
“Una presha ya kushuka?”
“Ndio!”
“Ngoja tukupe kitanda upumzike wakati mimi na mumeo tukiendelea na taratibu nyingine, hapa hakuna tunachoweza kufanya zaidi ya ninyi kusafiri haraka sana kwenda India vinginevyo tunaweza kupoteza mtoto,  tatizo lake limekomaa sana, alitakiwa kuwa amegundulika mapema lakini bahati mbaya madaktari mliopita mikononi mwao hawakugundua tatizo lake wakaendelea kumpa dawa ambazo hazikuwa sahihi!” alisema Dk. Msomekela na  alipokwishakutoa maagizo ya Salome kupewa kitanda pamoja na dawa za kumsaidia kupandisha mapigo yake,  yeye na Gilbert waliondoka kwenda moja kwa moja  Wizara ya afya kufanya mpango wa mgonjwa kusafirishwa kwenda India, waliporejea   dakika arobaini na tano baadaye walimkuta  Salome akiwa na hali nzuri kidogo.
“Vipi imekuwaje huko?”
“Hali ni mbaya, kuna wagonjwa  elfu moja wanaosubiri kusafirishwa! Hivyo kama sisi tunataka mtoto wetu aende kutibiwa ni lazima tukae kwenye foleni,   Faith awe wa elfu moja na moja! Sijui lini atapelekwa”
“Gilbert, tumia akili yako tuokoe maisha ya mtoto wetu, hatuwezi kuwa na mtoto mwingine tena!”
“Sawa, lakini nitafanyaje sasa? Acha nifikirie!”“Gilbert, tumia akili yako tuokoe maisha ya mtoto wetu, hatuwezi kuwa na mtoto mwingine tena!”
“Sawa, lakini nitafanyaje sasa? Acha nifikirie”
“Huyu ndiye mtoto pekee tuliyenaye,  tufanye  kila kinachowezekana kuokoa maisha ya Faith! Sitazaa tena maishani Gilbert!” aliongea Salome huku akimwangalia mumewe kwa macho ya kukata tamaa.
Maneno  ya Salome yaliuchoma moyo wa Gilbert moja kwa moja na kusababisha maumivu makali,  akagundua ni kweli alikuwa na wajibu wa kuokoa maisha ya mtoto wake hata kama angelazimika kutumia utajiri wote aliokuwa nao, roho ya Faith ilikuwa muhimu kuliko mali. Akiwaza hayo alirejea moja kwa moja kwenye kumbukumbu zake ubongoni,  akakutana na jina Mukesh Dhruve na  matumaini ya kuokoa maisha  ya mtoto wake yakarejea, akauona mwanga wa kumfikisha Faith India mapema kuliko kuendelea kusubiri mstari wa wagonjwa Wizarani.

Lilikuwa jina la mfanyabiashara kutoka India ambaye pia alijishughulisha na biashara ya vifaa vya kompyuta katika mji wa Mumbai, yeye na Gilbert walikutana    jijini London  miaka miwili kabla kwenye maonyesho ya kampuni ya vifaa vya Microsoft na kutokea kuwa marafiki kwa sababu walipangishiwa vyumba kwenye  hoteli moja! Wakaongea mengi katika muda wa wiki nzima walioishi pamoja,  hatimaye wakati wa kuagana walibadilishana kadi zao na Mukesh kumkaribisha Gilbert na familia yake nchini India ili apate kumpeleka kwenye maeneo ya kupumzika huko Goa.

Gilbert hakuwa na uhakika kama mtu huyo angeweza kumkumbuka lakini aliamini ndiye pekee angeweza kumsaidia kwenye tatizo lililokuwa likimkabili, alibaki amesimama huku akijaribu kukumbuka mahali alipoiweka kadi yake na kama aliondoka nayo London au aliitupa, akajilaumu kwa tabia yake ya kutotunza vitu vidogovidogo bila kujua baadaye vingemsaidia.
“Sijui niliiweka ofisini?...” alijiuliza bila kuwa na uhakika.
“Please Gilbert  do something,  our baby is dying!” (Gilbert tafadhali fanya  jambo, mtoto wetu anakufa!)
“Salome be patient, I am thinking of what to do!...let me go to the  office, I will be back in a short while” ( Salome kuwa mvumilivu,  nafikiria juu ya nini cha kufanya!...hebu acha niende ofisini, nitarudi baada ya muda mfupi)
“What are you going for?” (Unafuata nini?)
“I will let you  know  once I am back!” (Nitakuambia nikirudi!) Gilbert aliongea na kutoka mbio akikimbia,  mke wake hakuelewa ni kitu gani alikuwa akikifuata, akageuka na kumkumbatia mwanae kitandani.
Faith alikuwa akihangaika kuhema pamoja na kuwa na mashine ya hewa ya oksijeni puani, mbavu zilikuwa nje,  mashimo yakionekana katikati yake kila alipovuta  pumzi ndani! Alikuwa amekonda na kubaki mifupa tupu,  Salome hakuweza kuvumilia,  machozi yalianza kumtoka huku akiendelea kumwomba Mungu atende muujiza!  Hakuna picha iliyomuumiza kama kumwona mwanae wa pekee, akihangaika kitandani. Ghafla alishtukia nguvu zikimwisha mwilini, akaanguka sakafuni. Alipozinduka baadaye alikuwa amelazwa juu ya kitanda akiwa na dripu mkononi na pembeni alikuwepo Dk. Msomekela pamoja na Gilbert.
“Pole mke wangu!”
“Ahsante Gilbert lakini sijui kilichotokea?”
“Daktari anaweza kukuelezea!”
“Presha yako ilishuka ghafla mpaka tisini chini ya hamsini lakini tumejitahidi kuipandisha   na hivi sasa ipo mia moja kwa sabini, tuliza moyo Salome, vinginevyo wewe na mtoto wako wote mtakuwa wagonjwa,  Faith atapona tu wala usiwe na shaka!”
“Ahsante daktari…umefikia wapi mume wangu kuhusu suala la safari?”
“Nilikwenda ofisini kutafuta kadi ya rafiki yangu mmoja wa huko India, nilikutana naye London miaka miwili iliyopita,  bahati nzuri nikaipata na nimempigia  simu nikimwomba msaada! Amekubali kutusaidia lakini tutakachokifanya  ni kwamba,   inabidi atutumie barua ya mwaliko kama tunakwenda kumtembelea mimi, wewe na mtoto wetu ili tupate viza ya kuingia India, hatutasema mtoto wetu ni mgonjwa, tukifanya hivyo hatutaruhusiwa kupanda ndege!”
“Ahsante Gilbert,  ahsante kwa kujali, kwa hiyo nini kinaendelea hivi sasa?”
“Tayari amekwishatuma barua lakini ubalozi hivi sasa hawapokei maombi ya viza mpaka kesho,  tumwombe Mungu asaidie ili mtoto wetu afike hiyo kesho, tutapata viza na kuondoka!”
“Kweli?”
“Nakueleza ukweli mke wangu,  wala huna sababu ya kulia, mwanetu atapona!”
“Nitashukuru mno, nampenda mno Faith!”

Pamoja na  Faith kusumbua sana usiku,  alifanikiwa kuiona asubuhi na Gilbert alikuwa mtu wa kwanza kufika kwenye jengo la ubalozi wa India huko Oysterbay kando kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kuambiwa asubiri mpaka saa tatu kamili muda ambao ubalozi huanza kupokea fomu za maombi. Hakuweza kukaa ubalozini mpaka muda huo ikabidi arejee  hospitali kuendelea kumwona mtoto wake,  saa mbili na nusu aliondoka tena na kuwasili ubalozini saa tatu,  akachukua fomu na kuzijaza kisha kulipia visa ya haraka akitakiwa kuongeza kiasi cha shilingi elfu ishirini kwa kila viza moja.
“Hati za kusafiria?”
“Hizi hapa!”
“Kwani mnaosafiri ni wangapi?”
“Watatu, mimi, mke na mtoto wetu!”
“Hati ya mtoto?”
“Hana!”
“Sasa utasafirije na mtoto hana hati ya kusafiria?” Aliuliza mwanamke huyo wa Kitanzania mfanyakazi wa  ubalozi wa India.
“Mama nisaidie!”
“Sio rahisi!”
“Mwanangu anaumwa,  nampeleka hospitali!” Ilibidi Gilbert ajieleze kwa undani bila kuficha, mama huyo akamwonea huruma na kumtaka akimbie haraka ofisi za uhamiaji kutafuta hati ya dharura, Gilbert akaondoka kwa kasi ya ajabu mpaka makao makuu ya Uhamiaji ambako  kwa kutumia umaarufu wake alifanikiwa kupata hati hiyo na kurejea ubalozi wa India ndani ya dakika arobaini na tano  akamkabidhi mama huyo hati.
“Afadhali! Basi rudi saa saba kuchukua  hati zako zenye viza”
“Ahsante mama…” aliongea Gilbert akipenyeza mkono wenye shilingi lakini mbili kiganjani.
“Hapana mwanangu, nakusaidia tu!”
“Basi nakushukuru mzazi wangu, acha nikashughulikie tiketi kabla sijarudi hapa saa saba!”
“Hakuna shida!”

Gilbert alitoka nje ya ubalozi akikimbia,  moyo wake ulisharejewa na furaha kidogo baada ya matumaini ya safari kuanza kuonekana. Nje aliingia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi hadi ofisi za shirika la ndege la Kenya ambako alishughulikia taratibu zote za tiketi,  akakata tatu za kuondoka siku hiyo hiyo saa kumi na moja jioni.  Furaha aliyokuwa nayo hakutaka iwe yake peke yake,  alichokifanya ni  kuchukua simu ya mkononi na kupiga namba ya Salome, iliita kwa muda mrefu baadaye ikapokelewa na sauti nyingine tofauti.
“Hallo!”
“Naomba kuongea na mwenye simu!”
“Hawezi kuongea kwa sasa, anatibiwa!”
“Anatibiwa?”
“Ndio!”
“Kawaje tena? Mimi ni mume wake naitwa Gilbert!”
“Ni Dk. Msomokela anaongea hapa, Gilbert…presha ya mke wako imeshuka tena, tena safari hii imeshuka zaidi,  najaribu kadri ya uwezo wangu kuinyanyua! Nakushauri kama haupo mbali sana na hapa hospitali,  tafadhali rejea mara moja!”

Gilbert hakujibu kitu, alichofanya ni kukata simu na kuondoka kwenye ofisi za shirika la ndege la Kenya jengo la Peugeot  karibu kabisa na hoteli ya Moven Pick akiwaacha wafanyakazi ndani ya ofisi hiyo katika mshangao, hakuwa Gilbert  waliyezoea kumsikia,  wote walikuwa na uhakika kulikuwa na tatizo lililomsumbua. Walichosikia baada ya hapo ni muungurumo wa gari likiondoka kwa kasi na  dakika thelathini tu baadaye Gilbert alikuwa akiegesha nje ya jengo la hospitali na kuruka kabla gari halijasimama vizuri, hakukumbuka hata kufunga mlango.
“Njoo kwanza ofisini kwangu!” Dk. Msomokela alimwambia baada ya kukutana naye mlangoni na Gilbert akamfuata akiwa na wasiwasi mwingi.
“Daktari niambie, nini kimempata mke wangu?”
“Nimekuzia usiingie kwa sababu utamshtua tena,  presha yake imeanza kutengemaa kidogo,  mwache apumzike ila hali ilikuwa mbaya!sielewi ana presha ya aina gani Salome,  umefikia wapi kuhusu tiketi?”
“Safari yetu ni saa kumi na moja jioni,  tunatakiwa uwanja wa ndege saa tisa!”
“Gilbert nasikitika kukuambia kama hali ya mke akiendelea hivi sitaruhusu asafiri, atafia angani!”
“Daktari!”
“Ni kweli kabisa, presha yake inashuka mno na hali ya angani ninavyoifahamu mimi lazima inaweza kugharimu maisha yake!”
“Daktari tafadhali fanya kitu nisafiri na mke wangu!”
“Siwezi kuhatarisha maisha ya watu wawili,  hata kwa Faith sina jinsi tu kwa sababu ni bora kujaribu kuliko kubaki naye hapa akafa tukimwangalia!”
“Daktari! Nataka kusafiri na mke wangu,  fanya kitu fulani tafadhali,  mpe dawa ya kupandisha mapigo yake, nataka kama Faith atakufa afe sote tukiwa pamoja!”
“Sidhani kama itawezekana, wacha tuangalie!”
“Naweza kuingia?”
“Ingia lakini usimsumbue!”
“Sawa!”
Gilbert aliingia ndani ya chumba na kuwakuta wagonjwa wake wote wakiwa katika hali mbaya,  hakudiriki kuongea chochote akatoka nje na kuanza kulia kama mtoto mdogo,  akijaribu kutafakari ni kitu gani hasa kilichokuwa kikitokea katika maisha yake. Angekuwa ni mtu anayeamini ushirikina, lazima angehisi  kuna mkono wa mtu lakini huo haukuwa uwanja wake wa fikra.

 Alibaki hapo mpaka saa yake ya mkononi ilipogonga saa sita na nusu ndipo akaondoka na kuendesha gari hadi ubalozi wa India ambako alikabidhiwa  hati zake za kusafiria zikiwa na viza za kuwaruhusu  yeye, mke na mtoto wake kuingia katika nchi hiyo. Wasiwasi pekee aliobaki nao ni kama hali ya Salome ingeruhusu kusafiri na kama Faith angeruhusiwa kupanda ndege kwa hali aliyokuwa nayo.
“Daktari vipi hali yake?”
“Afadhali kidogo lakini hawezi kusafiri!”
“Mh!”
“Usigune Gilbert, unampenda mkeo?”
“Sana!”
“Usisafiri naye!”
Kauli hiyo ilimfanya Gilbert apige magoti chini na kuanza kumwomba Mungu atende muujiza lakini jambo hilo halikuwezekana mpaka saa tisa kamili, ndipo akaingia chumbani na kumkuta Salome akiwa macho! Alishindwa kuelewa aanze vipi kumwambia yeye asingesafiri lakini Dk.Msomokela akachukua jukumu la kufikisha ujumbe huo, Salome alilia  kuliko alivyowahi kulia.
“Daktari niache niende!”
“Haitawezekana Salome!”
“Hata nikifa ni sawa!”
“Siwezi kuruhusu jambo hilo!”
“Gilbert…!”
“Nakupenda na pia ninampenda Faith…nenda mume wangu, una baraka zangu zote, Mungu atasafiri na wewe pamoja na mwanangu, Faith hatakufa,  bali ataishi! Roho ya mauti inayomnyemelea mwanangu haina nguvu!”
“Amina!” Gilbert aliitikia na kukisogelea kitanda cha Faith ambaye tayari alishaandaliwa,  akambeba na kumshika mikononi mwake kisha kurejea tena kwenye kitanda cha Salome na kumpiga busu usoni,  wote wawili wakalia na baada ya hapo Gilbert akatembea kwenda mbele,  mlangoni akageuka kuangalia nyuma,  macho yao  yakagongana.
“Ubaki salama mke wangu, safari yangu ni ya masaa saba, nitakupigia mara nikifika Mumbai kukujulisha kinachoendelea, unasikia Salome?”
“Na..si..kia!”
Gilbert akaondoka, kichwani mwake akifikiria namna ambavyo angeingia kwenye ndege bila kugundulika kwamba mtoto wake alikuwa mgonjwa. Nje ya hospitali alikuta wafanyakazi wake ndio wanawasili kuja kusalimia mtoto,  akamwomba mmoja wao amwendeshe mpaka uwanjani na kurudi na gari.

ITAENDELEA SIKU YA KESHOOOOOOOOOOOOOOO

No comments

Powered by Blogger.